jueves, 5 de enero de 2017

TAFAKARI: JANUARI 6, KIPINDI CHA NOELI


KIPINDI CHA NOELI

JANUARI 6

Somo: 1Yoh 5:5-13

Zab: 147:12-13, 14-15, 19-20

Injili: Mk 1:7-11

Nukuu:

Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu?” 1Yoh 5:5

Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu,” 1Yoh 5:6 

Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli,” 1Yoh 5:7 

Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe,” 1Yoh 5:10

“Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima,” 1Yoh 5:12 

 “Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu,” Mk 1:8

“Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake,” Mk 1:10

“na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe,” Mk 1:11

TAFAKARI: “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”

Wapendwa wana wa Mungu, neema za Mungu zipo wakati wote katika maisha yetu. Tatizo langu na lako ni kwamba hatujiachii na kujifunua kwa neema hizo. Haturuhusu kuguswa na  neema hizo. Ni sawa na kwenda bafuni kuoga huku ukiwa na mwamvuli. Je, utaguswa na maji hayo? Ndiyo ya Bwana kwetu ni kujiachia kwake pasipo shaka yoyote. Hali hii ya kujiachia kwa Bwana hupaswi kutazama shindwa yako ya nyakati zilisopita.

Mungu hututazama kila siku katika upya wetu. Tunapojisalimisha kwake, Mungu hahesabu makaosa yetu yaliyopita. Rejea habari ya mwana mpotevu (Lk 15:11-32). Hakika angefanya hivyo hakuna ye yote kati yetu angeweza kusimama mbele yake.  Naye Mzaburi anasema, “Bwana, kama wewe ungeheabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?” Zab 130:3

Ni mara ngapi tunaanguka kifudifudi mbele ya Yesu na kujiachia kwake kwa yale yanayotusonga? Hakuna jambo lolote tumwombalo Yesu naye akatupiga kisogo. Yesu anatuambia hivi, “Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yetu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa,” Yoh 15:7. Ndugu yangu tunayesafiri wote katika tafakari hii, huwezi kuushinda ulimwengu wa roho bila kuwa na Yesu Mwana wa Mungu. Mtume Yohane analiona hilo na kuhoji nafsi zetu kwa kusema, Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu?” 1Yoh 5:5. Ni kweli isiyoshaka kwamba yapo mambo mengi katika maisha yetu tunakumbana nayo na hatuna majibu ya moja kwa moja. Bila kuwa na Yesu ndani yako ambaye ndiye njia, kweli na uzima, Yoh 14:6, ni vigumu sana kushinda sintofahamu zako.

Yesu Kristo ndiye kielelezo chetu katika sintofahamu zote zile katika maisha yetu. Huyu ndiye aliyekuja kwetu katika maji na katika damu. Hivyo katika ubatizo wetu tumefanywa wana wa Mungu kupitia kwake, yaani maji, na katika sadaka yake pale msalabani, yaani katika damu, tumefanywa huru kutoka utumwa wa dhambi. Hivyo, “Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu,” 1Yoh 5:6. Kwake Yesu ndiko kwenye utoshelevu wote katika mahangaiko yetu. Utoshelevu huu unawekwa wazi na Mungu mwenyewe siku ile ya ubatizo wa Mwanaye Yesu Kristo, “na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe,” Mk 1:11.

Hata hivyo ukweli huu juu ya Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, ulishathibitishwa na Yohana Mbatizaji kwa ubatizo wake ule wa toba na kusema, “Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu,” Mk 1:8. Ndani na katika Kristo Yesu lipo ondoleo la dhambi. Nguvu na mamlaka hiyo ya Kristo Yesu inafunuliwa kwa ishara hii,  “Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake,” Mk 1:10. Huyu ndiye Roho Mtakatifu na mwenzeshaji, na mwenye kutakatifuza yale yote ayafanyayo Baba na Mwana, kwa sababu Roho huyo ni tokeo la upendo wa Mungu Baba na Mwana-Yesu Kristo. Kweli hii ndiyo kiini cha yale yote tuyaaminiyo na kuyaishi kama Wakristo. Kweli hii yapasa kuwa ndani yako pasipo shaka.

Kweli hii ya Yesu ndani yetu imeshuhudiwa na Roho mwenyewe. Yesu anatoa ushuhuda huu wa Roho wa Mungu ndani yake kwa kusema, “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Alisemalo Kristo ndiye kweli, na alishuhudialo Roho ndiyo utakaso wenyewe. “Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli,” 1Yoh 5:7. Ndugu yangu wayaamini haya?

Ushuhuda huu wa Kristo kwa kinywa chake kuhusu Roho huyu wa Bwana ndani yake ni ushuhuda wetu pale tunapomwamini Kristo. Yote ayafanyayo Kristo si kwa faida yake bali ni faida yako na yangu. Hivyo amini yetu kuhusu Kristo ndiyo pona yetu kwa sababu misioni ya Kristo hapa duniani ni kwa ajili ya wokovu wako na wangu. Hivyo, “Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe,” 1Yoh 5:10. Ni vigumu sana kupata neema hizi za Mungu kama hatujiachii kwa Kristo katika kumwamini na kukaa ndani yake ili uzima wake uwe ndani yetu. Mpendwa katika Kristo, “Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima,” 1Yoh 5:12. Hivyo uzima wa kweli ni ndani katika Kristo.

Wapendwa wana wa Mungu, bado hatujachelewa. Sote mbele ya Mungu tu wapya na Yeye bila kuhesabu makosa yetu, huanza upya nasi kwani lengo lake ni kutupata kuliko kutupoteza. Hii ndiyo huruma ya Mungu kwetu. Hivyo ninapotambua huruma hii ya Mungu katika maisha yangu iwe nafasi ya kubadilika na kubadili mfumo mzima wa maisha yangu kama kweli nataka kuishi katika umilele. Hofu yangu iwe kwa Mungu aliye kila kitu katika maisha yangu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe,” 1Yoh 5:10

Tusali:-Ee Yesu Mwana wa Mungu, nasadiki pasipo shaka kwamba Wewe ndiye Njia, Kweli, na Uzima. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario