JUMATATU WIKI YA 2
YA MWAKA-I
Somo: Ebr 5:1-10
Zab: 110: 1, 2, 3, 4
Injili: Mk 2:18-22
Nukuu:
“Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa
katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu,
ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi,” Ebr 5:1
“Na hapana mtu
ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni,”
Ebr 5:4
“Vivyo
hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia,
Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa,” Ebr 5:5
“Yesu akawaambia,
Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao? Muda
wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga,” Mk 2:19
“Wala hakuna mtu
atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua
viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya
katika viriba vipya,” Mk 2:22
TAFAKARI: “Ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata.
Kutii ni bora kuliko dhabihu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kutii ni kutambua kuwa kuna kitu zaidi ya kile ulicho ambacho
kwa namna moja au nyingine kinaathiri uwepo wako hasi au chanya. Kutii hakuna
gharama yoyote kama utatambua kile ulicho na kile kilicho zaidi ambacho kina
uhusiano nawe katika kuwa, kutenda, kufikiri na kuamua. Kati ya mambo magumu
kufanya binadamu ni kutii. Kutii kunamlazimu mtu wakati mwingine kwenda kinyume
na ufahamu wake kiakili na kimantiki. Kutii wakati mwingine kutakulazimu
kuachilia yate uyafahamuyo kiufasaha. Kutii ni kujisalimisha kuliko kwa hiari
kwa kile ukifahamucho kwa undani. Kutii ni kuruhusu jambo lingine lifanyike
hata kama lile ulifanyalo una uhakika nalo.
Mungu
kwa nafasi yake atamtumia mmoja wetu kutimiza nia na matamanio yetu. Mpango wa
Mungu kwetu ni wa ajabu sana kuuelewa. Ila historia ya wokovu wetu inatuonyesha
wazi ukweli huu kwamba, Mungu hutumia vile vilivyo dhaifu kufifisha vile
vinavyojionyesha na kujipendekeza kuwa shupavu na hodari. Mama Bikiria Maria
alipohesabiwa haki mbele ya Mungu anatuambia ukweli huu kwa kusema, “Amefanya
nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk
1:51-52. Huyu ndiye Mungu anayesimama kutetea haki za wangonye na kuwa sauti
kwa wale wasio na sauti katika jamii. Kwa kutimiza jambo hili Mungu huchagua
kile kinachoonekana dhaifu machoni mwa watu hasa upande ule unaojihesabia haki.
Jambo la ajabu licha ya
udhaifu wetu kibinadamu, kwa sakramenti ya ubatizo, Mungu anatushirikisha mambo
makuu matatu; Ukuhani wake, Unabii, na Ufalme. Ni kwa namna hii ya ajabu “kila
kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika
mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi,” Ebr
5:1. Hivyo kwa namna ya kwanza, na katika ujumla wake kama wana wa Mungu, yote
tuyafanyayo si kwa mastahili yetu binafsi, bali yale yanayomhusu Mungu na Taifa
lake.
Wapendwa katika Kristo,
Mungu anayempenda na kumchagua ayafanye
yale anayoyataka ana sifa hizi tatu kadiri ya somo letu hili, yaani, waraka kwa
Waebrania: Kwanza kabisa, “awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye
kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu,” Ebr 5:2. Mungu
hatuambii mtu huyo lazima awe Mtakatifu kama Yeye alivyo, bali mtu huyo aweza
kutumika vyema kwa sababu naye ana hali ya udhaifu kama atakao wahudumia.
Waswahili wanasema, ‘zimwi likujualo halikuli likakwisha.’
Sifa ya pili ni
kuwajali wale atakao watumikia licha ya udhaifu wake. “Na kwa sababu hiyo
imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe,
kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi,” Ebr 5:3. Ni kwa kupitia wajibu huu aliopewa
ndipo atakapo tumia dhamana hiyo aliyopewa ya juu kabisa kujisahihisha makosa
yake, na kujitakasa dhambi zake kwa sadaka ya utumishi wake na huruma ya Mungu.
Na sifa ya mwisho mtarajiwa
huyo asiwe mtu wa kujikweza na kujihesabia haki, bali Mungu awe hofu yake. “Na
hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama
vile Haruni,” Ebr 5:4. Sifa hizo tatu kadiri ya somo letu la hili zituongoze
katika ufahamu wa kweli kutambua ni yupi anayetufaa kuwa kiongozi wetu.
Tumwombe Mungu kwa namna ya pekee atuongoze vyema katika chaguzi zetu za viongozi
wenye kuhesabiwa haki na kupewa kibali mbele zake Mungu.
Mfano na kielelezo hai cha
sifa zote hizo tatu ni Kristo Yesu. Na “Vivyo hivyo
Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia,
Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa,” Ebr 5:5. Ni jambo la ajabu sana leo kati
yetu kujitwaliya mambo haya makuu kwa kujitukuza pasipo sifa na siha. Leo wapo
kati yetu wanaojiinua kama mitume, manabii, na hata wapakwa (Wazee wa upako).
Hakuna mwenye uhalali wa kujihesabia haki pasipo Mungu Mwenyewe, au wale
waliowekwa wakfu (kutengwa) kwa sababu hiyo. Jambo hili halitegemei ukaribu
wetu au historia zetu katika huduma hiyo tuitoayo zaidi ya kuitwa katika maana
ya kuhesabiwa haki. Ni “kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani wa milele
Kwa mfano wa Melkizedeki,” Ebr 5:6. Kuhani Melkizedeki hakuwa na mtiririko ule
wa koo ya kikuhani-Walawi na akina haruni. Na kutoka asili hii ndipo tunapouona
wito wa padre kama kuhani. Padre tulio wengi tumetoka kwenye familia zisizokuwa
na majina, na wakati mwingine zilizodharaulika haswa.
Ndugu
yangu, Mawazo ya Mungu na njia zake siyo yetu na zetu, Isa 55:8. Ni kwa mantiki
hii ya Mungu kwamba, Kristo na leo Padre ambaye ni Kristo mwingine, “Alter
Christus,” aliye mfano wa Melkizedeki, “siku
hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti,
maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa
mcha Mungu na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata,”
Ebr 5:7-8. Na katika utii wake Kristo sote tumeponywa kwa sadaka yake pale
msalabani. Nasi kwa kumtii Mungu na kwa namna ya pekee Mwanaye Mpendwa
Yesu Kristo twahesabiwa haki hiyo ya kuwa wana wa Mungu. Hivyo “naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu
wa milele kwa watu wote wanaomtii,” Ebr 5:9. Na kwa tendo hilo la utii wa
Kristo, na Kristo mwingine ambaye ndiye Padre, “ametajwa na Mungu kuwa kuhani
mkuu kwa mfano wa Melkizedeki,” Ebr 5:10.
Na sasa kwa namna ya
pekee tumtazame Padre. Je, Padre ni nani hasa? Kama nilivyokwisha kusema, padre
ni Kristo mwingine, "Alter Christus." Padre ufahamika kwa kile
afanyacho. Kwa kinywa chake anaweza kutamka maneno ya Bwana, "mimi ndimi
njia, na ukweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi," Yoh
14:6. Padre ni mtumishi wa Mungu anayejitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa watu
wa Mungu.
Licha ya sadaka hiyo,
padre ni mwanadamu kama wanadamu wengine, aliyetwaliwa kati ya watu kwa mambo
ya muhusuyo Mungu, "maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu
amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo
na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na
wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu
hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake
mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya
dhambi, " Ebr 5:1-3.
Kama Kristo mwingine,
hakuna mtu anayependwa sana na kuchukiwa sana kama Padre. Lakini Padre hubakia
kuwa chumvi na mwanga wa dunia. Kuchukiwa kwa Padre ni kutokana na kuyatenda
mambo yamuhusuyo Mungu yanayopingana na mambo ya ulimwengu huu. Yesu Kristo
anasema,"mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao
si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu," Yoh 17:14.
Ndugu yangu,
wanaoteuliwa kuwa mapadre ni viumbe wanyonge wanaoshiriki unyonge wa ndugu zao.
Na hii inawawezesha kuwaombea ndugu zao bila unafiki. Padre ni zawadi kwa Mungu
ya watu kwa Mungu. Padre hutoa zaidi na hupokea kidogo, zaidi hulipwa chuki na
minong'ono. Kwa sadaka yake Padre inabidi apate heshima. Ni mtu anayemwakilisha
Kristo. Kama Mt. Francisco alivyosema, "kama ningekutana na malaika pamoja
na Padre, ningeweza kumsalimia kwanza Padre, kwani Malaika ni rafiki wa Mungu,
na Padre ni Mhudumu wa Mungu." Heshima ya Padre inatamkwa wazi na Bwana
wetu Yesu kristo, "awasikilizaye ninyi ananisikiliza mimi, naye awakataaye
ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma," Lk
10:16
Wapendwa, tusisahau
kwamba Padre hata baada ya upadrisho wake anaendelea kuwa mwanadamu. Na hali ya
kibinadamu ni hali ya unyonge, uchovu, kushawishika pamoja na kukata tamaa.
Kumbe si halali: Watu kukasirika wanapomwona Padre mnyonge kama wao. Kuwadai
Mapadre kuwa na akili kama malaika. Na, kutaka upendo wao uyeyushe ugumu wa
kila mkosefu au wawe na ufundi wa kutatua matatizo yote ya maisha.
Wapendwa, Padre ni
upendo wa Mungu: Palipo na huzuni Padre huleta furaha. Pasipo na haki Padre
huleta haki. Kwa Vijana, Padre huwatia moyo na kuwafundisha fadhila mbalimbali.
Padre ni utii kwa watu wote. Na kufikika na wote. Na, Padre ni uaminifu.
Wapendwa wana wa Mungu,
malaika hufuata pale Mungu alipo, lakini Mungu ufuata pale Padre alipo. Mt.
Yohane Maria Viane alisema, "acha eneo na sehemu yoyote bila Padre kwa
miaka ishirini, matokeo yake watu wataanza kuabudu wanyama." Padre kwa
Kanisa ni zawadi kubwa kuliko zawadi zote zitolewazo. Daima tuwaombee mapadre
wetu, na tuliombee Kanisa kama somo letu la Injili linavyochanganua changamoto
katika wito huu na ufuasi wa kila mmoja wetu ndani na katika Kristo Yesu.
Injili
ya leo tunaona wanafunzi wa Yesu wanashitumiwa kwa kutokufunga kadiri ya mila
na desturi za kiyahudu. Yesu anawakumbusha wasome alama za nyakati. Wazo kuu
hapa ni hili: nini hatma ya kile unachokifanya? Kama Yesu ndiye kila kitu, je wale
walio karibu naye wafuate lipi? Ni kwa mtazamo huo Yesu anawajibu, “Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu
bwana-arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao
hawawezi kufunga,” Mk 2:19. Hivyo kile wasichokijua jibu lake ni Kristo. Wakati
wa kuyafanya hayo utakuja kadiri na mila na desturi zetu. “Lakini siku zitakuja
watakapoondolewa bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku ile,” Mt 2:20.
Kristo ndiyo kila kitu
kwetu. Yesu anataka tuanze yote naye. Yesu hataki habari za historia zetu, bali
utayari wetu wa kuanza naye katika kweli na haki. “Wala hakuna mtu atiaye divai
mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile,
divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba
vipya,” Mk 2:22. Je, upo tayari kuanza yote na Kristo? Basi kuwa wazi kuhusu
wewe mwenyewe na jiachie mikoni mwa Kristo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nayaweza mambo yote katika yeye
anitiaye nguvu,” Flp 4:13
Tusali:
Ee Yesu Mwema, wewe ndiye haki yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario