lunes, 2 de enero de 2017

TAFAKARI: JANUARI 5, KIPINDI CHA NOELI


KIPINDI CHA NOELI

JANUARI 5

Somo: 1Yoh 3:11-21

Zab: 100:1b-2, 3, 4, 5

Injili: Yoh 1:43-51

Nukuu:

Maana, hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi,” 1Yoh 3:11 

Ndugu zangu, msistaajabu, ulimwengu ukiwachukia,” 1Yoh 3:13 

Yeye asiyependa, akaa katika mauti,” 1Yoh 3:14b. 

Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake,” 1Yoh 3:15 

Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?” 1Yoh 3:17

Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli,” 1Yoh 3:18 

Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu,” 1Yoh 3:21 

Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone,” Yoh 1:46

“Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona,” Yoh 1:48

“Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli,” Yoh 1:49

“Utaona mambo makubwa kuliko haya,” Yoh 1:50b.

“Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamum,” Yoh 1:51

TAFAKARI: Yeye asiyependa, akaa katika mauti.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, neno UPENDO siyo geni katika masikio yetu. Neno upendo pamoja na kwamba siyo geni katika masikio yetu ni neno ambalo limetumika mara nyingi kinyume na kile neno hili kinachowakilisha. Tafsiri ya upendo katika nyakati zetu leo imebeba taswira ya kufaidi kile kilicho kwa mwingine zaidi ya kufaidiana na kutaabikiana. Upendo wa kweli ni ule upendo ambao mara zote upo tayari kutoa kuliko kupokea. Ni upendo unaosukumwa na utu wa mtu kuliko kile alicho mtu yule kadiri ya mitazamo ya kijamii. Ninapomwana ye yote yule ni one utu wake na ubinadamu wake bila kusukumwa na rangi yake, nafasi yake, cheo chake, maumbile yake, imani yake, na mwonekano wake.

Huu ndio upendo anaotufundisha Yesu Kristo, yaani, “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Upendo huu unatuwajibisha kutenda kama atendavyo Yesu Mwenyewe. Utendaji wa Yesu ni ule wakutumika zaidi ya kutumikiwa. “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mk 10:45.  Ni utume wa kujitoa bila kujibakiza. Ni upendo wa kutoa chote nilichokuwa nacho na wakati huo huo kupungua katika maana ya kupoteza kile nilichokuwa nacho mwanzo. Upendo huu ni kama mwono wa Mshumaa. Mshumaa hutoa mwanga na wakati huo huo Mshumaa huo unateketea. Hii ndiyo maana ya upendo wa Yesu kwetu, nasi kama wafuasi wake twapaswa kufanya kwa wengine. “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo,” Yoh 15:14. Tunapofikia hatua hii ya upendo, sisi si watumwa tena bali ni rafiki zake Yesu kwa sababu tunajua na kuishi atendalo Yesu mwenyewe. “Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu,” Yoh 15:15.

Wapendwa wana wa Mungu, kupenda huku hakuna maana ya kwenda mbali na kutafuta wa kupenda au kuonyesha upendo wako huo. Mt. Fransisco wa Assis anasema, ‘hakuna haja ya kwenda mahali na kuhubiri habari njema bali tuhubiri habari njema hiyo kadiri tutembeavyo.’ Kwa maana nyingine, hubiri habari njema hiyo kuanzia pale ulipo. Na habari njema ya Mungu ni UPENDO wa Mungu kwa watu wote. Hivyo kama kupenda anza hapo ulipo. “Maana, hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi,” 1Yoh 3:11. Wakati fulani katika Taifa letu Tanzania tulikuwa na watu maarufu, na mmoja wa watu maarufu hao alijulikana kama Matonya. Umaarufu wa Matonya ulitokana na mbinu zake za kuomba msaada kutoka wa wenye nacho. Ni kweli pasipo shaka kwamba Matonya alikuwa mhitaji kwani alikuwa na ukoma. Ni jambo la rehema na baraka kumsaidia Matonya kwa namna yo yote ile. Ila kabla ya kufanya hivyo, je hakuna akina Matonya hapo ulipo? Je, kwenye familia yako hakuna akina Matonya? Je, katika jumuiya yako ya kitawa hakuna akina Matonya? Basi kama ni ukarimu uanze nyumbani kwako. Tusipoliona jambo hili, basi sote tu wauaji licha ya nafasi zetu tulizokuwa nazo. “Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake,” 1Yoh 3:15. Anza pale ulipo.

Binafsi nakerwa sana na tabia hii ya baadhi yetu wanapotoa msaada upenda kutembea na vyombo vya habari. Unatoa fedha, chakula au msaada wowote ule uku ukiwa katika mkao wa picha. Hii ni kwa faida ya nani??? Yesu Kristo anatupa angalizo kwa matendo haya yasiyokuwa na neema ndani yake. Naye anasema, “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 6:1. Ndugu yangu kutenda wema katika maisha yako yapaswa kuwa ni tabia yako kama mfuasi wa Kristo, na mwenye hofu ya Mungu. Mfano kiongozi wa ngazi ya juu serikalini kumtembelea yeyote yule mgonjwa bila kujali cheo, nafasi,  dini wala itikadi ya chama, isiwe ndiyo habari mkolezo. Huu ni wajibu. Kukoleza tendo hili kwa namna yoyote ile kwa onyesha upekee ambao unabeba sura ya upagani. Kiongozi huyo awe ni Mkristo Mwislam, au dini yeyote ile kutembelea wagonjwa yampasa kuwa ni tabia yake. Sipaswi kufanya hivyo tu kwa sababu ya nafasi yangu kama Raisi, na vile vile sipaswi kufanya hivyo tu kwa sababu ya nafasi yangu nilinayo katika jamii. Ikiwa mimi ni Mkristo basi nijue ni wajibu wangu kadiri mafundisho ya dini yangu, na hata maelekezo ya Maandiko Matakatifu, Mt 25:31-46. Ushabiki katika jambo hili na ukuzwaji wake unaharibu dhana nzima ya tendo hilo la upendo na huruma.

Ni wajibu wa kila Mkristo aliyebarikiwa na kuneemeka kwa kile alichokuwa nacho kukishikirisha kwa jamii ile inayomzunguka. Mali na utajiri ulionao umepewa bure na hivyo yakupasa kutoa bure. Huku ndiko kukaa ndani na katika Kristo. “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure,” Mt 10:8. Ila mara nyingi waweza kuona mtu yupo tayari kufanya mambo makubwa nje na mbali ya pale alipo wakati huo huo pale alipo kuna uhitaji mkubwa sana. Bila shaka tendo hili la mtu huyu linasukumwa na hali ile ya kutaka sifa. “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?” 1Yoh 3:17. Ni wazi upendo wa namna hii hauna ukweli ndani yake zaidi ya kutafuta sifa. Kupenda kwetu kuwe kwa kweli na siyo kwa maneno. Na tunapofanya tendo hili tusifanye kwa ajili ya kuonekana na watu, bali tufanye kwa sababu ni tabia yetu na wajibu wetu kama wafuasi wa Kristo katika kujali na kuwajibika. Tusianze basi kutafuta mbali wahitaji, bali tuanze pale tulipo. Hivyo, “Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli,” 1Yoh 3:18. AMINA!

Wapendwa katika Kristo, kupenda na kufanya kadiri ya mtazamo wa Kristo, ndiko kufunuliwa zaidi katika yale makuu katika Kristo. “Utaona mambo makubwa kuliko haya,” Yoh 1:50b. Hakuna kati yetu aliyepata hasara kwa sababu ya kupenda. Ni wazi kwamba tukiwa tayari kupenda kama Kristo tujiandae kuchukiwa kama Kristo alivyochukiwa. Wema wa Kristo ni chukio kwa uovu. Ni kama ilivyo mwanga na giza kutolandana. “Ndugu zangu, msistaajabu, ulimwengu ukiwachukia,” 1Yoh 3:13. Kuwa Mkristo katika kweli na haki ni vita. Ila ushindi katika vita hii ni kutenda mema. Ndugu yangu tuliyesafiri wote katika tafakari hii, kuwa Mkristo na mfuasi wa Kristo kuna mapaswa yake. Hivyo katika mapaswa haya ndipo ulipo utakatifu wako.

Tumsifu Yesu Kristo!

Kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani,” Efe 4:2-3

Tusali: Ee Yesu na Mwalimu wetu, tujalie neema ya kupenda pasipo kipimo. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario