martes, 30 de junio de 2015

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 13 YA MWAKA-B

JUMATANO WIKI YA 13 YA MWAKA-B
30/6/2015
Somo: Mwa 21:5,8-20
Zab: 33:7, 8-9, 10-11, 12-13
Injili: Mt 8:28-34
Nukuu
Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka,” Mwa 21:10

Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa,” Mwa 21:12

Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako,” Mwa 21:13

Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?” Mt 8:29

Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini,” Mt 8:32

Na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke mipakani mwao,” Mt 8:34

TAFAKARI: “Damu nzito kuliko maji.”

Wapendwa wana Mungu, usemi huu “damu nzito kuliko maji,” unajidhihirisha katika tafakari ya masomo yetu ya leo. Kwa maana nyingine chako ni chako tu hata kama kinadharaulika au kudharauliwa. Mama mzazi aliyepata uchungu wa kuzaa, na baadaye mtoto yule akawa na tabia mbaya, mfano: wizi wa kupindukia, mama huyu kwa vile ni mwanaye hawezi kamwe kumkana. Ni afadhali afe na mwanaye akiwa anachomwa moto kuliko kumkana. Katika somo la kwanza tunaona hali hiyo ikimtokea Ibrahimu baada ya kauli ya Sara mkewe kutomtaka mtoto wa Hajiri, Ishamaeli. Maneno ya Sara ni mazito sana na yasiyokuwa na chembe ya uzazi, na upendo ndani yake. Sara anamwambia Ibrahimu, “Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka,” Mwa 21:10. Tuelewe kwamba mwana huyu wa mjakazi, Ishmaeli halikuwa kusudi la Ibrahimu kuwa na mtoto nje ya ndoa yake. Ni Saha huyu huyu aliyemshawishi Ibrahimu kutembea na Hajiri ili amzalie mtoto, baada ya kuona umri wake umesogea. Ibrahimu anafadhaika sana kwa kitendo hiki cha mkewe Sara.

Hata hivyo, ikiwa yote hayo ni mpango wa Mungu katika safari ya ukombozi wa mwanadamu, ‘pasipo njia Mungu hufanya njia.’ Mungu analifumbua fumbo hili kwa Ibrahamu na kusema, “neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa,” Mwa 21:12. Fumbo la Mungu kati ya Sara, Hajiri, na Ibrahimu ni kwamba, “katika Isaka uzao wa Ibrahimu utaitwa.” Hapa ndipo kwenye mtego, na mkono wa Mungu. Mara nyingi Mungu aweza kufanikisha mambo yake kwa njia ya pekee na wakati mwingine si rahisi kufahamu kwa akili zetu kama binadamu.

Kwa upande wetu binadamu kuelewa mafumbo mazito kama haya twaitaji utulivu wa ndani. Ni katika utulivu Mungu hujidhihirisha. Mfano, Mungu anajidhihirisha kwa Nabii Isaya kwa namna hii: Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi; na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu,” 1Fal 19:11-12. Tunapopatwa na jambo la kutuhuzunisha, moyo wetu hupitia hatua mbalimbali kama upepo wa nguvu, tetemeko la nchi, na moto. Katika hali hizi zote za uchungu na hasira Mungu hawezi kamwe kujidhihirisha ndani yetu. Hivyo katika hali kama hiyo yakupasa kutulia na kutokufanya chochote zaidi ya kutafakari hali ile. Kwa maana nyingine usifanye maamuzi yoyote ukiwa katika hali ya hasira. Mwisho wa hasira  yako maamuzi uliyoyafanya yatakugharimu maisha yako, na hali yako. Ibrahimu hakuchukua taharuki ya kumlaumu mkewe Sara kwa kitendo kile kisichopendeza. Ibrahimu anazama katika tafakuri, na katika sintofahumu hiyo, Mungu anajidhihirisha. Mungu hamtupi mja wake hata mara moja. Mungu anampango na kila mmoja wetu, hata kama kwa namna tulivyo iliwashangaza watu au bado inawashangaza wele tunaoishi nao. Kuzaliwa kwako hakukutokana na makosa wala bahati mbaya, na maisha yako si tokeo la bahati tu ya asili.

Wazazi wako wanaweza kuwa hawakupanga kukuzaa lakini Mungu alipanga. Mungu hajashangazwa hata kidogo na kuzaliwa kwako. Kwa kweli, alitegemea uzaliwe. Hapo zamani kabla hujatungwa mimba na wazazi wako, ulitungwa katika mawazo ya Mungu. Alikufikiri kwanza. Si jambo baya, wala bahati au tukio la bila kutegemewa kwamba wewe unapumua kwa wakati huu. Uko hai kwa sababu Mungu alitaka kukuumba! Maandiko Matakatifu yanasema, “Bwana atatimiza kusudi lake kwangu,” Zab 138:8. Hivyo ni kwa mtazamo huu Mungu anampango na Ishmaeli. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako,” Mwa 21:13. Kwa maana nyingine Ishaeli ni damu ya Ibrahimu, hivyo si vizuri Ibrahimu kumtelekeza Ishmaeli.

Wapendwa wana wa Mungu, damu nzito kuliko maji. Somo la Injia tunaona ni kwa namna gani mapepo wanatambua mamlaka ya Yesu na kuweweseka. Mapepo wanapohisi uwepo wa Yesu, amani yao yote hutoweka. Hili ndilo lile jina lililopita majina yote, na kwalo hakuna nguvu za kuzimu zinazoweza kustahimili kishindo chake. Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile,” Mdo 16:18. Ni kwa namna hii mapepo yanakiri Jina la Yesu na mamlaka yake. Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?” Mt 8:29. Uwepo wa Mungu ni mwanzo na mwisho wa vyote, yaani alfa na omega. Katika maana hii, wanachojitetea hawa mapepe kuhusu muhula wao, hakina maana yoyote kwa uwepo wa Mungu. Taratibu za Mungu haziingiliwi na roho yoyote ile  au kiumbe chochote kile.  Ikiwa hivyo, huyu siye Mungu mwenye mamlaka (alfa na omega). Mamlaka ya Kristo ni ya milele kwa sababu,  Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3

Ni ukweli usiotia shaka kwamba wengi tunajiuliza kwa nini basi Yesu anayaruhusu yale mapepo yawaingie wale Nguruwe na kusababisha hasara kubwa kwa yule mfugaji? Kwa nini Yesu asingetumia njia nyingine na huyu anayejikwamua katika mazingira magumu kimaisha na kimapato kwa njia hii ya  ufugaji asipate hasara? Wapendwa wana wa Mungu, tunarudi pale pale kwamba, “damu nzito kuliko maji.” Yesu Kristo amekuja kumweka binadamu huru kutoka vifungo vya dhambi. Uhai wa binadamu ni lengo la kwanza na makusudi ya Mungu na uumbaji wake wote. Binadamu ni mtawala wa viumbe vyote, na kuviendeleza, binadamu akiwa kiumbe shirikishi cha Mungu katika uumbaji wake wa pili. Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi,” Mwa 1:26. Hivyo Yesu kuwaruhusu wale pepo kuwaingia wale Nguruwe kumelenga hadhi hii aliyopewa binadamu. Mungu hawezi kuacha sura na mfano wake upotee bure.

Hivyo Yesu anayaruhusu yale mapepo na kusema, “Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini,” Mt 8:32. Hadhi aliyonayo binadamu ni kubwa sana mbele ya uso wa Mungu. Yesu analisema jambo hili na kutufunulia kiu yake juu ya nafasi na uwepo wetu mbele ya Mungu. Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi,” Lk 12:6-7. Ndugu yangu kwa nini wajidharau basi na kujiona hufai mbele za hao wanaokuzunguka. Elewa jambo hili: Yesu mara zote anakuambia hivi, “nakupenda kuliko kitu chochote katika ulimwengu huu, na ndiyo maana sikuona aibu kufa kifo cha aibu kwa sababu yako.”

Kwa tendo hili Yesu alilolifanya, kuwaruhusu mapepo kuwaingia wale nguruwe, watu wa kijiji kile hawakumwelewa. Watu wale walijawa hofu na furaha. Furaha kwa sababu ya tendo lile la kimungu na watu wale kupona, na hofu kwa sababu hawakujua ni jambo lipi lingine baya litakaloweza kutokea kwao kama mtu huyu ataendelea kuwa kijijini pale. Kama kwa muda mchache tu ule nguruwe wale wote walipoteza uhai, itakuaje mtu huyu akiendelea kukaa nasi hapa kijijini mwetu? Wakasema nishiiiida! Hivyo  na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke mipakani mwao,” Mt 8:34. Ndugu yangu huyu ndiye Yesu anayetupenda bila kipimo.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU ASANTE KWA KUNIPENDA KAMA NILIVYO. AMINA

lunes, 29 de junio de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 13 YA MWAKA-B

JUMANNE WIKI YA 13 YA MWAKA-B
Somo: Mwa 19:15-29
Zab: 25:2-3, 9-10, 11-12
Injili: Mt 8:23-27
Nukuu:
Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea,” Mwa 19:17

Tazama, mtumwa wako ameona kibali machoni pako, nawe umezidisha rehema zako ulizonifanyia kwa kuponya nafsi yangu, nami siwezi kukimbilia mlimani nisipatwe na yale mabaya, nikafa,” Mwa 19:19

Ndipo Bwana akanyesha juu ya Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto toka mbinguni kwa Bwana,” Mwa 19:24

Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi,” Mwa 19:26

Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia,” Mt 8:25

Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu,” Mt 8:26 

Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?” Mt 8:27

TAFAKARI: “Tusipobadilikia na kumrejea Mungu, kiama ki juu yetu hata sasa.”

Wapendwa wana wa Mungu, kuangamizwa kwa Miji ya Sodoma na Gomora kwa matendo yao mbaya hakuna tofauti na ulimwengu wetu huu wa leo. Ni hivi jusi tu huko Marekani wamepitisha sheria ya kuhalalisha ndoa za jinsia moja. Mungu alivyomuumba mtu mwanamke na mwanaume alijua wazi ni kwa njia hiyo halali Taifa lake litakua na kuongezeka. Kwa hatua hii ya binadamu kutengua kile kilichokuwa sababu ya uumbaji wake, ni kupalia moto hasira ya Mungu.

Pamoja na juhudi alizozifanya Ibrahimu kutuliza hasira ya Mungu kwa kumtaka Mungu asiangamize miji ile ilihali wapo wachache wenye haki, juhudi hizo zinagonga ukuta kwa sababu uovu uliwaingia hadi wakawa vipofu mioyoni mwao na akilini mwao. Hata hivyo Mungu ni mwingi wa rehema na huruma. Familia ya Lutu inanasuliwa na angamizo hilo la moto. Tazama, mtumwa wako ameona kibali machoni pako, nawe umezidisha rehema zako ulizonifanyia kwa kuponya nafsi yangu, nami siwezi kukimbilia mlimani nisipatwe na yale mabaya, nikafa,” Mwa 19:19. Ila mke wa Lutu anabadilika na kuwa Jiwe la chumvi kwa kutokufuata masharti na maelekezo kutoka kwa malaika wa Mungu. Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi,” Mwa 19:26. Kosa lake ni kujeuka na kutazama yaliyokuwa yanatokea kule alikotoka.

