JUMATANO WIKI YA 1
YA MWAKA-I
Somo: Ebr 2:14-18
Zab: 105:1-2, 3-4, 6-7, 8-9
Injili: Mk 1:29-39
Nukuu:
“Basi,
kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo
hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani,
Ibilisi,” Ebr 2:14
“awaache
huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali
ya utumwa,” Ebr 2:15
“Naye mkwewe Simoni,
mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake,”
Mk 1:30
“Akamkaribia, akamwinua
kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia,” Mk 1:31
“Akawaambia, Twendeni
mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana
kwa hiyo nalitokea,” Mk 1:38
TAFAKARI: “Akamwinua
kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kwa kiasi kikubwa kila siku ya maisha yetu tunakumbana na
matukia mbalimbali na mengine hatuelewi sawa sawa. Mungu anapenda tumtafute
wenyewe hadi tumpate. Tukimpata Mungu kwa kumtafuta si rahisi kuachana naye. Na
Mungu hupenda kukutana nasi katika matukio mbalimbali, na wakati mwingine
matukio hayo huwa ya huzuni na kukata tamaa. Mungu kwa kufanya hivyo siyo
kwamba haoni wala hatujui, la hasha! Mungu anatujua hata kabla ya kuzaliwa
kwetu. Hivyo uwepo wako leo ni kusudi kubwa sana la Mungu. Mungu anataka katika
mahangaiko hayo sasa umtafute ili ufanye kazi naye.
Kila
tukio linalotokea katika maisha yako lichukulie kama somo la kumfahamu Mungu
zaidi na vizuri. Usikubali kamwe lawama ikawa ndiyo salamu yako ya kwanza
unapokabiliana na tatizo lolote lile. Salamu yako ya kwanza muulize Mungu hivi:
katika tukio hili wataka kunifundisha nini Ee Mungu wangu? Kumbe jambo la
kwanza yatupasa kupokea hali hiyo.
Njia
ya pili ya kutupeleka katika uwepo wa Mungu na ufahamu wake ni ‘ufunuo.’ Kwa
namna yoyote ile na kwa yeyote yule, Mungu huweza kujifunua kwake. Kwa vile
kila mmoja wetu yupo duniani hapa kwa kusudi maalum kadiri ya mpango wa Mungu,
ni Mungu huyo huyo ujifunua kwake kwa lengo la kumshirikisha makuu yake. Tendo
hili la UFUNUO ndilo lililoibeba historia nzima ya wokovu wetu.
Wapendwa wana wa Mungu,
kuwepo pale Mungu alipo ni kuwa ndani na katika Kristo. Na pale tunapokuwa na
Kristo, maisha yetu hutawaliwa na majaribu. Kwa vile Kristo ameshinda jaribu
juu ya ibilisi na ila zake, nasi kwa kuwa waaminifu kwa Kristo, utujalia nguvu
za kushinda majaribu hayo kwa sababu Yeye. “mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao
wanaojaribiwa,” Ebr 2:18
Na ni kwa namna hiyo
hiyo “basi, kwa kuwa watoto
wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa
njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi,” Ebr
2:14. Ni uwepo huo wa Kristo ndani ya maisha yetu, na pale tunaposhikamana naye
katika hali zote bila kusaliti chochote tunawekwa huru na Kristo mwenyewe. Ni
hiki ndicho Kristo alichokifanya kwetu kwamba, “awaache huru wale ambao kwamba
maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa,” Ebr 2:15
Na
lengo la Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14, yaani, Yesu Kristo, ni “kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote,
apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili
afanye suluhu kwa dhambi za watu wake,” Ebr 2:17.
Ni hii ni kwa kile akisemacho Mungu kuhusu
mwanaye, na kile mwana akisemacho kuhusu Mungu Baba.
Siku ya Ubatizo wa
Bwana tuliona kile Mungu alichokisema kuhusu mwana wake. “Kisha
likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni
Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye,” Mk 9:7. Je, ni nani unayemsikiliza?
Kwa upande wa pili kile asemacho Mwana, yaani Yesu kuhusu Baba yake tunaweza
kusoma, Yoh 8:12-59. Katika mahusiano ya Mwana na Baba, Yesu anasema nini
kuhusu hukumu? “Nami nijapohukumu, hukumu
yangu ni kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi na yeye
aliyenipeleka,” Yoh 8:16. Kumbe kujua pale Mungu alipo pamoja na ufahamu wake
ni kuwa na Kristo Yesu.
Ufunuo huo wa Mungu
wajionyesha moja kwa moja ndani na katika Kristo katika Injili ya leo. Tunaona
uponyaji wa Mama Mkwe wa Simoni Petro ulivyokuwa. “Naye
mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara
wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono,
homa ikamwacha, akawatumikia,” Mk 1:30-31. Je, ulipoguswa na Mungu na kuponywa,
ulikuwa tayari kutumika kama shukrani kwa Mungu? Huyu ndiye Mungu aliye hai na atupaye
uzima. Mungu huyu anayo mamlaka pia ya kuuchukua uzima huo. “Bwana huua, naye
hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye
hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu,” 1Sam 2:6-7.
Pamoja na ufunuo huo wa
wazi wa Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, lengo kubwa sasa ni sisi kumjua
Mungu na kumwelekea yeye katika umilele. Pamoja na ishara zote alizozifanya kwa
kuwaponya watu wenye shida mbalimbali, Mk 1:34, Yesu anawakumbusha wanafunzi
wake, na kwa upande mwingine tukiwa wewe na mimi kile alichokijia hapa duniani.
Naye “akawaambia, twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate
kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea,” Mk 1:38. Kwa ubatizo wako wewe
ni mmisionari. Hivyo peleka habari njema ya wokovu ukianza hapo ulipo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi
kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa
kamwe,” 2Pet 1:10
Tusali:
Ee Yesu Mwema, nikumbushe mara zote kusema asante kwa yale unayonitendea pasipo
mastahili yangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario