jueves, 19 de enero de 2017

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 2 YA MWAKA-I


JUMAMOSI WIKI YA 2 YA MWAKA-I

Somo: Ebr 9:2-3, 11-14

Zab: 47:2-3, 6-7, 8-9

Injili: Mk 3:20-21

Nukuu:

Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele,” Ebr 9:11-12

 “Basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?” Ebr 9:14

Mkutano wakakusanyika tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate,” Mk 3:20

“Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili,” Mk 3:21 

TAFAKARI: “Si kwa damu ya mbuzi na ndama, kwa sadaka yake Kristo yatosha.”

Wapendwa wana wa Mungu, kwa nyakati mbalimbali Mungu alifanya maagano na watu wake kwa malengo mbalimbali yakilenga ushirika wake na viumbe vyake, katika safari nzima ya kuvikomboa, na hasa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi. Agano hili lilifanya kuaminiana na kutekeleza maagizo yake kwa pande zote mbili. "Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda,” Kut 24:3. Mungu haikumpasa kujisainisha katika agano kwa sababu yeye mwenyewe ni UAMINIFU, na kwamwe katika Ukuu wake hawezi kwenda kinyume chake mwenyewe.

Maagano haya kama ishara ikiwa ni kielelezo kwa upande wa binadamu iliendana na uteketezaji wa viumbe vingi visivyo na doa. Damu ya viumbe hili  vilihesabika maka ndiyo muhuri na kusahilisha muungano huu wa kiagano. “Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote,” Kut 24:8. Hizi ni hatua za awali katika safari nzima ya mwokovu wetu. Je, kwa nini Mungu hakulifanya jambo hili mara moja tu na watu wake wakamwelewa? Bila shaka tendo na safari hii ya wokovu wa Mwanadamu umepita katika hatua mbalimbali kwa lengo la kumfanya mwanadamu huyu atambue uzuri na umaana wa thamani ya wokovu wake, na uwepo wa Mungu katika maisha yake.

Yesu Kristo ndiye anayebadili kabisa mwelekeo na mtazamo wa sadaka hizi za kuteketezwa. Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele,” Ebr 9:11-12. Kristo ndiye ukamilifu wa sadaka zote zile zitolewazo. Sababu kubwa ni Mungu kupendezwa na Kristo, “huyu ni Mwanangu, Mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.” Mt 17:5. Tendo hili la utambulisha wa Kristo kile alicho lilitanguliwa na tendo la kumwilishwa kwake. Huu ndio mpango wa Mungu wakati ulipotimia, Gal 4:4-5. Hivyo, Basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?” Ebr 9:14. Ndugu yangu unayemwamini Kristo elewa umekombolewa kwa damu yenye gharama kubwa. Ukristo wako ni wathamani sana. Hakuna sababu ya kujiona mnyonge hata kidogo. “Na kwa sababu hii ni mjumbe wa agano jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele,” Ebr 9:15 

Wapendwa wana wa Mungu, ulimwengu wa ushindani tunaoishi leo, ni ulimwengu uliopunguza kwa kiasi kukubwa thamani ya mtu na utu wake. Leo tunafurahia sana kukua kwa sayansi na teknologia na hivyo kurahisiha mambo mengi na wakati huo huo kuhathiri utu wa mtu. Katika hali hii ya ushindani ni wazi ‘mwenye nguvu upishwa apite.’ Ni ukweli pia katika hali hii ambapo tunaona utu wa mtu kutokuheshimiwa na wakati mwingine kulinganishwa na kitu, ni wazi kuna anguko kubwa sana la kukua kiroho.

Kukua kiroho ni kufanana na Kristo katika kuona, kufikiri, kuamua na kutenda. Ipo mifano mingi ya namna aonavyo Yesu. “Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena kuwaaga wakifunga sipendi, wasije wakazimia njiani,” Mt 15:32. Yesu anaona zaidi ya kile kionekanacho kwa macho ya kawaida. Ni kuona katika kuzama ndani ya fumbo zima ya kile ukionacho kwa macho. Namna hii ya kuona ni hatua ya kufanana na Kristo.

Yesu hufikiri tofauti akilenga lililo zuri na la umilele. Naye anatutaka tufikiri kwa mwelekeo huu, anasema, “Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao? Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii,” Mt 7:9-12. Kumbe kukua kiroho ni kuwafikiria pia wengine na kuwapenda kama unavyojipenda. Ni kutambua unaishi katika jamii, na unawajibu wa kufikiri na jamii husika.

Maamuzi ya Yesu yaliwashangaza wengi na hasa wale ambao waliosukumwa na hisia, hasiri, visasi, na hata utekelezaji wa sheria mbovu katika jamii. Yesu mara zote anakutaka utoapo hukumu uende mbali ya kile kinachokuruhusu kufanya au kutekeleza hukumu hiyo. Tazama jinsi Yesu anavyotoa hukumu juu ya mwanamke yule aliyeletwa kwake kwa kosa la uzizi. “Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati,” Yoh 8:7-9. Kumbe kukua kiroho ni kujiweka katika hali ya mtuhumiwa kabla ya kutoa hukumu husika. Lengo ni kumpata mwovu kuliko kumpoteza.

Kutenda kwa Yesu kulishangaza wengi na hasa wanafunzi wake. Kutenda kwa Yesu ni kwa kutumika kuliko kutumikiwa. “aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi,” Yoh 13:4-5, 12-14. Kumbe kufanana na Kristo ni kutenda kama alivyotenda. Kutenda kwa Yesu wakati mwingine kulitafsiriwa vibaya kwani kulienda zaidi ya uwezo wa mwanadamu. Na hili linajitokeza kwenye Injili yetu ya leo. “Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili,” Mk 3:21. Na yote haya Yesu anayafanya kwa upendo bila kujibakiza. Aliyafanya haya kiasi kwamba alikosa hata muda wa kula na wakati mwingine kupumzika kama mwanadamu. “Mkutano wakakusanyika tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate,” Mk 3:20. Ndugu yangu, embu tujichunguze tume zetu. Yawezekana tunajionea huruma sana na kutumika kidogo sana.

Wapendwa katika Kristo, namna hii ya kukua kiroho, yaani, kufanana na Kristo Yesu katika kuona, kufikiri, kuamua, na kutenda ndicho tunachotakiwa tuwe kama kweli sisi ni wafuasi wake Kristo. Maisha yako yakiongozwa na mfanano huu wa Kristo wa kuishi ndani na katika Kristo, kamwe hutofurahia anguko la mtesi wako, bali utamwombea huruma, msamaha, na upendo wa Mungu aliye hai. Ni Mungu tu aliye muumba mtesi wako kwa sura na mfano wake ndiye mwenye uwezo wa kumbadili na kuwa mwema.

Tumsifu Yesu Kristu

“Maana hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu,” Yak 2:13

Tusali:-Ee Yesu Kuhani wetu Mkuu, tukumbushe mara zote kutumika na siyo kutumikiwa. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario