KIPINDI CHA NOELI
JANUARI 4
Somo: 1Yoh 3:7-10
Zab: 98:1, 7-8, 9
Injili: Yoh 1:35-42
Nukuu:
“Watoto
wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na
haki,” 1Yoh 3:7
“atendaye dhambi ni wa
Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu,” 1Yoh 3:8
“Katika hili watoto wa
Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki
hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake,” 1Yoh 3:10
“Akamtazama Yesu
akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu!” Yoh 1:36
“Yesu aligeuka,
akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana
yake, Mwalimu), unakaa wapi?” Yoh 1:38
“Akawaambia, Njoni,
nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa
yapata saa kumi,” Yoh 1:39
“Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama,
akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro,
au Jiwe),” Yoh 1:42
TAFAKARI:
Yesu akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi,
(maana yake, Mwalimu), unakaa wapi?” Yoh 1:38
Wapendwa
wana wa Mungu, kila mmoja wetu kwa kuishi kwake hapa duniani utafuta maana ya
maisha yake. Hata pamoja na ukweli huu, swali ni hili; yote uyafanyayo mwisho
wake nini? Yohane Mbatizaji akiwa na wanafunzi wake wawili anamwona Yesu kwa
mbali na kusema, “Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu!” Yoh
1:36. Kwa maneno haya, Yohane Mbatizaji anaona hitimisho la yote kwa Yesu. Huyu
ndiye tumtazamiaye na tumtafutaye kwa sababu kwake upo ukamilisho wote. Pamoja
na ukweli huu, Yesu anauliza swali la msingi kabisa, ‘Mnatafuta nini?’ Kwa
maana nyingine Yesu anataka kujua haya kutoka kwako na kwangu; pamoja na
mahangaiko uliyonayo nini msingi wa maisha yako? Nini kisukumacho maisha yako
na kufanya ufanyavyo? Na mwisho, nini hatma ya hayo yote? Maisha ya mtu yaweza
kuongozwa na hali zifuatazo ambazo kwa uhakika hali hizo hazitatupeleka kule
Yesu aliko na anapotaka tuwe.
1. Watu wengi huongozwa na hatia.
Watu hawa hutumia muda wa maisha yao yote wakiepuka
lawama na kuficha aibu. Watu wanaoongozwa na hatia wanaonewa sana na kumbukumbu.
Wanaruhusu mambo yaliyopita kutawala mambo yao ya usoni. Wanajiadhibu bila
kujua kwa kuharibu mafanikio yao. Kaini alipotenda dhambi, hatia yake ilimtenga
na Mungu, na Mungu akasema, "utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake;
utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani," Mwa 4:12. Hali na mazingira
haya yanaeleza jinsi watu wengi walivyo siku hizi-wanatangatanga katika maisha
bila lengo. Mfano mzuri angalia katika vyama vyetu vya kitume. Wapo na tena
walio wengi huama chama kimoja cha kitume kwenda kingine na mwisho huishia
katika nyumba za sala. Nyumba za sala hapa ninamaanishisha vijikanisa
vinavyojiibua na kujiinua kwa wachungaji wao kuwa manabii.
Ndugu yangu, sisi ni matokeo ya muda wetu uliopita
lakini hatupaswi kuwa wafungwa wa muda huo. Kusudi la Mungu halifungwi na muda
wako uliopita. Ona! Alimbadilisha muuaji Musa na kuwa kiongozi mzuri;
akambadilisha Gidioni aliyekuwa mwoga akawa shujaa na hodari; anaweza kufanya
mambo ya ajabu na maisha yako yaliyobaki. Tazama pia maisha ya
Mt. Augustino wa Hippo kabla na baada ya kuongoka kwake.
Mungu ni mtaalam wa
kutupa mawazo mapya. "Heri aliyesamehewa dhambi, na kusitiriwa makosa
yake," Zab 32:1. Kwa maana nyingine twaweza kusema, "wana furaha kubwa
wale waliosamehewa hatia zao. Na wana amani wale waliotubu dhambi zao na Mungu
amefuta mashtaka yao." Ni kwa Kristo tu tupo huru tunapoziungama dhambi
zetu. “Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye
alivyo na haki; atendaye dhambi ni wa
Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu,” 1Yoh 3:7-8.
2. Watu wengi wanaongozwa na chuki na hasira.
Wapendwa wana wa Mungu, kati yetu wapo wanaoshikilia
maumivu (machungu) bila kuyaacha. Badala ya kutoka katika maumivu kwa kusamehe,
wanaendelea kuyakumbuka katika mawazo yao tena na tena. Baadhi ya watu
wanaongozwa na chuki kutunza ndani uchungu wao, na wengine huwalipukia watu
wengine. Hali zote hizi si nzuri na hazisaidii maishani. Chuki mara nyingi
huleta maumivu kwako kuliko yule unayemchukia. Mtu aliyekukosea anaweza kuwa
amesahau lile kosa na anaendelea na maisha yake vizuri, wewe unaendelea kuumia
na kuhangaika na yaliyopita.
Sikiliza ndugu yangu: Wale waliokuumiza wakati
uliopita hawawezi kuendelea kufanya hivyo sasa "isipokuwa" kama
utaendelea kutunza uchungu. Yaliyopita yamepita! Hakuna kitakachoyabadilisha.
Unajiumiza tu na uchungu wako. Kwa ajili yako, jifunze kutokana na hilo na
kisha achana nalo. Maandiko matakatifu yanatukumbusha kuwa, "kwani hasira
humwua mtu mpumbavu, nao wivu humwua mjinga." Ayu 5:2. Kuwa na hofu kiasi cha kufa kwa sababu ya
uchungu ni upumbavu, ni kitu kipumbavu kukifanya. Ndugu, kwa nini wajifungia
katika tanuru hili? “Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa
Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala
yeye asiyempenda ndugu yake,” 1Yoh 3:10.
3. Watu wengi wanaongozwa na woga.
Ndugu, woga hapa unaweza kuwepo kutokana na jambo baya
sana lililokupata au lililowapata, matarajio yasiyotekelezeka, kukulia katika
jamaa isiyo na uhuru, au hata maumbile ya asili. Bila kujua sababu, watu
wanaongozwa na woga mara nyingi hupitwa na nafasi kubwa kwa sababu wanaogopa
kuchukua hatua. Badala yake wanajitahidi kuwa salama, wakiepuka hasara na hivyo
hujaribu kulinda hadhi yao. Woga ni kifungo ambacho mtu hujifunga mwenyewe na
chaweza kukuzuia kuwa mtu yule ambaye Mungu anapenda uwe.
Unatakiwa kutoka humo
kwa silaha ya IMANI na UPENDO. "Katika pendo hamna hofu; lakini pendo
lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu, na mwenye hofu
hakukamilishwa katika pendo." 1Yoh 4:18. Kwa maneno mengine, upendo halisi
huiondoa hofu kwa kuwa hofu hulemaza, maisha ya hofu-hofu ya kifo, hofu ya
hukumu- ni maisha ambayo hayajakamilika katika upendo.
4.
Watu wengi wanaongozwa na mali
Ndugu tupo pamoja?
Tamaa yao ya kupata vitu linakuwa ndilo lengo la maisha yao yote. Jambo hili
haijalishi upo utawani au kwenye maisha ya ndoa. Msukumo huu wa kutaka zaidi
kila siku una misingi yake katika udanganyifu wa kuwa nikiwa na vingi nitakuwa
na furaha zaidi, nitakuwa wa muhimu, na nitakuwa salama; lakini mawazo hayo
yote matatu si ya kweli. Mali huleta furaha ya "muda mfupi tu." Na
sababu kubwa ndugu yangu, vitu havibadiliki, hivyo vinatuchosha na tunataka
vipya, vikubwa, na bora zaidi.
Kuna imani pia kwamba
nitapata mali nyingi nitakuwa wa muhimu. Umuhimu wako na mali ni vitu viwili
tofauti. Thamani yako haitegemei mali zako, Mungu anasema kitu cha muhimu
maishani mwako si vitu! Imani ya watu wengi kuhusu fedha ni kwamba kuwa nazo
nyingi kutanipa usalama. Huwezi! Tulio utawani hatuchoki kuwa na tumiradi
binafsi twa siri twingiiii. Usicheke ndiyo ukweli kwa baadhi yetu. Mambo
yanapokwenda vibaya kwenye huto tumiradi tupresha twa kupanda na kushuka
hatukomi. Yesu anawaambia wale wafuasi wa Yohane Mbatizaji, “Mnatafuta nini?”
Wanafunzi wale wakamjibu, Rabi, (maana
yake, Mwalimu), unakaa wapi?” Yoh 1:38. Anapokaa Yesu ndipo kwenye usalama
kupita vitu vyote na hali zote tunazoweza kufikiria. Mt. Augustino anasema,
“mioyo yetu haitulii mpaka itakapotulia kwako Ee Bwana.”
Ndugu yangu, utajiri
unaweza kupotezwa mara moja kwa sababu zisizozuilika. Usalama halisi unaweza
kupatikana katika kile ambacho huwezi kunyang'anywa, yaani uhusiano wako na
Mungu. Mt. Augustino anatuwasa kutoka kwenye kanuni yake, "kuna furaha
kubwa kuwa na vichache kuliko kuwa na vingi." Hata hivyo tatizo hapa ni
kipimo cha huo uchache na huo wingi. Bwana wetu Yesu Kristo anatupa angalizo
kwa jambo hili, na kusema, "hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili;
kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu, ama atashindana na huyu na
kumdharau huyu: hamwezi kumtumikia Mungu na mali." Mt 6:24.
5.
Watu wengi wanaongozwa na kutaka sifa
Ndugu yangu, wakati
mwingine watu hawa wanaruhusu matarajio ya wazazi, waume, au wake, watoto,
waalimu au rafiki zao kutawala maisha yao. Watu wazima bado wanajaribu kupata
sifa kwa wazazi wao ambao hawajafurahi kamwe. Wengine wanasukumwa na vikundi
vya marafiki, wanahofu wenzao watawafikiriaje. Kwa bahati mbaya, wale wafuatao
kundi au maoni ya mtu binafsi hupotea ndani yake. Ndugu yangu, kwa nini
kujifungia katika gereza hili la fikra na maoni?
Ndugu yangu mpendwa
katika Kristo, sijui funguo zote za mafanikio, lakini ufunguo mmoja wa
kushindwa ni kujaribu kumpendeza kila mtu. Kutawaliwa na maoni ya watu wengine
ni njia wazi ya kukosa makusudi ya Mungu katika maisha yako. Kuna nguvu nyingi
zinazoweza kuongoza maisha yako lakini zote mwisho wake ni mfu: kutotumia
vipawa ulivyo navyo, mahangaiko ya moyo, na maisha yasiyo ya utoshelevu.
Ndugu yangu, kuishi
maisha yanayoongozwa na malengo, ni kutawaliwa, na kuelekezwa na makusudi ya
Mungu. Hakuna kitu cha muhimu zaidi kama kujua malengo ya Mungu kwa maisha
yako, na hakuna mbadala kwa hilo-siyo mafanikio, utajiri, kujulikana, au anasa.
Bila malengo, maisha ni mwendo usio na maana, shughuli bila mwelekeo, na
matukio bila sababu. Bila malengo, maisha ni kitu duni, kidogo sana, kisicho na
umuhimu wowote.
Wapendwa wana wa Mungu,
usalama wetu upo ndani na katika Kristo. Yesu leo anatuambia, “Njoni, nanyi
mtaona,” Wanafunzi wale wa Yohane Mbatizaji waliionja amani ya kweli kwa muda
ule waliofuatana na Yesu na kukaa naye jioni ile. “Wakaenda, wakaona akaapo,
wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi,” Yoh 1:39. Unapogundua
siri hii usiacha mshirikisha na mwenzako furaha hii iliyopo ndani na katika
Kristo kama alivyofanya Andrea kwa ndugu yake Simoni. “Huyo akamwona kwanza
Simoni, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi (maana yake,
Kristo),” Yoh 1:4. Kwa tendo hili la Andrea (ushirikishaji na upashanaji habari
njema kwa wengine), Kristo inaifunua siri juu ya Simoni na kumpa uthibitisho.
Andrea “Akampeleka (Simoni) kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u
Simoni, mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe),” Yoh
1:42. Alichokifanya Andrea ni wajibu wa
kila mbatizwa kuwapeleka wale wote wenye hofu ya Mungu kwa Kristo. Wewe
uliyesafiri nami katika tafakari hii una deni hili kubwa kwa Kristo. Anza leo
kwa kushirikisha ujumbe huu kwa wengine.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ikinibidi kujisifu, nitajisifia
mambo ya udhaifu wangu,” 2Kor 11:30
Tusali:
Ee Yesu Mwema, u amani, furaha, haki, na upendo ndani ya mioyo yetu na maisha
yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario