JUMANNE WIKI YA 2 YA MWAKA-I
Somo: Ebr 6:10-20
Zab: 111:1-2, 4-5, 9, 10
Injili: Mk 2:23-28
Nukuu:
“Maana Mungu si dhalimu
hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa
mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia,” Ebr 6:10
“Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi,”
Ebr 6:15
“Akawaambia, Sabato
ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato,” Mk 2:27
“Basi Mwana wa
Adamu ndiye Bwana wa sabato pia,” Mk 2:28
TAFAKARI: “Na
hivyo kwa kuvumilia utaipata ile ahadi.”
Wapendwa
wana wa Mungu, ni mang’amuzi yangu na bila shaka yako pia kwamba Mungu hutenda
mambo makuu kwa watu ambao kadiri ya mtazamo wetu uliojijenga katika mila na
desturi utushangaza kabisa. Huyu ndiye
Mungu kama asemavyo Mama Bikira Maria, “Amewaangusha wakuu
katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:52. Mungu wetu aliye
haki, upendo, huruma na wema kamwe hatendi na kutazama kama sisi wanadamu.
Tatizo kubwa la mwanadamu huwa haoni vitu kama vilivyo, bali huviona vitu kama
alivyo yeye. Ni kwa mantiki hii mtu husongwa na mila na desturi zilizomkuza
katika maamuzi yake.
Mungu wetu hatazami kama sisi
tutazamavyo katika hulka na ushabiki wetu. Mungu hufanya kadiri na ukamilifu
wake. Nasi kama wanadamu tunaalikwa kila siku kuwa wakamilifu kama alivyo Mungu
wetu. “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu,
kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mk 5:48. Ni vyema ufahamu uwepo
wako hapa duniani. Ndugu yangu unanyesafiri nami katika tafakari hii, elewa
kwamba upo hapa nduniani kupigana kufa na kupona juu ya cheo chako ambacho ni
utakatifu wako. Mengine yote na fahari zake ni mbwembe tu. Huwezi kumwona Mungu
kama si mtakatifu. Je, unajua hilo? Na katika vita hii, uvumilivu wako ndiyo
mbivu yako kwa sababu, kwa kuvumilia utaipata ile ahadi, Ebr
6:15.
Ndugu yangu, maisha na
malengo yetu wakati mwingine haviendani. Unayo tamani na kuyataka wakati
mwingine hayafikiki. Ila tumaini la Mungu aliloweka juu yetu hawezi
kulitelekeza. “Maana Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile
mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi
sasa mngali mkiwahudumia,” Ebr 6:10. Hizi neema na baraka za Mungu anazotujalia
zinatuwajibisha kufanya kila mtu kadiri ya hali na wito wake. Kile ulicho leo
na sasa siyo kwa bahati mbaya. Wewe elewa ndiye mdomo, miguu, na mikono, ya
Kristo Yesu pale kusipofikika. “Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe
bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho; ili msiwe wavivu, bali
mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu,” Ebr 6:11-12.
Furaha ya kweli ipo
ndani yako na hakuna kitu kingine nje ya wewe kinachoweza kukupa furaha ya
kweli kama hutotambua kweli hii ndani yako. Mengine yote unayotegemea kufanya
kwa lengo la kukupatia furaha ni kujidanganya wewe mwenyewe kama hutoanza na
wewe mwenyewe. Ndugu yangu, “Mungu, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa
hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake, akisema,
Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza,” Ebr 6:13-14.
Kumbe kabla ya kuyataka hayo ya nje ni vyema kujua stamina yako kiroho na
kimwili. “Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na kwao ukomo wa
mashindano yote ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha,” Ebr 6:16. Je, wajua
stamina yako? Tatizo lako na langu ni hili, “tumejiumbia taswira zisizo zetu.
Tunaishi vivuli vya wengine.”
Somo letu hii la leo
kutoka kwa Waebrania latutaka kuona “neno hilo Mungu, akitaka kuwaonyesha zaidi
sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika,” Ebr 6:17.
Ikiwa maisha ni hatua, hivyo ishi yetu kila siku ni hatua kuelekea utimilifu
ambao ndiyo Kristo katika yote. Na kwa mantiki hiyo, Mungu “alitia kiapo
katikati; ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo
Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia
kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu, tuliyo nayo kama nanga ya roho,
yenye salama, yenye nguvu, yaingiayo hata mle mlimo ndani ya pazia, alimoingia
Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano
wa Melkizedeki,” Ebr 6:18-20. Huyu ndiye Mungu, na huu ndio upendo wa Mungu
kwetu.
Leo katika Injili Yesu
anatukumbusha lililo la muhimu. Ni kweli mila na desturi zetu zina umuhimu
wake, ila sauti ya Mungu ni muhimu zaidi kwa sababu ndiyo hatma yetu. Wanafunzi
wa Yesu wanakoselewa na kulaumiwa kwa kufanya lisilo sahihi siku ya sabato
kadiri ya mapokeo ya kiyahudi. Yesu anawajibu, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya
mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato,” Mk 2:27. Utu wa mtu ni kitu cha kwanza
kabisa kutazama zaidi ya mitazamo. Ndani ya mtu kuna chapa ya Mungu ndani yake.
Mtu lazima aheshimiwe kama alivyo bila kuangalia nafasi na cheo chake katika
jamii. Hivyo Kristo ndiye sababu ya yake yote kuyafanyayo. “
Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia,” Mk 2:28. Kristo
amekuja kuitakatifuza sheria na kuikamilisha. “Msidhani
ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali
kutimiliza,” Mt 5:17. Binadamu na utu wake kwanza, mengine yafuate.
Tumsifu
Yesu Kristo
“Maana
Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa
jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali
mkiwahudumia,” Ebr 6:10
Tusali:
Ee Yesu na Kiongozi wetu, nijalie uvumilivu katika maisha yangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario