martes, 27 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 30 MWAKA-B

JUMATANO WIKI YA 30 YA MWAKA-B
Sikukuu ya Simoni na Yuda, Mitume
28/10/2015
Somo: Efe 2:19-22
Zab: 19:2-3, 4-5
Injili: Lk 6:12-16
Nukuu:
Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni,” Efe 2:20 

Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana,” Efe 2:21

Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho,” Efe 2:22

akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote,  na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti,” Lk 6:13b-16 

TAFAKARI: “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, Kristo ni jiwe la pembeni.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Mitume Simoni na Yuda. Mitume kwa ujumla wao, yaani wale kumi na mbili, kwa maisha yao na ushuhuda wao wa Imani ndiyo msingi Imara wa Kanisa letu kama tunavyoliona hii leo. Akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote,  na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti,” Lk 6:13b-16. Sadaka yao kwa maisha yao ya Imani juu ya Kristo Yesu, Kanisa linaendelea kutimiza wajibu wake kama sakramenti ya wokovu wetu. Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la pembeni.

Ukristo wetu na Imani yetu imejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, na Kristo Yesu akiwa jiwe kuu la pembeni. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni,” Efe 2:20. Ni fahari ya kila aliyebatizwa kuishi ahadi zake za ubatizo na kuendeleza msingi huu imara wa Imani. Hivyo kila mmoja wetu kwa njia ya Kristo na kwa sadaka ya maisha yake na wito wake, ameunganishwa hekalu la Mungu. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana,” Efe 2:21. Mitume tunaowasheherekea leo ni mfano wa kuingwa kwetu. Mitume hawa walikuwa mashahidi na manabii katika kipindi chao. Maisha hayakuwa rahisi tunapolitazama Kanisa la Mwanzo. Wengi wao walikufa kwa kuuwawa kikatili, ila hakuna aliyemsaliti Kristo zaidi ya Yuda Eskariote. Leo miongoni mwetu akina Yuda wapo wengi sana. Ni ni changamoto ya Kanisa na maisha yetu ya kijamii.

Wapendwa wana wa Mungu, leo Kanisa linachangamoto nyingi sana. Ili kuzikabili changamoto hizi, yampasa kila mbatizwa kuishi ahadi zake za ubatizo. Pili, kila mmoja wetu kadiri ya wito wake ajitahidi kila siku kufanana na Kristo ambaye ndiye jiwe kuu la pembeni ambapo maisha yetu na sadaka yake upewa maana. Huu ni ushuhuda tosha wa ukimya hata pale ambapo Kristo hakubaliki kutokana na mitazamo tofauti ya Kiimani. Matendo yetu mema humwakilisha vizuri Kristo popote kuliko kile tukiaminicho kwa nadharia tu. Mtume Yakobo anatupatia changamoto hii kwa kusema, Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu,” Yak 2:18.

Wapendwa wana wa Mungu, tuwe waaminifu kwa wito wetu kila mmoja kadiri ya namna yake,  na upendo uliobeba matendo yetu mema kwa watu wote.

Tumsifu Yesu Kristo!


Watakatifu Simoni, na Yuda Mitume, Mtuombee.

No hay comentarios:

Publicar un comentario