JUMAPILI YA 4 YA
MWAKA-A
Somo I: Sef 2:3; 3:12-13
Zab: 146: 6-7, 8-9, 9-10 Mt 5:3
Somo II: 1Kor 1:26-31
Injili: Mt 5:1-12a
Nukuu
“Mtafuteni
Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake;
itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira
ya Bwana,” Sef 2:3
“Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana
hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala
hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu,” Sef 3:11
“Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao
watalitumainia jina la Bwana,” Sef 3:12
“Mabaki
ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa
hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu
atakayewaogofya,” Sef 3:13
“Maana,
ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini,
si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa,” 1Kor 1:26
“Bali kwa yeye ninyi
mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na
haki, na utakatifu, na ukombozi,” 1Kor 1:30
“Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila
neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini,
na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni,” Mt 5:11-12
TAFAKARI: “Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa
mbinguni.”
Wapendwa wana wa Mungu, sehemu kubwa ya maisha ya mwanadamu hapa
duniani ni kutafuta maana ya maisha yake, na kuipata ile furaha ya kweli.
Binadamu huyu ulifanya jambo hili anapoitazama historia yake kama somo kwa
lengo ya kuyarekebisha yale ambayo hayakwenda vyema kwa wakati huu aishipo
sasa, ili kule aendapo asipokujua vizuri kuwe na tumaini. Hivyo, somo la Injili
ya leo kwa upana wake linaelezea hali halisi katika mahangaiko ya mwanadamu, na
ulimwengu huu tunaoishi. Na kwa kulisema hilo, Yesu leo anatutaka tuzitafakari
kwa kina heri hizo alizozisema, Mt 5:3-12.
Lakini ili tuifikie furaha ile ya kweli ambayo hiyo ndiyo lengo
halisi, hatuna budi kuufahamu ulimwengu huu tunaoishi leo. Bila kuujua
ulimwengu huu ambapo ndipo tunapoishi, ni vigumu pia kuiona furaha ile ya kweli
inayoendana na malengo ya kuumbwa kwetu. Mimi na wewe tumeumbwa ili tuishi
milele. Kwa ufupi na kwa kina, Yesu anatupa siri ya hali halisi ya ulimwengu
huu tunaoishi leo. Naye anasema, “Amin, amin, nawaambia,
Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa,
lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha,” Yoh 16:20. Pamoja na mazingira kama
haya, na tunaposimama kwa lile lililo kweli na haki, Kristo hatotuacha kamwe.
Ni kwa sababu hiyo Yesu aliyatoa maisha yake, ili mimi na wewe leo tuwe huru
kutoka utumwa wa dhambi na uovu wake wote. “Basi ninyi hivi sasa mna huzuni;
lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna
awaondoleaye,” Yoh 16:22. Hivyo tuitafutapo furaha hiyo ya kweli hatuna budu kujua
hali ya ulimwengu wetu tunaoishi kama alivyotufunulia Bwana wetu Yesu Kristo.
Je, tunafanye nini sasa?
Jambo la kufanya ni
kuziishi heri alizotuambia Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili ya leo. Katika
tafakari hii sintozipitia heri hizo moja baada ya nyingine, bali niwatake
tutafakari heri hizo kwa kuyatazama mambo makuu manne ambayo kwa kiasi fulani
yanasema juu ya maisha yetu ya leo. Mambo hayo ni kama yafuatayo: Kwanza, kuwa
na nafasi ndani ya moyo wako. Pili, hapo ulipo fanya zaidi na achana na mazoea.
Tatu, hapo ulipo kuwa mzalendo kwa kujipokea, kuwapokea wengine, na kuipigania
jamii yako-Taifa lako. Na nne, kuwa alama na kielelezo hai cha amani ya kweli
hapo ulipo.
Wapendwa wana wa Mungu,
tuanze na hili la ‘kuwa na nafasi ndani ya moyo wako.’ Huwezi kuwa na furaha ya
kweli kama hakuna nafasi ya Mungu ndani ya maisha yako. Hofu ya Mungu ndani
yetu ni mizania ya kujipokea kama tulivyo, na kutufanya tujitahidi kufika pale
ambapo tunapatamani. Itakuaje basi kufanya hivyo kama huna nafasi ya Mungu ndani
yako? Kuwa na nafasi ndani ya moyo wako, Yesu ameizungumzia katika Injili ya
leo kwa mtindo huu, “Heri walio maskini wa
roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 5:3. Ni umaskini huu wa roho, yaani,
kuwa na nafasi ya Mungu ndani yako, kutakao kupeleka katika furaha ile ya
kweli, yaani, ufalme ule wa Mbinguni baada ya kuvishinda vita hivi hapa
duniani. Haya ndiyo maisha yale ya umilele kama lengo halisi la kuumbwa kwetu,
yaani, tumeumbwa tuishi milele.
Pili,
‘fanya zaidi na achana na mazoea.’ Hakuna saratani mbaya katika maisha ya
mtindo wowote ule, pale unapofikia hatua ya kuridhika na kila kitu, na kuacha
mambo yaende tu kama yalivyo, kwa vigezo kwamba kama juzi na jana ilikuwa
hivyo, basi hata leo na kesho itakuwa hivyo hivyo. Mwenendo huu wa maisha ni mwendo
wa ‘kufa pole pole’ huku ukiona. Kumbe kuishi maisha yenye malengo ni kufanya
zaidi ukijua siyo kwa sababu ya ubinafsi wako, bali kwa ajili ya wengine kwa
sasa na hata vizazi vijavyo. Mtume Paulo anatufafanulia vizuri kuhusu kweli hii
na kusema, “Mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya
mwenzake,” 1Kor 10:24. Na tutakuwa tunafanya hivyo siyo kwa kuutafuta utukufu
binafsi, bali kuifikia tumaini lile ambalo kila mmoja wetu bila kujali historia
yake, itikadi zake, familia au kabila, anatamani kuipata. Kwa Mkristo na mfuasi
wa Kristo aliye hai hufanya hivyo akijua ukweli huu kwamba, “hakuna mtu
miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa
Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu
mali ya Bwana,” Rum 14:7-8. Hivyo ndugu yangu, kulifikia tumaini hili yakupasa
wewe na mimi kuwa na njaa ya tumaini hilo. Ni katika mazingira haya Yesu
anasema, “Heri wenye njaa na kiu ya haki;
Maana hao watashibishwa,” Mt 5:6. Je, hali ipo vipi hapo ulipo? Jamii
inayokuzunguka inatenda haki nawe ukiwa mmoja wapo? Kama hilo halipo itakuwaje
basi uwe na furaha ya kweli? Changamoto hii ni yangu na yako pia. Tuwe na njaa
na kiu ya haki. La sivyo hatutaweza kushibishwa, yaani kuwa na furaha ya kweli.
Tatu, hapo ulipo ‘kuwa
mzalendo’ kwa kujipokea, kuwapokea wengine, na kuipigania jamii yako-Taifa
lako. Ndugu yangu, mizania ya haki na kweli, ipo ndani ya usafi wa moyo wa mtu.
Kuna msemo wa kifalsafa usemao kwamba, “mtu hutoa kile alichokuwa nacho.” Hivyo
huwezi kutoa kile usichokuwa nacho. Lakini naweza kuifikia mizania hii ya usafi
wa moyo kwa kufanya hatua hii muhimu sana katika maisha yangu, yaani, kujipokea
kama nilivyo. Hapa simaanishi tu kuyaona mazuri yako na mabaya yako ukaridhika nayo
na kutokufanya chochote. Wito wa kila mmoja wetu ni kuwa wakamilifu kama Baba
yetu wa Mbinguni alivyo makamilifu, Mt 5:48. Kama hili ndilo lengo msingi la
maisha na malengo yangu, sinabudi kuurekebisha udhaifu wangu ili kuufikia usafi
ule wa moyo kila siku ya maisha yangu. Hii siyo kazi ya siku moja.
Jambo hili, yaani,
‘kujipokea’ likichukua mkondo wake sawa sawa, mengine hufuata, yaani, kuwapokea
wengine, na kuwa tayari kwa maslahi mapana ya jamii inayokuninguka, na Taifa zima.
Huu ndio uzalendo tunaouzungumzia hapa, yaani, fanya yote kwa ajili ya wengine
kwa kulitazama tumaini lililo mbele yako na kwa wote. Katika kweli hii, jambo
hili litawezekana kama Yesu anasemavyo, “Heri
wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu,” Mt 5:8. Ni katika moyo ulio safi
utofautisha namna ya kufikiri kwetu, kuamua kwetu, na kutenda kwetu. Mlolongo
huu ndiyo ule unaotupatia cheo chetu halisi, yaani, utakatifu wako. Hivyo
tutamwona Mungu tu tukiwa na cheo hiki, yaani, Utakatifu kwa sababu Mungu wetu
ni Mtakatifu.
Na nne, ‘kuwa alama na
kielelezo hai cha amani ya kweli hapo ulipo.’ Ni moyo safi huo ambao utuwezesha
kuona kitu kama kilivyo, na kusema kama kilivyo, ili kibaki kama kilivyo katika
hali yake daima. Tatizo kubwa hapa mara nyingi mimi na wewe huvaa miwani ya
‘tulivyo,’ na kupoteza uhalisi wa jambo au kitu kama tulivyo. Miwani hii ya
‘tulivyo,’ yaweza kuwa itikadi zetu kisiasa na kidini. Miwani hii ya ‘tulivyo
inaweza kuwa pia familia zetu, koo zetu, na makabila yetu. Kwa mtindo huo, tutawezaje
kuwa wapatanishi wa kweli? Ndugu yangu, tunapoambatana na mambo hayo kwa
kushikamanana nayo au kung’ang’ana nayo kama yalivyo, twajisababishia upofu wa
kudumu. Ni vyema mimi na wewe tukatoka katika boksi hilo na kupata mwanga
halisi wa kuona vizuri ukweli wa kile tukitazamacho. Huku ndiko kuwa
‘wapatanishi’ kama asemavyo Yesu, “Heri
wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu,” Mt 5:9. Mungu yu mpatanishi
wetu katika maana nzima ya Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Ni
upananisho huu ambao kilele chake kilikuwa kifo cha Mwanaye Mpenzi pale
msalabani, ambacho kifo hicho kilituhesabia haki kuwa wana na warithi wa ufalme
wa Mungu. Hivyo leo mimi na wewe tunapokuwa wapatanishi tunamwakilisha Mungu
kama watoto wake. Na huu ndio uwana wa Mungu, yaani, kuwa mpatanishi pale
ulipo.
Mambo
yote manne tuliyoyaona hapa juu yanahitaji sadaka. Sadaka ya kwanza ni
kujikatalia nafsi yako mwenyewe ili uwe na mizania ya kweli na haki katika yale
yote utakayokutana nayo kwa kufikia malengo ya mambo hayo manne. Sadaka uitoayo
ina maana kwa sababu mbele kuna heri na tumaini. Kielelezo cha heri hiyo na
tumaini ni Kristo mwenyewe. Mateso na majaribu lazima tutakutana nayo katika
safari hii. Tunapoyaachia maisha yetu katika kiwango hiki,
Kristo kamwe hawezi kutuacha katika taabu hizo. Kristo hubaki kuwa faraja kubwa
kwetu katika dhiki na taabu hizo. Naye anatuambia nyakati kama hizo tuwe watu
wa kufurahi kwa sababu tunamruhusu Mungu kutenda mambo katika hali yetu ya
uduni na Mateso. Kwa msisitizo mkubwa Yesu
anasema, “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya
kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini,
na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo
walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12. Kuna furaha kubwa sana
moyoni kuhukumiwa kwa sababu tu umetenda haki na kuishuhudia kweli. Haya ndiyo
maisha ya ushuda hasa katika nyakati zetu hizi tunapoona na kushuhudia
ubabaishaji kila kona.
Wapendwa wana wa Mungu,
leo yako isisubiri kesho ili ujiandae. Kesho hiyo hujaifikia, na jana yako
ilishapita bila kufanya chochote. Hivyo, “Siku
ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu
wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika
mlima wangu mtakatifu,” Sef 3:11. Aliyejiandaa ndiye atakaye kuwa mikono salama
ya Mungu. Kundi hili ni lile la wenye
hofu ya Mungu, Masikini na walioonewa. “Lakini nitasaza ndani yako watu
walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la Bwana,” Sef 3:12
Wenye
hofu ya Mungu na wanyenyekevu wa moyo, hawana woga wala hofu kwa sababu maisha
yao yapo mikononi mwa Mungu. Nabii Sefania anawataja watu hawa kwa kusema,
“Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa
hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu
atakayewaogofya,” Sef 3:13. Hawa wanajua ni nani wanayemtumikia. Mungu huyu wa
kweli na hai hatotuangusha kamwe tunapojitoa kwake bila kujibakiza. Ndugu yangu
tuliye safiri wote katika tafakari hii, Hakika hakuna
lisilowezekana kwa Mungu! Yote yawezekana kwa IMANI.
Ndugu yangu, kuwa na utajiri iwe wa
kiroho na ule wa kushikika na wakati huo huo kubandukana nao, kutakuhitaji
unyenyekevu wa hali ya juu. Na waliofanikiwa sana katika maisha ni wale
waliojinyenyekeza sana katika maisha hata kama palikuwa na fursa ya wazi
kufanya vinginevyo. Na wakati mwingine tunashangazwa na tabia hizi za wachache
wetu kuishi maisha ya chini na ya kawaida kabisa licha ya mwamba mazingira na
nafasi aliyokuwa nayo katika jamii ni kubwa na ya kuheshimika. Hapa ndipo
tunapoona mkono wa Mungu ukifanya kazi pamoja na wale walio mridhia. Wakati
mwingine na kwa mshangao mkubwa, ‘Mungu huchagua mambo mapumbavu ya
dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili
aviaibishe vyenye nguvu,” 1Kor 1:27.
Huyu ndiye Mungu na “tena uvichagua vitu
vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili
avibatilishe vile vilivyoko,” 1Kor 1:28. Na watu wa mtindo huu pamoja na mambo
yote, hutambua maisha ni dhamana na hakuna cha kujivunia zaidi ya kuwa mawakili
wa kweli kwa kile walichokabidiwa kadiri ya wito na nafasi zao katika jamii. Na
katika hili Mtume Paulo anasema, “mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele
za Mungu,” 1Kor 1:29. Jambo hili linawezekana tu pale tunapokuwa tayari na kwa
moyo thabiti kuishi ndani na katika Kristo Yesu. Kwake ‘yeye tumepata kuwa
katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na
utakatifu, na ukombozi,’ 1Kor 1:30. Hivyo “aonaye fahari na aone
fahari juu ya Bwana,” 1Kor 1:31. Fahari hii utuongoza kuyaona maisha yetu kuwa
dhamana. Yesu Kristo anasema, "na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo
mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi;
naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi." Lk
16:48. Maisha ni dhamana. Na kadiri Mungu anavyokupa zaidi, ndivyo anakutaka
uwajibike zaidi.
Badala yake ni kuishi katika heri hizi
nane za shetani:-
- Heri
yao wanajumuiya waliochoka sana, waliobanwa na shughuli na kukosa kukutana
na wa wenzao katika shughuli za Jumuiya kila wakati. Kwa maana hao ni
wafuasi wangu waaminifu.
- Heri
yao wana-parokia wanaofurahia kutambua tabia za wenzao na mapungufu ya
watumishi wa Mungu. Kwa maana hao ndio vitendea kazi vyangu.
- Heri
yao waamini wanaosubiri kuambiwa kufanya kila kitu na kutegemea kupongezwa
hata kama hawakufanya chochote. Hakika hao naweza kuwatumia vyema.
- Heri
waamini wanaoguswa na kukwazika kwa vitu vidogovidogo na kuacha kwenda
Kanisani na kuacha kusali. Kwa maana hao ni wamisionari wangu.
- Heri
yao hao waamini wanaojitangaza au kudai kuwa wanampenda Mungu na wakati
mwingine wanawachukia waamini wenzao na ndugu zao. Hakika hao ni wangu
Milele.
- Heri
yao wanajumuiya watenganishi na waletao fujo na chuki. Wataitwa wana
wangu.
- Heri kwa wanafamilia wasiokuwa na muda wa kusali.
Maana
hao wananiombea mimi.
- Heri
yako wewe unayesoma haya na wewe unayeyasikia haya na kufikiri ni kwaajili
ya wengine na siyo wewe mwenyewe. Hakika nimeshakupata tayari.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Heri
ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa
ajili yangu,” Mt 5:11
Tusali:-Ee Yesu, furaha ya
kweli ni pale ninapokufia katika kweli na haki. Nipe ujasiri ya kukijongea kifo
hicho. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario