miércoles, 25 de enero de 2017

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 3 YA MWAKA-I


IJUMAA WIKI YA 3 YA MWAKA-I

Somo: Ebr 10:32-39

Zab: 37:3-4, 5-6, 23-24, 39-40

Injili: Mk 4:26-34

Nukuu:

“Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi,” Ebr 10:35-36.

“Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye,” Ebr 10:38

 Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi,” Mk 4:26

“Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake,” Mk 4:31-32

TAFAKARI: “Madhara ya kuficha na kutokukiri kosa ni kujiangamiza zaidi katika uovu.”

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna kati yetu asiyekuwa na mapungufu yake. Mapungufu yako yanathibitisha ubinadamu wako. Kuyatambua mapungufu yako ni hatua muhimu sana kuelekea ukamilifu ambao ndio wito wa kila mmoja wetu. “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Jambo la kushangaza ni kwamba kati yetu wapo ambo hawapendi na hawayakubali mapungufu yao na kuchukua hatua kuelekea ukamilifu. Badala yake huvaa vinyago ambavyo huwaharibu kabisa na kupoteza sura yao halisi. Wengi kati yetu tunaisha maisha ya kuigiza ilhali kwa uhakika tunasutwa na dhamiri na nafsi zetu.

Yesu leo anatupa aina mbili za mfano wa Ufalme wa Mungu. “Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi,” Mk 4:26. Maana yake, anayezikuza mbegu hizo na kuwa kile kilichokusudiwa na Mungu mwenyewe. “Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi,” Ebr 10:35-36. Na katika makuzi haya yaani maisha yako kila siku ni wakati wa wewe kuwa kile Mungu alichokusudia uwe. “Sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu,” Ebr 10:39. Hivyo ni wazi Mungu anapenda tuwe wanadamu kama alivyotuumba kwa sura na mfano wake. Tunapojaribu kuwa kitu kingine ni chukizo kwa Mungu na hapo tunakuwa wabaya kuliko hata shetani.

Mfano wa pili wa Ufalme wa Mungu ni huu; “Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake,” Mk 4:31-32. Hapa tunakumbushwa kwamba hakuna kisicho na umaana mbele ya Mungu katika mwonekano wake, iwe ukubwa au udogo. Hivyo hali yetu kama wafuasi wake Kristo pamoja na sintofahamu za maisha tunazokabiliana nazo kila sikku, tunakumbushwa jambo hili la fadhila, yaani, “Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang'anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo,” Ebr 10:34. Na mali hii njema ndani yetu ni imani thabiti tuliyo nayo kwa Kristo Yesu. Na “mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye,” Ebr 10:38

Ndugu yangu, vyote tuvionavyo vinaudhihirisha Utukufu na Uzuri wa Mungu, na kwayo kwa kuwa kile kilicho ufikia ukamilifu wake ambao ndio kusudio la kuumbwa kwake. Hivyo jipokee kama ulivyo na yakamilishe yaliyo ndani yako kadiri ya mpango wa Mungu katika ukamilifu wake.

Tumsifu Yesu Kristo!

Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako,” Zab 119

Tusali:-Ee Yesu Mwema, yakamilishe yote ndani yangu kwa sifa na utukufu wako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario