ALHAMISI WIKI YA 26 YA MWAKA-B
1/10/2015
Somo: Neh
8:1-12
Zab:
18:8-11
Injili:
Lk 10:1-12
Nukuu:
“Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu; msiomboleze wala
msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati,” Neh 8:9
“Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu,
tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa
Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu,” Neh 8:10
Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi
mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake,” Lk 10:2
“Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya
kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame kutoka
nyumba hii kwenda nyumba hii,” Lk 10:7
“Na mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni
vyakula viwekwavyo mbele yenu; waponyeni
wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia,” Lk 10:8-9
TAFAKARI: “Furaha na Amani ya kweli tunapojitoa bila kujibakiza ndani na
katika Kristo Yesu kuuishi na kuuhubiri Ufalme wa Mungu.”
Wapendwa
katika Kristo, neno furaha au amani la weza kuwa na maana tofauti tofauti kati
ya mtu mmoja na mwingine. Ni kweli pia kati yetu tunamwelekeo wa kuona furaha
yetu au amani yetu hutokana na “vitu.” Tulivyonavyo. Hivyo vitu fulani katika
maisha vinakuwa vigezo vya furaha na amani ya mtu. Kabla ya kuzama katika
tafakari hii ni vyema tuyatafakari maswali matatu ya Mhubiri.
Swali la
kwanza la muhubiri kuhusu “faida” anauliza kama ifuatavyo, “Mtu ana faida gani
ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua?” Ndugu yangu yawezekana kabisa kazi
yako ikawa sababu ya furaha na amani yako. Ni kweli kwamba sana unafanya kazi
na una nguvu za kufanya hivyo. Je, nguvu hizo zikikuishia na uzee
ukakunyemelea, kazi yako itaendelea kuwa sababu ya furaha na amani yako?
Tafakari sana jambo hili ndugu yangu.
Mhubiri
anaendelea kuuliza swali yake la pili na kusema, “Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha
nayo?” Mhu 3:9. Yawezekana furaha na amani
yako imejikita katika shughuli zako za kila siku kama vile biashara, maswala ya
siasa, ufundishaji, uimbaji, na tume mbalimbali kila mmoja kadiri ya nafasi na
wito wake. Je, hiyo tu ndiyo sababu ya furaha na amani yako? Je, utadumu katika
shughuli hiyo kwa muda gani? Umejaribu kujiuliza mwisho wa shughuli hiyo
utakuwaje? Je, utahimili ushindani wa shughuli hiyo daima? Bila shaka furaha na
amani katika swali hili la Mhubiri ipo hatiani.
Mhubiri
anatuuliza swali la tatu kuhusu faida na kusema, “Kwa maana mwenye hekima hupata faida gani
kuliko mpumbavu? Au Maskini ana nini kuliko yeye ajuaye kwenda mbele ya walio
hai?” Mhu 6:8. Wapendwa, mwenye hekima ni
yule mwenye uwezo wa kuona ukweli na uhalisia wa jambo kama ulivyo. Pili ni
yule ambaye kwa kupitia mang’amuzi ya maisha yake anakuwa tayari kuyatafutia
suluhisho matatizo anayokumbana nayo na hasa jamii ile anamoishi. Katika mwono
huu, mtu mwenye hekima huweza kuzisoma alama za nyakati za wakati wake na kuona
mbali zaidi kule anapoelekea licha ya kwamba bado hajaishi hali hiyo. Je, mtu
mwenye hekima kwa kuyajua hayo yote ndiyo msingi wa furaha na amani yake?
Mtu
mpumbavu ni yule ajifanyaye mwelewa kumbe si mwelewa katika uhasilia wa mambo
kama yalivyo. Ni mtu yule anayeshupalia ujinga kwa kiwango cha juu. Je, msimamo
huu kimaisha ndiyo sababu ya furaha yako? Na siku basi utakapotambua ukweli
kama ulivyo ndiyo itakuwa mwisho wa furaha na amani yako? Masikini ni ye yote
yule mwenye uhitaji. Kama sote ni wahitaji, basi sote ni maskini wa viwango
tofauti. Mbele ya walio hai ni wale wote wanaoishi katika umilele. Hawa ni
watakatifu wa Mungu. Bila shaka hawa wana furaha na amani ya kweli kwa sababu
wanamwona Mungu kama alivyo na wanaishi si tena katika imani na matumaini, bali
katika umilele wa upendo wa Mungu. “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo,
haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo,” 1Kor 13:13.
Wapendwa
wana wa Mungu, Mhubiri natupatia jibu la maswali hayo matatu na kusema, “Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa
mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili
na kujilisha upepo, wala faida hakuna chini ya jua,” Mhu 2:11. Je, kama hakuna
faida yo yote chini ya jua, furaha na amani yangu ya kweli naipata wapi? Yesu
anatuambia jambo hili wazi, “kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote,
akipata hasara ya nafsi yake?” Mk 8:36. Ndugu yangu unayesafiri nami kati
tafakari hii, furaha ya kweli tunaipata pale tunapokuwa watu wa kiasi, yaani
kuishi kwa uchache. Jambo hili tunaliona katika mfano ule wa talanta. “Vema,
mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya
mengi; ingia katika furaha ya bwana wako,” Mt 25:23. Furaha ya kweli tunaipata
pale tunaposhiriki mateso yetu kikamilifu na Kristo. Ni pale tunapoisha kweli
na haki bila kumwonea aibu Kristo. Ni pale tunapotesaka kwa ajili ya Kristo na
hasa kuwa sauti za wasiokuwa na sauti katika jamii dhalimu na ovu. Yesu anasema
hivi, “Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo
yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22.
Wapendwa wana wa Mungu, amani ya kweli ni ile tuipewayo na
Kristo mwenyewe, yaani tunapokuwa ndani na katika yeye. Amani hiyo siyo ile
tuipewayo na ulimwengu huu. Tukiwa ndani na katika Kristo hatuwezi kuishi
katika mifadhaiko wala woga. Yesu anatuambia, “Amani nawaachieni; amani yangu
nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu,
wala msiwe na woga,” Yoh 14:27. Na tunaipata amani hii tunapotenda kadiri
anavyotufundisha Kristo. Kuyatenda yale yampendezayo Mungu siyo yale
yafaidishayo nafsi na mwili tu. “Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa,
bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu,” Rum 14:17. Kuna faida
kubwa kuteswa kwa kutenda mapenzi ya Mungu kuliko kutenda mabaya. “Maana ni
afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa
kutenda mabaya,” 1Pet 3:17.
Hivyo wapendwa wana wa Mungu furaha yetu na amani yetu ya
kweli ni kutenda kadiri ya Mungu apendavyo, na kufanya hivyo bila kujibakiza.
Tunapoikubali hali hii tuwe tayari kupokea mateso na kadhia zote ndani na
katika Kristo. Hatuna sababu ya kuendelea kuomboleza na kusikitika kama tunaye
Mungu ndani yetu. Wana wa Israeli walipoipokea torati haikuwapasa tena
kuendelea kuomboleza na kufia masikitiko yao. Nabii Nehemia anawaambia
Waisraeli, “Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu; msiomboleze wala
msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati,” Neh 8:9. Kama
kweli ninayo imani na neno la Mungu, na Kristo aliyekufa kwa ajili yangu, sina
sababu ya kuwa na mashaka wala hofu juu ya maisha yangu na Kristo.
Wapendwa katika Kristo, furaha ya Bwana ni nguvu yetu.
Tunapojazwa amani na furaha ya Bwana ndani yetu hakuna cho chote tutakachofanya
bila kufanikiwa. Maisha yetu yatakuwa yanaongozwa kwa malengo ya Mungu
mwenyewe. Hivyo Nabii Nehemia anawaambia watu wake kwamba, “Enendeni zenu, mle
kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa
kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa
furaha ya Bwana ni nguvu zenu,” Neh 8:10. Je,
ni nani atakaye kuwa na nguvu juu yetu kama Mungu yu upande wetu? Hivyo mimi na
wewe ni sababu tosha ya kuuleta ujumbe wa amani na furaha ya Mungu kwa watu. Na
pale ambapo haipo furaha na amani hiyo, yatupasa kuiomba kwa Mungu, naye atatoa
kadiri ya mahitaji yetu. Kama jumuiya ya wenye hofu ya Mungu, Yesu anatualika
kuliomba hili kadiri ya maitaji ya kanisa lake, na kusema, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni
wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno
yake,” Lk 10:2. Hili ni jukumu la kila mbatizwa.
Kufikia lengo la kuutangaza ufalme wa Mbinguni kwa wengine,
sisi tuliopata habari hii ya wokovu yatupasa kulisimamia jambo hilo kwa weledi
mkubwa, kwa kuwa waaminifu kwalo, na kuushikila ukweli huu bila kutetereka.
Yesu anatutaka kuwa makini sana huko tuendako kuupeleka ujumbe wa wokovu. Naye
anasema, “Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya
kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame kutoka
nyumba hii kwenda nyumba hii,” Lk 10:7. Na lifanyike jambo moja kwa wakati. Hii
ni pamoja na kuwa makini kwa jambo lile lile tu. Tusibebe ajenda nyingi katika
safari hii ya uinjilishaji. Mambo hayo {mfuko, mkoba, viatu na wala kuwaamkie
mtu njiani} tukiambatana nayo yatatuchanganya na kutufanya tupoteze mwelekeo.
Tuambatane na kubeba yale tu tunayohitaji kwa utume huo. Tusipokuwa na uchache
wa vitu furaha na amani ya kweli hutoweka. Tusiuzunike pale ambapo tunaona
mambo hayakwenda kama tulivyotarajia. Kufanya hivyo ni kupoteza muda bure kwani
muda hautungoji hata kidogo.
Katika jambo hili Yesu anasema, “Na mji wo wote
mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake
semeni, Hata mavumbi ya mji wenu
yaliyogandamana na miguu yetu tunayakung'uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya
kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia,” Lk 10:10-11. Jambo la msingi la kuzingatia ni
kufanya yale tu tuliyotarajia kuyafanya na kuwa na mahusiano mazuri na wale
tuliokusudia kuwainjilisha neno la Mungu. “Na mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni
vyakula viwekwavyo mbele yenu; waponyeni
wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia,” Lk 10:8-9.
Tuyafanyapo haya kwa unyenyekevu bila kujibakiza huwa msingi wa furaha na Amani
yetu.
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU TUFANYE VYOMBO VYA FURAHA NA AMANI YAKO. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario