JUMAPILI
YA 29 YA MWAKA-B
18/10/2015
Somo
I: Isa 53:10-11
Zab:
33:4-5, 18-19, 20, 22
Somo
II: Ebr 4:14-16
Injili:
Mk 10:35-45
Nukuu:
“Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha, Na mapenzi
ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake,” Isa 53:10
“Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi
kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao,” Isa 53:11b
“Basi, iwapo tunaye
kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana
maungamo yetu,” Ebr 4:14
“Kwa kuwa hamna kuhani
mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye
alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi,” Ebr 4:15
“Wakamwambia, Utujalie
sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika
utukufu wako,” Mk 10:37
“Yesu akawaambia,
Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa
ubatizo nibatizwao mimi?” Lk 10:38
“Kikombe
ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa
kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa
tayari,” Mk 10:39b-40
“bali mtu
anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu,
atakuwa mtumwa wa wote,” Mk 10 43b-44
“Kwa maana Mwana wa
Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya
wengi,” Mk 10:45
TAFAKARI:
“Hakuna Utukufu pasipo Msalaba. Basi, tumika na siyo kutumikiwa ndani na katika
Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 29 ya mwaka “B.” Masomo yetu ya leo
yanatualika tutafakari juu ya Utukufu utupatao baada ya Msalaba. Na ili
tuufikie ufalme wa Mungu yatupasa kutumika na siyo kutumikiwa ndani na katika
Kristo. Utukufu ni tokeo la kukubali mateso katika mwono wa ukamilifu kwa kile
tukitamanicho kuwa, au tusichokijua lakini chenye mwono wa wokovu kwetu na kwa
wenzetu. Somo letu la kwanza na la pili yamezungumzia kwa kina juu ya dhana hii
ya msalaba au mateso, na uhusianao wake na Utukufu. Nabii Isa anatuonyesha ni
kwa namna gani mtu aweza kuteseka kwa ajili ya wengine kwa maridhio ya Mungu
Mwenyewe.
Mtu huyo aliyetabiriwa
na Nabii Isaya ndiye Kristo, neno aliyefanyika mwili, na hasa katika fumbo zima
la Pasaka. Nabii Isaya anatoa sifa na mwelekeo wa huyu aliye ufia ulimwengu kwa
sababu ya dhambi za watu ingawa yeye hakuwa na kosa lolote. “Lakini Bwana aliridhika kumchubua;
Amemhuzunisha, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake,” Isa 53:10.
Tunapoyatazama mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo ni dhahiri kabisa hayakwenda
tofauti na yale aliyoyatabiri Nabii Isaya. Tumehesabiwa haki kwa mateso ya
Kristo na kurudishiwa hadhi yetu kama wanadamu na warithi wa ufalme wa Mbinguni
ambapo uliondolewa kwa anguko la Wazazi wetu wa kwanza, Adam na Eva. Hivyo,
“Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki;
Naye atayachukua maovu yao,” Isa 53:11b. Ni ukweli usiotia shaka kwamba mimi na
wewe tumekombolewa kwa gharama kubwa sana na yenye thamani isiyo elezeka.
Ukweli huu anauthibitisha Mtume Petro kwa kusema, “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu
viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa
mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye
na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Kulipa shukrani hii kwa
Kristo aliyetufia ni kuwa tayari kutumika kwa ajili ya wengine bila kujibakiza
kama alivyofanya.
Kuhani
wetu huyu Mkuu Yesu Kristo, ndiye Hakimu wetu wa haki. Siku yaja na imekaribia
kwa kila mwenye punzi sasa ambapo tutatakiwa kujibu ni kwa namna gani
tumewapenda wengine na kujitoa kwao kama alivyofanya yeye, Kristo. Kulijibu
swali hili vizuri yatupasa kujua tupo leo katika ulimwengu huu kwa lengo gani
la muhimu. Ikiwa kwa miezi tisa tumboni ilikuwa maandalizi ya kuishi katika
ulimwengu huu, basi tuelewa tupo hapa duniani kwa maandalizi ya maisha ya
umilele. Hivyo kifo chake ni siku ya kuzaliwa katika maisha ya umilele endapo
ulijiandaa vyema. Kwa maana hiyo, ili tukutane na Kuhani wetu Mkuu huko
mbinguni yatupasa kuyashika vyema na kwa uaminifu maagano yetu tungali hapa
duniani. “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu,
Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu,” Ebr 4:14. Ni kweli pia katika
kuyashika maagano haya ya maisha, iwe maisha ya ndoa, utawa, au ukleri hatuwe
kukwepa misalaba. Tutakutana na Kristo aliyeushinda msalaba katika maagano yetu
haya iwapo tutayaishi maagano hayo kwa uaminifu. “Kwa kuwa hamna kuhani
mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye
alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi,” Ebr 4:15.
Uaminifu katika agano lako na Mungu ndiyo salama yako katika maisha ya umilele.
Wapendwa
wana wa Mungu, baada ya kuona uhusiano wa msalaba na utukufu tuupatao baada ya
kuyaishi kwa uaminifu maagano yetu katika maisha, Yesu katika injili ya leo,
anatupa changamoto ya msingi. Ni kweli hakuna mwanadamu anayependa shida kwa
urahisi. Kila mmoja wetu angependa kuishi ndoto yake hata kama haitekelezeki.
Binadamu yupo hivyo kwa sababu ndani yake Mungu amemwekea hali ya kutamani.
Tatizo siyo kutamani, ila tatizo lipo tunapoyaelekezea matamanio yetu. Yakobo
na Yohana wana wa Zebedayo wanaonyesha matamanio yao ya kuketi kuume na kushoto
mwa Yesu katika utukufu wake. Ndugu hawa wawili wanamdai Yesu awafanyie lolote
lile awezalo ili waikamilishe tamaa yao.
Tukizama
zaidi katika maneno ya ndugu hawa wawili katika mtazamo wa jamii yetu ya leo
Tanzania, tungeweza kusema kwamba, ndugu hawa wapo tayari hata kutoa rushwa ili
tu katika ufalme wa Kristo wawe pembeni yake. Katika jambo hili, Yesu Kristo
hayupo tayari kubomoa nguvu ya kimaadili aliyokuwa nayo hata kama angeona
inafaa kufanya hivyo. Kristo Yesu ni KWELI, NJIA, UZIMA, HAKI, AMANI, UPENDO,
na zaidi, hayo yote yamebebwa katika UNYENYEKEVU wake. Yesu anawauliza ndugu
hawa swali la msingi baada ya kuona hawajui wakiombacho. “Mwaweza kunywea
kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?” Lk 10:38. Yesu anawakumbusha ndugu hawa na sisi
pia kwamba “ukiona vinaelea ujue vimeundwa.” Hivyo, kufikia hatua fulani
kimaisha, iwe kimwili au kiroho inamapaswa yake. Ndugu hawa licha ya kutokujua
kwao kwa kile wakiombacho, hawakuacha kushupalia matamanio yao. Yesu kwa mara
nyingine haterereki katika misingi ya kweli na haki katika maadili. Naye
anawajibu, “Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao
mimi mtabatizwa; lakini habari ya
kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa
waliowekewa tayari,” Mk 10:39b-40. Hapa Yesu anagusa hatua ya pili katika
makuzi ya kiroho.
Wapendwa
katika Kristo, kama yote tulionayo na kile tulicho si mali yetu ni mali ya
Mungu, basi ni kwa namna hiyo hiyo kwamba ni Mungu mwenyewe mwenye kutuhesabia
haki. Tupo kama tulivyo kwa neema ya
Mungu. Mtume Paulo anatuambia, “Lakini kwa neema ya
Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali
nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya
Mungu pamoja nami,” 1Kor 15:10. Kumbe ni vyema kwanza kutimiza wajibu wetu
katika kuwajibika na kutumika kwa ajili ya wengine bila kujibakiza ndipo
tutakapo nyanyuliwa kadiri ya mapenzi ya Mungu na siyo yetu. Hii ndiyo hatua ya
pili ya kukua kiroho. Hatupaswi kujihesabia haki kwa yale tulionayo au yale
tuyafanyayo, bali tuwe tayari muda wote kutumika kwa ajili ya wengine bila
kujibakiza. Huu ndio unyenyekevu katika kujitoa kama asemavyo Yesu, kwamba,
“bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu,
atakuwa mtumwa wa wote,” Mk 10 43b-44. Hili ndilo tunalopaswa kulifanya kama
wafuasi wake Yesu, na watu wenye hofu ya Mungu. Tunaishi na kuyafanya
aliyofanya Kristo tukitambua ukweli huu kutoka kwake mwenyewe. “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika,
na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mk 10:45.
Wapendwa
katika Kristo, nimalize kwa mchapo huu. Alikuwepo mama mmoja aliyekuwa chongo
na mwanae Zawadi alimchukia kwa sababu ya kuwa chongo. Zawadi alijisikia aibu
kutembea na mama yake mwenye jicho moja na hakupenda watu wajue kuwa yule ni
mama yake.
Hata
alipokuwa shuleni Zawadi hakupenda mama yake amtembelee, na ilitokea mama yake
akamtembelea basi watoto wenzie watamcheka siku nzima na kumtania. Hii
ilimfanya Zawadi kujisikia vibaya sana na wakati mwingine kujuta kuwa na mama
wa aina hiyo.
Lakini
mama alimpenda mwanae na hakuonyesha kukasirika hata pale mwane alipomnyanyapaa
waziwazi.
Baadaye
Zawadi akakuwa akamaliza masomo yake na kupata kazi nzuri. Akafurahi kuwa sasa
amepata kazi atakuwa mbali na mama yake “chongo” anayemtia aibu.
Zawasi
akachagua kufanya kazi mji wa mbali na alipo mama yake. Akafanikiwa kazini kwa
kupandishwa cheo na akawa mtu mashuhuri mwenye mali na mwenye heshima kubwa
katika jamii yake.
Siku moja
asubuhi Zawadi alisikia wanawe wakilia wakipokua nje wakicheza. Alipowaukiza
wakasema kuna mtu anawatisha. Akatoka nje kujua nani anayewatisha wanawe.
Kufika akamkuta mwanamke mmoja mzee mwenye jicho moja (chongo). Kumbe wale
watoto walitishwa na chongo la yule bibi.
Zawadi
alipomtizama vizuri yule mwanamke akamgundua ni mama yake mzazi. Alikuwa
amechoka na amezeeka sana. Amedhoofika mwili na anaonekana mgonjwa
Zawadi
kwa hasira akamuuliza, “Mama umejuja kufanya nini hapa? Kama una shida
ungenipigia simu sio kuja. Kwanza nan kakuonyesha ninapoishi? Na nani kamruhusu
mlinzi kukufungulia mlango? Ona sasa umewatisha wanangu kwa chongo lako.”
Mama yake
akamjibu, “samahani mwanangu, sikujua naomba unisamehe.” Kisha Zawadi
akamchukua mama yake akamtoa nje na kumpeleka kituo cha basi ili arudi
kijijini.
Baada ya
siku chache kupita, yule Zawadi akapata taarifa kuwa mama yake ni mgonjwa sana
na anahitaji kumuona. Akaondoka kwa siri kwenda kijijini ili akasikie mama yake
anataka kumwambia nini.
Zawadu
alipofika akakuta watu wengi wamekusanyika nyumbani kwao. Alipouliza akaambiwa
mama yake alifariki baada ya kuugua sana bila msaada wowote.
Alipoingia
ndani Zawadi akakuta barua aliyoandika mama yake. Barua ilisomeka hivi:
“Kwako
mwanangu mpendwa wa pekee Zawadi. Naandika barua hii nikiwa kwenye maumivu
makali sana na sijui kama nitapona. Nimeugua nikakosa matibabu kwa kutokuwa na
fedha. Sikuwa na mtu mwingine wa kumueleza shida yangu zaidi yako wewe mwanangu
wa pekee. Lakini nilipojitahidi kuja kwako angalau unisaidie matibabu
ulinifukuza na kudai nawatisha wanao kwa chongo langu! Uliniumiza sana mwanangu
sitisahau maishani mwangu ila nimekusamehe.
Baba yako
alifariki ukiwa mdogo sana. Nami sikubahatika kupata mtoto mwingine. Nilikulea
kwa nguvu zangu zote na umasikini niliokuwa nao nilikuwa nikitegemea baadaye
utanisaidia lakini umenitelekeza na kunitupa kwa sababu tu mimi mama yako ni
chongo! Hivyo unaona aibu kuwa nami.
Nisamehe
kwa kuwatisha wanao kwa chongo langu, nisamehe kwa kuja kwako bila taarifa,
nisamehe kwa kukufanya uchekwe na wenzio kwa kuwa mimi mama yako ni chongo.
Lakini
naomba nikupe siri ambayo hukua unaijua ewe mwanangu. Wewe ndiye uliyezaliwa
ukiwa chongo. Ulikuwa na jicho moja tu. Nikaumia sana kuona mwanangu ana jicho
moja, atawezaje kuishi na kukabiliana na changamoto za maisha. Nikaomba
madaktari wanitoe jicho langu moja wakupe wewe. Niliona ni heri mimi niwe
chongo kwa kuwa nimeshaona mengi sana duniani.
Zawadi,
ulipowekewa jicho langu nilifurahi kukuona una macho mawili nikajua utaweza
kuzikabili vema changamoto za dunia hii. Na hakika jicho langu limekusaidia
kwani wewe ni mtu mashuhuri na tajiri sana kwa sasa.
Lakini
kwa jinsi ninavyoumwa najua nitakufa. Ila nafurahi kwamba nakufa nikiwa
nimetimiza haya ya moyo wangu. Kwa kutumia jicho langu umeweza kuwa msomi mzuri
na tajiri unayeheshimika na jamii yote. Wasalimie wajukuu zangu na waambie wawe
na amani hawataniona tena nikienda kuwatisha na chongo langu. Tafadhali litunze
jicho langu.
Akupendaye,
Mama.”
Alipomaliza
kuisoma barua hii akalia sana. Akatamani mama yake afufuke amuombe msamaha na
amlipe kwa wema wake aliomtendea. Lakini haikuwezekana tena. Alikuwa kesha
chelewa!
Wapendwa
katika Kristo, mafanikio yako yanaweza kuwa ni matokeo ya Wazazi wako, mke
wako, mume wako, dada yakeo au mchumba wako. Je, unatambua nafasi yao kati ya
hao katika mafanikio yako au unapuuza tu?
Kwa namna
ya pekee yawezekana wapo walijitoa sadaka sana ili uweze kuwa hapo ulipo.
Jiulize kwa mfano wazazi wako wamefanya mangapi kukufikisha hapo ulipo? Leo kwa
mfano akina Mama zetu ni wafia dini katika Kanisa la leo na jamii ya leo.
Wanataabika sana juu ya familia na watoto wao.
Wapo miongoni mwetu jicho
lao ni wale ambao vibarua alivyokuwa anafanya ili wewe usome. Pengine jicho
lake ni namna alivyokuwa akijinyima kwa kuvaa nguo moja mwaka mzima ili upate
ada ya shule na mahitaji mengine. Wengine tumesoma na kufikia hapa tulipo kwa
mama zetu kufanya biashara za kuuza ndizi na pombe kila kikicha. Je, umewahi
kumshukuru mtu huyo kwa kwa kutoa jicho lake kwa ajili yako?
Kwa kifo na ufufuke wake
Bwana wetu Yesu Kristo tumepewa jicho la kuuona na kuurithi ufalme wa Mbinguni.
Ndugu yangu, shikamana naye katika kujitoa bia kujibakiza kama kielelezo cha
kutumika kwako ndani na katika Kristo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ee Bwana unifanye chombo
cha Amani yako,” Mt. Franscisco wa Assis
No hay comentarios:
Publicar un comentario