IJUMAA WIKI YA 2
YA MWAKA-I
Somo: Ebr 8:6-13
Zab: 85:8, 10, 11-12, 13-14
Injili: Mk 3:13-19
Nukuu:
“Maana, awalaumupo,
asema Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, Nami nitawatimizia nyumba ya Israeli
na nyumba ya Yuda agano jipya,” Ebr 8:8
“Maana hili ndilo agano nitakaloagana na
nyumba ya Israeli Baada ya siku zile, asema Bwana; Nitawapa sheria zangu katika
nia zao, Na katika mioyo yao nitaziandika; Nami nitakuwa Mungu kwao, Nao
watakuwa watu wangu,” Ebr 8:10
“Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na dhambi
zao sitazikumbuka tena,” Ebr 8:12
“Kwa kule kusema, Agano
jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa
kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka,” Ebr 8:13.
“Akaweka watu kumi na
wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo,” Mk
3:14-15
TAFAKARI: “Nitawapa
sheria zangu katika nia zao, Na katika mioyo yao nitaziandika; Nami nitakuwa
Mungu kwao, Nao watakuwa watu wangu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, ni hali ya ubinadamu wetu kurudisha kwa kiwango kile kile cha
uovu tulichotendewa na watesi wetu. Ila kwa kufanya hivyo hata kama kutatupatia
furaha na amani, amani na furaha hiyo ni ya muda mfupi tu. Uovu si asili ya
ukamilifu ambao ni Mungu mwenyewe. Kumbe amani ya kweli tunaipata pale
tunapoushinda uovu kwa wema. Tusipoteze muda kushindana na uovu, bali tuenende
kwa kutenda mema. “Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu
akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili,” Mt 5:39. Kumgeuzia mtesi wako
shavu la pili kuna maana ya kutokulipiza kisasi zaidi ya kuenenda katika
kutenda mema. Wengi kati yetu twaonekana waovu na watenda maovu kwa sababu
katika maisha yetu hatujawahi kuonyeshwa upendo wa kweli.
Mungu
anaweka agano na wana wa Israeli na kwa namna ya pekee analiweka agano hilo
nasi leo kwa kusema, “Nitawapa sheria zangu katika nia zao, Na
katika mioyo yao nitaziandika; Nami nitakuwa Mungu kwao, Nao watakuwa watu
wangu.” Huyu ni Mungu asiyependa kumpoteza ye yote yule aliye muumba kwa sura
na mfano wake. Sheria tunayopewa kumbushwa leo, ni upendo ule wa kimungu,
yaani, kupenda bila kipimo, Yoh 13:1. Kama wafuasi wake Kristo tunaalikwa
kuishi upendo huu wa Mungu bila licha ya mapungufu yetu. “Nao hawatafundishana
kila mtu na jirani yake, Na kila mtu na ndugu yake, akisema, Mjue Bwana; Kwa
maana wote watanijua, Tangu mdogo wao hata mkubwa wao,” Ebr 8:11. Kao la Bwana
ni kuishi katika upendo wake siku zote za maisha yetu tukitumainia tumaini lile
la milele. “Kwa sababu nitawasamehe
maovu yao, Na dhambi zao sitazikumbuka tena,” Ebr 8:12. Agano hili jipya la
Mungu linatuweka karibu sana na Mungu, kwani huu ndio wakati wa wokovu, na
Kristo ndiye Njia, Kweli, na Uzima. Je, nifanye nini?
Ndugu yangu, jambo la
kufanya ndilo hili, jitahidi kila siku kutambua vipawa vyako na vitendee haki
kwani kwa kuvijua ndivyo utakavyoweza kumtumikia Mungu vizuri katika maisha
yako. Usipoteze muda wako kuvikodolea macho vipawa vya wengine na kutokufanya chochote
kuhusu vile alivyokupa Mungu ambavyo bado hujavigundua. Moja ya kuwa mikono
salama ya Mungu ni kufanya mapenzi yake, na hasa kuwa mwaminifu kwa kile
unachokifanya sasa. Kwa kuliwezesha hili, Yesu anawafunda wanafunzi wake
waenende katika idadi ya watu kumi na mbili kama moja ya njia ya kufanya vizuri
na kuwa na mshikamano. Hivyo Yesu, “akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa
pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena
wawe na amri ya kutoa pepo,” Mk 3:14-15. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Wabaya
huinama mbele ya wema, Na wasio haki malangoni mwao wenye haki,” Mit 14:19
Tusali:-Ee Yesu, wajue
kile tulicho, tuwezeshe katika hicho tulicho tukutumikie kwa ukamilifu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario