JUMAMOSI WIKI YA 27 YA MWAKA-B
10/9/2015
Somo: Yoe 3:12-21
Zab: 96:1-2, 5-6, 11-12
Injili: Lk 11:27-28
Nukuu:
“lakini Bwana atakuwa kimbilio la watu wake, na ngome ya wana
wa Israeli,” Yoe 3:16b
“Misri itakuwa ukiwa, na Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu
ya dhuluma waliowatenda wana wa Yuda; kwa sababu wamemwaga damu isiyo na hatia
katika nchi yao,” Yoe 3:19
“Nami nitaitakasa damu yao ambayo sijaitakasa; kwa maana Bwana
ndiye akaaye Sayuni,” Yoe 3:21
Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya,” Lk 11:27b
“Lakini yeye alisema, Afadhali, heri
walisikiao neno la Mungu na kulishika,” Lk 11:28
TAFAKARI: “Heri walisikiao
neno la Mungu na kulishika.”
Wapendwa
wana wa Mungu, ni kweli kwamba kila mmoja wetu ana historia yake, na wakati
mwingine historia hiyo ni mbaya na isiyopendeza kwa jamii inayomzunguka na hata
mbele za Mungu. Lakini Mungu wetu ambaye ni mwingi wa rehema, huruma, upendo na
msamaha yupo tayari kuanza upya na kila mmoja wetu na kuandika historia mpya
naye. Jambo hili linawezekana tu pale unapojitambua ulikopotoka na kuwa tayari
kufanya toba ya kweli. Huyu ndiye Mungu anayemzungumzia Nabii Yoeli kwamba
ndiye kimbilio la watu wake waliotayari kubadilika. Mungu huyu ndiye ngome
isiyotikisika mara tunapojisalimisha kwake. Mungu huyu ni tofauti na miungu
mingine, mfano, pesa, umaarufu, na nguvu na utawala wa kimabavu. “Lakini Bwana atakuwa kimbilio la watu wake, na ngome
ya wana wa Israeli,” Yoe 3:16b.
Mungu wetu huyu aliyetayari kuanza nasi upya na kuandika
historia mpya, anatudai kwa upendo mkubwa kulisikia neno lake na kulishika.
Kulishika neno la Mungu ni kulitafakari na kulifanya sehemu ya maisha yako.
Maandiko Matakatifu yanaonyesha dhana hii ya maisha ya mtu kufanywa mapya baada
ya kulisikia neno la Mungu na kulishika. Mungu wetu huyu aliye na subiri kwa
kila mmoja wetu, utupatia muda wa kutosha kabisa. Tatizo letu kubwa ni pale
tunaposhindwa kutumia fursa hiyo.
Wapendwa, namba 40 katika Maandiko Matakatifu husadifu subira
ya Mungu ya kutupa muda wa kutosha kujeuka, kumrudia, na kuanza historia mpya
ndani yetu. Mfano; Maisha ya Nuhu yalibadilishwa kwa siku 40 za mvua, Musa
alibadilishwa kwa siku 40 katika mlima Sinai, Wapelelezi walibadilishwa kwa
siku 40 katika Nchi ya Ahadi, Eliya alibadilishwa pale Mungu alipompa siku 40
za nguvu kutokana na mlo mmoja, Mji mzima wa Ninawi ulibadilika Mungu alipowapa
watu siku 40 za kugeuka, Yesu alitiwa nguvu kwa siku 40 jangwani, na wanafunzi
walibadilishwa kwa siku 40 za kuwa na Yesu baada ya ufufuo. Je, wayapima maisha
yako na mahangaiko yako kwa namna yoyote ile, iwe ugonjwa au kutokupata kazi
kwa muda mrefu kama ni moja ya nafasi Mungu aliyokupa kusikia na kulishika neno
lake ili akubadilishe?
Wapendwa wana wa Mungu, tunapolitazama Taifa la Israeli licha
ya kukengeuka kwao mara kwa mara na kupata adhabu za kutisha, Mungu hakuacha
kuwa tumaini lao pale walipomrudia kwa toba na unyenyekevu. Mungu huyu aliyehai
katika umilele wote, hakuacha kamwe kuwapa matumaini mapya. Naye anasema, “Misri itakuwa ukiwa, na Edomu itakuwa jangwa
tupu, kwa sababu ya dhuluma waliowatenda wana wa Yuda; kwa sababu wamemwaga
damu isiyo na hatia katika nchi yao,” Yoe 3:19. Je, leo tunapolitazama Taifa
letu la Tanzania tupo salama? Miaka 54 si haba kulisikia neno la Mungu na
kulishika. Je, uhuru wetu na maisha tunayoishi leo kama Taifa huru ndiyo haki
yetu na upendo wa Mungu Baba kwetu? Tutaishi hivi kwa kulalamika hadi lini?
Wapendwa wana wa Mungu, njia sahihi na yakufanya kwa sana ili
kulinusuru Taifa letu mikononi mwa kundi dogo linalojineemesha na kuishi kwa
dhuluma kwa jasho la Watanzania walio wengi ni
kumrudia Mungu kwa sala, Maombi, na toba atuongoze vyema katika kumpata
Viongozi wenye hofu ya Mungu na watakao tenda kadiri ya hofu hiyo. Pamoja na
mateso na mahangaiko yetu kupitia historia nzima ya Taifa letu, Mungu anasema, “Nami nitaitakasa damu yao ambayo sijaitakasa;
kwa maana Bwana ndiye akaaye Sayuni,” Yoe 3:21. Mungu wetu aliye hai yupo
tayari kuanza upya na kila mmoja wetu, pia na kundi kubwa kama Taifa kwa sababu,
“kwa kuwa walipo wawili watatu wakekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo
katikati yao,” Mt 18:20.
Ukweli wa jambo hili ndio leo Yesu anaukazia Yeye Mwenyewe
aliye ufunuo wa wazi wa Mungu Baba. Kutokana na ishara nyingi alizokuwa
anafanya Yesu mbele za watu, mama mmoja hakuweza kuizuia furaha yake. Hivyo
alitamka kwa furaha na kusema, “Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya,” Lk 11:27b. Nani kama Mama? Ni uthibitisho ulio wazi kwamba
Yesu alipata malezi mazuri kama mwanadamu. Sifa na utukufu kwanza Mungu na kwa
Mama Bikira Maria. Pamoja na furaha hii ya huyu Mama, Yesu anatutaka tuende
ndani na mbali zaidi. Kila mmoja wetu yampasa kulisikia neno la Mungu na
kulishika kama nilivyosema kwa kina hapo mwanzo. Hii ndiyo furaha kubwa sana ya
Mungu na wateule wake, yaani, Watakatifu wote huko Mbinguni. Naye Yesu alimjibu
mama yule, “Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika,” Lk
11:28. Ndugu uliyesafiri nami katika tafakari hii, neno la Mungu lina nafasi
gani katika maisha yako ya kila siku? Je, ni kitu gani kinachokupa uzima wako
kila siku? Na mwisho, siku yako kila siku huanza na kitu gani? Jibu maswali
hayo vyema. Majibu yako ndiyo
ukaribu au umbali wako na Mungu anayekupa uhai kwa hayo unayofikiri ndiyo uhai
wako.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; Ana
heri kila mtu ashikamanaye naye,” Mit 3:18. “Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na
faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi,” Mit 3:14
No hay comentarios:
Publicar un comentario