domingo, 18 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 29 YA MWAKA-B

JUMATATU WIKI YA 29 YA MWAKA-B
19/10/2015
Somo: Rum 4:20-25
Zab: Lk 1:69-70, 71-72, 73-75
Injili: Lk 12:13-21
Nukuu:
bali na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki,” Rum 4:24-25

Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?” Lk 12:14

Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo,” Lk 12:15

Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu,” Lk 12:20-21

TAFAKARI:Uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Maisha ni dhamana.”

Wapendwa Taifa la Mungu, masomo yetu ya leo na hasa Injili, yanatualika tutafakari kwa undani maisha yetu na uhusiano wake na mali. Ndugu moja anamwendea Yesu mbele ya mkutano na kumwamuru amwambie ndugu yake amgawie urith wao, Lk 12:13. Badala yake, Yesu anamuuliza swali la msingi na la kushangaza. Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?” Lk 12:14. Swali hili linatutaka kuweka bayana nini maana ya maisha yetu na mahusiano yake na mali. Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, elewa leo kwamba maisha yako ni dhamana hapa duniani, na mali tulizo nazo tumeazimwa tu kwa muda. Mali ni za Mungu.

Wapendwa wana wa Mungu, muda wetu hapa duniani na nguvu zetu, akili, nafsi, mahusiano, na mali zetu zote ni zawadi toka kwa Mungu ambazo ametukabidhi tuvitunze na kuvitumia vizuri. Sisi ni mawakili wa yale Mungu atupayo. Wazo hili la uwakili huanza na utambuzi wa kuwa Mungu ndiye mmiliki wa kila kitu na kila mtu duniani. "Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake." Zab 24:1. Hivyo Yesu anamtahadharisha kijana yule na sisi pia kwa kutuambia kwamba, “Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo,” Lk 12:15. Uzima wako na furaha yako ya kweli haitokani na wingi wa mbali ulizokuwa nazo. Kwa maana nyingine, vitu hivyo kwa kuwa navyo kwa wingi havituhesabii haki mbele za Mungu. Ndugu yangu, kama humwamini yule aliyefufuliwa kutoka wafu yaani, Kristo Yesu, wingi wa utajiri wako ni bure kabisa kwa sababu mali zote ni za Bwana ukiwa na wewe mwenyewe. Mtume Paulo anasema, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki,” Rum 4:24b-25. Hivyo wingi wa mali zako bila Imani juu ya Kristo mfufuka ni bure.

Hakika "hatumiliki" chochote kwa wakati wetu mfupi wa kuishi duniani. Mungu "hutukopesha" dunia tunapoishi hapa. Ilikuwa mali ya Mungu kabla hujaja, na Mungu anamkopesha mtu mwingine ukifa. Je unabisha? Ndugu, ukweli ni kwamba unaifurahia dunia hii kwa muda mfupi tu. Injili ya leo inatuambia kwamba asiyefahamu ukweli huu ni MPUMBAVU kama mkulima yule tajiri aliyetaka kufurahisha nafsi yake kwa kusema, ‘pumzika basi, ule, unywe, ufurahi,” bila kujua ni nani aliye sababu ya uzima wake. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu,” Lk 12:20-21. Ndugu yangu bado furaha yako ipo kwenye mali?

Mungu alipowaumba Adamu na Hawa, aliwakabidhi uangalizi wa uumbaji wake na akawaweka kuwa wadhamini wa uumbaji wa mali yake. "Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi," Mwa 1:28

Ndugu unayesafiri nami katika tafakari hii, kazi ya kwanza ambayo Mungu aliwapa wanadamu ni kuangalia na kutunza "vitu" vya Mungu duniani. Wajibu huu haujaondolewa kamwe. Ni sehemu ya malengo yetu leo. Kila kitu tunachokifurahia yapasa tukione kama dhamana ambayo Mungu ameiweka mikononi mwetu. "Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu." 1Kor 4:2

Yesu mara kwa mara anaonyesha kuwa maisha ni dhamana na anatoa mfano wa talanta, mfanya biashara alikabidhi watumishi utajiri wake alipo safiri. Aliporudi alitathmini kazi ya kila mtumishi na kumpa ujira sawasawa na kazi yake. Yule tajiri anasema,  "vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya Bwana wako," Mt 25:21.

Ndugu, mwisho wa maisha yako duniani utatathminiwa kulingana na ulivyotumia yale Mungu aliyokukabidhi. Hii inamaana kwamba mambo yote unayofanya, hata yale mambo madogo madogo ya kila siku, yana matokeo ya umilele.
Kama utaona mambo yote kuwa dhamana, Mungu anaahidi zawadi tatu katika maisha ya milele. Kwanza, utapewa "uthibitisho". Atasema, "kazi nzuri! umefanya vyema." Kisha "utapandishwa" daraja na utapewa jukumu kubwa katika umilele: "nitakuweka uwe mwangalizi wa vitu vingi." Na mwisho utakaribishwa katika "karamu." "Njoo ushiriki katika furaha ya Bwana wako.

Watu wengi wanashindwa kufahamu kuwa pesa ni jaribu na dhamana toka kwa Mungu. Mungu anatumia pesa kutufundisha kumtegemea; na kwa watu wengi fedha ni jaribu kuu kupita yote. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi,” 1Tim 6:10. Mungu anaangalia jinsi tunavyotumia pesa ili kupima jinsi gani tunaaminika. "Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli?" Lk 16:11. Ndugu yangu, unapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, unampimaje yule leo anayekuja kwako nakuomba ridhaa ya uongozi na  kusimamia mali ya umma kwa uaminifu? Je, historia yake huko nyuma inathibitisha ukweli wa hiki anachokiomba leo? Tusiwakabidhi fisi zizi la kondoo. Hakika kondoo hawatakuwa salama.

Huu ni ukweli wa muhimu sana. Mungu anasema kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya ninavyotumia pesa zangu na hali yangu ya kiroho. Jinsi ninavyotawala pesa zangu "utajiri wa dunia" ni kigezo cha kiasi gani Mungu anaweza kunikabidhi baraka za kiroho, "utajiri wa kweli".

Hebu jiulize ndugu yangu, Je, namna ninavyotumia fedha zangu yaweza kumzuia Mungu kufanya mambo zaidi maishani mwangu? Je, ninaweza kuaminiwa katika utajiri wa kiroho? Wapo watu wachache katika mazingira na maisha yetu, waliweza kuthibitisha uhusiano wa moja kwa moja baina ya walivyotumia pesa zao na hali ya kiroho ya maisha yao. Pesa au utajiri wao havikuwa kipao mbele katika maisha yao. Watu na maisha yao ya dhiki ilikuwa kero zake na mara zote alijitahidi kutafuta suluhu ya kero hizo za watu. Mtu wa namna hii ndiye tunayeweza kuumpa dhamana ya kusimamia mali ya umma. Alilolisema ndilo alilolifanya. Dhima hii ndiyo iliyompa nguvu ya Kimaadili. Mfano wa mtu huyu ni Baba yetu wa Taifa; Julius Kambarage Nyerere, aliyetutangulia katika haki. Mungu amlaze mahali pema peponi. Sina shaka katika maisha yake. Ipo siku atapewa uangalizi mkubwa zaidi na Mama Kanisa na kuwa Mwombezi wetu-Mtakatifu.

Yesu Kristo anasema, "na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi." Lk 16:48. Maisha ni dhamana. Na kadiri Mungu anavyokupa zaidi, ndivyo anakutaka uwajibike zaidi.

Tumsifu Yesu Kristo!


“Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu; Bali haki huokoa na mauti.” Mit 11:4

No hay comentarios:

Publicar un comentario