ALHAMISI WIKI YA 1
YA MWAKA-I
Somo: Ebr 3:7-14
Zab: 95:6-7, 8-9, 10-11
Injili: Mk 1:40-45
Nukuu:
“Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja
wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai,” Ebr 3:12
“Lakini
mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu
wa dhambi,” Ebr 3:13
“Kwa maana
tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabit wetu kwa
nguvu mpaka mwisho,” Ebr 3:14
“Akaja
kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka,
waweza kunitakasa,” Mk 1:40
“Naye akamhurumia,
akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na
mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika,” Mk 1:41-42
“Akamkataza kwa nguvu,
akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote,
ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika
kwako, iwe ushuhuda kwao,” Mk 1:43-44
TAFAKARI: “Naye
akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.
Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.”
Wapendwa wana wa Mungu,
pamoja na uovu tulionao, hali hiyo isiwe kibali cha kuendelea kufanya uovu
tukijidanganya kuwa Mungu hayaoni matendo yetu. Mungu wetu ni Huruma, Upendo,
Msahama, Haki na Kweli. Kukaa kwake kimya pale tunapomkosea kunathibitisha mambo
makuu mawili: kwanza, kunathibisha ukweli wa sifa hizo nilizozitaja kuhusu
Mungu. Pili, Mungu hataki tuangamie bali tuongoke na kumrudia. Mungu hutupa muda
wa kutosha kwa ajili ya wongovu wako. Bwana wa Majeshi asema hivi, “Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake
alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa
hai. Kwa sababu atafakari, na
kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa,”
Eze 18:27-28. Hivyo Mungu hafurahii hata kidogo kuangamia kwa mtu kutokana na
dhambi zake. Tatizo ni pale tunapojifariji nafsi zetu kwamba bado tuna muda wa
kufanya maamuzi.
Mungu wetu hachezewi
rafu wala hapewi rushwa. Yanipasa kuishi kweli ndani yangu mwenyewe na kweli
hiyo ijithihirishe kwa Mungu kwa matendo yangu mema na yanayompendeza Mungu.
Yesu mwenyewe anatukumbusha kweli hii na kusema, “Si
kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali
ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 7:21. Hivyo nionje
moyoni nitamkayo mdomoni. Hakika nisipoyafanya mapenzi ya Mungu nijiandaye kwa
kupigwa mshangao kama walivyopingwa na mshangao wana wa Israeli. “Hapo baba
zenu waliponijaribu, wakanipima, Wakaona matendo yangu miaka arobaini,” Ebr 3:9
Wapendwa wana wa Mungu,
tumeona kwa undani kwamba Mungu wetu si wakuchezewa na wala si wamajaribio.
Sehemu yetu ya pili tumtazame Mungu wetu katika kutenda kwake. Mungu wetu
hutenda kadiri unavyojiachia kwake bila kujibakiza. Ingawa hatumuoni kwa macho yetu ya kibinadamu, Mungu wetu yu
hai. “Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa
kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai,” Ebr 3:12. Hivyo Injili yetu ya leo inathibisha jambo hili. “Akaja
kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka,
waweza kunitakasa,” Mk 1:40. ‘Ukitaka, waweza kunitakasa.’ Maneno haya yamebeba
kauli ya kujiachia pasipo shaka.
Ni kumruhusu Mungu
atende kadiri aonavyo na kumpendeza. Nasi waja wake tunajua wazi kabisa hawezi
kutupatia kile kisicho uzuri wake. “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi
mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa
maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye,
mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au
akiomba samaki, atampa nyoka? Basi
ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi
sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?” Mt 7:7-11
Kwa kuona nia ya mtu yule na kujiachia
kwake pasipo shaka, Yesu “akamhurumia, akanyosha
mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na mara ukoma
wake ukamtoka, akatakasika,” Mk 1:41-42. Wewe na mimi leo yawezekana ukoma wetu siyo wa
ngozi bali haya yafuatayo; choyo, wivu, kiburi, jeuri ya pesa, jeuri ya
madaraka, ukatili, dharau, kejeli, kutojali utu wa watu, matusi, lugha
zisizofaa kwa watu, na mengine mengi tu yasiyompendeza Mungu. Katika hali hii
na mazingira haya huwezi kuwa mshirika na Kristo Yesu hata kidogo. “Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana
na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho,” Ebr 3:14. Yanipasa
kujifunza kwa Kristo Yesu huruma, upendo, unyenyekevu, upole, kweli, na haki.
Ni wajibu wa kila aliyebatizwa kukemea na kuonya aina hizo za ukoma
nilizozitaja hapo juu hata kama atendayo hayo ujiona mkubwa kama tembo na
wengine ni sisimizi tu. “Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili
mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi,” Ebr 3:13
Ndugu yangu tuliyesafiri wote katika tafakari
hii, wamwamini Yesu Mwana wa Mungu? Baada ya uponyaji huu, Yesu anamwamuru mtu
huyu aende kwa makuhani kujitambulisha. Kujitambulisha kwa makuhani ilikuwa ni
wajibu wa lazima ili kupata kibali cha kushiriki tena maisha katika jamii. Wale
wote ambao walifikwa na ukoma walitengwa na jamii na kuishi sehemu yao wenyewe.
Makuhani ndio waliokuwa na uwezo kisheria wa kuwatenga hawa wenye ukoma na
kuwarudishia stahiki zao pale wanapopona ugongwa huu. “Akamkataza kwa nguvu,
akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote,
ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika
kwako, iwe ushuhuda kwao,” Mk 1:43-44. Yesu anathibitisha kweli yeye ni Masiha
na Mfalme wa Upendo na Amani, na Haki. Yesu anaturudishia heshima na
kutambulika kwetu tena kati ya watu. Hakika “wala yaliyo juu, wala yaliyo
chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu
ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu,” Rum 8:39. AMINA!
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa
kuwa Bwana ndiye mwenye haki, Apenda matendo ya haki, Wanyofu wa moyo watamwona
uso wake,” Zab 11:7
Tusali: Ee Yesu
Mwema, wajua ukoma wa kila mmoja wetu, twakaka nawe twaomba tutakase. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario