JUMAMOSI WIKI YA 3 YA MWAKA-I
Somo:
Ebr 11:1-2, 8-19
Zab:
Lk 1:69-70, 71-72, 73-75
Injili:
Mk 4:35-41
Nukuu:
“Basi imani ni kuwa na
hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1
“Hawa wote wakafa
katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na
kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi,” Ebr
11:13
“Naye mwenyewe
alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu,
si kitu kwako kuwa tunaangamia?” Mk 4:38
“Akaamka,
akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa
shwari kuu,” Mk 4:29
“Akawaambia,
Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?” Mk
4:40
“Wakaingiwa
na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?” Mk
4:41
TAFAKARI:
“Hamna imani bado?”
Wapendwa wana wa Mungu,
wazo kuu la leo, yaani, ‘imani katika maisha na sintofahamu zake tukilenga lile
tumaini la kweli, yaani, uwepo wa Mungu, tunalipata kutoka somo letu la leo,
yaani, waraka ule kwa Waebrania kama tulivyosikia. Maisha kama zawadi ya Mungu
kwetu na mali yake, yana changamoto zake. Maisha ni changamoto kwa sababu
yanatuwajibisha kuishi kadiri ya kile tulichoitiwa na ndani ya hicho kitu,
yaani, wito huo, ndipo penye ule utakatifu ambalo ndilo tumaini lako mara baada
ya maisha ya hapa duniani. Maisha ni changamoto katika maana ya kwamba, tupo
hapa duniani kwa muda mfupi tu. Hivyo, maisha yamaanisha ‘kuzaliwa, kustawi, na
mwisho wa siku kunyauka.’
Kama kweli nataka
kulifikia tumaini lile, yaani, uzima wa milele, yanipasa kuishi kadiri ya
mapenzi ya Mungu, na wakati huo huo kujiandaa vyema kwa sababu siijui siku wala
saa ya kutwaliwa kwangu katika ulimwengu huu. Na Yesu katika hili anasema,
“Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja
mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa,” Lk 12:39. Kumbe
huu ndio wito wa kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu, na ndiyo maana halisi ya
kukesha. Kukesha tu haitoshi kama sintojiandaa vyema kwa sababu siri ile ya
siku ya mwisho imefichwa kwangu. Hivyo Yesu anasema, “Nanyi jiwekeni tayari,
kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu,” Lk 12:40
Hata hivyo kuzikabili sintofahamu za
maisha kadiri ya wito wangu, na wakati huo huo kukabiliana nazo, yanipasa kuwa
na uelewa sahihi wa imani ya kweli. Waraka huu kwa Waebrania Somo unaelezea “imani
ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr
11:1. Kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo ni ‘kutokuwa na shaka yoyote ilhali
ukiwa umeyakabidhi yote mikono mwa Mungu katika maana ya ufahamu wa kweli wa
kile ukiaminicho, na wakati huo huo umaana wake (rationality and significativity).’
Imani tu bila kubeba ufahamu wake na umaana wake ni kishawishi kikubwa cha
kuanguka kwenye ujinga na upumbavu. Ni kwa mantiki hii ‘imani siyo ushuhuda tu
uliobebwa katika miujiza na alama nyingine kama hizo.’ Imani ni zaidi ya hayo
licha kwamba kama yapo katika kweli uimarisha imani changa. Imani ni zaidi ya
ishara tuzionazo kwa sababu, Imani “ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr
11:1b.
Maisha huwa na maana
kwa kila changamoto tunayokutana nayo kwa sababu maisha hayo yamepewa maana kwa
imani ile ya kweli ibebayo maisha yako kama nilivyokwisha sema kuhusu imani.
Muono huu wa imani ndiyo utupao tumaini hata pale tunapozungukwa na changamoto
katika maisha na sintofahamu zake. Ni ndani ya maisha haya yenye maana “kwa
imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa
urithi; akatoka asijue aendako,” Ebr 11:8. Ibrahimu hakushikamana na mali na
mazingira yake aliyoyazoea kwa sababu aliona maisha mengine kwa imani na
tumaini la kweli hata kama hayakuwa yamefunuliwa wazi kwake kwa wakati ule. Ni
mara ngapi kwa kukosa maana ya maisha na imani ya kweli twafa kwa shinikizo la
damu tunapoamuriwa kuhama vituo vyetu vya kazi tulivyovizoea? Ibrahimu ni
tofauti kabisa kwa sababu, “kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi,
kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo,
warithi pamoja naye wa ahadi ile ile,” Ebr 11:9. Kumbe kitu cha maana katika
maisha yetu si pale tulipo, bali maisha ya pale tulipo. Mtu wa kuyaboresha yawe
mazuri zaidi na sehemu nzuri zaidi ya kuishi ni wewe mwenyewe kwa sababu u
kiumbe shirikishwa cha Mungu katika uumbaji wa pili na unaoendelea. Maisha
yasiyo na maana hata kama utakuwa huru, ni sawa na kuishi gereza lisilokuwa na
kikomo.
Ni katika ufahamu huu
na umaana wake katika maisha yabebwayo na imani ya kweli na tumaini la kweli,
“Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba; alipokuwa amepita wakati wake;
kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu,” Ebr 11:11. Tukumbuke kuwa
Sara alibeba mimba akiwa na umri wa miaka 90, na Ibrahimu akiwa na miaka 100,
Mwa 17:17, kitu ambacho kwa hali ya kawaida ni vigumu kutokea, ila kwa Mungu
vyote vyawezekana tunapojisalimisha kwake. Hata pale Mungu alipoyafanya yale
yasiyowezekana, yaani, kuipatia familia hii mtoto-Isaka, Ibrahimu hakukosa utii
mbele ya Mungu kwa sababu imani yake ilimfanya ayaweke matumaini yake yote kwa
Mungu. Hivyo, “kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na
yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee,” Ebr 11:17.
Kwa uhakika Ibrahimu anatambua kwamba, “Nchi na
vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1.
Ibrahimu hapati maana ya maisha yake kwa utajiri aliokuwa nao, bali tumaini
lile alilokuwa nalo kwa Mungu mwenye milki zote na kila kitu kwake.
Kujisalimisha kwa Mungu
katika ufahamu na umaana wake ndiyo maisha yenyewe kuelekea lile tumaini la
kweli, yaani, maisha ya umilele. Ni katika kujisalimisha huku na katika maana
hiyo, “hawa wote (Ibrahimu na Sara) wakafa katika imani, wasijazipokea zile
ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa
wageni, na wasafiri juu ya nchi,” Ebr 11:13. Ndugu yangu, “Mungu ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye
aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu,” Isa 45:18,
na mwisho wa siku wale wote walio yasalimisha maisha yao kwake pasipo shaka,
kwa ufahamu na umaana wake, “waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya
mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea
mji,” Ebr 11:16. Ugoto wa maisha yetu hapa duniani ni mwanzo wa maisha ya
milele mbinguni kwa sababu tumeumbwa ili tuishi milele.
Injili ya leo
inatufundisha kwamba tukiamini nguvu na uwepo wa Mungu yote huwa salama. Maisha
ni kama chombo cha kusafiri baharini, kuna nyakati husongwa na dhoruba kali. Chombo chetu cha kusafiri,
yaani, “Mtumbwi” pale tulipo, iwe maisha ya ndoa, au kitawa huanza kuzama
kutokana na dhoruba kali, yaani,
“changamoto” nyingi katika maisha. Hata hivyo, katika hali hii Bwana
wetu Yesu Kristo si kwamba yupo mbali na dhoruba hizi. Katika sintofahamu
habarini, wanafunzi wake Yesu walianza kupiga mayowe kwa hofu ya kuzama maji.
Yesu alikuwa nao, ila kalala. Wanafunzi wanamlalamikia Yesu wakiwa na tafsiri
ya Yesu kutokujali kuagamia kwao. Yesu hana muda wa kujibizana nao zaidi ya
kuokoa maisha kwanza. “Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza,
utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu,” Mk 4:29. Ndipo Yesu akawaambia, “Mbona mmekuwa
waoga? Hamna imani bado?” Mk 4:40.
Mara nyingi tunapopatwa na matatizo na
mahangaiko katika maisha tunakosa utulivu na kuhangaika hapa na pale, kuagua
kwa mganga wa kienyeji moja na mwingine, na kufanya matambiko kwa kila mzimu
aliyeko kwenye ukoo. Kitu cha kwanza ndugu yangu unachopaswa kufanya ni
kuutafuta utulivu wa ndani. Utulivu wa ndani tunaupata kwa Kristo mwenyewe kwa
kuwa na Imani naye. Yesu anatuambia, “Njoni
kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu;
kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini
mwenu; kwa maana nira yangu
ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi,” Mt 11:28-30. Je, yupo zaidi ya Yesu? Kwa
akili zako tu bila Yesu hutoweza, kwa umashuhuri wako tu bila Yesu hutoweza,
kwa utajiri wako tu bila Yesu hutoweza, na kwa nguvu ya madaraka yako tu bila
Yesu hutoweza pia. Basi na tuwe na hofu ya Mungu ndani yetu hata kama
hatujamjua Yesu. Tuongozwe na dhamiri njema katika utu wema.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na
mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao,” Zab 86:5
Tusali:-Ee Yesu Mwema,
wajua kuamka kwangu na kudondoka kwangu. Kamwe usiniache kugaagaa katika tope
la dhambi zangu. Wewe u tumaini la kweli, na kwako twapata tulizo la kweli.
Niinue. Amina.
No hay comentarios:
Publicar un comentario