martes, 24 de enero de 2017

TAFAKARI: SIKUKUU YA WATAKATIFU TIMOTEO NA TITO, MAASKOFU


SIKUKUU YA WATAKATIFU TIMOTEO NA TITO MAASKOFU

JANUARI 26

Somo: 2Tim 1:1-8

Zab: 24:1-2, 3-4, 5-6

Injili: Mk 4:21-25

Nukuu:

“kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu,” 2Tim 1:2

“nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo,” 2Tim 1:5

“Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi,” 2Tim 1:7

“Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu,” 2Tim 1:8

Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi,” Mk 4:22

“Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa,” Mk 4:24

“Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa,” Mk 4:25

TAFAKARI:Kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Watakatifu Timeteo na Tito Maaskofu. Timoteo na Tito, wanafunzi na washirika wa Mtume Paulo walikuwa mstari wa mbele kwa kulijenga na kuliimarisha Kanisa la Efeso, na baadaye huko Crate. Wote wawili walielekezwa na Mtume Paulo kwa barua zilizojulikana kama barua za kichungaji. Ndani ya maelekezo ya barua hizi kulikuwa na matamko hasa pale kulipotokea upotoshwaji wa jambo fulani, na maonyo kwa mafundisho ya waamini na wachungaji.

Somo letu la kwanza tunaona Mtume Paulo akiandika barua hii angali gerezani. Na hapa inaonyesha yale aliyowaandikia Wafilipi sasa yameshatokea. Hivyo Paulo Mtume anamtuma Timoteo kwao ili naye apata habari zao. “Walakini natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo afike kwenu karibu, nifarijiwe na mimi, nikiijua hali yenu. Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami, atakayeiangalia hali yenu kweli kweli. Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu. Ila mwajua sifa yake, ya kuwa ametumika pamoja nami kwa ajili ya Injili, kama mwana na baba yake. Basi, natumaini kumtuma huyo mara, hapo nitakapojua yatakayonipata,” Flp 2:19-23

Ni kweli kwamba Mtume Paulo alipendezwa sana na utendaji, ushiriki, na ushupavu  wa imani aliokuwa nao Timeoteo. Mtume Paulo anamchukulia Timoteo kama mwanaye. “Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu,” 2Tim 1:2. Imani aliyokuwa nayo Timoteo ilikuwa thabiti, na kamwe hakutetereshwa na jambo lolote. Akiwa gerezani Paulo anayasema haya juu ya Timoteo, “nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo,” 2Tim 1:5

Kama ilivyokuwa uhusiano wa karibu wa Mtume Paulo na Timoteo, ndivyo ilivyokuwa kwa Tito. Barua ndogo kwa Tito tunaona Mtume Paulo anakutana kwa mara ya kwanza na Tito huko Antiokia bila shaka mwaka (48 bk), na Tito alimsindikiza Mtume Paulo kwenye ule mtaguso wa Yerusalemu, Mdo 15. “Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nalipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja nami,” Gal 2:1. Kwa nyakati mbalimbali Tito anawatembelea Wakristo wa Korintho. “Lakini ahimidiwe Mungu atiaye bidii ile ile kwa ajili yenu katika moyo wa Tito. Maana aliyapokea kweli yale maonyo; tena, huku akizidi kuwa na bidii, alisafiri kwenda kwenu kwa hiari yake mwenyewe,” 2Kor 8:16-17. Mtume Paulo alimtuma huko kwa sababu kuu mbili; kwanza, kuimarisha maisha ya imani ya jumuiya hiyo ya Korintho. Na pili, kwa shughuli za kimisionari.

Uinjilishaji huu ulikuwa mgumu sana kwa sababu walipambana na kila aina ya upinzani kwa ajili ya habari njema ya wokovu. Mtume Paulo anajua taabu zote hizo na anasema, “Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi,” 2Tim 1:7. Ni kwa kuushinda woga habari njema zilienea kila pande za dunia. Nasi leo tunajionea na kujivunia majitoleo yao katika kulihubiri neno la Mungu. Ujumbe anaotupatia leo Mtume Paulo kuhusu habari njema ya wokovu ni huu: “Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu,” 2Tim 1:8. Yanipasa mimi na wewe kusimama imara katika imani thabiti pale nilipo. Anza umisionari huo hapo ulipo kwa kuona kama Kristo, kuwaza kama Kristo, Kuamua kama Kristo, na kutenda kama Kristo.

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna binadamu asiyetaka kupendwa na hakuna asiyeyajua maumivu ya kutokupendwa. Upendo ni sehemu muhimu sana kwa mtu yeyote yule ikiwa ni pamoja na makuzi yake. Upendo wa kweli utuweka pia karibu na viumbe vile visivyo na utashi, mathalani; paka na mmbwa. Tunapowaonyesha upendo wa dhati viumbe hivi visivyo na utashi hutambua upendo huo na kwa namna moja au nyingine hurudisha upendo huo kwetu. Je, kama viumbe hivi visivyo na utashi urudisha upendo kwetu kwa yale tunayowafanyia itakuwaje vizuri na vyema tukipendana sisi kwa sisi?  Hivyo ni vyema “tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia,” Ebr 10:24-25. Na siku hiyo ni kiama ya kila mmoja wetu.

Tumeumbwa ili tuwe na ushirika wa kweli sisi kwa sisi. Hivyo hakuna aishiye kama kisiwa bali tunategemeana katika kukamilishana. Na hili ndilo lile tumaini litupelekalo kwa Kristo aliyemwaminifu kwetu, na kwa Mungu Baba. Ni wajibu wangu na wako kulishika “sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu,” Ebr 10:23. Ukamilisho huu huja pale tunapotambua uwezo na mapungufu yetu. Hivyo kujitoa kwa ajili ya mwingine ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Hii ndiyo changamoto ya upendo kwamba ujitoavyo ndivyo navyo utakavyokirimiwa siku ile ya mwisho. ‘Kipimo cha upendo ni kupenda bila kipimo,’ Mt. Augustino. Naye Yesu “Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa,” Mk 4:24. Je, usipofanya chochote juu ya jirani yako ili hali unajua wajibu huu itakuaje?

Katika jambo hili Yesu anasema, “Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa,” Mk 4:25. Mwenye kitu ni yule anayetambua anao wajibu wa kufanya zaidi kwa ajili ya wengine. Na asiye na kitu ni yule anayefikiri hana wajibu wa kufanya chochote kwa ajili ya wengine na hasa wenye uhitaji. Kwa hawa kundi la pili Yesu anasema, “hata kile alicho nacho atanyang’anywa.”

Ndugu yangu, lazima tuelewa kwamba siyo sisi tuliyeanza kumpenda Mungu, bali ni Mungu mwenyewe alianza kutupenda, na kwa pendo hilo alichagua kutuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Hivyo kupenda ni amri ya Mungu mwenyewe aliyoiweka ndani mwetu, ndani ya mioyo yetu. Hivyo upendo huo lazima uzae matunda kwa kujitoa kwa wengine bila kujibakiza. Na Yesu analisema jambo hili kwa ufasaha, “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16. Ndugu yangu lazima ufanye kitu kwa ajili ya baraka na neema Mungu anazokujalia kila siku.

Hakuna shaka ya baraka na neema za Mungu pale tuyafanyapo mapenzi ya Mungu bila kujibakiza. Tulivyo navyo vyote ni mali yake mwenyewe na tunapovitumia kwa mapenzi yake ndivyo tunavyozidishiwa na kubarikiwa zaidi. “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1. Je una kilicho chako zaidi ya dhambi zako? “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake, Ebr 10:19-20, na tupendane kama alivyotupenda upeo, Yoh 13:1. Ndugu yangu, hakuna aliyekuwa masikini kwa kutoa, na ndivyo ilivyo kwa baraka huvuta baraka.

Tumsifu Yesu Kristo!

Watakatifu Timoteo na Tito Maaskofu. Mtuombee

“Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani,” Mit 11:28

Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!” 1Kor 9:16

Tusali:-Ee Yesu, nifundishe kupenda kama unavyonipenda. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario