jueves, 12 de enero de 2017

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 1 YA MWAKA-I


JUMAMOSI WIKI YA 1 YA MWAKA-I

Somo: Ebr 4:12-16

Zab: 19:8, 9, 10, 14

Injili: Mk 2:13-17

Nukuu:

“Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo,” Ebr 4:12

 “Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi,” Ebr 4:15

 “Hata alipokuwa ameketi chakulani nyumbani mwake, watoza ushuru wengi na wenye dhambi waliketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwa maana walikuwa wengi wakimfuata,” Mk 2:15

 Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi,” Mk 2:17

TAFAKARI:Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

Wapendwa wana wa Mungu, utabiri wa malaika juu ya kuzaliwa kwa Yesu, uliweka wazi juu ya kile anachokijia Yesu katika ulimwengu huu. Malaika Gabriel anamtoa hofu Yusufu mume wa Bikira Maria juu ya mimba ile kwani Yusufu alikuwa mtu wa haki na hakupenda makuu. Hivyo njia ya pekee ni kumwacha kimya kimya mkewe. Malaika akamwambia Yusufu, “Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao,” Mt 1:20-21. Hivyo Yesu anathihirisha ukweli huu katika Injili ya leo wakati Mafarisayo wanapowashambulia wanafunzi wa wake kuona Yesu anakula na watoza ushuru na wenye dhambi. “Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi,” Mk 2:17. Kristo amekuja na yupo muda wate kutupatanisha na Mungu Baba. Kristo kwetu leo ni daraja imara kuelekea uzima wa milele.

Hakuna hata mmoja kati yetu asiyehitaji huruma, msamaha, na upendo wa Mungu. Hata kama twajiona wenye haki na wasio na hatia, bado tunaitaji upendo wa Mungu. Pendo lake Yesu utuvutia tuwe wake milele. “Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao,” Yoh 17:26. Hivyo uwe una afya ya mwili na roho, au hauna afya hiyo bado wahitaji pendo la Mungu.

Basi wapendwa wana wa Mungu, tusipoteze muda mwingi kuzichunguza dhambi za watu kama walivyopoteza muda huo Mafarisayo na kusahau wongofu wao wenyewe. Yesu anasema hili juu ya yeyote yule mwenye kupoteza muda wake kwa kuzitazama dhambi za mwenzake bila kuhangaikia wongofu wake mwenyewe. “Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako,” Mt 7:5. Ninapogundua mwenzangu kaanguka katika dhambi, tendo lile liwe kioo cha kujitazama kwanza ndani ya nafsi yangu kabla ya kuhukumu. Tendo hilo liwe kielelezo cha mimi kuiona huruma ya Mungu ndani yangu na kwa yule aliyedondoka katika dhambi. Na mara zote nionapo tendo hilo nijiulize hivi; “ya mwenzangu yamejulikana, yangu yamesitiriwa kwa muda tu, yanipasa kutubu.”

Tusipoona na kuonja huruma ya Mungu ndani ya nafsi zetu na kwa wenzetu, hatuwezi kukua kiroho. Nisipoonja hali hii ndani yangu, ukristo wangu na huduma niitoayo haina maana yoyote  zaidi ya uigizaji tu. Na kunakuwa kiroho kila siku tunapolisikia neno, lipokea neno, litafakari neno, lishirikisha neno, na kuwa shuhuda na neno la Mungu. Na kinyume chake ni sawa, yaani, huwezi lishuhudia neno pasipo lishirikisha  neno hilo kwa wengine. Huwezi lishirikisha neno kama hujalitafakari neno hilo kwa undani. Na hutoweza lipokea neno kama hujalisika.

Jambo la msingi kupita yote ni kulijua neno la Mungu na kulishika kikamilifu. Hii ndiyo hekima ya kwanza kabisa inayolenga sababu ya kuumbwa kwetu na kuwa katika ulimwengu huu. Uzima huu tunaupata katika neno la Mungu. Neno la Mungu ndiyo kirutubisha na kijenga kinga ya mwili na roho. Tukikosa kirutubisho hiki, hakika afya yetu itakuwa katika mashaka na tuupatapa ugonjwa wowote ule hatutakuwa salama kwa sababu hatuna kinga.

Hivyo kulichagua neno la Mungu ni muhimu kuliko fimbo za enzi na vitu vya enzi, wala mali sikuifananisha na kitu cha thamani; mradi dhahabu yote ya nchi ni kama mchanga kidogo, Hek 7:8-9. Katika neno vyote vilikuwa kama Mungu alivyoamuru. Mungu aliumba kwa neno na vyo vilifanyika kama tunavyoviona. Hivyo “Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo,” Ebr 4:12.

Wapendwa wana wa Mungu, je tunashiriki neno hili kikamilifu katika jumuiya zetu? Mbona leo jumuiya zetu zimekuwa za kina mama na watoto tu? Vijana wa kike na wakiume mpo wapi? Ni vyema kujua kweli hii juu ya nafasi na upendo wa Mungu kwetu, yaani, “hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu,” Ebr 4:13. Mimi na wewe hatuna chochote cha kumficha Mungu. Na kama kipo na tunafanya hizo ni sawa na falsafa ya mbuni, yaani, kuficha kichwa chake kwenye mbawa zake na sehemu yote ya mwili wake kubaki wazi. Huku ni kujifariji kipumbavu.

Ndugu yangu, pamoja na udhaifu wetu kama wanadamu, ni vema kushika vyema maagano yetu. Hapo tutakutana na kuhani wetu mkuu Yesu Kristo. Yeye hakutereka kwa kile alichokijia licha ya mateso na kifo kile cha aibu pale msalabani. “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu,” Ebr 4:14. Na kuhani huyu ndiye aliye pekee na mwenye uwezo wa kuchukuliana nasi hata katika udhaifu wetu. Hiki ndicho alichokijia kwa ajili yako na yangu. “Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi,” Ebr 4:15. Kwake Kristo ipo na rehema. “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji,” Ebr 4:16. Na ndani na katika Kristo Yesu hatutapungukiwa chochote.

Tumsifu Yesu Kristo.

Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,” Zab 145:8

Tusali:-Ee Yesu Mwema, nakutumainia. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario