JUMATATU WIKI YA 30 YA MWAKA-B
26/10/2015
Somo: Rum 8:12-17
Zab: 68:2, 4, 6-7, 20-21
Injili: Lk 13:10-17
Nukuu:
“kwa maana kama
tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo
ya mwili kwa Roho, mtaishi,” Rum 8:13
“Kwa kuwa wote
wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu,” Rum 8:14
“Kwa kuwa hamkupokea
tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo
kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba,” Rum 8:15
“na kama tu watoto,
basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa
pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye,” Rum 8:17
“Yesu alipomwona
alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako,” Lk 13:12
TAFAKARI: “Je, wataka kuishi?”
Wapendwa wana wa Mungu, bila shaka tunapotazama historia ya
uumbaji wa ulimwengu huu, na wokovu wa mwanadamu, utagundua kwamba Mungu
anapenda mwanadamu huyu aishi milele. Mwanadamu huyu ili aishi milele, yampasa
kutafuta na kutenda mema na kuishi kadiri ya mpango wa Mungu. “Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi;
hivyo Bwana, Mungu wa majeshi, atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo,” Amo 5:14.
Mahusiano kati ya mwanadamu na Mungu hujengwa
katika matendo mema.
Mungu kwa
kutuumba kwa sura na mfano wake, na kama tulivyo wanadamu ni ushahidi tosha
kwamba hana mpango wa kuvunja uhusiano wake na huyo aliyemuumb. Binadamu
mwenyewe kwa utashi wake huvunja uhusiano wake na Mungu kwa kufanya ayapendayo
na hasa kujipenda yeye zaidi na siyo Mungu. Kujipenda huku zaidi kuliko Muumba
wake kunavutwa na matendo yake ya mwili. Huku ndiko kufa kusiko kwa makusudi ya
Mungu, “kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka
kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi,” Rum 8:13. Uzima
wa mtu upo pale anapoongozwa na matendo ya roho. Matendo haya ya roho ndiyo
yanayotufanya watoto wa Mungu kwa sababu ndani yake upo wema na uzuri wa Mungu.
“Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa
Mungu,” Rum 8:14.
Wapendwa wana wa Mungu,
kadiri ya mpango mzima wa Kanisa, twampokea roho huyu tunaposhiriki vyema
masakramenti yake na kuishi kadiri ya neema tuzipatazo kwenye sakaramenti hizo.
Maisha haya ya hofu ya Mungu umwondolea mtu huyo hofu ya kibinadamu ambaye
mwisho wake ni kuukosa ufalme wa Mungu. “Kwa kuwa hamkupokea
tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo
kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba,” Rum 8:15. Kwa maana hiyo, sisi si watumwa
tena tunapoishi ndani ya Kristo na katika Kristo na kumpa nafasi Roho Mtakatifu
afanye kazi ndani yetu. Huku ni kikiri tu hai ndani ya Kristo na kumwita Baba
wa uzima wetu. Ukiri huu unatupa nafasi ya kuwa watoto wa Mungu na warithi
pamoja na Kristo. “Na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio
pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja
naye,” Rum 8:17. Je, unashaka juu ya jambo hili?
Injili ya
leo inatupa maisha mapya ndani ya Kristo pale tunapomwamini. Maisha ni mali na
zawadi ya Mungu kwetu. Hakuna mbadala kuhusu uhai wa mtu. Yesu analithibitisha
hili kwa kuvunja taratibu za kisinagogi na kisabato kwa kumponya mwanamke aliyekuwa na pepo wa
udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha
kabisa. Mateso na mahangaiko yetu ufikia kikomo chake tukiwa na imani pasipo
shaka juu ya Mwana wa Mungu. Yesu hakuweza kukaa kimya anapoona udhaifu wa mama
yule licha ya kwamba taratibu za kisinagogi na kisabato hazikumruhusu kufanya
aliyoyafanya. “Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika
udhaifu wako,” Lk 13:12. Tendo hili linaibua mjadala mkubwa kuhusu uhalali wa
Yesu kutoa huduma ile. Jambo la ajabu Wayahudi waliheshimu taratibu zao hizo,
bila kuona upendo na huruma ya Mungu kwao na watu wengine. Je, kwa nini basi
mimi na wewe tunajisikia vibaya mmoja wetu atendapo jambo jema na lenye
kumpendeza Mungu? Ndugu uliyesafiri nami katika tafakari hii kama unataka
kuishi ndani na katika Kristo fuata lililo jema na tenda mema siku zote.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno
mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka,” Yoh 14:24
No hay comentarios:
Publicar un comentario