Ni kweli uliowazi kwamba, msukumo wa kupitisha sheria ziendazo kinyume, uhalisia, na makusudi ya Mungu (kiimani), mara nyingi husukumwa na migandamizo ya kisiasa, na ajenda binafsi, hivyo kuweka uhalali wa serikali hiyo kuendelea kuwa madarakani. Ukweli wa kitu ubakia kuwa kweli hata kama kwa wakati huu wengi walio vipofu mioyoni mwao na akilini mwao wataubeza. Bila shaka yaliyotokea Sodoma na Gomora ndiyo yanayotokea kwenye miji na jamii yetu leo, na mfano hai ni hili lililopitishwa huko Marekani.

Uzinifu wa hali hii ni chukizo kwa Mungu. Huku ni kwenda kinyume kabisa na makusudia ya uzazi na maana ya Ndoa Takatifu. Tendo la ndoa ni Takatifu linapofanywa kwa utaratibu aliouweka Mungu mwenyewe. La sivyo hatuwezi kukwepa adhabu ya Mungu. Ndipo Bwana akanyesha juu ya Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto toka mbinguni kwa Bwana,” Mwa 19:24. Dhambi ya uzinifu katika Agano la jipya imekemewa sana na Kristo.

Amri hii si tu kuwa inazuia uzinzi na uasherati bali pia uchafu wa aina zote kwa kutenda, kwa maneno na hata kuwaza. Katika hubiri la mlimani Yesu aliifundisha na kuifafanua amri hii akasema: “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake,” Mt 5:27-28. Wale wote wanaoitwa kwa jina la Mungu hawapaswi kuwa wenye kuwaka tamaa za uzinzi na uasherati.

Amri hii inahusu kuheshimu kifungo cha ndoa. Maandiko Matakatifu yanasema kuwa “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu” Ebr 13:4. Ndoa ni takatifu na inawaunganisha mme na mke kuwa mwili mmoja. Maandiko yanasema: “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Mwa 2:24.

 Ukubwa wa Uvunjaji wa Amri Hii ni hayo niliyokwisha kusema kwenye jamii yetu leo, na mbaya zaidi hili lililotokea Marekana kwa kupitishwa sheria ya kutambua ndoa za jinsia moja. Kwa mantiki hii, sidhani kama kuna mtu ambaye hajui jinsi udhalimu wa uasherati na uzinzi ulivyokithiri katika ulimwengu huu. Kiwango cha uvunjaji wa amri hii ni kikubwa na kinatisha. Mioyo ya watu imekufa ganzi kwa uovu huu. Katika baadhi ya mataifa na hata baadhi ya madhehebu ya dini uzinzi, uasherati, ushoga, ndoa za mikataba na za watu wa jinsia moja vyote vimepitishwa na kuhalalishwa kisheria.

Mtandao wa internet umejaa picha za uchi na matendo ya kujamiiana (ponografia). Mataifa yenye nguvu yanashinikiza mataifa mengine ili nayo pia yaruhusu na kuhalalishwa ushoga kuwa moja ya haki za binadamu. Wanadamu hawaoni tena udhambi/ ubaya wa dhambi hii.

Kumbukumbu za  kuongezeka kwa ushoga nchini Marekani zipo hivi: Newsweek, Machi 12, 1990 “47% ya Wamarekani wanaamini kuwa mahusiano ya kimapenzi kati ya wanaume wanaokubaliana yapaswa kuhalalishwa.” Baada ya kutafakari haya yote, Bill Graham, mhubiri maarufu, alisema “Kama Mungu hatakuja hivi karibuni na kukikomesha kizazi hiki, itabidi aombe radhi kwa aliyowatenda wakazi wa Sodoma na Gomora”. Inatisha, watu wamevuka mipaka yote. Je, nini mtokea ya udhalimu huu?

Kwanza kabisa, uvunjaji wa amri hii ni kati ya mauovu ambayo yalisababisha watu wa wakati wa Nuhu kuangamia kwa gharika na miji ya Sodoma na Gomora kuangamizwa kwa moto kadiri ya mtazamo w asomo letu la leo. “Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele… Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani …,” Mwa 6:1-5. Yesu anasema watu wa wakati huo “walikuwa wakioa na kuolewa” Lk 17:27. Hii ni sawa na kusema walikuwa wakioa na kuacha na kuoelewa na kuachika, hawakufuata wala kuheshimu taratibu za ndoa. Kwa ukengeufu huo Mungu akawaangamiza. Maandiko Matakatifu yanaliweka wazi jambo hili, “uasherati, uzinzi na kuingilia kinyume na maumbile ni udhalimu,  sehemu yao ni katika ziwa la moto” 1Kor  6:9.

Wapendwa wana wa Mungu, amri hii inakataza kila aina ya uchafu na udhalimu wa kujamiiana, na kila aina ya mihemuko inayoongoza huko. Kila wazo na tendo linaloelekezwa huko ni uvunjaji wa amri hii na ni kinyume cha mapenzi ya Mungu. Maandiko yanasema: “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu …? Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu”. 1Kor 6:18-20

Injili inatutaka tuwe watu wa Imani ya kweli. Hatuwezi kumkiri Yesu kuwa ni njia, kweli na uzima, na wakati huo huo kukosa Imani naye. Imani hii thabiti ni kwa vipindi vyote; wakati wa mambo yakiwa shwari na wakati wa migogoro katika jamii. Leo swala la uzazi, familia, na mahusiano ni changamoto kuwa sana. Yatupasa kusimama katika kweli, na kulisema jambo hilo kwa Imani iliyo kweli. Haitoshi kupiga kelele tu kuwa tunaangamia, bali tunapopiga kelele tunaangamia tuwe tumesimama imara katika Imani.

Ni kweli yatupasa kumwendea Yesu muda wote, na hasa katika mikwamo iliyozidi akili na maarifa yetu. Mitume wanalifanya jambo hilo wanapoona chombo chao cha kusafiria kikiwa matatani. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia,” Mt 8:25. Kanisa kama chombo kielekeacho uzima wa milele, na sakramenti ya wokovu wetu kwa wabatizwa wote, mara zote hukaa kama familia na kupeleka maombi mbele ya Kristo ambaye Kanisa ni mwili wake. Tufanyapo jambo hilo kama mwili wa Kristo ulioingiliwa na udhaifu (dhambi), twapaswa kusimama katika Imani ya kweli. Yesu anatoa karipio kwa wanafunzi wake na si pia katika nyakati zetu na kusema, “Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu,” Mt 8:26. Je, ndugu yangu, unaimani kweli kwa kile umwombacho Mungu? Au waenda kwake ukiwa na wasiwasi? TUZIOMBEE FAMILIA ZETU ILI ZIBAKI SALAMA.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU KITAZAME KIZAZI CHETU UTUHURUMIE. AMINA

domingo, 28 de junio de 2015

TAFAKARI: SHEREHE YA WATAKATIFU PETRO NA PAULO MITUME

SHEREHE YA MT. PETRO NA PAULO, MITUME
29/6/2015
Somo: Mdo 12:1-11
Zab: 33
Somo II: 2Tim 4:6-8, 17-18
Injili: Mt 16:13-19 
Nukuu:
Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi,” Mdo 12:11

Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda,” 2Tim 4:7

Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina,” 2Tim 4:18

Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16

Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18

Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni,” Mt 16.19

TAFAKARI: “Utume si lelemama, bali ni kuvumilia hadi ushindi wa kweli.”

Wapendwa wana wa Mungu, neno utume si geni masikioni mwenu. Ila tusikiapo neno utume yatupasa kwanza kabisa tuelewa ukweli huo na uhasilia wa maisha hayo ya kiutume kwamba hayana uhusiano na faida binafsi. Ni utumishi uliotukuka, na usiojifungamanisha na maslahi binafsi. Ni msukumo wa maisha unaotutaka kujitoa zaidi kwa ajili ya wengine bila kujali faida yetu binafsi. Utume kamwe hauwezi kuwa na malengo ya faida binafsi. Mtu anapokuambia ametoka utume, au anaenda utume ni vyema kuelewa kwamba anaenda kumenyeka, kutaabika na kujichosha kwa ajili ya wengine. Msukumu huu haupaswi usukumwe na ufahamu au vigezo vya wale tunaowahudumia, ila kwa kila tunayemuhudumia bila kujali anatujua au la.

Hivyo leo Mama Kanisa anavyosherehekea siku ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, anasadifu ukweli huu, yaani watu hawa walikuwa ni MAJITU YA SIFA, katika maana ya kwamba waliyatoa maisha yao bila kujibakiza pasipo woga wowote. Ingawa sitazama sana katika wasifu wa Petro na Paulo Mitume, ila historia ya maisha yao inaonyesha jambo hili. Petro anajulikana zaidi kama kiongozi na mwakilishi wa Kristo katika kundi la wale wa mwaminio Kristo na kuyaishi maagizo yake. Paulo anasimama kama mmisionari shupavu aliyeyafanya yote ndani na kwa ajili ya Kristo. Hivyo leo Kanisa linasheherekea zawadi ya maisha yao katika kutenda na kulisimamie lile alilolianzisha na kuliacha Kristo, na kulipeleka duniani kote kama Kanisa la kimisioni.

Ni wazi watu hawa wawili yaani Petro na Paulo wanayafanya mambo haya makubwa katika maisha yao kwanza kwa kujitambua wao wenyewe, na pili kuishi utambuzi huo katika kukutana na Kristo kila siku. Ukomvu wao wa Imani ni matokea ya kumtaabikia Kristo kila siku katika kuutoa ushuhuda wa kweli. Somo la kwanza linaeleza kwa undani ni kwa namna gani Petro aliutoa ushuhuda huo bila woga. Mwisho anasema maneno haya baada ya kutoka gerezani kwa miujiza. “Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi,” Mdo 12:11. Ufahamu huu kwa Petro hauna tena shaka juu ya kile anachokiamini.

Injili ya leo kwa namna nyingine inatupa wasifu wa Petro kwa undani na kutuelekeza nini hasa maana ya kiti chake na nafasi yake kati ya Mitume. Mtume Petro ndiye pekee aliyejibu swali ya Yesu kwa ufasaha, licha kwamba kwa mujibu wa Yesu jibu lile ni ufunuo kutoka kwa Mungu. Yesu anapowauliza wanafunzi wake, Je, watu wanasema kuwa mimi ni nani, Petro anajibu baada ya ukimya mkuu: “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16. Yesu anaridhika na jibu hili, na hapo hapo anamnyenyekesha Petro kwa kusema, “Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 16:17. Ufahamu huu wa Petro, na kufunuliwa huku kwa siri hii juu ya Kristo, kunamhesabia haki juu ya kiti kile alichokikalia hadi leo, Petro kama halifa wa kwanza, na Mababa watakatifu waliomfuata kama maalifa wa Kristo. Yesu mwenyewe anaweka kiti hiki rasmi kwa kusema, “wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18. Wapendwa, Kanisa letu linamisingi yake. Moja ya misingi yake hiyo ni uongozi Imara usio wa yumbishwa.

Wapendwa, baada ya kuwekwa rasmi kiti hicho kama alama ya uongozi imara kichungaji, anayekalia kiti hicho anapewa mamlaka kamili juu ya wale watakao kuwa chini ya uongozi huo. Yesu anayatoa mamlaka hayo kwa kusema, Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni,” Mt 16.19. Kwa kupitia kiti na mamlaka haya, Kanisa linakuwa rasmi chombo cha msamaha na huruma ya Mungu. Kanisa pia linapewa mamlaka ya kufundisha, kuonya, kukataza na hata kufungia yale yanayoenda kinyume cha Imani na ufuasi wa Kristo.

Ndugu yangu, chuma kinapoitwa “Iron Still,” kimepita katika moja mkali sana. Uimara wa chuma hiki ni tokeo la chuma hicho kuvumilia joto hilo kali bila kupoteza uhasilia wake. Mitume, na hasa Petro na Paulo ambao leo Mama Kanisa anawasherekea, walitaabika vya kutosha kuhusu jina la Yesu. Somo la Pili linaeleza kwa undani mahangaiko na taabu alizozipata Mtume Paulo. Mtume Paulo anasema kama ni vita ameishinda na mwendo ameumaliza. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda,” 2Tim 4:7. Faida kubwa aliyoipata katika utume wake huo wa pekee ni kuilinda Imani ambayo si kwa faida yake mwenyewe, bali kwa Kanisa zima. Msingi wa maisha ya Mtume Paulo ni kauli mbiu yake hii: “kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.” Flp 1:21. Hii ni hatua ya juu kabisa kwa mfuasi wa Kristo. Hapa ni kuishi kile unachokiamini na kukubali kuyapata yote kutokana na imani hiyo.

Wapendwa wana wa Mungu, hatua aliyoifikia mtume Paulo ni hatua ya kutokutishika na jambo lolote. Ni hatua ya kuishinda hofu na kuukumbatia uzima wa milele ingawa tunajua wote lazima tutakufa. Ni kujiachia katika mikoni ya Kristo, na kuacha yeye atende kadiri apendavyo. Ni kutokuwa na shaka yoyote juu ya: sababu ya kuja kwake Yesu Kristo kwetu, kuteseka kwake, kusulubiwa kwake, kifo chake na ufufuko wake. Mtume Paulo analiweka fumbo hili kwa maneno haya: Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina,” 2Tim 4:18. Je, ninaweza kuyatamka maneno haya bila hofu yoyote ninapokabiliwa na changamoto za maisha yangu ya kila siku? Ndugu yangu Utume si lelemama, bali kuvumilia hadi ushindi wa milele.

Tumsifu Yesu Kristo!


WATAKATIFU PETRO NA PAULO MITUME, MTUOMBEE. AMINA.

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 13 YA MWAKA-B

JUMATATU WIKI YA 13 YA MWAKA-B
29/6/2015
Somo: Mwa 18:16-33
Zab: 102:1-2, 3-4, 8-9, 10-11
Injili: Mt 8:18-22
Nukuu:
Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu?” Mwa 18:23

“Bwana akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao,” Mwa 18:26

Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi?” Mwa 18:32a

"Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi,” Mwa 18:32b 

Basi Bwana alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake,”Mwa 18:33

Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako,” Mt 8:19

Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake,” Mt 8:20

Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu,” Mt 8:21

Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao,” Mt 8:22

TAFAKARI: “Okoa nafsi yako na wenzako kwa kuishi kadiri impendezavyo Mungu.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, ni kweli kwamba hatupo ulimwenguni humu kwa bahati mbaya. Tupo ulimwenguni humu kwa malengo ya Mungu kila mmoja kadiri ya wito wake. Pamoja na malengo hayo mazuri ya Mungu, uwepo wetu hapa duniani ni mwendelezo wa ukombozi wa kila mmoja wetu kwa nafasi yake binafsi, na kwa upande wa pili kila mmoja wetu kwa ukombozi wa wingine. Hivyo kwa lengo hili la pili, Mtume Paulo anasema, Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine,” Flp 2:4. Somo la leo linatuelekeza kuyatafakari makuu haya. Wokovu si tendo tu lenye kubeba maana ya mtu mmoja aliye mwema, bali kwa yule mwema mmoja katikati ya waovu Mungu huwa na huruma kwa kundi HILO.  Hapa ndipo kulipobeba maana ya swali ya Ibrahimu na jibu la Mungu. Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu?” Mwa 18:23. Mungu anamjibu Ibrahimu na kusema, “Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao,” Mwa 18:26.

Ukweli ni kwamba Mungu hututakia mema kila siku na hapendi tuangamie kwa jambo lolote. Tumepewa uhuru wa kufanya lililo jema, na hata kwenda kinyume cha yale yasiyompendeza Mungu. Ni kwa uhuru huo huo tunaweza kumrudia Mungu kwa toba na majuto. Mungu anatujua jinsi tulivyo na yupo tayari kutupokea jinsi tulivyo. Ibrahimu anazidi kumdadisi Mungu na kupima uwezo wake wa kusamehe. Mungu anaonyesha hana kigezo chochote cha kusamehe ilihali muhusika yupo tayari kuiacha njia yake mabaya na kumfuata. Ibrahimu hachoki mdadisi Mungu kuhusu huruma yake. Naye akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi?” Mwa 18:32a. Mungu anaweka msimamo wake wazi na kumjibu Ibrahimu, “Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi,” Mwa 18:32b. Je, tunasababu yoyote kupata adhabu ya Mungu kwa mwelekeo huu wa Mungu kuwa tayari kusamehe makosa yetu?

Sodoma na Gomora ni miji iliyosikika kwa kutokuishi maadili mema. Kulikuwa na kila aina ya dhambi. Ukimya wa Mungu siyo kwamba hakuona maovu hayo, bali Mungu anatuamini kwamba ukweli utatuweka huru tunapogundua na kuacha njia zetu mbaya. "Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” Yoh 8:32. Kweli hii ndiyo tunayoitafuta kila siku ya maisha yetu kila mmoja na wito wake. Kwa “Kuwa” utawani, au maisha ya ndoa kama yalivyo haitoshi, ila kuuishi ukweli wa maisha hayo kama yalivyo ndio kunakoleta utofauti. Wapo tulioingia mifumo hiyo ya maisha kama yalivyo na mwisho wa siku tumejikuta ni watupu kabisa. Kumbe yanipasa kila siku kuuutafuta ukweli juu ya maisha hayo na kuuishi ukweli huo kila siku, na majira yote.

Hili ndilo analolizungumzia Yesu katika Injili ya leo. Si swala la kumfuata popote Yesu aendapo, ila kujua nini maana ya kumfuata Yesu, na matakwa yake. Kumfuata Yesu kadiri ya injili ya leo ni “KUACHA” utaratibu na matamanio tuliyoyazoea. Kauli ya kutangaza nia ya kumfuata Yesu ni rahisi sana kama anavyojinadi mwandishi huyu, na kusema, Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako,” Mt 8:19. Akilijua hilo ni jambo rahisi kutamka kama nia, Yesu anamjibu mwandishi huyu, “Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake,” Mt 8:20. Kwa maana nyingine Yesu anataka kumwambia jambo hili: je, upo tayari kuyaacha mazuri haya ya ulimwengu na ufahari wake wote,  na kuwa tayari kutaabika na kudharauliwa kwa sababu yangu? Hapa ndipo tunaposhindwa wengi. Ni sawa na kusema, “utawa ninaupenda, ila ufukara siupendi.” Ni sawa na kusema, “maisha ya ndoa nayapenda, ila uzazi siupendi.” Huu ni mkanganyiko wa hali ya juu.

Kumfuata Yesu Kristo inamaanisha pia kujibadua kutoka katika mnaso wa mazoea, au uhasilia. Hapa yatupasa kujipanga vizuri katika hatua hii. Wengi tumeshindwa kujibabanua na kujibandua kutoka mnaso wa kiasili tuliokuwa nao kutokana na uhasili wa maisha yetu kama binadamu. Hakuna kati yetu aliye kisiwa wala aliyedondoka kama mana jangwani. Sote tumetoka katika familia, na familia hizo zinaushawishi mkubwa kuhusu hatma ya maisha yetu ya kila siku. Ila leo Yesu anasema JIMAMANUE NA JIBANDUE KUTOKA JELA HIYO.  Mnaso huu utupelekea kujiuliza moja ya maswali haya ya kifamilia tunayoyaishi kila siku. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu,” Mt 8:21. Ni hekima na busara pia kwenda kuwazika wazazi na hata kuwahudumia hadi siku ya mwisho ya maisha yao kadiri ya amri ya nne, “waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,  upate heri, ukae siku nyingi katika dunia,” Efe 6:2-3. Ila Yesu anatupa jibu la uhakika tunapoamua kumfuata. Yesu anasema, “nifuate; waache wafu wazike wafu wao,” Mt 8:22.” Hatukatazwi kuwazika wazazi wetu, bali tunaonywa kuwa “mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria,” Gal 5:18. Je, ndugu yangu wewe unaongwa na nini?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUFUNULIE FUMBA LA MAISHA YA WAKFU KILA SIKU. AMINA

sábado, 27 de junio de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 13 YA MWAKA-B

JUMAPILI YA 13 YA MWAKA-B
28/6/2015
Somo I: Hek: 1:13-15, 2: 23-24
Zab: 29:2, 4, 5-6, 11, 12a, 13b
Somo II: 2Kor 8:7-9, 13-15
Injili: Mk 5:21-43
Nukuu:
“Yaani, Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea,” Hek 1:13

“Kwa maana aliviumba vitu vyote ili vipate kuwako, na nguvu za uzazi zilizomo ulimwenguni ni za kuleta siha, wala hakuna ndani yake sumu yoyote ya uharibifu, wala ahera haina milki kama ya kifalme hapa duniani,” Hek 1:14

Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9

bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe sawasawa,” 2Kor 8:14

Kama ilivyoandikwa, Aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa,” 2Kor 8:15 

Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi,” Mk 5:22-23

Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona,” Mk 5:25-28

Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena,” Mk 5:34

Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu,” Mk 5:36

Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana,” Mk 5:40

Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka,” Mk 5:41

TAFAKARI: “Umeumbwa uishi milele, liguse vazi la Yesu, Inuka.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya kumi na tatu ya mwaka “B” wa Kanisa. Masomo yetu yote matatu ya leo yanalenga katika fundisho hili: “Umeumbwa uishi milele, liguse vazi la Yesu, Inuka.” Wapendwa wana wa Mungu, nikuombe basi tusafiri wote katika tafakari hii yetu ya leo. Mungu anakupenda na mara zote haachi kukuwazia mazuri.

Mauti ni kati tukio kubwa linalomtia hofu mwanadamu. Tunapata hofu kwa sababu hatujui kule tuendako, na hata habari tuambiwazo kuhusu huko tuendako hatuzisadiki. Ndugu yangu, hakuna ukweli na uhakika wa kule tuendapo zaidi ya ukweli wa sadaka ya Bwana wetu Yesu Kristo pale Msalabani. Kwa kifo chake msalabani, mauti haina nguvu tena juu ya maisha yetu. Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo,” Rum 5:17. Ndani na katika Kristo hatuna hofu tena kuhusu mauti. Kifo chetu leo, na kwa yeyote yule anayemwamini Kristo, na kuishi kadiri ya imani hiyo, kifo kimebaki kuwe ni mlango tu wakuelekea kule tulipoandaliwa, yaani uzima wa milele. Ni kwa sababu hii, “Yaani, Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea,” Hek 1:13. Wewe na mimi tumeumbwa ili tuishi milele.

Uthibitisho wa jambo hili, yaani tumeumbwa ili tuishi milele, ni uumbaji wa huu ulimwengu na uratibishaji wake ulio wa namna ya pekee kabisa. Mazingira la ulimwengu huu, yaani sayari tunayoishi, yameandaliwa kwa makusudi makubwa ya uhai wetu. “Kwa maana aliviumba vitu vyote ili vipate kuwako, na nguvu za uzazi zilizomo ulimwenguni ni za kuleta siha, wala hakuna ndani yake sumu yoyote ya uharibifu, wala ahera haina milki kama ya kifalme hapa duniani,” Hek 1:14.  Ila dunia hii ni mahali tu pa maandalizi ya ule uzima wa milele. Hapa siyo makao yetu ya kudumu. Ni kweli kabisa twapaswa kuufanya ulimwengu huu uendelee kuwa sehemu salama ya kuishi, ila siyo mwisho wa kila kitu. Twapaswa kujiandaa vizuri tukiwa hapa duniani, ila hatupaswa kuwekeza nguvu zetu zote hapa duniani kama ndiyo sehemu yetu ya kudumu. Tupo safarini, tunapita kuelekea kule tulipoandaliwa, yaani maisha ya umilele.

Uzima huu wa milele ambao ndiyo shabaha yetu tungali hapa duniani, tunaweza kuufikia kwa neema ya Kristo mwenyewe. Licha ya kwamba wale wasiomjua Kristo bado waweza kuokolewa kwa dhamiri zao safi wangali hapa duniani, tendo la kuongozwa katika dhamiri iliyo safi ni neema au zawadi kutoka kwa Mungu. Haya si mastahili yetu binafsi. Kwa upande wako na mimi tunayemjua Kristo na kujaribu kuishi kadiri ya matakwa yake kila siku, twaitaji Neema yake. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Hakika huu ni upendo wa ajabu sana kwetu kwa kufanywa matajiri kwa Kristo kukubali kuwa masikini.

Umasikini wa Bwana watu Yesu Kristo uliotupatia utajiri wetu mwili na roho, unatuwajibisha kwa tendo hilo hilo kufa kila siku kwa ajili ya wengine. Kila mmoja wetu kadiri ya wito na vipaji vyake alivyopewa bure, yampasa kupungua pale alipo ili uhai uongezeke pale alipo. Tunakufa kwa ajili ya wengine si kama adhabu au kujionyesha kwamba tunaweza, bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe sawasawa,” 2Kor 8:14. Haya ndiyo maisha ya kisadaka tuyapasayo kuyaishi kila siku kama Wakristo, na wenye hofu ya Mungu.

Ndugu yangu, ukweli ni kwamba hakuna aliyefilisika kwa kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Kadiri tujitoavyo sadaka bila kujibakiza ndivyo kwa namna hiyo hiyo tunaongezewa pale tulipojitoa bila kujibakiza. “Aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa,” 2Kor 8:15. Hii ndiyo maana halisi ya sadaka ya Kristo pale msalabani, na fundisho kwa wale wote wamwaminio.

Injili yetu ya leo inaeleza kwa upana fumbo sababu ya kuumbwa kwetu na dhamiri mzima ya Mungu juu ya kuumbwa kwetu. Tumeumbwa tuishi milele, hivyo yatupasa kuligusa vazi la Yesu, na mara zote kuinuka kama ishara ya uhani ndani mwetu. Yesu anaanza safari yake kwa kupata taarifa ya kuzidiwa kwa mtoto wa Mkuu wa sinagogi. Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi,” Mk 5:22-23. Yesu anapokea wito huo, na akiwa njiani tazama mwanamke mwenye ugonjwa wa kutoka damu kwa muda wa miaka kumi na mbili, anapata uponyaji na msiba wake kutoweka.

Uponyaji wa mwanamke huyu ni tokeo la msukumu wa Imani wa kulishika vazi la Yesu.Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona,” Mk 5:25-28. Je, vazi la Yesu leo ni lipi?

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna shaka kabisa leo katika Kanisa vazi la Yesu li hai na lina nguvu sana. Vazi la Yesu katika Kanisa leo ni neema na uponyaji tuupatao kupitia masakaramenti yake, na wahudumu wake waliowekwa wakfu kwa sababu hiyo. Hizi ndizo chemichem za uhai na uzima. Je, ni mara ngapi nashiriki neema hizi? Kama ninavyovikwazo, ninampango ngani kuondokana na vikwazo hivyo? Je, nitaishi hivi hadi lini katika hali hii ya kufa na msiba huu?

Baada ya uponyaji wa ajabu wa mwanamke huyu, hatua iliyofuata ni kujisalimisha mbele ya Yesu. Kujisalimisha kwake mbele ya Yesu, kunamhesabia haki ya uzima wa milele. Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena,” Mk 5:34. Ndugu yangu, katika hatua mbalimbali za maisha Yesu ametuponya kwa kujua au kutokujua, ila hakuna hata mara moja tumejisalimisha kwake. Je, kujisalimisha kuna maana gani?

Kila mtu hatimaye hujisalimisha kwa mtu au kitu fulani. Kama sio kwa Mungu, utajisalimisha kwa matarajio au maoni ya watu wengine, au pesa, chuki, hofu, au kwa kiburi chako au tama mbaya, au ubinafsi. Ulibuniwa kumwabudu Mungu-na kama utashindwa kumwabudu, utatengeneza vitu vingine (sanamu) ili uvipe maisha yako. Unao uhuru wa kuchagua usalimishe maisha yako, lakini huko huru na matokeo ya uchaguzi huo. E. Stanly Jones alisema, “kama hutajisalimisha kwa Kristo, utajisalimisha kwa machafuko.” Kujisalimisha si njia bora tu ya kuishi; bali ni njia pekee ya kuishi. Hakuna kitu kingine cha kukufanikisha. Njia nyingine zote hukuongoza kwenye kukukatisha tamaa, na kuziangamiza nafsi. Tafsiri ya King James huita kujisalimisha “huduma yenu yenye maana.” Rum. 12:1 Tafsiri nyingine inasema,  “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana,” Rum 12:1. Kusalimisha maisha yako si hisia za kipumbavu lakini ni tendo la akili na busara ambalo unaweza kulifanya kwa ajili ya maisha yako. Ndiyo maana Paulo alisema, “Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye,” 2Kor 5:9 Nyakati zako za busara zitakuwa zile ambazo unasema ndiyo kwa Mungu.

Wapendwa katika Kristo, baada ya mwanamke huyu kujisalimisha na kupokea uzima, Yesu anapewa taharifa ya kule aendapo kwamba binti yule aliye mgonjwa kesha fariki. Kristo anavunja hofu yetu juu ya umauti na kusema, “Usiogope, amini tu,” Mk 5:36. Tunaamini kwamba uzima wapatikana kwa Kristo tu. Huyu ndiye Bwana wa Uhai. Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai,” Mt 22:32. Hata hivyo waliokuwa kwenye msiba hawasadiki maneno haya ya Yesu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana,” Mk 5:40. Yesu anathibitisha kweli hii leo kwamba, kifo siyo mwisho wa kila kitu. Hivyo hakuna sababu ya kuogopa, bali “kuamini tu.”

Ndugu yangu, tunapokwelekea Kristo katika majonzi na dhiki zetu huyafuta machozi yetu na kuturudishia furaha ya kweli. Fuhara hiyo ndiyo hii; INUKA! Kwa maana nyingine “TOKA KWENYE KABURI HILO,” na uwe huru. Hivyo Yesu akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka,” Mk 5:41. Yesu leo anakuambia wewe na mimi INUKA! Yesu anatuambia tumwamini na wala tusiogope. Uzima tuutamanio ni kwa Kristo tu twaweza kuupata.

Zebedayo ambaye alijulikana kwa jila la “kadogoo,” alileta hofu kubwa kwa majirani zake kwa ujambazi wake uliokithiri. Alikoswa mara nyingi kuchomwa moto, na hata kupigwa risasi. Alishawahi kufungwa mara nyingi tu, hata hivyo hakuona sababu ya kuacha ujambazi wake.

Siku moja usiku alivamia nyumba mtaa wa jirani kwa lengo la kuiba dhahabu. Alifanikiwa kuingia hadi ndani na kwa bahati nzuri au mbaya siku ile kulikuwa na mama mwenye nyumba tu. Mama huyu aliingiwa na hofu kumwona Kadogoo akiwa ndani na amebeba Bastola. “Nataka zile dhahabu mara moja, la sivyo ujiandae kufa,” Kadogoo alisema bila kupepesa macho. “Dhahabu utapata zote, je, leo ushakula chakula?” Mama mwenye nyumba alimjibu kwa ujasiri. “Sikuja hapa kuhubiri injili, nipe dhahabu zangu nisepe kabla kiwingu hakijatanda hapa,” Kadogoo alimjibu kwa hasira.

Hivyo mama yule alichukua dhahabu yote iliyokuwa kwenye kabati na kumkabidi. Kadogoo akiwa anataka kuondoka, Mama yule alimwita na kumwambia, “Hapa pia nina laki nane naona zitakusaidia.” Kadogo alipokuwa anapokea fedha zile, mara moja mama yule alimtengea chakula kilichokuwepo na kumwambia, “Kula ushibe na ujue Mungu anakupenda kama ulivyo.”

Kadogoo alimwangalie yule Mama kama dakika tano hivi bila kusema chochote, na mwisho akafungua kinywa chake na kusema, “siwezi kukumbuka ni lini nilianza kuimba na hata kuwadhuru watu kwa kuchukua vilivyo vyao kwa nguvu. Pia, sijawahi kukutana na mtu aliye jasiri kama wewe ambaye umeweza kuniambia kitu ambacho sijawahi kuambiwa hata na mzazi wangu aliyenizaa. Hivyo naomba niondoke kama nilivyokuja.”

Mara Kadogo aliacha zile dhahabu na fedha na kuondoka. Kuanzia siku ile Kadogo alipita kwa kila aliyemtendea vibaya na kuomba msamaha. Hivi leo Kadogo ni mmoja wa viongozi wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Je, ni mara ngapi tuna mwona Kristo kwa wale ambao kwa tabia zao tumeshawatenga? Mama huyu amekuwa sababu ya uzima kwa Kadogoo, kwa kuthubutu kulitenda tendo lile la Yesu-INUKA! Ni kwa kuwagusa wengine ambapo hawajawahi kuguswa twawapatia uzima wa kweli.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU NIPE UZIMA WAKO WA KWELI KILA SIKU, NA NIFANYE SABABU YA UPONYAJI NA UZIMA KWA WENGINE. AMINA