ALHAMISI WIKI YA 29 YA MWAKA-B
22/10/2015
Somo: Rum 6:19-23
Zab: 1:1-2, 3, 4, 6
Injili: Lk 12:49-53
Nakuu:
“Nasema kwa jinsi ya
kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wa miili yenu. Kwa kuwa kama mlivyovitoa
viungo vyenu vitumiwe na uchafu na uasi mpate kuasi, vivyo hivyo sasa vitoeni
viungo vyenu vitumiwe na haki mpate kutakaswa,” Rum 6:19
“Lakini sasa mkiisha
kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, mnayo
faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele,” Rum 6:22
“Kwa maana mshahara wa
dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu
Bwana wetu,” Rum 6:23
“Je! Mwadhani ya
kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano,”
Lk 12:51
“Kwa kuwa tokea sasa
katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili,
wawili kwa watatu,” Lk 12:52
“Watafarakana baba na
mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu
na mkwewe, mkwe na mkwe mtu,” Lk 12:53
TAFAKARI: “Lenga kwenye
ukamilifu ingawa kuna udhaifu pia.”
Wapendwa
wana wa Mungu, moja
ya njia ya kukua kiroho ni ule utayari wa kujisahihisha makosa. Asiyependa
kujisahihisha makosa yake na kuwa tayari kufuata njia iliyo sahihi, ni vigumu
kwa mtu huyo kubadilika na kukua kiroho. Ukweli huu ni kwa kila mwenye hofu ya
Mungu, na kwa namna ya pekee wale wenye dhamana ya uongozi. Utayari wa
kujisahihisha makosa ni moja ya sifa ya kiongozi bora na makini. Na kwa kupitia
yeye wengi huona mwanga kwa sababu yeye ni kioo cha jamii husika.
Katika shughuli zetu za kila siku si kila mara mambo
yatakwenda vema. Tunaweza kukosea hapa na pale. Basi tuwe tayari kusahihishwa
na kujisahihisha. Tujisahihishe kweli. Tunajifunza kutoka makosa yetu na ya
wenzetu. Zaidi ya hayo tusiyaache makosa yatokee kwa makusudi. Tujitahidi
kuzuia makosa na mapungufu mengine yoyote yasitokee. Tulenge kwenye ukamilifu
ingawa kuna udhaifu pia.
Masomo yetu ya leo yanalenga katika fundisho hili la
ukamilifu ingawa kuna udhaifu kama wanadamu. “Nasema kwa jinsi ya
kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wa miili yenu. Kwa kuwa kama mlivyovitoa
viungo vyenu vitumiwe na uchafu na uasi mpate kuasi, vivyo hivyo sasa vitoeni
viungo vyenu vitumiwe na haki mpate kutakaswa,” Rum 6:19. Kila mmoja wetu
naujua udhaifu wake, na anajua ni kiungo gani cha mwili wake kinachomtatiza
kuufikia huo ukamilifu. Pamoja na binadamu kuwa na viungo vingi, embu tuutazame
kiungo ULIMI. Kiungo hiki ulimi kimezungumzwa mara 85 katika Maandiko
Matakatifu. Mtume Yakobo anatuambia hivi kuhusu ulimi: “Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa
katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo
wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum,” Yak 3:6. Mbaya zaidi ulimu kwa
kiasi kikubwa ulimi huu haujazungumziwa vizuri kadiri ya Maandiko Matakatifu.
Ulimi unaweza kufarakanisha kila kitu, iwe imani, dini, siasa, umoja wetu kama
Taifa, na hata mahusiano ya karibu kwa wapendanao. Ni muhimu sana mtu kuutumia
ulimi wake vizuri hasa pale tunapotaka kutoa ujumbe wowote ule. Hivyo, “Mtu akidhani ya kuwa anayo
dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini
yake mtu huyo haifai,” Yak 1:26. Ndugu yangu, kama kweli wewe una hofu ya
Mungu, iweje basi umnenee binadamu mwenzako mabaya ilihali nawe unaelekea huko
huko unapomnenea mabaya mwenzako? Kwa nini basi unakata tawi ulilolikalia
mwenyewe?
Wapendwa
wana wa Mungu, lengo la kujisahihisha katika madhaifu yetu ni kuupata huo
utakaso ili tuweze kuufikia huo uzima wa milele tulioandaliwa. Huko ndiko
kuwekwa huru kutoka utumwa wa dhambi, na kuhesabiwa haki kadiri ya mapenzi yake
Mungu. “Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na
kufanywa watumwa wa Mungu, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni
uzima wa milele,” Rum 6:22. Je, mwenzangu hupendi
faida hiyo itokanayo na kuushinda udhaifu wako? Basi anza sasa kujichunguza ni
wapi kila mara wajikuta unadondoka katika dhambi. Anzia hapo hapo kujisahihisha
na kupata huo utakaso. Kama wewe ni Mkristo Mkatoliki baada ya kujichunguza na
kuona mkwamo wa wewe kukua kiroho, usichoke kujongea sakramenti ya upatanisho.
Kajipatanishe na Mungu, hakimu mwenye haki na upendo wa kweli.
Mpendwa mwenye hofu ya
Mungu, wakati ndiyo sasa. Tatizo kubwa la kutokujisahihisha na kujisalimisha
kwenye utakaso ni pale mtu anapofikiri bado anao muda wa kutosha kufanya hivyo.
Muda kamwe haumsubiri mtu. Unapoguswa na ujumbe huu chukua hatua mara. Hakuna
kesho kama hakuna leo. Na unaloweza kulifanya leo lisingoje kesho. Kudumu
katika hali ya dhambi kwa muda mrefu kuna madhara mengi sana katika maisha yako
ya kiroho. Moja ya dhara kubwa ni kuwa katika hali hatarishi ya umauti. “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni
uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu,” Rum 6:23. Je ndugu yangu
unayesafiri nami katika tafakari hii hupendi karama ya Mungu, yaani, uzima wa
milele tuupatao katika Kristo Yesu Bwana wetu?
Uzima huo
wa milele ndani na katika Kristo Yesu tunausikia leo kutoka katika kinywa chake
mwenyewe hasa kwa maneno haya ya kuchukua hatua tukiwa tunajitathimini maisha
yetu ya kiroho. Naye anatuambia, “Je! Mwadhani ya
kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano,”
Lk 12:51. Ni mafarakano katika maana ya vita dhidi ya ubinadamu wetu. Kumfuata
Kristo katika ukamilifu yakupasa kuushinda ubinadamu wako kwa kulenga ukamilifu
ingawa udhaifu upo. Ni kwa kupitia Kristo aliyeushinda uovu kwa wema, yaani
kuwa tayari kufa kwa ajili yangu na wewe weweza kuishinda vita hii. Msalaba ni
ishara ya huo ushindi wa wema dhidi ya uovu. Mimi na wewe, “nisione fahari juu ya
kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu
umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Je, watambua nguvu ya msalaba katika
maisha na wokovu wako?
Wapendwa kama upo tayari
kufanywa upya katika ukamilifu ndani na katika Kristo Yesu, uwe tayari kupokea
sintofahamu kwako na wale walikuwa nawe karibu kwa sababu ya ubinadamu wako na
yale waliyokuwa wakiyafurahia kutoka kwako. Ukiwa rafiki wa kweli na karibu wa
Yesu, giza la uovu litakuwa na vita kubwa na mwanga wa Kristo ndani ya maisha
yako. Hivyo Yesu anatupatia changamoto hii kwa kusema, “Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano
wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu,” Lk 12:52. Hii ni vita
Takatifu ya kiroho yenye kulenga ukamilifu wa kweli utupelekao kwenye uzima wa
milele. Yesu hakuishia hapo tu. Anatuambia vita hii huenda hata kwa ndugu zetu
wa damu. Je, upo tayari kufarakana na familia yako, Baba, Mama, na ndugu zako
katika kweli na haki juu ya Kristo Bwana na mwokozi wako?
Katika
ukweli huo wa kuelekea ukamilifu na uzima wa milele, Yesu anatuambia, “watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti
yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu,” Lk 12:53.
Unapoamua kumfuata Kristo hakuna mbadala wake ikiwa ni pamoja na kutazama
nyuma. Ni heri kuwa baridi au moto kuliko kuwa vuguvugu katika Imani. “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa
ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,”
Mt 10:22. Kwa maana nyingine, hakuna utukufu pasipo msalaba. Mtihani mkubwa
kupita yote kwa mwanadamu ni kushindwa kufanya maamuzi ya kina kuhusu hatma ya
maisha yake. Pale tunaposhikwa kigugumizi cha kuacha mazoea yetu na kufuata
njia mpya na mwelekeo mpya katika maisha, mwanadamu huishia masikini wa mwili
na roho.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni
ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?” Zab 27:1
No hay comentarios:
Publicar un comentario