viernes, 23 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 29 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 29 YA MWAKA-B
24/10/2015
Somo: Rum 8:1-11
Zab: 24:1b-2, 3-4ab, 5-6
Injili: Lk 13:1-9
Nukuu:
Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti,” Rum 8:2  

Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho,” Rum 8:5 

Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani,” Rum 8:6 

Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu,” Rum 8:8 

Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake,” Rum 8:9

Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu,” Rum 8:11

Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo?” Lk 13:2 

Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo,” Lk 13:3 

Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate,” Lk 13:8-9

TAFAKARI:Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.

Wapendwa wana wa Mungu, tunapotafakari masomo ya leo ni vema kufahamu jambo hili la msingi kuhusiana na uumbaji wetu na sababu ya kuishi kwetu. Napenda kuyachukua maneno haya ya Mtume Paulo kwamba, “kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina,” Rum 11:36. Jambo la msingi hapa ni ukweli kwamba Mungu hakuhitaji kukuumba wewe, bali alichagua kukuumba kama ulivyo kwa furaha na utukufu wake. Kwa maana hiyo, maisha yetu hapa duniani yapaswa kuufunua, kuuonyesha Utukufu wa Mungu, na furaha yake.

Ndugu zangu katika Kristo, mwanadamu angali akiwa hapa duniani utoa Utukufu wa Mungu na furaha yake kwa kufanya mambo yafuatayo: Kwa kumwabudu Mungu, yaani maisha yake yote, kwa kuwapenda watu wengine bila kubaguana, kwa kuishi na kuwa kama Kristo, kwa kutumia vipaji kwake vyote kwa ajili ya wengine, yaani kufaidiana, na kwa kueneza habari njema za Mungu kila pande za dunia. Hata hivyo licha ya ukweli huu, mwanadamu huyu anaweza kuufunua utukufu wa Mungu na furaha yake kwa kutenda matendo ya roho, Gal 5:22-23, na siyo yale ya mwili yasiyo na uzima ndani yake, Gal 5:19-21. Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani,” Rum 8:6. Mtu hawezi kumpenda Mungu kama anafuata matendo ya mwili wake tu. Ni kweli kwamba kiini cha dhambi ni pale mtu anapojipenda yeye zaidi kuliko Mungu. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu,” Rum 8:8. Hivyo basi kama tunataka kuishi na kuwa kama Kristo lazima tufuata sheria ya roho, yaani, matendo ya roho, ambayo ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria, Gal 5:22-23. Uzima huu tuupatao kwa matendo ya roho upo ndani ya Kristo pale tunapotaka kuishi na kufanana naye.  Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti,” Rum 8:2. Hivyo kwa kuishi na kufanana kama Kristo tunaufunua Utukufu wa Mungu na furaha yake ya kutuumba.

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, kwa upande mwingine, sheria ya dhambi ni matendo yale yasiyo na uzima ndani yake, na kwayo kamwe hatuwezi kuurithi ufalme wa Mungu. Matendo haya ni haya;  uasherati, uchafu, ufisadi,  ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo.  Mtume Paulo anasisitiza kwamba, “katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21. Je, hutaki kuurithi ufalme wa Mungu na maisha ya umilele?

Kuishi na kutenda kwetu ili kuwe kwa sifa na utukufu wake Mungu kwa tulazimu kufikiria mambo ya roho.  Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho,” Rum 8:5. Ndugu yangu, utawezaje basi kuishi na kufanana na Kristo kama muda wote wa ufuata mwili na kufikiri mambo ya mwili? Hii ni changamoto kwa kila mmoja wetu. Ni kweli kwamba hatuwezi kuyawaza ya roho kama hatuna mwili. Jambo la msingi na la kufahamu hapa ni kwamba ‘vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele,’ Rum 11:36. Hivyo hakuna kilicho chako katika maana ya umiliki halali zaidi ya dhambi zako. Sasa nifanye nini katika hali hii?

Wapendwa katika Kristo, tunahitaji roho wa Kristo ndani yetu ili tuyafuate matendo ya roho na mwisho tuwe mali ya Kristo. Roho huyu ni zawadi kwetu kutoka kwa Mungu, na hufanya kazi ndani yetu kadiri apendavyo yeye kututumia kadiri ya mpango mzima wa Mungu. Hivyo, “ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu,” Rum 8:11. Hapa ndipo tunapoona Upendo na Huruma ya Mungu kwetu. Mungu hapendi hata mmoja wetu apotee kwa sababu ya dhambi zake. Mimi na wewe tunapewa kila siku fursa ya kutubu na kumrudia Mungu. Katika mantiki hii yanipasa kuzitazama dhambi zangu, kuzitubu, na mwisho kuwa huru kutoka utumwa huu wa dhambi. Ni kwa namna hiyo hiyo sina haki wala sababu ya msingi kuwanyooshea vidole wengine ilhali mimi mwenyewe nahitaji Upendo na huruma ya Mungu.

Injili ya leo inatuasa kutumia vyema fursa hii ya upendo na huruma ya Mungu kwa kuishi matendo ya roho na kuachana na matendo ya mwili. Tusipoteze Muda mwingi kuzitazama dhambi za watu wengine na hata maafa ya watu wengine tukafikiri kwamba wao ni waovu kupita sisi. Yesu analiona hilo kwa wayahudi wanapomsimulia tukio lile la Pilato kuchanganya damu za Wagalilaya na dhabibu zao. Yesu akawaambia, “Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo?” Lk 13:2. Je, nasi tunatofauti na hao Wayahudi kwa fikra na matendo yetu? Ndgu yangu, mimi na wewe tunaambiwa hivyo hivyo na Yesu. Kati yetu wapo watu hodari sana wa kuyasema maovu ya watu wengine na wakati mwingine wayasemayo na kuyashuhudia hayana ukweli wowote juu ya kile wakisemacho au kukishuhudia. Uzushi katika jamii yetu leo umekuwa ndiyo wimbo tuupendao na uujazao vinywa vyetu. Je, tumepata nafasi ya kuyachunguza maisha yetu kwa undani? Kama hatufanyi jambo hili hatuwezi kuepuka kuwa wanafiki. Yesu anatukaripia kwa nguvu zote kuhusu unafiki wa mtindo huu na kusema, “Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako,” Mt 7:5. Hakuna njia ya kuepukana na unafiki huu kama hatutafanya tafiti moyo na kufanya toba ya kweli. Nawaambia,  lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo,” Lk 13:3. Kilichowapata wengine kwa mtindo ule ule kitatupata nasi tusipotubu na kumrudia Mungu.

Mungu wetu ambaye ni Upendo na Huruma humjalia kila mmoja wetu nafasi na muda wa kutosha kujirekebisha. Mungu huyu asingekuwa hivyo, tusingeendelea kuishi hata kwa sekunde moja tungali na madhambi zetu. Ukimya wa Mungu juu ya dhambi zako siyo kwamba haoni kinachoendelea ndani yako, bali anakupa  muda wa kutosha kufanya tafiti moyo na toba ya kweli. Mungu wetu ni huruma kama mtunza bustani alivyomjibu mmiliki wa mtini kwa kutokuzaa matunda yake kwa miaka mitatu mfululizo. “Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate,” Lk 13:8-9. Mungu wetu ni Mvumilivu sana kwa sababu anatupenda sana. Ni kwa sababu ya Upendo wake Mungu alichagua kutuumba kama tulivyo kwa sifa na utukufu wake. Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii yatupasa kutumia vyema nafsi na muda tulionao kuyatenda matendo ya roho.

Tumsifu Yesu Kristo!


“Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?” Zab 130:3

No hay comentarios:

Publicar un comentario