miércoles, 14 de octubre de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 28 YA MWAKA-B

ALHAMISI WIKI YA 28 YA MWAKA-B
15/10/2015
Somo: Rum 3:21-30
Zab: 130:1b-2, 3-4, 5-6ab
Injili: Lk 11:47-54
Nukuu:
Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia,” Lk 11:52 

Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii,” Rum 3:21

 ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti,” Rum 3:22

Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani,” Rum 3:27

Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria,” Rum 3:28 

TAFAKARI: “Twahesabiwa haki ndani na katika Kristo na siyo matendo ya sheria yenye kumpendezesha mwanadamu.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni vyema kufahamu kwa undani tofauti ya “sheria ya Mungu,” na “matendo ya sharia.” Kulijua agano jipya ya Mungu inakupasa kujua tofauti kati ya sheria ya Mungu na matendo ya sheria. Sheria ya Mungu ndiyo Torati. Torati hii ilijumuisha vile vitabu vitano vya Musa. Jambo la ajabu sana ni kwamba Wayahudi hawakuishika Torati kama ilivyowapasa kufanya na hasa zile nyakati za Yesu. Wayahudi walifuata tafsiri ya Torati na masimulizi yake, yaani, TALMUD. Kwa maana nyingine TALMUD ndiyo iliyojulikana kama “matendo ya sheria,” kwa maelezo ya Mtume Paulo katika nyaraka zake zote alisema juu ya matendo ya sheria. Hivyo tunaposikia “matendo ya sheria,” tuelewe siyo Torati ile aliyopewa Musa na kuwaasa wana wa Israeli waishike kwa ajili ya wokovu wao.

Katika agano jipya tunaona mgogoro mkubwa sana kati ya mitazamo hii miwili, yaani “Sheria ya Mungu,” na “Matendo ya sheria.” Hiki ndicho Yesu anachokikosoa na kukikemea anapokutana na Mafarisayo, waandishi na wana-sheria. Tunaposoma Mwinjili Mathayo hasa sura ile ya 23, tunakutana na makaripio makubwa sana kati ya Yesu na Mafarisayo kuhusu ukweli wa Sheria ya Mungu, yaani, ukweli kuhusu Torati na “Matendo hayo ya sheria, yaani tafsiri ya Torati, TALMUD. Yesu hakuacha kuweka wazi ukweli kuhusu Sheria ya Mungu, yaani, maana halisi ya Torati hasa aliposema, “msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,  yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata yote yatimie.” Mt 5:17-18. Wapo wengi kati yetu wanafikiri kwamba Mtume Paulo anapoongelea Matendo ya sheria anaongelea kuhusu Torati. Na hivyo Torati haina maana yoyote tunapokubali kuwa ndani na katika Kristo Yesu. La hasha! Torati, sheria ya Mungu ndiyo msingi wa sheria zote. Kristo kaja tu kuzitimiliza. Hivyo Mtume Paulo anaopoongelea Matendo ya sheria anaongelia kuhusu TALMUD. TALMUD ni ukweli wa Mungu uliochakachuliwa kwa malengo la kibinadamu na kupotoshwa.

Kwa mantiki hii unaweza kuona mkazo wa masomo yetu ya leo upo wapi. Kwanza kabisa tunaona ukweli wa kutokubaliana na mafundisho haya yaliyobeba dhana ya kitalmud. Ukweli wa Mungu wapaswa kubaki kama ulivyo na kuheshimiwa kwani katika ukweli huo sisi sote kutakuwa huru na kuurithi uzima wa milele. Mungu wetu hujidhihirisha katika sheria, yaani Torati na Manabii na siyo hiyo tafsiri yake yenye kubeba uelewa wa kibinadamu na masimulizi yake, yaani Talmud.Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii,” Rum 3:21. Maisha ya kweli ni maisha ya ufufuko ambayo kwayo twayaishi kwa ajili ya Kristo na kwa sababu ya Kristo. Huyu ndiye njia tuipasayo kuifuata, ndiyo kweli ituwekayo huru, na uzima tuutarajiao na kuuishi, yaani umilele. Huku ndiko kuishi katika IMANI ndani na katika Kristo. Hivyo, ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio,” Rum 3:22a. Msingi wa Imani katika Kristo upo katika Upendo wa kweli na katika kweli. Huku ndiko kuliko kweli katika kuzishika amri za Mungu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10. Mtazamo huu wa upendo juu ya sheria na amri za Mungu ndiyo mimi na wewe tunaopaswa kuishi leo. Ni katika upendo, Yesu alikubali kufa kwa ajili yako na mimi, na ni katika upendo huu kwa kuzishika amri zake Kristo Yesu atajidhihisha kwako. Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21. Hiki ndicho Kristo anachotaka kutoka kwako na kwangu.

Wapendwa wana wa Mungu, kujisifu kwetu hakuna chochote zaidi ya udhaifu wetu. Mtume Paulo anasema, Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu,” 2Kor 11:30. Hakuna kilicho chetu kizuri kama si cha Mungu na mali yake mwenyewe. Mali yangu halali na ikinipasa kwenda kifua wazi ni dhambi zangu. Hivyo ninaitaji huruma na msamaha wa Mungu kila siku ili niishi katika neema yake. Naitaji Imani dhabiti kuelewa ukweli huu, na ni katika Imani hiyo nitaishi kweli katika sheria yake. Ndugu yangu, ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani,” Rum 3:27. Hivyo hatuhesabiwi haki kwa sheria ya matendo. Tunahesabiwa haki kwa upendo wa Mungu mwenyewe na anavyoona inampendeza hasa tunapoishi katika kweli, haki na Imani thabiti. Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria,” Rum 3:28. Msingi huu wa Maisha ndiyo walioukosa Mafarisayo na Wana-sheria.

Mafarisayo na Wana-sheria waliishi kweli ya Mungu walioipindisha kwa manufaa yao wenyewe. Waliukataa ukweli na maarifa ya kumjua Mungu katika kweli na haki. Tendo hili ni sawa na kukataa ufunguo wa kweli na uzima. Mpendwa uliyesafiri nami katika tafakari hii, njia ya kweli leo katika maisha yako ya kiroho ni Kristo Yesu Mwenyewe. Kristo Yesu ni kweli tuipasayo kuichuchumilia kwa gharama zote. Na mwisho, uzima wa kweli upo kwa Kristo Yesu Mwenyewe. Kwa mankiti hii Yesu haoni haya kuwakaripia Mafarisayo na Wana-sheria kuhusu ukweli huu. Naye anasema, Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia,” Lk 11:52. Ufunguo wa maarifa na kweli kuhusu siri ya Mbinguni upo kwa Kristo Yesu peke yake. Hivyo kuijua siri hii yatupasa kuishi ndani na katika Kristo. Hakuna ufunuo wa Mungu ulio wa wazi zaidi ya Kristo Yesu.

Tumsifu Yesu Kristo! 


“Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma,” Yoh 17:3

No hay comentarios:

Publicar un comentario