JUMATATU WIKI YA 1
YA MWAKA-I
Somo: Ebr 1:1-6
Zab: 97: 1, 2b, 6, 7c, 9
Injili: Mk 1:14-20
Nukuu:
“Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika
manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na
sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya
ulimwengu,” Ebr 1-2
“Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya
nafsi yake akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa
dhambi aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu,” Ebr 1:3
“amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina
alilolirith lilivyo tukufu kuliko lao,” Ebr 1:4
“Kwa maana alimwambia
malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, Mimi
nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana?” Ebr 1:5
“Hata tena, amletapo
mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu,” Ebr
1:6
“akisema, Wakati
umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15
“Yesu akawaambia, Njoni
mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,” Mk 1:17
“Mara wakaziacha nyavu
zao, wakamfuata,” Mk 1:18
TAFAKARI: “Wakati
umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.”
Wapendwa
wana wa Mungu, maisha yanayoongozwa na malengo lazima yasukumwe na kauli mbiu
yenye mwelekeo wa umilele. Ufupisho wa kile ambacho Kristo anakifanya ndani ya
maisha yetu kimejumuishwa katika kauli mbiu hii: “Wakati
umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15.
Kauli mbiu hii ya Yesu imeweka wazi muda maalum wa kuanza mradi huu wa umilele,
kudumu kwa mradi huu kabla ya kufikia umilele, mapaswa ya mradi huu, na kielelezo kinacho sadifu mradi huu.
Kwa ujumla maisha ya hapa
duniani ni ya muda mfupi ukilinganisha na umilele. Hivyo kauli mbiu hii ya Yesu
inatutaka kutambue ukweli huu wa uchache wa muda tungali hapa duniani.
Ninapopata nafasi ya kuishi hata kwa dakika moja nielewa muda huo haujirudii
tena na nishapunguza muda wa maandalizi kuelekea umilele. Kwa maana nyingine
yanipasa kuishi nikijua nina muda na wakati huu tu katika maisha yangu.
Wakati kwa Mkristo umetimilizwa
na Kristo mwenyewe kwa tendo la Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1.14. “Mungu,
ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia
nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa
mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu,” Ebr 1:1-2. Hivyo Kristo
ndiye dira ya maisha yako na yaliyo mafupi hapa duniani katika dhana nzima ya
kujiandaa na umilele. Ufalme wa Mungu umekaribia kwa sababu Neno huyu, yaani,
Emmanueli, ni Mungu pamoja nasi, Mt 1:23. Mungu ambaye hapo mwanzo alioneka
yupo mbali sana na watu sasa kamwilishwa na kuwa sawa na sisi isipokuwa
hakutenda dhambi, 1Pet 2:22.
Pamoja na ukweli kwamba
sasa tupo karibu sana na Mungu kupitia mwanaye Yesu Kristo, hiyo haimaanishi
wakovu ni bwerere! La hasha! Yatupasa kutubu na kuamini habari njema, yaani
Injili. Toba yetu ni kuanza upya na Mungu kupitia mwanaye Mpenzi Yesu Kristo.
Ni kuuvua utu wetu wa zamani na kuuvaa utu mpya kama asemavyo Paulo Mtume. “Ikiwa
mlimsikia mkafundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika Yesu, mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza
utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia
zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa
kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli,” Efe 4:22-24. Habari njema
iwe kweli habari njema kwako na wote wale waliokata tamaa katika maisha yao,
wewe ukiwa mjumbe wa habari hiyo yenye matumaini. Kristo ndiye tumaini jipya
kwetu sote katika safari yetu hii kuelekea maisha ya umilele.
Huna wakati mwingine
tena katika maisha yako wa kufanya jambo hili ninalokuwambia. Kama Mungu
ilifika mahali akasema basi na inatosha, kwa nini wewe usiseme pia basi
inatosha kwa kuanza upya na Mungu? Ni Mungu huyu, “ambaye alisema zamani na
baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa
siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena
kwa yeye aliufanya ulimwengu,” Ebr 1:1-2. Leo tunapewa nafasi ya kuongea naye
moja kwa moja na bila chenga.
Wapendwa katika Kristo,
katika Ukuu na Umungu wake Mwokozi na Mkombozi wetu, “Yeye… ni mng'ao wa
utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake,
akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;
amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo
tukufu kuliko lao,” Ebr 1:3-4. Hivyo mwisho wa maisha yetu hapa duniani utakuwa
na maana na uhakika wa umilele ndani na katika Kristo Yesu. Jamani Mungu yupo
na hatuna uzima pasipo Yeye.
Hivyo ishi yetu leo
siyo tena ishi ile inayosukumwa na mitazamo ya watu, ikiwa ni pamoja na mila na
desturi zetu zilizopotofu. Kuishi kwetu leo ndani na katika Kristo siyo
kuwapendezesha wanadamu, bali Mungu mwenyewe, Gal 1:10. Vile vile ishi letu leo
siyo tena ile kwamba ulimwengu huu ndiyo kikomo cha kila kitu na kutufanya
kuwekeza hapa duniani. Yote tuyafanyayo, tena kwa ukamilifu wake, yawe ni moja
ya njia ya kutufikisha katika umilele ambao ndio kikomo cha kila kitu.
Tumeumbwa na Mungu tuishi milele kama Yeye alivyo wa milele.
Ukitizama kwa makini
chagua ya Yesu kwa wale Mitume wake utaona ukweli huu. Ni kama vile Yesu
anataka kusema hivi, “najua kazi yako ndiyo kila kitu kwako, ila hili
nikuambialo ni muhimu na lina umilele ndani yako.” Yesu hakudharau waliyokuwa
wanayafanya kabla wale aliowachagua, bali aliwaonyesha lililomuhimu na lakudumu
katika kufanya. “Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi
wa watu,” Mk 1:17. Pamoja na sintofahamu hii, Mitume na wanafunzi hawa wa Yesu
wanaacha kazi zao na kumfuata Yesu. “Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata,” Mk
1:18. Nani kati yetu leo atakuwa tayari kuacha mkate wake, kazi yake nzuri na
yenye mshahara ulio nona na kumfuata mtu tu asiyemjua vizuri? Ni changamoto kubwa sana!
Ila ndugu yangu
tuliyesafiri wote katika tafakari hii, kama unataka kuishi katika umilele,
yakupasa kuiisikia sauti ya Mungu. Yote tuliyonayo hapa duniani kama yalivyo licha
ya uzuri na umuhimu wake, hayana umilele kama yatakosa muunganiko hai na Mungu.
Tunaangaika sana kuvipata vitu hivyo tena kwa jasho na gharama kubwa, ila
ukweli ni kwamba ipo siku tutaviacha na kwenda bila kitu. Kumbe tumia muda wako
vizuri katika utume wako kwa sababu hilo litadumu milele hata baada ya maisha
yako hapa duniani.
Tumsifu Yesu Kristo!
Msijiwekee
hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni,
kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo
utakapokuwapo na moyo wako,” Mt 6:19-21
Tusali: Ee Yesu Mwema,
tujalie fadhila ya kiasi ili tuishi kwa unyofu kadiri ya mpango wako katika
maisha yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario