JUMAPILI WIKI YA 3
YA MWAKA-A
Somo I: Isa 9:1-4
Zab: 27: 1, 4, 13-14
Somo II: 1Kor 1:10-13, 17
Injili: Mt 4:12-23
Nukuu
“Watu wale waliokwenda
katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru
imewaangaza,” Isa 9:2
“Umeliongeza
taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, Kama furaha ya wakati wa mavuno,
Kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara,” Isa 9:3
“Kwa
maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea,
kama katika siku ya Midiani,” Isa 9:4
“Kwa
maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe,
ya kwamba iko fitina kwenu,” 1Kor 1:11
“Maana
Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima
ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika,” 1Kor 1:17
“Tokea
wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa
mbinguni umekaribia,” Mt 4:17
“Akawaambia,
Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,” Mt 4:19
“Mara wakaziacha nyavu
zao, wakamfuata,” Mt 4:20
“Mara
wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata,” Mt 4:22
TAFAKARI: “Mara wakaziacha nyavu
zao, wakamfuata,” Mt 4:20
Wapendwa
wana wa Mungu, ikiwa leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya tatu ya mwaka “A”
wa Kanisa, mtihani mkubwa na mgumu kwa mtu yeyote yule siyo hii tuifanyayo
mashuleni na hata vyuoni, bali ni mtihani huu wa “kuamua/maamuzi,” uwe nini
katika maisha yako. Si rahisi kufanya maamuzi hayo na kuchukua njia nyingine
mpya kabisa usiyojua kifuatacho huko mbeleni. Mtu huwa na uhakika kwa kile
alichokiishi jana na anachokiishi leo na sasa. Huu ni mzunguko wa kawaida
katika maisha ya kila mmoja wetu. Kuwekeza maisha yako yote kwa kile
usichokijua humjengea mtu hofu.
Na moja
ya sababu kubwa ya kutokusonga mbele kimaendeleo, mwili na roho ni kushindwa
kuwa na uamuzi au maamuzi kwa muda na wakati ufaao. Na sababu kubwa ya kukwama
ni pale unapoishi imani au fikra za uongo/zisizokuwa kweli. Ahadi na unafuu wa
maisha wa hapa na pale kama mvua za rasha-rasha uchangia sana zubaisho la
maamuzi msingi ya maisha ya mtu. Wengi katika kundi hili hujipoteza wenyewe kwa
kulandani na stadi mpito za maisha, na makundi rika. Je, hujawahi kuona hadi
leo wapo wazee vijana katika muono ila katika uhalisi ni sawa na gari yenye
bodi mpya lakini injini yake kwisha kabisa? Na mara nyingi ni pale tunapoweka
tumaini pasipo tumainiwa.
Je,
hujawahi kuona vijana wazee ambao hujikataa kuishi kile walicho na fursa
walizokuwa nazo na badala yake kuishi namna nyingine kabisa? Hawa ni sawa na
gari zuri sana lakini mafundi walisahau kuweka gia ya kurudi nyuma. Mfumo wa
gari hili ni ‘mbele-kwa-mbele. Kundi hili ni wale ambao yanapowazidi/yanapowashinda
hawakosi kujitundika wenyewe, au kuwatundika wengine. Furaha yao ni kufa pamoja
kwa sababu hawana uwezo wa kurudi nyuma na kutazama pale waliojikwa. Mfumo wa
maisha yao ni sawa na gari lisilo na gia ya kurudi nyuma.
Mitume
wa Yesu Kristo walifanya uamuzi wa kuacha yale waliyoyazoea na yaliyokuwa
yanawapa usalama na kufuata kile wasichokijua wakijisalimisha kabisa katika
hicho. “Mara
wakaziacha nyavu zao, wakamfuata,” Mt 4:20.
Idadi kubwa kama siyo
yote ya Mitume Mtume wa Yesu walikuwa wavuvi. Kazi hii iliwapa usalama, mahitaji
yao, na mkate wao wa kila siku. Yesu
anawaita wamfuate nao wanaacha pale pale waliyokuwa wanafanya na kumfuata.
Uamuzi huu ni mzito sana. “Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya
Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye,
wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi,” Mt 4:18. Embu fikiri leo
kwa kazi unayofanya hasa wale wanaopata kipato kilichonona, aje mtu tu na
kukuambia nifuate. Nini kitakuwa kitu cha kwanza kufanya? Bila shaka utaanza
kumpiga maswali mazito na mwisho kumchukulia kama mwendawazimu hivi.
Mitume hawa wanayaacha
yote na kumfuata. Yesu “Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa
watu,” Mt 4:19. Kuwa wavuvi wa watu ni mabadiliko mazima ya mfumo, namna ya
kutenda, na kuishi. Hapa ndipo tunaposema Mitume hawa walikuwa majitu ya sifa.
Mioyo yao ilikuwa na ushupavu wa hali ya juu. Ni vigumu sana mtu kuubadili
mfumo wa maisha yake aliouzoea.
Wapendwa
wana wa Mungu, maisha yanayoongozwa na malengo lazima yasukumwe na kauli mbiu
yenye mwelekeo wa umilele. Ufupisho wa kile ambacho Kristo anakifanya ndani ya
maisha yetu kimejumuishwa katika kauli mbiu hii: “Tubuni; kwa maana ufalme wa
mbinguni umekaribia,” Mt 4:17. Kauli mbiu hii ya Yesu imeweka
wazi muda maalum wa kuanza mradi huu wa umilele, kudumu kwa mradi huu kabla ya kufikia
umilele, mapaswa ya mradi huu, na
kielelezo kinacho sadifu mradi huu.
Kwa ujumla maisha ya
hapa duniani ni ya muda mfupi ukilinganisha na umilele. Hivyo kauli mbiu hii ya
Yesu inatutaka kutambue ukweli huu wa uchache wa muda tungali hapa duniani. Ninapopata
nafasi ya kuishi hata kwa dakika moja nielewa muda huo haujirudii tena na
nishapunguza muda wa maandalizi kuelekea umilele. Kwa maana nyingine yanipasa
kuishi nikijua nina muda na wakati huu tu katika maisha yangu.
Wakati kwa Mkristo
umetimilizwa na Kristo mwenyewe kwa tendo la Neno kufanyika mwili na kukaa
kwetu, Yoh 1.14. “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa
sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika
Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu,” Ebr
1:1-2. Hivyo Kristo ndiye dira ya maisha yako na yaliyo mafupi hapa duniani
katika dhana nzima ya kujiandaa na umilele. Ufalme wa Mungu umekaribia kwa
sababu Neno huyu, yaani, Emmanueli, ni Mungu pamoja nasi, Mt 1:23. Mungu ambaye
hapo mwanzo alioneka yupo mbali sana na watu sasa kamwilishwa na kuwa sawa na
sisi isipokuwa hakutenda dhambi, 1Pet 2:22.
Wapendwa wana Mungu, pamoja na ukweli kwamba maisha ni jukumu la muda
mfupi, twahitaji hekima ya kutosha kuendana na jukumu hilo la muda Mfupi,
yaani, maisha. Hekima hiyo iniongoze kutambua bila shaka kwamba niliukuta
ulimwengu huu, na nitauacha siku moja ulimwengu huu. Hivyo nielewe ninao wajibu
licha wa muda mfupi kuufanya ulimwengu huu mahali salama pa kuishi, na
paendelee kuwa hivyo hata nitakapo ondoka katika ulimwengu huu. Kwa mantiki
hiyo, mimi na wewe tuwe daima vyombo vya amani, na habari njema. Ingawa tunayo
mengi ya kufanya, hili la kuwa ‘chombo cha amani na habari njema’ liongoze na
kutafsiri yale yote tuyafanyayo. Na tusema daima kama Mtume Paulo, “Maana
Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima
ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika,” 1Kor 1:17. Msalaba wa Kristo
ndiyo kielelezo halisi (mti) ambacho wokovu wetu ulitundikwa juu yake.
Na wokovu wetu
ulijidhihirisha wazi pale Mungu alipochukua hali yetu ya ubinadamu, yaani,
‘neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, “Verbum
caro factum est.” Huu ni upendo mkubwa sana wa Mungu kwetu, na unyenyekevu
wa hali ya juu alioufanya. Mtume Paulo analinena tendo hili kama NEEMA ya ajabu
sana kwetu, ambayo Mungu anakubali kuwa masikini ili mimi na wewe tuwe
matajiri. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa
maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa
matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Hili ndilo kusudio kubwa la Mungu kwetu
la kuchukua hali yetu ya ubinadamu. Mungu anaridhia tendo hili pasipo shuruti
yoyote. Ni upendo tu.
Hakuna shaka yoyote
kwamba kwa tendo hili Mungu yupo tayari kuanza upya nasi. Huu ni ushindi mkubwa sana kwetu, tunapotolewa
katika giza na kuwekwa kwenye mwanga. “Watu wale waliokwenda katika giza
Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru
imewaangaza,” Isa 9:2. Hakika ingawa tunajua siku moja tutakufa, ila kuanzia
sasa kifo hakina nguvu na mamlaka tena kwetu. Jambo hili ndilo litakalo
kamilisha safari yake hapa duniani. Ubinadamu huu wa Yesu, ambao ni tokea zima
la fumbo hili la kumwilishwa ndio uwezekano wa sisi kuwepo pale alipo Mungu,
yaani, Mungu Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Watu wale waliokwenda katika giza
Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru
imewaangaza,” Isa 9:2
Tusali:-Ee Yesu na Mkombozi wetu, tujalie hekima
ya kusoma alama za nyakati zetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario