viernes, 13 de enero de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI YA 2 YA MWAKA-A


JUMAPILI WIKI YA 2 YA MWAKA-A

Somo I: Isa 49:3, 5-6

Zab: 40: 2, 4, 7-8, 8-9, 10

Somo II: 1Kor 1:1-3

Injili: Yoh 1:29-34

Nukuu:

akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa,” Isa 49:3

“Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu),” Isa 49:5

“naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia,” Isa 49:6

“Wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu,” 1Kor 1:2b

 Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo,” 1Kor 1:3

“Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu,” Yoh 1:30

“Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu,” Yoh 1:34

TAFAKARI:Wewe u mtumishi wangu, na katika wewe nitatukuzwa.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya pili ya mwaka “A” wa Kanisa. Masomo yetu yote ya leo yanatutafakarisha siri iliyopo ndani ya kila mmoja wetu, na kusudi la Mungu lenye kufunua furaha na utukufu wake, kwa sababu ndivyo ilivyompendeza kutuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Hivyo, “Wewe u mtumishi wangu, na katika wewe nitatukuzwa,” asema Mungu leo juu yako.

Somo letu la kwanza, ingawa Mungu anawazungumzia wana wa Israeli, somo hili linaelezea pia umuhimu wa uwepo wako na wangu katika dunia hii, na malengo yake. “Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu),” Isa 49:5.

Ndugu yangu, ungali bado hujazaliwa Mungu kesha fahamu jina lako na makusudi yake. Hizi ndizo neema za Mungu kwetu licha ya kutokuwa na stahili nazo. Neema hizi anazimimina kwetu bila kipimo. Ni upendo wake Mungu kwetu usio na kipimo. Kwa kutambua ukweli huo, Mtume Paulo anasema, Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami,” 1Kor 15:10. Hatuna cha kujivunia kwa kile tulicho. Kwa sababu hiyo, yapo mambo makuu matatu yatupasa kufahamu ili kujua makusudi ya Mungu katika maisha yetu hapa duniani. Jambo la kwanza ni hili; kwa hali yo yote nitakayokuwa nayo lazima nijipokee kwanza, na kwa namna hiyo ndivyo neema za Mungu zifanyavyo kazi ndani yangu.

Pili, Mungu hutupa majukumu ya kufanya hapa duniani. Hatupo hapa kushangaa shangaa na kujiingiza katika mambo ya watu wengine. Mtume Paulo anatoa onyo: “Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe. Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema,” 2The 3:11-13. Tupo katika ulimwengu huu kwa malengo maalumu, na kupitia malengo hayo kazi ya Mungu hutendeka. Mungu anawaambia Waisraeli na anakuambia wewe na mimi pia, “Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa,” Isa 49:3. Mungu hutukuzwa tufanyapo vyema yale tunayoyaishi kadiri ya wito wetu. Wakati mwingine hatutambui wajibu huu mkubwa mbele ya Mungu kwa kuwajibika vilivyo kwenye tumishi zetu ndogondogo na wakati mwingine zile zisizo julikana rasmi na jamii.

Mfano:- Mama lishe anayewahudumia wachimba mifereji pembezoni mwa jiji, wajenzi wa nyumba na hata makanisa, wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, na vyuo, yawezekana hakuna mwenye kuguswa na huduma hii hata kidogo. Ila angalia akina mama lishe hawa wanavyojituma na kudamka usiku wa manane kuandaa watakavyovihudumu kwa siku. Faida waipatayo ni ndogo sana ukiliganisha na muda wanaoutumia kuwahudumia vibarua hawa walio wanyonge kama wao. Hii ni neema ya Mungu! Ni ukweli usio shaka kwamba katika huduma hii ya akina mama hawa tunawapata huko waalimu, mafundi wakuu, maaskari, madaktari, makasisi, wanasheria, mawaziri, na rais. Katika jambo hili Mungu anasema, “Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia,” Isa 49:6. Ndugu yangu, yale tujitoayo bila kujibakiza katika utume wetu, ni nuru kwa watu wa Mungu, na kwetu ni wokovu wa milele.

Lakini jambo la kushangaza mimi niliye mtawa na mkleri leo hakuna nilichochangia zaidi ya kukaa kimya pale nilipotakiwa kusema na kukemea uovu na manyanyaso wayapatayo kundi hili. Wewe kama askari au mgambo wa jiji umetoa mchango gani katika kundi hili zaidi ya kuwadhalilisha? Wewe kama mwanasheria umetoa mchango gani katika kundi hili zaidi ya kuminya haki zao? Wewe kama daktari wa afya umetoa mchango gani katika kundi hili zaidi ya kuwakebehi kuwa ni wachafu na viumbe hatarishi wa afya ya binadamu? Wewe kama waziri husika umetoa mchango gani katika kundi hili zaidi ya amri ya kuwafukuza kama wakimbizi katika nchi yao? Na wewe kama rais umetoa mchango gani zaidi ya kuwapandishia kodi na kuchukua hata kile kidogo walicho nacho? Yatupasa kutafakari kwa kina. Yapo makundi mengi sana katika jamii yetu leo kama akina mama lishe hawa.

Ndugu yangu, Kristo Yesu aliye dira na kielelezo hai kwetu, ni yote na katika yote kama ashuhudiavyo Yohana Mbatizaji: “Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu,” Yoh 1:30. Anatupenda kama tulivyo na amekubali na yupo nasi muda wote ili tufahamu upendo wake kwetu. “Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo,” Yoh 10:14-15. Taswira ya upendo huu wa Kristo kwetu ndiyo kielelezo cha uchungaji wake kwetu.

Uchungaji huu wa Kristo haubagui wale wasiopenda ulishaji wake. Huduma anayotoa Kristo habagui hata wale wanaompinga. Hivyo yupo kwa ajili ya wote kwa wakati wote. Kujitenga na Kristo ni kukataa upendo wake anaotupa bure wakati wote. Kristo analitambua jambo hilo na anasema, “Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja,” Yoh 10:16. Ni mara ngapi tunawatenga wale ambao wanapingana na mawazo yetu hata ikiwa kwa nia nzuri?

Ndugu yangu katika Kristo, na wale wote tuliopewa dhamana na Mama Kanisa kama viongozi, tujifunze unyenyekevu wa Yohana Mbatizaji. Yohana Mbatizaji aliyafanya yote kadiri ya hali na nafasi yake kama mwandaaji njia. Yohana Mbatizaji hakupindisha kweli hii ili ajikweze mwenyewe. Naye anasema, “wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji,” Yoh 1:31. Siri ya yule anayeandaliwa njia, yaani, Kristo Yesu, inafunuliwa kwa mwandaaji njia, Yohana Mbatizaji. Naye anasema, “wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu,” Yoh 1:33. Huu ni unyenyekevu wa hali ya juu.

Kujishusha na kujinyenyekeza kwa kutambua ukomo wa maisha yako ni njia na wezekano la kufunuliwa mambo kubwa katika maisha yako. Ni hatua ya kukua kiimani, na baadaye kuwa msingi imara wa imani isiyotetereka. Na hili linaonekana wazi kwa Yohana Mbatizaji kama asemavyo, “Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu,” Yoh 1:34. Yohana Mbatizaji hana shaka juu ya ufunuo huu wa Kristo.

Na Paulo “aliyeitwa kuwa mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu,” 1Kor 1:1, baada ya kuongoka kwake alikuwa mwaminifu lakini alijikuta gerezani. Yohane Mbatizaji alikuwa mwaminifu lakini alikatwa kichwa. Mamilioni ya watu waaminifu wameuawa, wamepoteza kila walichokuwa nacho, au maisha yao yamekoma wakiwa hawana kitu. Lakini mwisho wa maisha haya si mwisho, bali mwanzo wa maisha mapya ya umilele. Mtume Paulo hata katika hali ya mateso na mahangaiko yake, hakuiruhusu ile roho ya uasi. Hivyo aliendelea kuwakumbuka na kuwatakia mema ndugu na jamaa zake katika njia hii ya Kristo aliye yote ya maisha yake, na katika yote ayatendayo. Naye anasema, “Wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu,” 1Kor 1:2b. Muona huu wa Mtume Paulo hauna ubaguzi ndani yake, kwani kila mmoja wetu anao wito wa kuwa mtakatifu licha ya hali na mazingira anayoishi. Na sote kwa pamoja twahitaji neema na baraka za zake Mungu. Hivyo, kwa vile kapewa bure na tena kwa neema tu, Mtume Paulo naye anatoa bure. “Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo,” 1Kor 1:3. Je, nalitambua hilo katika utume wangu? Au ndio ule msema wetu kwamba, “mkono mtupu haulambwi!”

Ndugu niliyesafiri nawe katika tafakari hii, naomba nisikuchoshe. Katika macho ya Mungu, mashujaa wa imani sio wale waliopata mali, wenye mafanikio na nguvu katika maisha haya, bali ni wale wanaoyaona maisha kama jukumu la muda mfupi na kuutumia kwa uaminifu, wakitumaini kupokea thawabu yao katika umilele. "Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi. Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao, maana amewatengenezea mji," Ebr 11:13, 16. Asante kwa kusafiri nami. Tafakari na chukua hatua. Na mara zote tujitazamapo katika hali zote kama yalivyo majira ya mwaka na tusema kama Mtume Paulo, “Namshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kwa sababu ya neema ya Mungu mliyopewa katika Kristo Yesu,” 1Kor 1:4.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu,” Yoh 1:34

Tusali:-Ee Yesu, uliyetuachia mfano hai kama Mchungaji Mwema, nijalie siku zote moyo wa kutumika na siyo kutumikiwa. Amina.

No hay comentarios:

Publicar un comentario