JUMATANO WIKI YA 4 YA MWAKA-I
Somo:
Ebr 12:4-7, 11-15
Zab:
103:1-2, 13-14, 17-18a.
Injili:
Mk 6:1-6
Nukuu:
“Ni kwa ajili ya
kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi
asiyerudiwa na babaye?” Ebr 12:7
“Kila adhabu
wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye
huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani,” Ebr 12:11
“mkaifanyie
miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali
kiponywe,” Ebr 12:13
“Tafuteni
kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu
atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya
Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa
unajisi kwa hilo,” Ebr 12:14-15
“Huyu si yule
seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni?
Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake,” Mk 6:3.
“Yesu akawaambia,
Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake,
na nyumbani mwake,” Mk 6:4
TAFAKARI:
“Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake,
na nyumbani mwake.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Yesu anatukumbusha wajibu muhimu sana, yaani, tuviheshimu na kuvienzi
vilivyo vyetu. Pamoja na hayo yote, hukumu yetu iwe ya kweli na haki. Waswahili
wanasema, “masikini mnyongeni, ila haki yake mpeni.” Ni wazi watu wa nyumbani
mwake waliyastaajabia yale aliyoyatenda Yesu lakini hawakuutafakari Umungu
wake, bali waliutazama zaidi ubinadamu wake tena katika mwono wa historia yake.
Nao wanashangaa na kusema, “Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu
yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu?
Wakajikwaa kwake,” Mk 6:3. Hivyo leo ni wito kwetu kwamba tusimdharau mtu kwa
vile tunaifahamu historia yake na asili yake, bali tumtazama katika upya wake.
Ni jambo la kushangaza
leo kuona katika jamii yetu Tanzania baadhi yetu kuwaweka watu fulani, au
makabila fulani, na hata ukanda fulani wa nchi walipotoka kama watu wasio na
maana na kutokuwa na jema lolote. Bila shaka ubaguzi huu unakusudi lake
kimkakati. Hata hivyo mikakati yote miovu ni chukizo kwa Mungu. Kuhusu hatari
hii, Yesu anasema, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe,
na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake,” Mk 6:4. Kutokuheshimka na kupokeleka
kwetu hakutoki nje ya jamii tunayoishi. Mchawi ni sisi wenyewe. Dhambi hii ya
kubaguana kunakotokana na familia zetu, koo zetu, makabila yetu, na elimu zetu
ni mbaya na yakuogopwa sana. Machafuko mengi ya kijamii na hata kufikia hatua
ya mauaji ya kimbari huanza na chokochoko hizi. Hakuna binadamu aliye na
thamani zaidi ya binadamu mwingine. Wewe ni nani na una ubora gani zaidi hata
umdharau mwenzako kutokana na familia yake, ukoo wake, au kabila lake? Tuelewe
kwamba mengine yote hapa duniani ni MBWEMBWE TU!
Tukubali wakati
mwingine tunafanya vibaya sana hata kama jambo hilo linatumika kama utani.
Utani upo kwa watani, na siyo kwa kila anayejisikia kufanya hivyo. Tuwahesimu watu
na utu wao. Tofauti zao ndio uzuri wa Mungu. Hatukuumbwa ili wote tufanane kwa
kila kitu. Ikiwa hivyo basi sisi si watu tena bali mitambo-“robots.” Tumuombe Roho Mtakatifu akaye nasi ili tuweze kuyaona
matakatifu kwa wale wote tunaoishi nao na wanaotuzunguka.Yote yasiyoongozwa na
Roho wa Bwana yanamadhara sana katika maisha yetu. Mungu hatosita kutufundisha
kwa njia nyingine ili tumrudie. Na hii ndiyo kazi ya mwalimu yeyote yule au
mlezi ye yote yule anayejitambua.
Ndugu
yangu, kushindwa kwa mwanafunzi kwa maana nyingine kwa weza dhihirisha
kushindwa kwa mwalimu. Kufaulu mtihani wa maisha kwa tegemea sana maisha
yanayoongozwa na malengo. Na kufikia lengo lolote lile katika maisha kunaitaji
“nidhamu” kama kiungo muhimu sana. Licha ya nidhamu kukuweka katika mstari
sahihi kuelekea pale unapopataka, nidhamu hiyo hiyo ukuwajibisha pia pale
unaporegea. Na nidhamu hii ndiyo aizungumziayo Yesu na kusema, “Jitahidini kuingia
katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka
kuingia, wasiweze,” Lk 13:24. Hivyo hakuna yeyote kati yetu asiyependa
mafanikio mazuri katika maisha. Hata hivyo kuyapata na kuyafikia mafanikio hayo
mazuri kutakuitaji “nidhamu na maadili” kwa kile ukichuchumiliacho.
Nidhamu na maadili ndicho kiongoza njia cha
kufika pale unapopatamani. Nidhamu na maadili mema katika maisha
hutustahimilisha hata pale tunapokata tamaa na kukosa mwelekeo kama tokeo la
sintofahamu katika maisha. “Ni kwa ajili ya
kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi
asiyerudiwa na babaye?” Ebr 12:7. Nidhamu na maadili mema hukupa maana na
ufahamu wa maisha unayoyaishi leo kama tokeo la jana, na kesho kama tokeo la
leo. Kwa mantiki hii ya nidhamu na maadili katika maisha, “Kila adhabu wakati
wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea
wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani,” Ebr 12:11.
Maisha yenye nidhamu na
maadili mema humjenga mtu mwili na roho. Kumbe si vyema sana kujionea huruma na
kulalama kwa mambo ambayo yapo chini ya uwezo wako kubadilika na kusonga mbele
katika furaha ya kweli. “Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti
yaliyopooza, mkaifanyie miguu
yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali
kiponywe,” Ebr 12:12-13. Ndugu yangu, licha ya kwamba baadhi ya vidonge vya
malaria ni vichungu, twawajibika kuvimeza kwa sababu tunataka kupona. Na pona ya ye yote yule mwenye hofu ya Mungu ni
hii: Kutafuta “kwa bidii kuwa na amani na
watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;
mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije
likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo,” Ebr
12:14-15. Ndugu yangu, bila utakatifu hutoweza muona Mungu kwa sababu Yeye ni
Mtakatifu.
Tumsifu
Yesu Kristo
“Mtukuzeni Bwana,
Mungu wetu; Sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu; Maana Bwana, Mungu wetu,
ndiye Mtakatifu,” Zab 99:9
Tusali:-Ee Bwana Yesu,
tujalie amani na watu wote. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario