domingo, 4 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMATATU YA WIKI YA 27 YA MWAKA-B

JUMATATU WIKI YA 27 YA MWAKA-B
5/10/2015
Somo: Yon 1:17, 2:10
Zab: Yon 2:3-5, 8
Injili: Lk 10:25-37
Nukuu:
Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu,” Yon 1:2

Naye akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata,” Yon 1:12

Bwana akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku. Bwana akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona pwani,” Yon 1:17, 2:10

“Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Lk 10:25

Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako,” Lk 10:27
Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi,” Lk 10:28

Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo,” Lk 10:37

TAFAKARI: “Fanya hivi nawe utaishi milele.”

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na mbwembwe zote za mwanadamu hapa duniani, ni wajibu wa kila mmoja wetu kujiuliza swali hili la msingi alilouliza mwana-sheria mmoja wa Kiyahudi kwa Yesu kuhusu uhai. Mwana-sheria huyu anamuuliza Yesu hivi; “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Lk 10:25. Msingi wa swali hili haupo kwenye uhai tu wa leo na kesho, bali uhai katika umilele wake. Tuelewe kwamba mwanadamu ameumbwa kuishi milele, na hayo ndiyo makusudi ya Mungu katika uumbaji wa mwanadamu. Tatizo kubwa la mwanadamu ni mbwembwe nyingi alizokunazo akisahau kuwa muda aliopewa hapa duniani hausimami kumsubiri. Mhubiri anatuwasa na kusema, “ mwanadamu hadumu katika heshima, bali amefanana na wanyama wapoteao,” Zab 49:12. Fahari ya mwanadamu ni yule aliyemuumba, yaani Mungu wake. Mengine yote ni mbwembwe tu! Mche Bwana, Mungu wako, umtumikie yeye; ambatana naye, na kuapa kwa jina lake. Yeye ndiye fahari yako, na yeye ndiye Mungu wako, aliyekutendea mambo haya makubwa, ya kutisha, uliyoyaona kwa macho yako,” Kum 10:20-21. Ndugu unayesafiri nami katika tafakari hii, elewa kwamba utajiri wako, ufahamu wako (kiwango cha elimu ulicho nacho), umaarufu wako, nk, bila Mungu ni bure kabisa.

Yesu kabla ya kumjibu vizuri mwana-sheria yule wa kiyahudi alitaka kujua uelewa wake wa Maandiko Matakatifu (Torati) yanasema nini kuhusu uhai wa Milele. Mwana-sheria yule akamjibu kwa staha, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako,” Lk 10:27. Yesu anaridhika na jibu hili na amamwambia hivi; “Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi,” Lk 10:28. Kuishi kwetu hapa duniani ambapo kunatupelekea kuishi milele baada ya kifo kama wanadamu kwatuwajibisha kufanya kwa weledi mkubwa mambo makuu mawili.

Moja, mpende Mungu wako kwa moyo wako wote, roho yako yote, na nguvu zako zote. Kwa maana nyingine ni kutumia vyote Mungu alivyokujalia ili umpende na ubaki kumpenda daima. Afya yako njema, akili yako ya pekee, utajiri wako, na umaarufu wako hapa nduniani isiwe sababu ya kujitenga na upendo huu wa Mungu. Hayo Mungu aliyokujalia kwa namna ya pekee isiwe sababu ya kuwakejeli wenzako ambao kwa mtazamo wako wa kibinadamu waona hawastahili mema yoyote mbele ya uso wa Mungu. Ndugu yangu, hata yale tunayoyaona kwa macho yetu kama udhaifu wa mtu na wengine, Mungu wakati mwingine utumia udhaifu huo kutufundisha siri ya maisha na uhai tuliopewa na Mungu mwenyewe. Maisha  na uhai tuliyonayo ni mali na zawadi yake Mungu. Mimi na wewe tumepewa uhai huu na kuazimwa kwa muda tu hapa duniani kama sababu ya kuutumia vyema uhai huu ili tuishi milele baada ya muda ambao kila mmoja wetu kapewa kadiri ya mapenzi yake Mungu. “Maana siku zangu zinatoweka kama moshi, Na mifupa yangu inateketea kama kinga,” Zab 102:3.

Pili, nimpende jirani yangu kama nafsi yangu. Jirani yangu ni yeyote yule ninayekutana naye na wale wote wanaonizunguka, yaani, wahitaji na wasio wahitaji. Jirani yangu ni kama kioo cha kujitazama ukamilifu wangu mbele ya Mungu. Je, udhaifu wa jirani yangu unasema nini kuhusu maisha yangu mimi niliyejiinua na kujiona safi na mwema kuliko wengine? Yesu, anakemea hali hii kwa Mafarisayo na Waandishi, na kwetu pia. Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi,” Mt 23:2-3. Mtazamo huu wa ugeugeu na kujiinua mbele za Mungu pasipo mastahili yoyote ndio sababu ya mfano wa Msamaria mwema. Wafarisayo ambao kwa kiasi kikubwa walijiinua na kuwa wepesi kuwahukumu wengine, wanashindwa kuokoa uhai ambao ni mali na zawadi ya Mungu kwa vile tu muhitaji huyu mhusika hakuwa Myahudi. Wakati mwingine tunashindwa kusimama katika kweli kwa vile tu mhusika siyo kutoka familia yetu, ukoo wetu, kabila letu, au kutoka Kanda yetu. Wenye mitazamo kama hii ilihali wanajiita wafuasi wa Kristo, basi Kristo huyo huendelea kusulubiwa kwa matendo yao. Kristo huyo siyo fahari ya maisha yao. Mimi na wewe kama wafuasi wa Kristo hatuna kitu kingine cha kujivunia zaidi ya Msalaba wa Kristo.  Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Je, tusikemee maovu? La hasha! Mkemeapo Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa,” 1Pet 2:1, 21, 23-24. Je, nauona udhaifu wangu ninapoutazama udhaifu wa mwingine?

Wapendwa wana wa Mungu, Yesu anapomwambia mwana-sheria yule afanye tathimini kati ya wale wayahudi na yule Msamaria aliyetoa msaada kwa mhitaji yule aliyepata kipigo na wanyang’anyi, mwana-sheria anaelewa soma lile na kumjibu Yesu, “Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo,” Lk 10:37. Wapendwa yatupasa kusimama katika kweli na haki, hivyo tutende yote kwa upendo na huruma ya kweli. Tusipolifanya jambo hilo basi tujiandae kusutwa na dhamiri zetu katika umiele wote.

Tunaona Nabii Yona anasutwa na dhamiri yake pale anapokataa kusimama katika kweli na haki kuupeleka ujembe wa wokovu kwa watu wake. Baada ya kugundua yeye ndiye tatizo la kuchafuka kwa baharí anakiri udhaifu huo na kuhamuri haki ya Mungu itendeke. Naye anatoa suluhu la tatizo na kuwaambia, “Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata,” Yon 1:12. Ukweli wa Mungu, haki ya Mungu, na upendo wake kwetu hatuwezi kuubadili kama kweli Mungu anapenda kumtumia mmoja kati yetu licha ya udhaifu wa mtu huyo. Haki hii, kweli hii, na upendo huu wa Mungu unajidhihirisha katika agizo hili analopewa Nabii Yona. Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu,” Yon 1:2. Hili ni agizo la Mungu. Mungu huweza kumtumia ye yote kati yetu licha ya udhaifu wa mtu huyo mbele ya macho ya wanadamu. Anachotaka Mungu tuwe na furaha ya kweli. Haya ndiyo mabadiliko katika nyanja za mwili na roho. Kwa kukaidi kwake Yona, Bwana akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku,” Yon 1:17. Kwa vile Mungu wetu ni UPENDO, na baada ya Yona kupata somo juu ya kile alichoamuriwa na Bwana wa Majeshi, “Bwana akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona pwani,” Yon 2:10. Tusipo ukiri udhaifu wetu na kufanya kadiri ya matakwa ya Mungu, hatutawezwa kutapikwa, yaani, kunusuriwa kutoka katika majanga yanayotushikilia. Je, hutaki kutapikwa?

Tumsifu Yesu Kristo!


Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu,” 1Sam 2:2

No hay comentarios:

Publicar un comentario