JUMATATU WIKI YA 3 YA MWAKA-I
Somo:
Ebr 9:15, 24-28
Zab:
98:1, 2-3ab, 3cd-4, 5-6
Injili:
Mk 3:22-30
Nukuu:
“Na kwa sababu hii ni
mjumbe wa agano jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa
yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa
milele,” Ebr 9:15
“Kwa sababu
Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa
patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu
kwa ajili yetu,” Ebr 9:24
“kadhalika Kristo naye,
akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara
ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu,” Ebr 9:28
“Nao waandishi
walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, Kwa mkuu wa pepo
huwatoa pepo,” Mk 3:22
“Akawaita, akawaambia
kwa mifano, Awezaje Shetani kumtoa Shetani?” Mk 3:23
“Amin, nawaambia,
Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu
hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele,” Mk 3:28-29
TAFAKARI:
“Mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele.”
Wapendwa wana Taifa la
Mungu, hakuna yeyote kati yetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe. “Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana;
naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa
Bwana, naye pia amshukuru Mungu. Kwa
sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa
nafsi yake. Kwa maana kama
tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama
tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:6-8. Ni katika mazingira
haya kwamba hakuna kilicho mali yetu wenyewe isipokuwa dhambi zetu. Hivyo
unapofikia hatua ya kukata tamaa na kutokuona msaada wowote kutoka kwa
aliyekuumba, ni kumkufuru Roho Mtakatifu ambaye ndiye mfariji wetu na mwenye
kutuunganisha katika umoja ule Mungu Baba anaoutaka tuwe nao. Roho Mtakatifu
ndiye ayatakatifuzaye yote yaliyoumbwa na Mungu Baba, ukiwemo ulimwengu huu
tunaoishi wenye shida na raha zake.
Ndugu yangu unayesafiri
nami katika tafakari hii, elewa kwamba kukata tamaa kwa jambo lolote lile na
kutokuona nguvu, upendo, msamaha, na huruma ya Mungu kwa kile kinachokusibu, ni
kumkufuru Roho Mtakatifu. Yesu analiweka wazi jambo hili na kusema, “Amin,
nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru
zote; bali mtu atakayemkufuru
Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele,” Mk 3:28-29. Kama unajua wakati fulani ulifanya
ndivyo sivyo na kumkosema Mungu na jirani yako na huoni sababu ya kupokea
huruma hii ya Mungu isiyo na kipimo ni kumkufuru Roho Mtakatifu. Hiyo siyo
furaha ya Mungu hata kidogo. “Mtafuteni
Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu
asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa
Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa. Maana
mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana,” Isa
55:6-8. Mungu wetu siyo Jitu katili lenye kusubiri kutuadhibu pale
tunapodondoka katika dhambi. Hali letu ya dhambi inamuumiza sana Mungu kwa
sababu ndani yetu ipo chapa yake. Tumeumbwa kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27.
Kwa kutenda dhambi na kukaa katika hali ya dhambi hatumwakilishi Mungu. Tunajiwakilisha
wenyewe. Ila huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.
Ndugu yangu unayemwamini Kristo elewa
umekombolewa kwa damu yenye gharama kubwa. Ukristo wako ni wathamani sana.
Hakuna sababu ya kujiona mnyonge hata kidogo. “Na
kwa sababu hii ni mjumbe wa agano jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa
kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao walioitwa waipokee
ahadi ya urithi wa milele,” Ebr 9:15
Wewe
na mimi tunawewa angalizo linatuelekeza pia kumtazama vizuri Kristo katika
maisha yake na sadaka ya maisha yake aliyoitoa bila kujibakiza. “Kwa
sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano
wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu
kwa ajili yetu,” Ebr 9:24. Ndani na katika Kristo kuna uondoleo la dhambi zetu
na ukombozi kwa sadaka yake pale msalabani. “Kadhalika Kristo naye, akiisha
kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya
pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu,” Ebr 9:28. Je, unacho
chochote cha kujivunia zaidi ya dhambi zako?
Wapendwa
katika Kristo, kama yote mazuri ni mali yake Mungu, kilicho chetu ni dhambi
zetu wenyewe. Na kama tulivyo navyo ni mali ya Mungu, basi yatupasa kumtolea
kile kilicho bora zaidi hata katika umasikini wetu. “Maana
walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao
uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao,” 2Kor 8:2. Huku ndiko
anakokuzungumzia Mtume Paulo kupanda kwa ukaribu na kuvuna kwa ukaribu, na
kupanda haba na kuvuna haba. “Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna
haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu,” 2Kor 9:6. Hatupaswi kuutazama
udogo na umasikini wetu katika kutoa kama tendo la ukarimu na la Ibada.
Kuangalia udogo ulio nao na umasikini wako katika kutoa ni kujifungia neema na
baraka za Mungu. Hakuna Masikini asiyekuwa na kitu cha kumpa Mungu, na hakuna
Tajiri asiyekuwa mwitaji.
Wapendwa
katika Kristo, tuyafanyapo yote ndani na katika Kristo, hatuwezi kukosa msaada
wa Kristo kwa yale tuyafanyo hata kama tukiwa katika sintofahamu ya jambo
lolote lile. Naye Yesu anatuambia, “nanyi
mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao
na kwa mataifa. Lakini hapo
watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile
mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi
msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu,” Mt 10:18-20. Ndugu
yangu, kwa nini sasa unakata tamaa na maisha?
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Ni nani
atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au
njaa, au uchi, au
hatari, au upanga? Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda,
kwa yeye aliyetupenda,” Rum 8:35,37
Tusali:-Ee Yesu Mwema,
tuvishe katika bonde hili la uvuli wa mauti. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario