JUMANNE WIKI
YA 3 YA MWAKA-I
Somo:
Ebr 10:1-10
Zab:
40:2-4ab, 7-8a, 10, 11
Injili:
Mk 3:31-35
Nukuu:
“Basi torati, kwa kuwa
ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa
dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote
kuwakamilisha wakaribiao,” Ebr 10:1
“Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na
toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za
dhambi hukupendezwa nazo,” Ebr 10:5-6
“Ndipo aliposema,
Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi
alisimamishe la pili,” Ebr 10:9
“Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande
zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu!” Mk 3:34
“Kwa maana mtu ye
yote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na
mama yangu,” Mk 3:35
TAFAKARI: “Mtu ye yote
atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama
yangu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kufanya mapenzi ya Mungu ni moja ya kuikana nafsi kuacha
kuegemea mwili wako. Ni kuwa na mtazamo wenye mwelekeo wa kutoka ndani kwenda
nje. Ni kinyume cha mtazamo wa kawaida ambao mara zato huwa nje kuelekea ndani.
Ni kuushinda umimi kwa kufungua mlango kwa ajili ya wengine. Mara nyingi mambo
hayaendi vizuri iwe kwenye taasisi za kijamii au za kidini mmoja
anapotangulizwa ndugu “umimi” mbele.
Yesu
anafungua mlango kwa ajili ya wengine na kuwaza kwanza kwa ajili ya wengine
pale anapotafutwa kwa njia njema na wazazi wake. “Akawatazama
wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu
zangu! Kwa maana mtu ye yote
atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama
yangu,” Mk 3:34-35. Yesu anatutaka tuvuke uhusiano wa kidamu kama kweli tunampenda
Mungu. Utayari huu wa kwenda nje ya mipaka ya kifamili, kiukoo, kikabila, na
hata utaifa wetu ni fursa ya kutufanya kuyafanya mapenzi ya Mungu. Niwe tayari
kutumika bila kujibakiza kwa watu wote bila kutazama uhusiano wa kidamu.
Yesu Kristo, ambaye anabeba
dhambi za sisi wanadamu, analo jambo moja tu la kufanya. Nalo ni kufanya
mapenzi ya Mungu, na si yake. Huu pia ni unyenyekevu wa hali ya juu. Ni sadaka
kubwa sana mtu anapoazimia kuutoa uhuru wake wote kwa sababu ya mtu mwingine.
Kuwa tayari kufanya yote bila kujibakiza kwa maelezo ya mtu mwingine bila
kuhesabu faida ni sadaka kubwa sana. Hii ni sadaka kubwa sana isiyo na kipimo.
“Ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza,
ili kusudi alisimamishe la pili,” Ebr 10:9. Utii ni sadaka kubwa sana unayeweza
kutoa. Huwezi kuwa mtii kama si mnyenyekevu.
Ndugu yangu, mbele yetu
yupo Mama yetu Bikira Maria, tujifunze kuwa wanyenyekevu kama Mama yetu Bikira
Maria. Anza zoezi hili pale ulipo. Lianze kwenye familia yako na lifanye kadiri
ya nafasi yako katika hiyo familia kwa kuyatimiza yote yanayokuhusu kwa
unyenyekevu. Pili, lifanye jambo hili katika sehemu yako ya kazi, na sehemu
yeyote unapowajibika kwa ajili ya wengine. Ndugu yangu, ni wazi kabisa
ukilifanya hili kwa moyo mkunjufu Mungu atakutumia katika mambo yake makuu
kadiri ya hitaji la watu wake na utukufu wake.
Tukirudi kwa Kristo
mwana wa Mungu, Yeye ni wokovu na hatenganishwi na ujumbe huu wa wokovu hapa
duniani. Na Kanisa ikiwa ni mwili wake Kristo, wokovu ndiyo msingi wa uwepo
wake leo na sasa na hata mwisho wa nyakati. Hivyo ujumbe huu ni furaha na amani
kwetu kwa sababu kwa njia ya Kanisa kama chombo na Sakramenti, wokovu
unapatikana. Na hii ndiyo maana halisi ya Kanisa kama chombo na Sakramenti ya
wokovu. Kwa mantiki hii, Kanisa lina wajibu mmoja tu wa kufanya, yaani, mapenzi
ya Mungu ikiwa ndiyo msingi na kielelezo cha wokovu wetu, na mwisho
kufikia maisha ya umilele. Na kwa namna
hiyo, “Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo
mara moja tu,” Ebr 10:10. Sadaka yake na majitoleo yake yanatosha. Kristo ndiye
utimilifu wa yote katika yote.
Wapendwa wana wa Mungu, Masiha wetu “kwa hiyo
ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea
tayari; Sadaka za kuteketezwa na
sadaka za dhambi hukupendezwa nazo,” Ebr 10:5-6. Kwa maana nyingine uwepo wa
Kristo ambao ni uwepo wa Mungu katika maisha yetu unatosha. Kwa mantiki hii,
“torati hubaki kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe
ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi
wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao,” Ebr 10:1. Kristo Yesu ndiye kamilisho
lenyewe.
Maisha ya Kristo na sadaka yake pale Msalabu
ulifuta sadaka zote na kwa sadaka yake ilikuwa kielelezo cha sadaka hai zote,
na wokovu na uzima wetu. “Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa
dhambi,” Ebr 10:4. Kwa hiyo uwepo wake Kristo ambao ni uwepo wa Kanisa ni kufanya mapenzi ya Mungu. Na Kanisa
kwa maana nyingine ni wabatizwa wote, na katika uhai wa kuishi ahadi zao za
ubatizo. Huu ndio wito wa Kanisa.
Hivyo kuwa na umoja na
Kristo na Mungu Baba, ni kuyafanya mapenzi yake kwa uaminifu. Ni kuishi kama
alivyoishi Mtume Paulo. Naye anakiri kwamba, “kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi
nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya
kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami,” 1Kor
15:10. Huku ni kuishi kwa kuyafanya mapenzi ya Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
Ikinibidi kujisifu, nitajisifia
mambo ya udhaifu wangu. Lakini
kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu
ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake. Maana
kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe,” 2Kor 11:30; Gal 6:4-5
Tusali:
Ee Yesu, tujalie fadhila ya unyenyekevu ili tuyafanya yote kwa sifa na utukufu
wako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario