IJUMAA WIKI YA 1
YA MWAKA-I
Somo: Ebr 4:1-5, 11
Zab: 78:3, 4bc, 6c-7, 8
Injili: Mk 2:1-12
Nukuu:
“Basi, ikiwa ikaliko
ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana
ameikosa,” Ebr 4:1
“Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha
ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi,” Ebr
4:11
“Wakaja watu wakimletea
mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne,” Mk 2:3
“Na walipokuwa
hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo;
na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza,”
Mk 2:4
“Naye Yesu, alipoiona
imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi
zako,”Mk 2:5
“Lakini
mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi,
(hapo amwambia yule mwenye kupooza)” Mk 2:10
TAFAKARI: “Mwana
wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi.”
Wapendwa
wana wa Mungu, maisha ni pamoja na kuzikabili changamoto za kila siku. Ila
jambo la kukumbuka ni kwamba changamoto hizi ziwe sehemu za makuzi yako kimwili
na kiroho. Mtu ukua kimwili na kiroho anapoikabili changamoto husika kwa
mwelekeo ulio sahihi na bila kupoteza malengo yake kuelekea kule kuliko
sahihi-uzima wa milele. Wengi wetu hupenda kuzikabili changamoto kwa njia
rahisi na za mikato. Ukweli ni kwamba chochote kile ‘rahisi’ kwisho wa siku
huwa ‘ghali.’
Wapo
pia baadhi yetu uzikabili changamoto kwa mtazamo ‘mfanano’ kwa lengo la
kujiridhisha nafsi baada ya kutamani kitu hicho kwa muda mrefu bila kukipata.
Mfano kama ulitamani gari kama alilokuwa nalo jirani yako na hukuwa na uwezo wa
kulinunua, inapotokea nafasi ya kupata hata lililo bovu ila linamfanano na lile
la jirani yako na lipo chini ya uwezo wako kifedha, mtu huyu ulinunua tu ili
kukidhi tamaa ya moyo wake. Ila vilivyo ‘rahisi’ mwisho huwa ‘ghali.’ Matokeo
yake ni kwamba badala ya kusonga mbele kimaisha hurudi nyumba kwa sababu
matunzo ya gari hili bovu ulilolinunua ujeuka kuwa kitafuno cha fedha na mali
zako zote ulizokwisha kukusanya muda mrefu kwa shida na taabu.
Somo la Injili leo tunaona mamlaka
aliyokuwa nayo Yesu yanahojiwa. Wengi wanamwona Yesu katika mtazamo ‘mfanano.’
Licha ya ishara nyingi alizozifanya Yesu baadhi ya watu hawakuona zaidi na
ishara zile. Wapo walimchukulia Yesu kama mwana mazingaumbwe fulani hivi.
Lakini Yesu anasema, “Kama sizitendi kazi za Baba yangu,
msiniamini; lakini nikizitenda,
ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa
Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba,” Yoh 10:37-38. Kwa kutambua ukweli
huu, Yesu anayasema maneno haya bila kupepesa macho kutokana na kutokulipokea
tendo lile kama tendo la Mungu baada ya kumponya mtu yule aliyekuwa amepooza. Na
kwa kutambua yaliyokuwa mioyoni mwao, Yesu akawaambia, “lakini mpate kujua ya
kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia
yule mwenye kupooza)” Mk 2:10.
Wapo kati yetu hadi leo hawaamini uwezo
wa Yesu na nafasi yake katika fumbo zima la Utatu Mtakatifu. Utatu Mtakatifu
huu, yaani Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, ni umoja usiogawanyika. Ilipo
nafsi moja katika utendaji na nafsi nyingine uwepo hapo hapo.
Mungu wetu si kama mtu katili mwenye
kuwashurutisha watu kama alivyo kamanda wa vita. Kama mzazi aliyekomaa
kimaadili, Lk 15:11-32 (soma habari ya
mwana mpotevu), Mungu uruhusu yale tuyapendayo ili tujionee wenyewe kama
waswahili wasemavyo, ‘mtoto akilia wembe mpe.’ Lakini pamoja na uwezo huo,
Mungu kamwe hazivunji ahadi zake kwa waja wake. Ni wewe na mimi kuwa waaminifu,
na kutokuikubali roho ile ya uasi. “Basi, ikiwa ikaliko
ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana
ameikosa,” Ebr 4:1
Ingawa twapenda kuwa huru na ndiyo
ilivyompendeza Mungu kutuumba, uhuru huo kamwe usitutenge na Mungu. Mungu anapokosa
nafasi katika maisha yako, nafasi hiyo uchukuliwa au kutawaliwa na kitu
kingine. Kitu hicho ndicho huwa dira na msukumo wa maisha yako. Kiongoza dira
hicho chaweza kuwa ulevi, fedha, chuki, majungu, wivu, zinaa, nk. Unapoikubali
roho hizi ndani yako na kuruhusu kuwa roho hiyo kuyaongoza maisha yako, basi
ujue ni kwa namna hiyo hiyo tunamkataa Mungu kuwa kiongozi wa maisha yetu. Hapa
hapatakuwa na usalama hata kidogo. Kwa vile Mungu alikuumba huru na anataka uwe
huru, hawezi kuzuia hali hiyo ndani yako ingawa ni mbaya kwa sababu hakukunyima
utashi. “Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile;
kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani
mwangu,” Ebr 4:3.
Ishi yetu hapa dunia kwa
nyakati zote isitutenge na Mungu hata pale tunapolemewa na dhiki kubwa katika
maisha. “Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote
asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi,” Ebr 4:11. Matatizo na mahangaiko
yetu ya kila siku yasiwe sababu ya kututenga na Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mimi na Baba tu
umoja,” Yoh 10:30
Tusali:
Ee Yesu Mwema, tujalie utulivu wa ndani kwa sababu kwako upo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario