IJUMAA WIKI YA 27 YA MWAKA-B
9/10/2015
Somo:
Yoe 1:13-15, 2:1-2
Zab:
9A:2-3, 6, 16, 8-9
Injili:
Lk 11:15-26
Nukuu:
“Jikazeni mkaomboleze,
enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha
katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka
ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu,” Yoe 1:13
“Naye akajua mawazo
yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa;
na nyumba juu ya nyumba huanguka,” Lk 11:17
“Lakini, ikiwa mimi
natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia,” Lk
11:20
“Mtu ambaye si pamoja
nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya,” Lk 11:23
TAFAKARI: “Tuachane na yaliyo yetu na
kibinadamu zaidi tushikamane na kweli ambaye ndiye Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu, Mtume Paulo
anatuasa jambo la msingi sana, na hasa maana ya
maisha ya ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo kwetu sisi wafuasi wake.
Mtume Paulo anasema, “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo,
yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1.
Kuyatafuta yaliyo juu kwa maana nyingine ndiko kushikamana na kweli ambayo
ndiyo Kristo. Kuyatafuta yale ya juu Kristo aliko,
ni kuishi katika neema za ufufuo, yaani maisha ya utakaso na yasiyo na hatia.
Ni kupiga vita kwa kweli kuushinda ubinadamu wetu kwa kufanana na kuwa zaidi
kama Kristo.
Kila
mbatizwa ni Kristo mwingine “Alter Christus.” Kwa sababu hii na
kwa maana hiyo, yatupasa kila siku kuachana na yaliyo yetu na ya kibinadamu ili
kushikamane na kweli ambaye ndiye Kristo. Tunaporejea katika somo la kwanza kutoka
katika kitabu cha Nabii Yoeli, tunakutana na tatizo la wana wa Israeli la
kutokufanana na kufanya yale atakayo Mungu. Kutokana na kuasi kwao na kufuata
njia zao, na hasa Makuhani, Mungu hayupo tayari kupokea sadaka zao. Nabii Yoeli
anawaasa Makuhani hao kufanya toba ya kweli na kujenga uhusiano tena na Mungu. “Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi
wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa
Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika
nyumba ya Mungu,” Yoe 1:13. Kwa mazingira haya ya kuasi hasa kwa Viongozi hawa
wa dini, inaonyesha dhahiri kwamba hali ilikuwa mbaya sana kwa mtu mmoja mmoja.
Tuelewe kwamba kile kilichokuwa kinatolewa sadaka kilitoka mikononi mwa kila Myahudi
katika upekee wake. Ni dhahiri kama sadaka hiyo inakataliwa ni kwa namna hiyo
hiyo Mungu hakupendezwa na maisha ya kila mmoja katika upekee wake.
Katika somo letu la Injili ikiwa ni mwendelezo ule ule wa
kumkomboa mwanadamu, Yesu anapata shutuma za kutoa pepo kwa kutumia nguvu za
Pepo Mkuu- Beelzebuli. Je,
mawazo hayo ya kishirikina yanatoka wapi kwa wana hawa wa Israeli? Kama kweli
walikuwa wanamwabudu Mungu mmoja, iweje wawe na mawazo kama hayo? Wapendwa wana
wa Mungu, tusipoachana na yaliyo yetu na ubinadamu wetu hatutaweza kuondokana
na hisia za kishirikina. Ni wazi kwamba licha ya kuwa walimwamini Mungu moja,
watu hawa hawakuachana na yaliyo yao na ubinadamu wao. Hisia hizo mbaya juu ya
uwezo wa Yesu wa kutoa pepo kwa nguvu walisiyoijua, zinakuja kwa sababu
miongoni mwao walikuwa na mazoea ya kufanya hivyo. Mara nyingi mtu humwekea hisia mbaya mtu mwingine kwa
kile ambacho yeye huwa anakifikiri na kukitenda.
Kutokana na tuhuma hizo za Wayahudi juu ya uwezo wake Yesu
wa kutoa pepo, Yesu akiyajua mawazo yao, anawafikirisha kidogo na kusema, “Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe
hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka,” Lk 11:17. Hoja hapa ni
kwamba, kama Yeye, yaani Kristo, anayafanya hayo yote na watu wanapona kwa
kuutoa utawala wa pepo, kuna sababu gani ya kufanya hivyo kwa maana ya kwenda
kinyume cha yule aliyempa nguvu hizo yaani Beelzebuli? Kwa kufanya hivyo kama
hoja yao inamshiko ni kujichanganya kwa utawala huo wenyewe. Ila Yesu
anawaambia kwama hayo yote anayafanya kwa uwezo wa Mungu mwenyewe. Na kwa
mantiki hiyo Ufalme wa Mungu huu kati yao tayari. Hawana sababu ya kuwa na
hofu. “Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha
Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia,” Lk 11:20. Ni mara ngapi
tunapata nguvu na uponyaji kwa njia ya sala na maomba na mara tupatapo tena
shida kama hiyo tunakosa imani na kwenda kwa waganga wa kienyeji? Kwa nini basi
unatapatapa katika Imani?
Wapendwa wana wa Mungu, kujitenga kwetu na Mungu kwa
kufuata mambo yetu na ubinadamu wetu ndiko kunakotunyima neema na baraka zake.
Tunajifungia milango wenyewe na tunapokosa neema na baraka hizo tuna mtafuta
mchawi aliyeturoga. Ni sawa na mlevi aliyepoteza ufunguo kwenye Kilabu cha
pombe akawa usiku kucha anatafuta ufungua barazani mwa jirani yake eti kwa
sababu tu pale kuna mwanga. Je, ataupata ufunguo huo? Ndiyo maana Yesu leo
anatuambia maneno haya mazito, “Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu
asiyekusanya pamoja nami hutawanya,” Lk 11:23. Ndugu yangu, hakuna namna
nyingine tuwezayo kupata neema na baraka kama hatutajisalimisha moja kwa moja
kwa Kristo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo
kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo,” Efe 2:13
No hay comentarios:
Publicar un comentario