SIKUKUU
YA EPIFANIA, TOLEO LA BWANA
JANUARI
6
Somo
I: Isa 60:1-6
Zab:
72: 1-2, 7-8, 10-11, 12-13
Somo
II: Efe 3:2-3a, 5-6
Injili:
Mt 2:1-12
Nukuu:
“Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na
utukufu wa Bwana umekuzukia,” Isa 60:1
“Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa
kuzuka kwako,” Isa 60:3
“Ndipo
utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa
wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa utakuwasilia,” Isa 60:5
“ikiwa
mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa
siri,” Efe 3:2-3a
“Siri
hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume
wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja
nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake
iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili,” Efe 3:5-6
“Yesu alipozaliwa
katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa
mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko
wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki,
nasi tumekuja kumsujudia,” Mt 2:1-2
“Basi mfalme
Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye,” Mt 2:3
“Akawapeleka
Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha
kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie,” Mt 2:8
“Wakaingia nyumbani,
wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao
walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na
manemane,” Mt 2:11
“Nao wakiisha
kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia
nyingine,” Mt 2:12
TAFAKARI:
“Mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia
mwanga wa kuzuka kwako.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Epifania, yaani, Toleo la Bwana. Leo
Mama Kanisa anatukumbusha mambo makuu matatu muhimu. Kwanza, ni ufunuo na
udhihirisho wa Kristo katika ulimwengu. Ni ufunuo wa Kristo kwa Mataifa yote ya
ulimwengu ambapo kunajidhihirisha kwa wataalamu wa nyota-Mamajusi, wakiongozwa
na nyota ile ya ajabu. “Na mataifa wataijilia
nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako,” Isa 60:3. Wokovu
wa Yesu Kristo unajionyesha kama nuru au mwanga
wa alfajiri unaoliondoa jiza na uvuli wa mauti ambao unautawala
ulimwengu. Mungu mwenyewe ndiye pambazuko.
Siku ya leo
inadhihirika wazi machoni mwa wanadamu kwamba Kristo ndiye Mfalme wa ulimwengu
wote, kwa ajili ya watu wote, na mmiliki wa utajiri wote. “Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka
na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa
utakuwasilia,” Isa 60:5. Ukweli
huu unajifunua kwa tunu zile alizopewa mtoto Yesu. “Wakaingia nyumbani,
wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao
walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na
manemane,” Mt 2:11.
Toleo hili la Bwana la
dhihirisha ukuhani wa Kristo kwa tunu ile ya uvumba. Huyu ndiye kwa huduma yake
atavitakatifuza vyote katika ulimwengu huu na kuvikomboa. Tendo hili linakwenda
sambamba na sadaka ile atakayo itoa pale Msalabani. Tendo hili la upendo mkubwa
wa Mungu kwa wanadamu leo linajifunua kwa tunu hii ya manemane. Manemane
yanatabiri kifo chake kama ilivyo taratibu za Wayahudi kuhifadhi Maiti na
kuzika. “Akaenda Nikodemo naye, (yule
aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na uudi,
yapata ratli mia. Basi wakautwaa
mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama
ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika,” Yoh 19:39-40. Mambo haya makuu
matatu yanajifunua kwetu leo.
Pili,
toleo hili la Bwana, Epifania, linatupa namna ya kuishi kama Wakristo-wafuasi
wa Kristo. Tendo hili ya kufunuliwa na kudhihishwa kwa Kristo ulimwenguni pote
linatuondoa katika hali ile ya kuwa wakristo wa kidunia na kutufanya Wakristo
wa ulimwengu-wamishionari. Leo tunafanywa Wakristo wa tabaka la ulimwengu wote
na siyo Mkristo wa kidunia. Wakristo wa kidunia kadiri ya Rich Warren,
humtazama Mungu kwanza kwa ajili ya kukidhi haja zao binafsi. Wanapenda
kuhudhuria mikutano na semina za kujenga, lakini hutawakuta katika mkutano wa
umisheni kwa sababu hawaupendelei. Maombi yao yanajali mahitaji yao binafsi,
baraka, na furaha yao. Ni ile imani ya ‘mimi kwanza.’ Waaminiwa mtindo huu husukumwa
mara zote na swali hili: Je, Mungu anawezaje kufanya maisha yangu kuwa na
furaha? Wanapenda kumtumia Mungu kwa malengo yao badala ya wao kutumiwa kwa
malengo yake (Mungu).
Wapendwa
wana wa Mungu, kinyume cha hapo, Wakristo wa tabaka la ulimwengu mzima wanajua
waliokolewa ili watumike na kutayarishwa kwa ajili ya utume. Wako tayari
kupokea jukumu la mtu binafsi na wanafurahia upendeleo huo wa kutumiwa na
Mungu. Wakristo wa tabaka la ulimwengu wote ndio watu pekee walio hai
kikamilifu katika sayari hii. Furaha yao, uhakika na hamasa yao vinaambukiza
kwa sababu wanajua wanafanya tofauti. Wanaamka asubuhi wakitazamia Mungu
kufanya kazi kuwapita katika njia mpya. Je, unataka kuwa Mkristo wa aina gani?
Leo katika toleo la Bwana, Mungu anakualika kushiriki katika tendo kubwa kuliko
yote, la aina yake na la muhimu sana katika historia-ufalme wake. Hivi ndivyo
Yesu alivyowaambia wanafunzi wake kabla ya kapaa, “Nimepewa
mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi,
enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba,
na Mwana, na Roho Mtakatifu; na
kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja
nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari,” Mt 28:18-20. Tendo hili linamfanya
Kristo kuendelea kudhihika ulimwenguni kote.
Tatu, toleo hili la Bwana
leo linatukumbusha kwamba uinjilishaji hapa duniani ni jambo la pekee. Yapo
malengo matano ya Mungu kwa maisha yako hapa duniani. Mungu alikuumba ili uwe
mshiriki katika jamii yake, kielelezo cha tabia yake, mtu anayetukuza utukufu
wake, mtumishi wa neema yake, na mjumbe wa Habari zake Njema. Katika malengo
haya matano, hii la tano linaweza tu kutendwa hapa duniani. Yale mengine manne
utaendelea kuyafanya milele kwa namna fulani. Hivyo kutangaza Habari Njema ni
muhimu sana; una muda mfupi tu wa kushirikisha wengine ujumbe wa maisha yako na
kutimiza utume wako.
Ujumbe
wa Mtume Paulo kwa watu wa mataifa anaonyesha mpango wa wokovu wa Mungu
umejifunua wazi kwa Watakatifu, Mitume wake na Manabii. Hata hivyo watu hawa wa
mataifa wameupokea wokovu wa Mungu kwa ufunuo wa Roho. Watu hawa wa Mataifa ni
warithi pia wa ahadi hizi za Mungu. Katika mpango huu wa wokovu hakuna tena
matabaka. Hii ndiyo siri kubwa inayoibuliwa leo kwa tendo hili la toleo la
Bwana. “Siri
hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume
wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja
nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake
iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili,” Efe 3:5-6. Sote tu huru ndani na katika Kristo. Hivyo tuna
mwili mmoja tu wa Kristo, nalo ndilo Kanisa. Sote tu viungo vya mwili huo mmoja
na Kanisa hilo moja yaani Kanisa la Kristo. Kwa utarajibu na mwono huu, sote
tunashiriki fumbo la Kristo kwa Sakramenti ya Ubatizo. Kristo katika mtazamo
huu ndiye mrithi wa kweli wa ahadi zile za Mungu. “Basi ahadi zilinenwa
kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali
kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo,” Gal 3:16
Yesu Kristo Mfalme na
Masiha kwa mara ya kwanza anakutana na wana wa ulimwengu wote. Injili ya Matayo
inatajirisha simulizi la toleo la Bwana kwa vielelezo vya Kibiblia-Maandiko
Matakatifu. Unabii ule wa Nabii Mika unatimia, yaani; (nyota Yakobo, zawadi za
dhahabu na uvumba). Kristo ndiye Mfalme Mpya wa Wayahudi, na Musa mpya,
mwakilishi wa ulimwengu mzima. Tendo hili la toleo la Bwana ni tishio kwa falme
nyingine la ulimwengu huu. “Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na
Yerusalemu pia pamoja naye,” Mt 2:3. Habari za ufalme huu mpya ni habari njema kwa
masikini na wenye hofu ya Mungu. Wale wote wasio na hofu ya Mungu huongozwa na
mipango miovu ya shetani. Mungu hata hivyo uiweka mipango yao miovu wazi kwa
ajili ya kuwanusuru wanyonge na waadilifu wake. “Nao wakiisha kuonywa na Mungu
katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine,” Mt 2:12.
Huyu ndiye Mungu asiyeshindwa katika mipango yake kwa wapendwa wake. Na huyu
ndiye tunayesujudia leo siku ya Epifania, toleo la Bwana.
Je, ungepata leo nafasi
ya kumtolea Yesu tunu ungempa kitu gani? Mathias Makyadi kutoka Kongo alikuwa
ni mmoja wa wanavisi kati ya wanovisi kumi wa shirika fulani la kimisionari.
Kila wiki mmoja wa wanovisi hupewa muda wa saa moja kutafakari mbele ya
Ekaristi Takatifu. Waweza kutumia muziki wa ala ukuongoze katika tafakuri yako
au ukimya tulivu.
Tendo la kufanya
tafakuri lilikuwa gumu sana kwa Mathias Makyadi. Hivyo ilipofika zamu yake
ulikuwa mtihani mkubwa sana. Hata hivyo Mathias alimwambia Yesu wa Ekaristi
hivi, “kutafakari kwa ukimya kadiri ya utaratibu uliozoeleka hapa mimi siwezi.
Hivyo naomba nikupe kile nilichonacho kama shukrani na upendo wangu kwako.”
Mathias aliondoka na kwenda chumbani mwake akachukua redio kaseti yake na
kuweka mziki wa kwao “ndombolo” na kucheza kwa nguvu zake sote, kwa kutumia
akili yake yote, na moyo wake wote.
Mara aliingia Mlezi
wake kwenye kile kikanisa kwani kelele zile
zilisikika kila viambata vya nyumba ile ya Unovisi. “Kwa nini unafanya kelele
mahali hapa na kucheza mbele ya Yesu wa Ekaristi?” Mlezi wa wanavisi alisema
kwa jazba na hasira. “Baba, hiki ndicho ninachoweza kumpa Yesu wa Ekaristi kilicho
cha thamani kubwa na ninachoweza kumpa kwa moyo wangu wote,” Mathias amjibu
Mlezi wake kwa upole. Baada ya kuyatafakari maneno yale ya Mathias, Mlezi wake
aliondoka bila ya kusema neno.
Wapendwa wana wa Mungu,
kila mmoja wetu anacho kitu cha kumpa Yesu leo kama walivyofanya Mamajusi na
alivyofanya Mathias. Lakini zaidi ya yote, mimi na wewe tunaweza kumpa dhambi
zetu kwani ndiyo mali yetu halali. Tunapojitazama sisi na huruma ya Mungu,
tutazame mali hii halali tuliyonayo. Kristo Mfalme, ni Huruma, Upendo, Msamaha,
Haki, na Kweli. Zawadi hii ataibadilisha na kuwa nyeupe kama sufu. “Haya,
njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa
nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa
1:18
Tumsifu Yesu Kristo!
“Na majeshi yaliyo mbinguni
wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi,” Ufu
19:14
Tusali:
Ee Yesu, nijalie neema ya kutopoteza furaha yako ndani ya moyo wangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario