martes, 6 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 27 YA MWAKA-B

JUMATANO WIKI YA 27 YA MWAKA-B
7/10/2015
Somo: Yon 4:1-11
Zab: 85:3-6, 9-10
Injili: Lk 11:1-4
Nukuu:
“kwa maana nalijua ya kuwa wewe u Mungu mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya,” Yon 4:2c

Basi, sasa, Ee Bwana, nakuomba, uniondolee uhai wangu; maana ni afadhali nife mimi kuliko kuishi,” Yon 4:3 

Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.]” Lk 11:2

Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu],” Lk 11:4

TAFAKARI: “Mungu anakupenda kama ulivyo kwani ni mwingi wa huruma, rehemu, hughairi mabaya.”

Wapendwa wana wa Mungu, bila shaka ulishajikuta una ukavu wa sala na kutokuona uwepo wa Mungu na wakati mwingine kama umesahaulika kwa sababu tu yawezekana unaishi katika hali ya hatia. Kuishi katika hatia fulani ni sawa na kujiweka mwenyewe katika gereza na kushindwa kutoka ilhali ufunguo unao.

Mtu anayeisha katika hatia, hutumia muda wa maisha yake yote kupekua lawama na kuficha aibu. Hivyo watu wanaoongozwa na hatia wanaonewa sana na kumbukumbu. Wanaruhusu mambo yaliyopita kutawala mambo yao ya usoni.Wanajiadhibu bila kujua kwa kuharibu mafanikio yao. Kaini alipotenda dhambi, hatia yake ilimtenga na Mungu, na Mungu akasema, "utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani," Mwa 4:12. Hii inawaeleza jinsi watu wengi walivyo siku hizi-wanatangatanga katika maisha bila lengo. Mfano mzuri angalia katika vyama vyetu vya kitume. Wapo walio wengi huama chama kimoja cha kitume kwenda kingine na mwisho huishia katika nyumba za sala. Nyumba za sala hapa ninamaanishisha vijikanisa vinavyojiibua na kujiinua kwa wachungaji wao kuwa manabii.

Ndugu yangu, sisi ni matokeo ya muda wetu uliopita lakini hatupaswi kuwa wafungwa wa muda huo. Kusudi la Mungu halifungwi na muda wako uliopita. Ona! Alimbadilisha muuaji Musa na kuwa kiongozi mzuri; akambadilisha Gidioni aliyekuwa mwoga akawa shujaa na hodari; anaweza kufanya mambo ya ajabu na maisha yako yaliyobaki. Tazama pia maisha ya Mt. Augustino wa Hippo kabla na baada ya kuongoka kwake.

Mungu ni mtaalam wa kutupa mawazo mapya. "Heri aliyesamehewa dhambi, na kusitiriwa makosa yake," Zab 32:1. Kwa maana nyingine twaweza kusema, "wana furaha kubwa wale waliosamehewa hatia zao. Na wana amani wale waliotubu dhambi zao na Mungu amefuta mashtaka yao."

Kwa namna hii tunamwona Nabii Yoha anajihukumu na kuchagua kufa kwa sababu ya kuhisi Mungu amemtenga na kumwacha. Hata hivyo Nabii Yona anajua kwa uhakika Mungu anayemtumikia jinsi alivyo, na kusema, “nalijua ya kuwa wewe u Mungu mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya,” Yon 4:2c. Hata pamoja na kujua ukweli huu, bado Yona haoni uwepo wa Mungu katika shida zake. Hivyo kwa kukata tamaa anaamua afe. Basi, sasa, Ee Bwana, nakuomba, uniondolee uhai wangu; maana ni afadhali nife mimi kuliko kuishi,” Yon 4:3. Uhai huo ambao Yona anaotaka kuuondoa siyo mali yake. Uhai ni mali ya Mungu na zawadi ya Mungu. Kujiua kwa kukimbia matatizo siyo njia sahihi ya kufanya. Na kukata tamaa ni kumkufuru Roho Mtakatifu. Dhambi hii haisamehewi. “Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa,” Mt 12:31

Pamoja na hatia alizokuwa nazo mtu, Mungu hubaki kuwa HURUMA, MSAMAHA, UPENDO NA AMANI yetu. Huruma hii na upendo huu wa Mungu, tunaiona katika sala ya Baba yetu ambayo leo mmoja wa wanafunzi wa Yesu anamwomba Yesu awafundishe namna ya kusali. Katika sala hii inatufundisha na kuweka wazi ni nani aliyekimbilio letu la pekee, na mapaswa yetu tungali hapa duniani. Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.]” Lk 11:2. Jambo lingine la msingi ni huruma ya Mungu kwa msamaha wa makosa yetu inayotokana na kiwango kile kile cha sisi kuwasamehe wale waliotukosea. Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu],” Lk 11:4. Wapendwa wana wa Mungu, kama kipimo cha kupenda ni kupenda bila kipimo kama asemavyo Mt. Agustino, basi ni hivyo hivyo masharti ya kusamehe ni kusamehe bila masharti.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUJALIE NEEMA YA KUVUMILIA MATESO. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario