martes, 17 de enero de 2017

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 2 YA MWAKA-I


JUMATANO WIKI YA 2 YA MWAKA-I

Somo: Ebr 7:1-3, 15-17

Zab: 110:1, 2, 3, 4

Injili: Mk 3:1-6

Nukuu:

“Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki,” Ebr 7:1

“ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani,” Ebr 7:2

“hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele,” Ebr 7:3

 “Akaingia tena katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza; wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki,” Mk 3:1-2

 Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza,” Mk 3:4 

Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena,” Mk 3:5 

TAFAKARI: “Wewe u kuhani milele Kwa mfano wa Melkizedeki.”

Wapendwa wana wa Mungu, Mungu wetu hakufanya makosa kutuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Ni kwa namna hiyo ilimpendeza kutuumba na kuweka chapa yake ndani yetu nasi leo ni wanadamu. Ni kwa ubinadamu wetu huu hadi siku ya mwisho wa uhai wetu hapa duniani ndivyo Mungu anapenda tuwe. Ni tatizo kubwa sana pale tunapokataa ubinadamu wetu na kutaka kuwa kitu kingine. Binadamu anapoukataa ubinadamu wake anakuwa mbaya kuliko shetani. Hata wale Malaika waliomwasi Mungu walitaka kuwa zaidi ya kile walichoumbwa kuwa na hivyo wakageuka kuwa Mashetani.

Binadamu anapokataa kuwa kile alicho kadiri ya uwezo na mipaka ya Mungu aliyependezwa awe, na kibinadamu huyo kuchukua nafasi ya Mungu hugeuka kuwa Shetani. Huku ndiko kuasi kulikofanywa na Malaika. Ushetani wa mtu ni mtu mwenyewe! Shetani ni roho, kwayo yenyewe haiwezi kufanya chochote nje ya mtu bila kuikubali roho hiyo. Shetani kama roho-hasi. hufanya kazi ndani ya mtu kama mwezeshaji wa ile roho. Hivyo, “shetani wa mtu ni mtu mwenyewe.”

Mara nyingi kinachotuponza kutokuukubali ubinadamu wetu na mapungufu yake ni yale tunayoyapokea kutoka kwa watu na namna wasemavyo juu yetu. Hapa ndipo sifa ujijengea mizizi, umaarufu unapokuzwa, uwezo unapoabudiwa kwa wale wanaokupaka mafuta kwa mgongo wa chupa, na nafasi ya pesa na utajiri unaposhika hatama. Yeyote yule anayeyakubali haya na kuyafanya kuwa sehemu ya maisha yake, hatochelea kuwa Shetani. Kama wabisha jaribu!

Ndugu yangu unaweza kuchezea haki za watu kwa kujificha nyuma ya kivuli cha mitutu, vifaru vya kijeshi, na magari ya maji washa washa ili kuzima sauti zao, ila ipo siku Mungu atasimama na kusema inatosha juu ya watu wangu unaowanyanyasa. Hapo ndipo kwenye kulia na kusaga meno. Jambo la kufahamu ni hili, “mara zote elewa kwamba wewe siyo kipimo cha ukweli kwa hayo unayoyalazimisha yawe kwa manufaa yako na kile ukiwakilishacho kisicho kweli na haki, iwe jamii, taasisi, au chama chako cha siasa.” Mungu mara zote huzungumza na watu. “Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao,” Mt 18:20.

Wapendwa wana wa Mungu, Mungu wetu hututakia mema muda wote. Tatizo letu ni pale tunapotaka Mungu kufanya kadiri tuonavyo sisi. Tatizo kubwa ndani ya utashi wetu ni kwamba mara nyingi hatuoni vitu kama vilivyo bali huviona kama tulivyo. Injili ya leo Yesu anaturudisha katika makusu ya Mungu mwenyewe naye akiwa Mungu, yaani, Neno aliyefanyika mwili na kukaa kwetu. Ni kweli isiyo shaka kwamba mara nyingine ufahamu wetu unagota kwenye mila na desturi zetu na kutufanya kuendana na mitazamo hiyo ambayo haina uhai ndani yake zaidi ya ufu. Yesu hafanyi lolote kwa kujificha. “Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati,” Mk 3:3. Kila mtu lazima aone yale ayafanyao Yesu. Yote ayafanyayo Yesu katika maisha yetu siyo mazingaumbwe. Ni kweli kabisa wapo baadhi yetu kwa kuyakuza majina yao uishia katika nguvu za giza na kuvaa miwani ya Kristo. Kujitabanahisha kuwa mwema, karibu na masikini, na kuwa karibu na Kristo bila kuyaishi hayo kwa dhati ni chukizo mbele ya Mungu. Mwisho ya hayo yote ni maigiza aibu juu yako. Wahenga utukumbusha hili; “mwisho wa ubaya ni aibu.”

Yesu hachoki kutuelekeza kwa kile kilicho haki na kweli mbele ya Mungu na uzima wetu wa milele. Yesu anauliza swali la msingi sana juu ya mila na desturi zetu juu ya uhai ambao ni mali ya Mungu na zawadi ya Mungu kwetu. “Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza,” Mk 3:4. Kwa namna nyingine Yesu anakuuliza wewe na mimi hivi: “je kile unachokiamini kinakuzuia kutenda lililo jema ambalo kwa uhalali ni zaidi ya kile unachokiamini?” Mila na desturi zetu zinaitaji kutakatifuzwa kwa sababu zimejawa hofu nyingi bila maelezo ya kina kwani lengo lake huwa utiii bila kuhoji. Utii upofu. Na ukitaka kuchunguza kwa undani mila hizi zilikuwa kwa manufaa ya wale walioziweka au kuzifanya. Pamoja na ukweli kwamba Yesu hakupata jibu ya swali lake, Yesu hakuacha kufanya lililo jema mbele ya Mungu Baba na watu wake kwa hofu ya macho ya watu na misimamo yao. “Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena,” Mk 3:5.

Ndugu yangu uliyesafari nami katika tafakari hii, ukweli utatuweka huru na si vinginevyo. “Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:31-32. Tuipende kweli, tuisimamie haki, na tutende mema hata kwa wale wenye mawazo kinzani nasi. Huu ndio mfano wa ukuhani wa Melkizedeki asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na ukomo,” Ebr 7:16. Kwa upendo wa Mungu usio na kipimo, wewe na mimi tumeitwa kuuishi ukuhani huu wa Melkizedeki. Ni kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki, ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani,” Ebr 7:1b-2. Pasipo upendo, haki, na amani hapana Mungu. Zaidi, ni kuujenga ufalme wako binafsi ambao Mungu asemapo “basi inatosha,” maporomoko yake ni zaidi udongo tifutifu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?” Zab 27:1

Tusali:-Ee Yesu na Mkombozi wetu, tukumbushe mara zote kwamba maisha ni dhamana. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario