JUMAMOSI WIKI YA 28 YA MWAKA-B
17/10/2015
Somo: Rum 4:13, 16-18
Zab: 105:6-7, 8-9, 42-43
Injili: Lk 12:8-12
Nukuu:
“Kwa maana ahadi ile
ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa
sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani,” Rum 4:12
“Naye aliamini kwa
kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama
ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako,” Rum 4:18
“Nami nawaambia, kila
atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika
wa Mungu,” Lk 12:8
“na mwenye kunikana
mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu,” Lk 12:9
“Na kila mtu
atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho
Mtakatifu hatasamehewa,” Lk 12:10 +
“msifadhaike
kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema; kwa kuwa Roho Mtakatifu
atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema,” Lk 12:11b-12
TAFAKARI: “Maisha
yanayoongozwa na ushuhuda wa Imani ya kweli.”
Wapendwa
wana wa Mungu, barua kwa Waibrania yatufundisha kwamba, “imani ni kuwa na
hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1. Kuwa
na hakika na jambo ni kutokuwa na shaka na jambo au kitu hicho katika maana ya
uwepo wake. Hali hii humpelekea mtu kuwa na MATUMAINI hata kama hajakipata
ukweli wa jambo hilo au kukiona kitu hicho. Ukweli na hali hii hauwezi kumtia
mtu shaka kwa vile avionavyo au asivyoviona. Matumaini haya humjaza mtu UPENDO
wa ajabu wa kumpenda Mungu na kutambua uwepo wake katika maisha halisi ya kila
siku ya mtu. “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu
amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale
wamtafutao,” Ebr 11:6. Uwepo wa Mungu aliye hai humjengea mtu IMANI ya malengo
thabiti katika maisha yake. Kuishi maisha yenye malengo na yaliyojengwa katika
msingi thabiti wa imani ya kweli, msingi huo humpa mtu MAANA ya maisha yake.
Matokeo
ya maisha haya yenye malengo humfanya mtu kutambua SIRI ya maisha yake hapa
duniani na kutambua kwamba tumeumbwa ili tuishi milele. Imani ya mtu huonekana
katika USHUHUDA wa maisha yake. Mtu huanza kutambua umuhimu wa muda, na hivyo
hawezi kuchezea muda wake. Hali hii humfanya mtu awe KARIBU sana na Mungu kwa
sababu jambo la msingi ni kuutafuta uso wa Mungu. Hivyo, “Mtakeni Bwana na nguvu
zake; utafuteni uso wake siku zote,” 1Nya 16:11. Ni katika ukaribu huu na Mungu
wenye msingi katika imani ya kweli, Mungu hufanya nasi mipango mikubwa kuhusu
wokovu wetu na watu wengine. Hivyo Ibrahimu anahesabiwa haki na kushirikishwa
mpango wa wokovu wa Mungu kwa sababu ya Imani yake. “Kwa maana ahadi ile
ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa
sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani,” Rum 4:12. Hili ndilo tunda la
imani (KUHESABIWA HAKI) pasipo shaka juu ya uwepo wa Mungu.
Jambo la
msingi la kutafakari hasa tunapoyatazama maisha ya Ibrahimu ni hasa pale
tunapotazama ubinadamu wake. Mazingira na hali aliyokuwa nayo Ibrahimu, yaani
Uzee wake, na aliyokuwa akiyapokea maagizo kutoka kwa Mungu ingekuwa vigumu
kwake kuyapokea maagizo hayo na kuyaamini kama angejitazama jinsi alivyo na
udhaifu aliokuwa nayo. Hata hivyo hakuona shaka kwa yale yaliyojidhihirisha
katika maisha yake, na yale ambayo ilimpata kuyatazamia. Hivyo Ibrahimu “aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa
baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako,” Rum
4:18. Mara nyingi Mungu anashindwa kufanya mipango mikubwa kwangu na wewe kwa
sababu tunajitazama sana katika udhaifu wetu na hivyo hatuoni sababu yoyote ya
Mungu kufanya hayo makubwa kwetu. Mtume Paulo anatukumbusha jambo la msingi
sana katika maisha yetu ya kiroho na hasa katika udhaifu wetu. “Kwa hiyo
napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya
Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu,” 2Kor 12:10.
Hivyo, historia yako mbaya na udhaifu wako kibinadamu, visiwe ukuta wa
kutoyaona mema ya Mungu na kupokea neema zake. Huna sababu ya kutokufanya
chochote kwa vile wajiona ovyo kupita vitu vyote. Mungu yupo tayari na muda
wote kusubiri ukiri wako, yaani,
kuachana na dhambi au uovu wako huo na kuanza Naye upya.
Wapendwa
wana wa Mungu, hatuna kitu chochote cha kumficha Mungu wetu. Mungu kesha
tupatia namna ya kumfikia kwa kupitia uwepo wa Mwanaye Yesu Kristo. Yesu ananiambia
mimi na wewe kwamba, “Mimi ndimi njia, na
kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Je, ndugu
yangu tunayesafiri pamoja katika tafakari hii wasadiki maneno hayo ya Yesu
Kristo? Kusadiki maneno haya ya
Kristo Yesu ni kukiri kwamba katika maisha ninayoishi leo na sasa Yesu Kristo
yupo hai ndani yangu, na kwa wale wote wanaonizunguka. Nisipolifanya jambo hili
nisijeshangaa siku ya mwisho napishana na Kristo Yesu katika maana ya
kutokunitambua mbele ya Baba yake wa Mbinguni. “Nami nawaambia, kila
atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika
wa Mungu,” Lk 12:8. Ukiri wangu katika maisha na ushuhuda mbele za watu, ndiyo
salama yangu mbele ya Mungu. Kinyume chake ni kwamba, “na mwenye kunikana
mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu,” Lk 12:9. Inasikitisha
kwamba wapo miongoni mwetu ambao watakanwa milele kwa vile tu walishindwa
kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yao na kuuishi ukweli huo kwa Imani iliyo
hai. Wakati mwingine matatizo yako yanaweza kuwa sababu ya kutokuona uwepo wa
Mungu na hali hiyo ikakufanya ukate tamaa kabisa. Je, kunasababu ya kukata
tamaa tukifikiri kuwa Mungu ametuacha? Ukimya wa Mungu juu ya matatizo yako
siyo kwamba haoni wala hajali. Mungu anajua ni wakati gani unaofaa kukupa kile
anachoona kitakufaa katika maisha yako ya umilele. Hivyo Mungu hawezi kukusahau
kabisa kwasababu alikuumba kwa sura na mfano wake, na anampango madhubuti na
maisha yako. Yesu anatuamba, “lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu
zimehesabiwa zote,”Mt 10:30. USIOGOPE hasa pale mambo yanapoanza kwenda ndivyo
sivyo. Huo nao ni mtihani wa imani yako. Mungu anajua utashinda tu
ukimtumainia. Mungu utuwazia mema kila wakati. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo
ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho,” Yer
29:11. Ndugu yangu huna sababu ya kukata tamaa.
Kukata tamaa katika maisha ni kosa kubwa sana kulifanya kama
unaishi kwa malengo. Kosa hili au dhambi hii ni kumkufuru Roho Mtakatifu. Kwa
tendo hili hatuwezi kupata msamaha wake. “Na kila mtu
atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho
Mtakatifu hatasamehewa,” Lk 12:10. Je, ni mara ngapi nimemkufuru Roho Mtakatifu
kwa kukata tamaa? Roho Mtakatifu
utuondolea mifadhahiko yote hasa pale tunaposhindwa kujitetea kutokana na
mazingira yetu, hali zetu, na ubinadamu wetu. Tunapokuwa na Roho Mtakatifu,
huyatakatifuza yote na kuyafanya mapya na yenye nguvu. HivyoYesu anatuambia,
“msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema; kwa kuwa Roho Mtakatifu
atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema,” Lk 12:11b-12. Je, naitaji
silaha gani zaidi ya kiroho kumshinda Roho Mtakatifu?
TAFAKARI NA CHUKUA HATUA!
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni
ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?” Zab 27:1
No hay comentarios:
Publicar un comentario