KUMBUKUMBU YA WAAMINI WOTE MAREHEMU
2/11/2015
Somo I: Hek 3:1-9
Zab: 23:1-3a, 3b-4, 5, 6
Somo II: Rum 5:5-11
Injili: Yoh 6:37-42
Nukuu:
“Bali roho zao wenye haki wamo mkononi mwa
Mungu, wala maumivu hayatawagusa,” Hek 3:1
“Na kufariki kwao kulidhaniwa kuwa ni hasara
yao, na kusafiri kwao kutoka kwetu kuwa ni uharibifu wao; bali wao wenyewe wamo
katika amani,” Hek 3:2b-3
“Wenye kumtumaini watafahamu yaliyo kweli, na
waaminifu watakaa naye katika upendo; mradi neema na rehema zina wateule wake,”
Hek 3:9
“Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia,
Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,” Rum 5:6
“Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa
kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8
“Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake,
tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye,” Rum 5:9
“Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa
mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima
wake,” Rum 5:10
“Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu
sitamtupa nje kamwe,” Yoh 6:37
“Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote
alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho,” Yoh 5:39
“Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila
amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua
siku ya mwisho,” Yoh 6:40
TAFAKARI: “Roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu, wala maumivu
hayatawagusa.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa pote
duani anaadhimisha Misa Takatifu kwa heshima ya Waamini Marehemu Wote
waliotutangulia katika haki. Kanisa la wana wa Mungu limegawanyika katika
makundi makuu matatu. Katika mgawanyiko huo lipo Kanisa la hija, yaani Kanisa
linalosafiri hapa duniani ikiwa ndiyo mahali pa kujindaa kwa ajili ya uzima wa
milele. Lipo Kanisa la toharani, ambalo tunaamini ni Kanisa linaloteseka, na
kwa kiasi kikubwa linategemea maombezi ya Kanisa la hija na la Watakatifu Wote
Mbinguni. Mgawanyiko wa mwisho ni Kanisa la Watakatifu wa Mungu, ambalo ndilo
mwombezi wa Kanisa la hija na linaloteseka, yaani Toharani. Kanisa hili ndilo
lililodhihirika la wateule wa Mungu, na wote waishio humo wanafana na Kristo na
kufurahia Utukufu wake na kumwona Mungu kama alivyo. Lakini “wapenzi, sasa tu wana
wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa
atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo,” 1Yoh
3:2.
Wapendwa wana wa Mungu, tungali hapa duniani yatupasa kuishi
katika matumaini hayo niliyoyasema pasipo shaka yoyote tukijua wazi kwamba
maisha ya umelele yakilinganishwa na haya ya duniani, tu hapa kwa muda mfupi
sana. Hivyo, “kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye
alivyo mtakatifu,” 1Yoh 3:3. Kanisa hili la
hija linatoa sadaka hii ya Misa Takatifu kwa matumaini makubwa likijua kabisa
kwa sadaka ile ya Bwana wetu Yesu Kristo pale msalaba ni kielelezo cha utakaso
wa Kanisa hili linaloteseka huko toharani lipate Utakakatifu. “Wenye kumtumaini watafahamu yaliyo kweli, na
waaminifu watakaa naye katika upendo; mradi neema na rehema zina wateule wake,”
Hek 3:9. Kanisa la hija linawajibu huu
kama sakaramenti ya wokovu kwa watu wote. Mungu pekee ambaye ni Huruma, Upendo,
na Msamaha na Haki ndiye mwenye kuwahesabia haki wote waliotutangulia na hasa
Kanisa hili la toharani.
Haki hiyo ya Mungu
tutahesabiwa kutokana na sadaka ya damu
ya Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo pale Msalabani. Hivyo, “Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake,
tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye,” Rum 5:9. Yapo maswali mawili ya msingi kwako
na kwangu tutakayo ulizwa siku ya Mwisho. La kwanza; Je, umefanya nini na
upendo wa wangu [Mungu] kupitia mwanangu Yesu Kristo kwa sadaka yake pale
msalabani? La pili; Je, umefanya nini na
vipaji nilivyokupa? Ili uweze kujibu vizuri siku ya mwisho yakupasa kujiandaa
vyema kuyajibu maswali haya sasa kupitia ushuhuda wa maisha yako leo. Hatuwezi
kuwa na kesho yenye matumaini ya kweli kama hatuishi leo yenye matumaini ya
kweli.
Wapendwa katika Kristo,
maisha ya ushuhuda wa kweli yanagharama zake. Kama yalivyo majira ya mwaka,
yaani, kipindi cha baridi, joto, vuli, na kipupwe, ndivyo yalivyo maisha ya
binadamu. Yatupasa kuwa wastahimilivu katika vipindi vyote vya shida, taabu,
mateso na furaha, na hata kufa kwa ajili ya haki na kweli. Pamoja na maumivu
tutakayoyapata katika safari hii ya kuelekea uzima wa milele, roho zetu zenye
haki zitakuwa mikononi mwa Mungu. “Bali roho zao
wenye haki wamo mkononi mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa,” Hek 3:1. Imani
na matumaini ndiyo dira ya kushinda na kufikia hatua hii muhimu.
Maisha ya ulimwengu wa leo ni maisha yenye
kusukumwa na falsafa ya umimi na ujimbilikiziaji wa mali. Katika hali hii ni
vigumu sana jamii inayokuzunguka kusadifu majitoleo yako kwa wahitaji. Tupo
kwenye ulimwengu wa kila mtu na yake na wakati wake. Hata katika hali na
changamoto hizi tusimuonee aibu Kristo Yesu hasa tunapojali na kuithaminisha
damu yake iliyomwagika pale msalabani. Kufa katika hali hii hakuna hasara
yoyote. “Na kufariki kwao kulidhaniwa kuwa ni hasara yao, na kusafiri kwao
kutoka kwetu kuwa ni uharibifu wao; bali wao wenyewe wamo katika amani,” Hek
3:2b-3. Tunayo amani na matumaini kwa sababu Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,
na hasa pale tulipokuwa hatuna nguvu za kuushinda uovu. “Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo
alikufa kwa ajili ya waovu,” Rum 5:6.
Licha ya udhaifu wetu
upendo wa Mungu unajidhihirisha kwetu kwa kumtoa mwanaye afe kwa ajili yetu
tungali tuna dhambi. Huu ni upendo Mkubwa sana kwetu. “Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa
kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8.
Sadaka hii ya Yesu pale Msalabani ni upatanisho wetu na Mungu, na kurudishiwa
hadhi ya kuwa wana wake Mungu, waridhi wa ufalme wake, na maisha ya uzima wa
milele. Hivyo, “Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa
mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima
wake,” Rum 5:10. Je, tufanye nini sasa?
Wapendwa wana wa Mungu, wenzetu wesha tutangulia katika haki ni
jukumu langu mimi na wewe tuishi kama tunayo siku hii ya leo na muda huu wa
sasa. Hakuna kati yetu anayejua litakalotokea kwake sekunde moja ijayo. Kristo
Yesu yupo daima kutusubiri na anayemwendea hawezi akampoteza. “Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu
sitamtupa nje kamwe,” Yoh 6:37. Kumwendea
Kristo ni kuwa karibu naye kila wakati. Ni kuishi maisha yasiyo na hatia. Ni
kuupigania ukamilifu ingawa udhaifu upo. Ni kuishi maisha ya kisakramenti na
kuchota huko neema na baraka za Mungu kila wakati na kwa kila nafasi tuipatayo
kushiriki masakramenti hayo. Ni kuwa waaminifu katika sheri na amri za Bwana
kwa kuzishika na kuziishi. Ni kuwa tayari kupokea neema na huruma ya Mungu, na
kuwa vyombo vya amani na upendo katika kusambaza neema na huruma hiyo ya Mungu
kwa watu wengine.
Kwa kuyashika na kuyaishi
haya kamwe Kristo Yesu awezi kutuacha leo, siku ya kufa kwetu, na mwisho siku
ya ufufuo wetu. Kwa kufanya hivyo tutakuwa kwenye mpango wa wokovu wa Bwana
wetu Yesu Kristo, naye atayatimiza mapenzi ya Mungu kwetu. “Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote
alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho,” Yoh 5:39. Kumtazama Mwana na kumwamini kuna
maanisha kujazwa uzima wa milele. Ndugu yangu unaye safiri nami katika tafakari
hii, tunamzama Mwana na kumwamini tunapowajali wahitaji hasa wagonjwa,
wafungwa, wenye njaa, wenye kiu hasa ya haki, wageni, na walio uchi, Mt
25:36-40. “Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila
amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua
siku ya mwisho,” Yoh 6:40. Je, hujakutana na Kristo Yesu bado kwa kumtazama na
kumwamini? Usinde mbali bali anza hapo hapo ulipo utakutana naye.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa maana kwangu mimi
kuishi ni Kristo, na kufa ni faida,” Flp 1:21
No hay comentarios:
Publicar un comentario