Sikukuu ya
kuongoka kwa mtume paulo
Somo: Mdo 22:3-16
Zab: 117:1bc, 2
Injili: Mk 16:15-18
Nukuu:
“Mimi ni
mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji
huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi,
nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi; nikawaudhi watu wa Njia hii hata
kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake,” Mdo 22:3-4
“Kama Kuhani Mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote
pia, ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili
niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe,”
Mdo 22:5
“Ikawa
nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru
kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote,” Mdo 22:6
“Nikaanguka
nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana?
Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi,” Mdo 22:7-8
“Akasema,
Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule
Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake,” Mdo 22:14
“Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo
uliyoyaona na kuyasikia,” Mdo 22:15
“Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi
zako, ukiliitia jina lake,” Mdo 22:16
“Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe,” Mk 16:15
“Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,”
Mk 16:16
“Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio;
kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha,
hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya,”
Mk 16:17-18
TAFAKARI: “Kwa maana utakuwa
shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia.”
Wapendwa
wana wa Mungu, simulizi la kweli la kuongoka kwa Mtume Paulo limesimiliwa mara
tatu kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo 9:1-19, 22:3-16, na 26:9-18.
Kristofania-“Tokeo la Yesu,” njiani kuelekea Damasko ni tukio la msingi na
lililojenga upya maisha na mtazamo wa Mtume Paulo. Mtume Paulo anasema, “alipoona
vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake;
mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu,” Gal 1:16. Ni kweli isiyo
shaka kwamba unapokutana na Yesu katika maisha yako hawezi kukuachi hivi hivi.
Mtume Paulo ambaye kabla ya kuongoka kwake alitambulika kwa jina la Sauli,
aliitetea vilivyo dini yake ya kiyahudi katika dhamiri ambayo kwake aliona safi
na inafaa. Sauli alithibitisha jambo hili kuhusu imani, “na heri kuwa joto au
baridi katika imani, kuliko kuwa vuguvugu.” Msimamo huu wake katika imani
anaukiri mwenyewe kwa maneno yake: “Mimi
ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji
huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi,
nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi; nikawaudhi watu wa Njia hii hata
kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake,” Mdo 22:3-4.
Hakika Sauli hakuwa na mchezo wala salehe juu ya imani na dini yake.
Kuongoka
kwa Paulo kunaambatana na viashirio viwili vya wito wa kimasiha, yaani, kuona
na kusikia ambavyo vinajirudia katika somo hili kwa msisitizo. “Ikawa
nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru
kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Akasema, Mungu wa baba
zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na
kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa
maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na
kuyasikia. Nikamwona, naye
akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako
katika habari zangu,” Mdo 22: 6, 14, 15, 18. Msingi wa ushuhuda wa kuongoka
kwake Paulo unajengwa na haya: “Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote,
wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Nikamwona,
naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda
wako katika habari zangu. Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana
nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya
uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako,” Mdo 22:15,
18; 26:16
Utume
wake Paulo, wakimisioni, unapata nguvu na mamlaka katika msingi huu: “Naye
akaniambia, Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa
Mataifa. Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo
kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa
Israeli. Nikikuokoa
na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao; uwafumbue macho yao, na kuwageuza
waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea
Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa
kwa imani iliyo kwangu mimi,” Mdo 22:21; 9:15, 26:17-18
Kwa
mantiki hiyo, Paulo ‘aliona’ nuru ya mwanga. “Ee
Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo
mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote,” Mdo
26:13. Na alipoona nuru hii alitiwa upofu na Yesu Mfufuka kama ishara ya
kuuzika utu wake wa zamani na kufufuka naye kuelekea uzima. “Na nilipokuwa
sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa
pamoja nami, nikaingia Dameski,” Mdo 22:11. Ni kabla ya kutiwa upofu huu
alisikia ‘sauti’ ya Bwana na kumweleza kile kilichomsikitisha. “Nikaanguka
nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani,
Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi,” Mdo 22:7-8.
Sauti hii ndiyo inayompa uhakika wa kile alichokifanya kuwa si halali wala
haki, na hivyo kumtaka kubadili misioni yake ya zamani na kuanza upya na Kristo
kwa kutoa ushuhuda huo mbele ya watu wote, na hasa mataifa alichokisika na
kukiona. “Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu
wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia,” Mdo 22:15
Wito wa
Paulo ni ‘wongofu’ wa kweli. Maneno ya Ananias yenye hofu na mashaka juu ya
Sauli aliyekuwa anamfahamu kwa ukatili wake, yanapata ufafanuzi wa kile
kilichomtoke Sauli njiani kwa maneno ya Yesu. Huyu si Sauli tena bali Paulo aliyebadilishwa
na Kristo. Ni Paulo mwongofu na mtu mpya sasa. “Lakini
Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya
mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; hata hapa ana
amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako. Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule
kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonyesha yalivyo mengi
yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu. Anania akaenda zake, akaingia mle
nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye
aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu,”
Mdo 9:13-17. Yule aliyekuwa mtesi wa Watakatifu wa Mungu sasa ndiye chombo
kiteule kitakachochukua jina la Yesu mbele ya Mataifa na kuteseka kwa ajili ya
jina hilo. Ni kwa kupitia Jina hili lenye nguvu kupita majina yote, Yesu
anatuhaidi haya; “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu
watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika
nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono
yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya,” Mk 16:17-18
Misioni aliyopewa Mtume Paulo siku ya kuongoka kwake ndiyo
maneno ya mwisho ya Yesu kabla ya kupaa kwake, kwa walio wake juu ya utume wa
kimisioni kwa watu wote, na kuihubiri Injili kwa kila kiumbe. “Akawaambia,
Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe,” Mk 16:15.
Tunasoma pia ujumbe huu mahusi kutoka, (Mk 13:10; 14:9; Mt 28:18-20; Lk 24:47).
Hata hivyo huu utume wa kimisioni na wa dharura ulitimia kwa ufanisi mkubwa wa
wafuasi wake Yesu. “Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana
nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!” 1Kor 9:16. Hapa tunaweza kuona mkazo na utofauti
kwa namna Mtakatifu Paulo alivyouchukulia kwa upekee utume wake wa kimisionari.
Hakika ni Mtume wa mataifa na jitu la sifa!
Hata
hivyo, sharti linalowekwa kwa wale ambao wanataka kufaidika na ‘Habari
Njema,’ni KUAMINI na KUBATIZWA (Yoh 3:18; Mdo 2:38; 16:31-3). Haya mambo mawili
ni muhimu sana kwa imani hai na ya wazi inayohitimishwa kwa fumbo la Sakramenti
ya ubatizo. “Kwa
kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika
Kristo mmemvaa Kristo. Hapana
Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke.
Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi,
mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi,” Gal 3:26-29. Kristo
ndiye kielelezo chetu na ndiye njia, kweli, na uzima, na mtu hawezi kwenda ya
Baba bila kupitia kwa Yesu, Yoh 14:6. Hivyo hivyo hakuna awezaye kwenda kwa
Yesu kama hajavutwa na Baba. “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na
Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:44. Ndugu yangu
tuliyesafiri sote katika tafakari hii, watambua umuhimu wa Yesu katika maisha
yako na hatma ya umilele wako? Kama bado, ni wakati wa kutafakari na kuchukua
hatua.
Tumsifu Yesu Kristo!
Mtakatifu Paulo Mtume, Utuombee.
“Na
uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo
uliyemtuma,” Yoh 17:3
Tusali: Ee Yesu Mwema, tufanye vyombo vya amani, upendo, haki, na
habari njema pale tulipo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario