domingo, 29 de enero de 2017

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 4 YA MWAKA-I


JUMANNE WIKI YA 4 YA MWAKA-I

Somo: Ebr 12:1-4

Zab: 22:25b-27, 28, 30, 31-32

Injili: Mk 5:21-43

Nukuu:

“tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu,” Ebr 12:2.

“Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu,” Ebr 12:3.

Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule,” Mk 5:25-29

 “Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena,” Mk 5:34.

“Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu?”

Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu,” Mk 5:35.

TAFAKARI: “Usiogope, amini tu.”

Wapendwa wana wa Mungu, neno “usiogope” lipo mara 366 katika Biblia Takatifu. Hii ina maana Mungu anatuambia kila siku “usiogope”. Unapokuwa na hofu ya kitu chochote, basi kitu hicho ndicho chenye uwezo wa kuamua hatima yako. Kwa watu wa Mungu tunatakiwa tuelekeze hofu yetu kwa Mungu tu na si kwingineko kwani tutakapoielekeza kwa Mungu yeye ni mwaminifu na atatuelekeza kufanya ya Mbinguni.

Maandiko Matakatifu, Biblia, inatuambia haya kuhusu HOFU:- “Bwana wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu,”Isa 8:13. “Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi. Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo,”Lk 12:4-5. “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili,” Ufu 21:8.

Hofu haileti madhara ya kiroho tu bali hata ya kimwili. Huleta mshituko na penye hofu pana wasiwasi, palipo na haya huleta magonjwa ya “Organic” {sehemu za mwili zifanyazo kazi maalumu} na hitilafu katika shehemu hizi husababisha vidonda vya tumbo {ulcers}, shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya ini, upungufu wa damu mwilini, n.k

Kadiri ya Maandiko Matakatifu haya ni baadhi ya magonjwa yanayosababishwa na hofu: “Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, utungu umenishika, kama utungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu, nisiweze kuona. Moyo wangu unapiga-piga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha,” Isa 21:3-4

Leo Yesu anakuambia wewe na mimi “usiogope, amini tu.” Yawezekana shida, mahangaiko, na hata ugonjwa ulio nao umekuwa tishio kwako kiasi kwamba umefikia mahali na kukosa mwelekeo. Hata kama kuna hali ya umauti, Yesu anakuambia, “usiogope, amini tu.” Injili ya leo tunaona Yesu anaponya na kurudisha uzima kwa watu wawili kwa nyakati tofauti.  Msingi wa ponyaji zote hizi mbili, yaani mwanamke yule aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka 12, na binti yule wa Yairo mmoja wa wakuu wa sinagogi, ni kukubali uwepo wa Kristo na kuwa na Imani thabiti.

Kama kweli wewe U mfuasi wa Kristo huna sababu ya kuwa na hofu na mashaka juu yake hata kama Dada mauti yu pembeni yako. Usiogope, amini tu. Kuhusu Imani, Yesu anatusihi; “Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu,” Mt 17:20b. Mwanamke yule mwenye kutoka damu kwa muda wa miaka 12 anachukua ujasiri na kuishinda hofu na kulishika vazi la Yesu. Naye anapata uponyaji. “Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule,” Mk 5:25-29. Hakuna kitu kibaya kama hofu. Wengi hufa bila hata kudhuriwa kwa sababu ya hofu.

Kwa tendo hili Yesu anagundua nguvu kumtoka mwilini mwake, hivyo anawauliza wanafunzi wake ni nani aliyemshika? Kwa upande wa wanafunzi wake Yesu swali hili linaonekana halina maana kwa sababu Yesu alikuwa amesongwa pande zote na watu. Yesu kuuliza kwake huku si kupoteza muda, bali kumpa hakikisho la kweli la huruma ya Mungu mwanamke yule. Hivyo baada ya kuangalia huku na huku, mwanamke yule akiwa na hofu anajisalimisha kwa Mfalme wa Amani, Yesu Kristo. “Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote,” Mk 5:33. Kujisalimisha huku kunamrudishia Amani, Furaha, na Nguvu. Naye Yesu anamwakikishia hayo na kumwambia, “Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena,” Mk 5:34. Msiba wake wa miaka kumi na mbili umeondolewa leo. Ndugu yangu unayesafiri nami, bila shaka nawe unamsiba wako unaokusumbua. Kristo ndiye njia, kweli, na uzima, Yoh 14:6. Yawezekana kote ulipopita kutafuta njia umezidi kupotea. Yawezekana kote ulipotafuta kweli kuhusu tatizo lako umegonga mwamba. Na yawezekana pia uzima unaoupigania ndio unazidi kudhoofu na kunyauka. Kristo ndiye jibu halisi la hayo matatu: njia ya kweli, kweli halisi, na uzima thabiti.

Baada ya kulitenda jambo hilo kuu, Yesu anaelekea kwa binti yule wa Yeiro. Alipokaribia tu nyumbani kwa Yairo, Yesu anapokelewa na habari ya huzuni. “Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu?” Kristo Yesu akiwa ndiye uzima, anamwondolea hofu na mashaka Yairo na kusema, “Usiogope, amini tu,” Mk 5:35. Maneno haya ni mazito sana licha ya uchache wake. Je, unayaamini? Yesu anaenda mbali zaidi pale tunapomwamini angali tukiwa katika sintofahamu zetu. Yesu anaingia ndani na wanafunzi wake wale watatu tu [Petro, na Yakobo, na Yohana] na kusema, “Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu,” Mk 5:39.

Wapendwa wana wa Mungu, unapokutana na Yesu katika mahangaiko yako na kubaki naye katika imani thabiti, tatizo hilo ni sawa na kupita tu. Ni usingizi wa muda mfupi na utaamka katika utu mpya ndani na katika Kristo. Maneno haya ya Yesu yanaonekana kama kejeri kwa wale wasiokuwa na Imani. “Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana,” Mk 5:40.

Ukweli ni kwamba ufahamu wako kuhusu maisha na yote yanayokuzunguka ni mdogo sana ukilinganisha na yale Mungu ayajuaye kuhusu maisha yako na mazingira yanayokuzunguka. Ufahamu wa yote yaliyojificha U na Mungu. “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3. Huyu ndiye Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili akakaa kwetu, Yoh 1:14. Yesu ndiye Uzima wa kweli, na hili analifanya na kudhihirisha nguvu na mamlaka yake. “Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka,” Mk 5:41. Ndugu yangu, ‘usiogope, amini tu.’

Mahangaiko yako hayana umilele. Hilo silo kusudio la kuumbwa wako. Umeumbwa ili uishi milele. Yule Kijana “Mara akasimama, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu,” Mk 5:42. Ndugu yangu, mwanamke yule aliteseka kwa miaka 12, na kijana huyu anarudishiwa uhai wake akiwa na umri wa miaka 12. Wafuasi wa Yesu walikuwa 12 katika huduma yao, na walikusanya makapu 12 ya masalia ya vipande vya mkate na samaki. Na Maandiko Matakatifu yanatuambia pia kulikuwa na makabila 12 ya Wayahudi. Ujumbe tunaopata hapa ni kwamba namba 12 ni UKAMILIFU, ILIYOTOSHA, na YAKUTOSHA. Ukamilifu huu ni pale Mungu anaposema basi inatosha juu ya mahangaiko ya mateso yako na yangu. Tosha yake kwetu ni Amani ya kweli, Furaha ya kweli, na Nguvu. Basi hatuna sababu yoyote ya kufurahia uovu, au kuwa na hofu juu ya kitu chochote kile ila hofu ya Mungu tu.

Wapendwa wana wa Mungu, Waswahili husema ‘ukiona vinaelea ujue vimeundwa.’ Chochote kile kionekanacho na kupendeza machoni petu kina historia yake. Na historia kama mang’amuzi yenye kugusa hisia na maisha ya watu husika, ndiyo msingi wa kile wakiheshimucho na kukitukuza. Ni kwa maana hii hatuwezi kulitazama Kanisa leo katika uimara wake, ueneaji wake,  uinjilishaji wake, na kushamiri kwake, bila kutambua sadaka kubwa aliyoitoa Yesu Kristo pale Msalabani, na wote waliomfuata wakiwemo Mitume wake, na wafiadini Watakatifu waliomwaga damu zao kwa ajili ya imani ya kweli, na katika kweli na haki. Na ndiyo maana, “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu,” Ebr 12:2. Hili ndilo tumaini letu KUU kama wafuasi wake.

Kutokana na ubinafsi na umimi uliokithiri miongoni mwetu na kutufanya sanamu za kuabudiwa, ulimwengu leo siyo sehemu salama pa kuishi. Kila kukicha imekuwa mchezo wa karata wa kupata na kupoteza. Lakini swali kubwa hapa ni hili; ‘tunapata kwa ajili ya nini na nani, na tunapoteza kwa ajili ya nini na nani? Ni kweli iliyo wazi kwamba, kama mimi na wewe leo tutakuwa tayari kuishi Ukristo wetu na kumfanya Kristo aonekane kwa wengine hasa wanyonge, utawala huo wa kweli na haki utaingia vitani na utawala wa ubinafsi na umimi wenye kuabudiwa na kutukuzwa. Jambo la kusikitisha ni kwamba, utawala huu wa kweli na haki hauna Jeshi wala mahakama kama ulivyo utawala ule wa ubinafsi na umimi. Silaha kubwa ya utawala huu wa haki na kweli ni UPENDO.

Na sababu ya silaha hii ni hizi mbili: Moja, ni juu ya lile lililo kuu, “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo,” 1Kor 13:13. Na la pili ni kuhusu uzito wa sadaka ambayo mtu aweza kuitoa kwa ajili ya wengine. Kristo ndiye kielelezo chetu katika hili; Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Hakuna tutakachopoteza kwa kufanya tendo hili kwa sababu aliyetuweka huru leo na kupata mastahili ya kuwa wana wa Mungu na warithi wa ufalme wa Mungu, ndiye Kristo aliyeushinda uovu kwa kifo kile cha Msalaba. “Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu,” Ebr 12:3. Na kwa upande wetu katika vita hii dhidi ya uovu, ‘hatujafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi,’ Ebr 12:4. Na kama wafuasi wa Kristo tu askari wa mwanga dhidi ya giza ambalo ndilo uovu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena,” Mk 5:34.

Tusali:-Ee Yesu Mwema, twakiri ndani ya mioyo yetu kwamba hakuna lisilowezekana kwako na kwa Mungu Baba. Tujalie imani ya kweli katika ukiri huu. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario