JUMANNE WIKI YA 30 YA MWAKA-B
27/10/2015
Somo: Rum 8:18-25
Zab: 126:1b-2abc, 2cd-3, 4-5, 6
Injili: Lk 13:18-21
Nukuu:
“Kwa maana nayahesabu
mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa
kwetu,” Rum 8:18
“Kwa maana viumbe
vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu,” Rum 8:19
“Wala si hivyo tu; ila
na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi
zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu,” Rum 8:23
“Bali tukikitarajia
kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi,” Rum 8:25
“Umefanana na punje ya
haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa
angani wakakaa katika matawi yake,” Lk 13:19
“Umefanana na chachu
aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote
pia,” Lk 13:21
TAFAKARI: “Tukilinganisha na umilele, maisha ya hapa duniani ni mafupi
sana. Imani thabiti ndiyo kielelezo cha kuufikia umilele huo, Ufalme wa Mungu.”
Wapendwa wana wa Mungu, ili kutimiza vizuri
maisha yako hupaswi kusahau ukweli wa aina mbili: Kwanza, yakilinganishwa na
umilele, maisha ni mafupi sana. Pili, dunia ni makazi ya muda tu. Hatuwezi
kukaa hapa kwa muda mrefu, hivyo usijishikamanishe sana nayo. Mfalme Daudi
aliomba, "Bwana, nijulishe mwisho wangu, na kiasi cha siku zangu ni kiasi
gani; nijue jinsi nilivyo dhaifu," Zab 39:4
Mpendwa katika Kristo, usisahau kuwa
maisha ya hapa duniani ni sawa na kuwa ugenini. Haya si makazi yako ya kudumu,
au hatma yako ya mwisho. Unapita tu! Unatembea tu duniani. Mfalme Daudi
anatukumbusha, "Mimi ni mgeni katika nchi, usinifiche maagizo yako,"
Zab 119:19, na Mtume Petro anasema,
"na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo,
kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa
kama wageni." 1Pet 1:17. Waamini wa kweli wanafahamu wazi kwamba kuna
mambo mengi ya maisha kuliko hii miaka michache tunayoishi hapa duniani.
Ni katika mtazamo huu
somo la kwanza na Injili yanatutafakarisha kuyaona maisha ya hapa nduniani ni
mafupi na hivyo ni muhimu kuyachuchumilia yake ya milele, yaani, ufalme wa
mbinguni. Katika hali hii IMANI thabiti ndani na katika Kristo kicho kielelezo
chetu leo na sasa ili kuufikia uhalisia huo. Imani hiyo inatupa nguvu ya
kuyakabili mateso na mahangaiko yetu ya kila siku za uhai wetu hapa duniani
tunapomtazama Jemedari wetu Yesu Kristo aliyeyashinda mateso. Ni kwa Imani hiyo Mtume Paulo anasema, nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu
kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu,” Rum 8:18. Kila kiumbe chenye uhai kina shauku hiyo ndani
mwake kwa sababu uwepo wake si wa bahati mbaya. Vyote vilivyoumbwa vinaufunua
Utukufu wa Mungu na furaha ya Mungu. “Kwa
maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu,”
Rum 8:19. Kufunuliwa huku ndiko kujionyesha wazi kwa Utukufu wa Mungu na furaha
yake.
Utukufu wa Mungu na furaha
yake ufikia kilele chake pale ambapo binadamu anapoishi kama binadamu katika
utimilifu, ukamilifu, na makusudi ya kuumbwa kwake. Ukweli huu ni kwa viumbe
vyote kama vilivyo. Sisimizi uufunua Utukufu wa Mungu na furaha yake anapoishi
kweli kama sisimizi katika utimilifu, ukamilifu, na kusudi la kuumbwa kama
sisimizi. Kufikia lengo hili kote kwa viumbe vyote na hasa mwanadamu kwa hitaji
sadaka kubwa. “Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya
Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani,
ukombozi wa mwili wetu,” Rum 8:23. Kwa upande
wa mwanadamu moja ya sadaka hiyo ni kuyakubali mateso na mahangaiko kama sehemu
ya kutakaswa kwake. Mateso haya katika Imani thabiti ndani na katika Kristo
huwa tarajio lisilokuwa na shaka na lenye msingi imara. Ni kweli kwamba, “tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi,” Rum
8:25. Je, Imani hiyo itupelekeayo kwenye
Ufalme wa Mungu ina mfanano gani?
Jibu la swali hili
limetolewa katika injili ya leo. Yesu anauliza aufananishe na nini na ufalme wa
mbingu? Kwanza Yesu anasema ufalme huu, “Umefanana na punje ya
haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa
angani wakakaa katika matawi yake,” Lk 13:19. Maana yake nini? Ndugu yangu
unayesafiri nami katika tafakari hii, Imani ni kuamini na kusadiki pasipo shaka
yale mambo madogo madogo yanayoonekana na yasiyooneka na yenye kuufunua utukufu
wa Mungu. Punje ya haradali ni ndogo sana. Lakini katika udogo huu mwisho wake
huwa mti mkubwa na ndege wa angani wakakaa katika matawi yake. Imani si jambo
la siku moja, bali Imani ukua hatua kwa hatua kadiri tunavyoishi na kuona vitu na
mazingira yake kwa mwono wa Kimungu, (Kila kitu kuwa na sababu yake)
Pili,
Yesu anasema ufalme wa Mungu “umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi
tatu za unga, hata ukachacha wote pia,” Lk 13:21. Imani ya kweli na thabiti ni
nguvu ya ndani ya ajabu kwa mtu ambayo hubadili kabisa mwonekano wa vitu kwa
mtu, utendaji, na hata namna ya kuyachukulia mambo. Chachu katika uchache wake
hubadili kabisa mwono na umbo wa kile kilichochachushwa. Imani hii ndiyo
inayotupa nguvu na dira mpya ya kuyaona maisha kwa namna ya pekee licha ya
ufupi wake na sababu ya kuishi kwetu hapa duniani, katika maana ya makazi ya
muda mfupi. Makazi haya ni sehemu ya maandalizi ya maisha ya umilele ambayo
ndiyo ufalme wenyewe wa Mungu.
Hivyo ndugu yangu tunapoishi hapa duniani mambo haya yatupasa
kuyazingatia. Moja, msingi wa wa maisha
wetu lazima ujengwe katika haki. Kwani, “yaliyo haki kabisa ndiyo utakayoyafuata, ili
upate kuishi na kuirithi nchi upewayo na Bwana, Mungu wako,” Kumb 16:20. Pili,
tusienende katika tamaa za wanadamu. “Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali
katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani,” 1Pet 4:2.
Na tatu na mwisho, kuishi kwetu kuwe ndani na katika Kristo. “Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida!” Flp
1:21. Kristo ndiye mtetezi wetu na mwokozi wetu. Amina
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia
ndani yangu, Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee,” Zab 51:10-11
No hay comentarios:
Publicar un comentario