miércoles, 28 de octubre de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 30 YA MWAKA-B

ALHAMISI WIKI YA 30 YA MWAKA-B
29/10/2015
Somo: Rum 8:31b-39
Zab: 109:21-22, 26-27, 30-31
Injili: Lk 13:31-35
Nukuu:
“Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?” Rum 8:31b 

Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki,” Rum 8:33

Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea,” Rum 8:34

Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda,” Rum 8:37 

Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu,” Rum 8:38-39

Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika,” Lk 13:32 

Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka,” Lk 13:34 

Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana,” Lk 13:35

TAFAKARI:Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?”

Wapendwa wana wa Mungu, Mwana falsafa Spinoza aliwahi kusema “kifo hakiwezi kuepukika. Ni lazima tutakukufa. Kinachotusumbua ni hofu kuhusu kifo. Hivyo yatupasa kuishinda hofu. Na hivyo ni vizuri kufikiri kuhusu uhai.” Mpendwa, je wamwamini Kristo Yesu? Kama unamwamini Kristo Yesu hakuna sababu ya kuwa na hofu kuhusu kifo. Kristo Yesu kwa maisha yake, mateso, kifo, na ufufuko wake ni jibu kuhusu aina zote za uovu na kifo. Kristo Yesu ndiye kielelezo chetu kama wafuasi wake. Kristo Yesu ametupatia mfano na jibu kwamba hakuna uovu wowote unaoweza kudumu katika umilele wake. Yesu haogopi vitisho wala kifo.

Yesu anapoambiwa aondoke kwa kuwa Herode anataka kumuua aliwajibu, “Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika,” Lk 13:32. Mnyama huyu Mbweha alitafsiriwa kama mtu asiye na msimamo, kigeugeu na mwongo. Kristo hawezi kutishiwa na mtu wa hali hii na kuacha kutoa huduma kwa watu ikiwa ndiyo sababu na mpango kazi wake kwa watu wote. Ni kwa kupitia Kristo vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema,” Mt 11:5. Kristo pia anaufunua utukufu wake mara baada ya kuushinda uovu anaposema, ‘siku ya tatu nakamilika.’

Mateso tunayoyapata leo au tuliyokwisha yapata kupia wazazi wetu, siyo kwamba historia hiyo ya uovu Mungu haioni. Wakati utimiapo vyote vitafanywa upya. Yesu anapoutazama mji wa Yerusalemu anayakumbuka na kuyaona mateso na uovu wa manabii wake walifanyiwa na kusema, Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka,” Lk 13:34. Huu kwetu ni wito wa kuongoka na kuacha njia zetu mbaya na kujisalimisha kwa Kristo. Tusisubiri hadi siku ya Mwisho kwani hatutakuwa na muda tena wa kujisalimisha kwake. Utakuwa muda wa kupokea ukumu yetu kila mmoja kadiri alivyotenda. Yesu anasema, Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana,” Lk 13:35. Je, kuna sababu ya kusubiri hadi siku ya mwisho? Ndugu yangu natuanze kuishi maisha ya ufufuko kabla ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.

Maisha baada ya ufufuko ni maisha yaliyokamili. Tunayaishi maisha haya ya ufufuko kwa kuhesabiwa haki na kwa kuzaliwa mara ya pili kwa Roho Mtakatifu. Hivyo si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu,” Tit 3:5-7. Je, una sababu yoyote ya kuwa na hofu juu ya maisha yako ukiwa na Kristo?

Tukiwa ndani na katika Kristo tu wateule wa Mungu na hakuna wa kutushitaki kwa sababu Mungu kwa kupitia mwanaye Mpenzi ndiye anayetuhesabia haki. Basi Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki,” Rum 8:33. Katika hali hii hakuwa wa kutuhukumia adhabu kwa sababu tumeshayasalimisha maisha yetu kwa Kristo mwenyewe aliyekubali kufa kwa ajili yetu. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake,” Rum 6:5. Hapa adhabu ya kifo na hofuzimebatilishwa kwa kifo chake Kristo. Hivyo Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea,” Rum 8:34.

 Ndugu yangu, Kristo akupende vipe tena uamini anakupenda? Huku ndipo Kristo alipotupenda upeo na wakati ulipofika aliyatoa maisha yake kwa sababu yako na yangu. “Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh 13.1. Upendo huu hadi leo Kristo anauthibitisha kwetu tunapoutazama msalaba akiwa ameifungua mikono yake na kusema, ‘tazama ninavyokupenda nimekubali kufa kwa sababu yako.’

Tunapo jisalimisha kwa Kristo hakika nguvu za giza na uovu wa aina yoyote ile hauwezi ukashinda kwa sababu Kristo anatupenda.  Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda,” Rum 8:37. Kutokuwa na Imani pamoja na kutengemea vitu vingine mfano pesa na mamlaka fulani ni moja ya vizuizi vinavyotufanya kushindwa kujisalimisha kwa Jemedari wetu Yesu Kristo.

Wapendwa wana wa Mungu, tunapojisalimisha kwa Kristo hakuna kitu wala kiumbe chochote kinachoweza kututenganisha na upendo wake. Paulo anasema, kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu,” Rum 8:38-39. Ndugu yangu tunayesafiri wote kwenye tafakari hii, bado tu hujakata shauri la kujisalimisha kwa Kristo? Kama bado anza sasa taratibu. Wengine inawachukua muda mrefu na wengine ni rahisi tu. Moja ya njia ya kujisalimisha kwa Kristo ni kuwa tayari kufanya atakayo na apendayo Kristo hata pale tusipotaka kufanya hivyo.

Tumsifu Yesu Kristo!


 Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu,” Rum 8:1

No hay comentarios:

Publicar un comentario