KIPINDI CHA NOELI
JANUARI 3
Somo: 1Yoh 2:29-3:6
Zab: 98:3cd-4, 5-6
Injili: Yoh 1:29-34
Nukuu:
“Kama
mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa
na yeye,” 1Yoh 2:29
“Tazameni,
ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo
tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye,”
1Yoh 3:1
“Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba,
Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla
yangu,” Yoh 1:30
“Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu
ni Mwana wa Mungu,” Yoh 1:34
TAFAKARI:
“Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu,”
Wapendwa
wana wa Mungu, kweli juu ya Kristo na mafundisho yake upenya kwenye mioyo yetu
na kutufanya tujisute nafsi zetu. Kule kote tunapojaribu mbadala wa maisha
tunajikuta tukigonga ukuta kwa sababu maisha ya Mkristo bila Kristo ni maigizo
tu yasiyokuwa na uhalisia wa mambo. Maisha ya mtindo huo yanaakisi mambo makuu
mawili;
Moja,
ni kuasi ikiwa ni tokea la dhambi kama asemavyo Mtume Yohana: “Kila atendaye
dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi,” 1Yoh 3:4. Hali hii ututenga na
kile cheo chetu kilicho cha thamani kuliko vyote, yaani, utakatifu wako. Ni kuishi pasipo tumaini la kweli ambalo
ndani na katika Kristo Yesu tunatakaswa kwa sababu Yeye ni Mtakatifu. Hivyo “kila mwenye matumaini haya katika yeye
hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu,” 1Yoh 3:3.
Jambo
la pili ni kuishi kile tusichokijua ilhali twajiita Wakristo wa majina tu. Na
hali hii pia chanzo chake ni dhambi, uasi. Ni kuishi Ukristo huria. Ukristo
usiojali wala kuwajibika. Ila kuwa na
hofu ya Mungu na kukaa ndani na katika Kristo Yesu ni kuishinda dhambi, kumwona,
na kumtambua Kristo. “Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye
dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua,” 1Yoh 3:6
Na
ukweli ni kwamba, “hakuna wokovu katika
mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa
wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:12. Pamoja ya yote tuyapatayo
kwa kusoma tauhidi/teolojia na falsafa, kutuwezesha kufahamu fumbo hili la
Mungu kujifunua kwa binadamu, jambo moja ambalo sina mashaka nalo ni maisha
baada ya kifo.
Ndugu
yangu, wote waliokuja kabla na baada ya Kristo na kuanzisha mifumo ya kimaisha,
walikufa. Ni Kristo mwenyewe aliyekufa na kufufuka. Ni kwa Kristo tu tunapoweza
kujifunza siri ya kifo na maisha baada ya kifo hiki kinachotukabili muda wowote
wa maisha yetu. Huu ndiyo upendo wa Mungu Baba kwetu sisi wanadamu kwa kumtoa
mwanaye mpendwa kufa kwa ajili ya dhambi zetu. Kifo cha mwanaye mpendwa ndiyo
sababu ya thamani yetu leo mbele ya Mungu na kuwa warithi wake.
Thamani
hii mbele ya Mungu inagharamu zake. “Tazameni,
ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo
tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye,”
1Yoh 3:1. Gharama hii mbele ya Mungu ni kukataliwa na ulimwengu kama
alivyokataliwa Kristo. Leo wakristo wengi sehemu mbalimbali wanatengwa na kuuwa
kwa sababu ya Kristo.
Furaha yetu ni kwamba
tunaye mchungaji mwema anayetuthamini na kutujua si tu kwa majina yetu, bali
hata mahitaji yetu. “Mimi ndimi mchungaji
mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo,” Yoh 10:11.
Ameutoa uhai wake kwetu na anautoa kila mara tunapoisikia sauti yake. Kristo
hatotuacha kamwe wala kujitenga nasi yatakatopotokea majanga kwetu tukiwa na
imani naye na katika njia pamoja naye. “Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye
kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia;
na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya,” Yoh 10:12. Yesu Kristo kwetu si mtu
wa mshahara wala mwajiriwa fulani ambaye hulipwa kwa kazi yake.
Kristo kwetu ni yote na
katika yote. Kama ashuhudiavyo Yohana Mbatizaji: “Huyu
ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa
mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu,” Yoh 1:30. Anatupenda kama
tulivyo na amekubali na yupo nasi muda wote ili tufahamu upendo wake kwetu. “Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu
nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama
vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya
kondoo,” Yoh 10:14-15. Taswira ya upendo huu wa Kristo kwetu ndiyo kielelezo
cha uchungaji wake kwetu.
Uchungaji huu wa Kristo haubagui wale wasiopenda ulishaji wake. Huduma
anayotoa Kristo habagui hata wale wanaompinga. Hivyo yupo kwa ajili ya wote kwa
wakati wote. Kujitenga na Kristo ni kukataa upendo wake anaotupa bure wakati
wote. Kristo analitambua jambo hilo na anasema,
“Na kondoo wengine ninao, ambao si
wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha
kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja,” Yoh 10:16. Ni mara ngapi tunawatenga
wale ambao wanapingana na mawazo yetu hata ikiwa kwa nia nzuri?
Ndugu yangu katika
Kristo, na wale wote tuliopewa dhamana na Mama Kanisa kama viongozi, tujifunze
unyenyekevu wa Yohana Mbatizaji. Yohana Mbatizaji aliyafanya yote kadiri ya
hali na nafasi yake kama mwandaaji njia. Yohana Mbatizaji hakupindisha kweli
hii ili ajikweze mwenyewe. Naye anasema, “wala
mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja
nikibatiza kwa maji,” Yoh 1:31. Siri ya yule anayeandaliwa njia, yaani, Kristo
Yesu, inafunuliwa kwa mwandaaji njia, Yohana Mbatizaji. Naye anasema, “wala
mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia,
Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa
Roho Mtakatifu,” Yoh 1:33. Huu ni unyenyekevu wa hali ya juu.
Kujishusha
na kujinyenyekeza kwa kutambua ukomo wa maisha yako ni njia na wezekano la
kufunuliwa mamba kubwa katika maisha yako. Ni hatua ya kukua kiimani, na
baadaye kuwa msingi imara wa imani isiyotetereka. Na hili linaonekana wazi kwa
Yohana Mbatizaji kama asemavyo, “Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu
ni Mwana wa Mungu,” Yoh 1:34. Yohana Mbatizaji hana shaka juu ya ufunuo huu wa
Kristo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kama mkijua ya
kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye,”
1Yoh 2:29
Tusali: Ee Yesu Mwema,
tujalie nuru ya upendo wako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario