martes, 17 de enero de 2017

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 2 YA MWAKA-I


ALHAMISI WIKI YA 2 YA MWAKA-I

Somo: Ebr 7:25-8:6

Zab: 40:7-8a, 8b-9, 10, 17 (8a-9a)              

Injili: Mk 3:7-12

Nukuu:

Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu,” Ebr 7:26 

 “Maana kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe vipawa na dhabihu; kwa hiyo lazima huyu naye awe na kitu cha kutoa,” Ebr 8:3

 “Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu,” Mk 3:11 

Akawakataza sana, wasimdhihirishe,” Mk 3:12

TAFAKARI:Kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe vipawa na dhabihu.”

Wapendwa wana wa Mungu, tofauti katika utendaji zipo na hatuwezi kuzizuia kwa sababu kila mmoja wetu ni tofauti na wapekee. Tunachotakiwa kufanya ni kuruhusu ndani ya mioyo yetu na katika utendaji wetu, umoja katika utofauti. Mfumo huu unatija sana katika maendeleo ya mwanadamu ikiwa ni watu na mazingira yanayomzunguka. Ni kwa namna hii vipaji hukuzwa, na jamii hufaidika navyo. Vipaji na karama hizo ni kwa kufaidiana na wala isiwe sababu ya kujiinua kwa chochote kile kwa sababu tumepewa bure nasi twapaswa kuvitoa bure, Mt 10:8. Na tufanyavyo hivyo twafananishwa na wale “watumikiao mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni, kama Musa alivyoagizwa na Mungu, alipokuwa tayari kuifanya ile hema; maana asema, Angalia ukavifanye vitu vyote kwa mfano ule ulioonyeshwa katika mlima,” Ebr 8:5. Nione furaha kwa nafasi niliyopewa na jamii kuwahudumia wote pasipo kuwabagua kwani kwa kupitia huduma hiyo watu wana wa Mungu uneemeshwa na Mungu utukuzwa.

Kama ilivyokuwa kwa Daudi wasifu ule aliopewa na wanawake wale walioyaona makuu ya Mungu kupitia kifo kile cha Goliathi, “Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake,” 1Sam 18:7, mapepo pia wanaona utofauti uliopo kwa Yesu kwa kile alicho na huduma ile aitoayo.Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu,” Mk 3:1. Jambo la ajabu Yesu hayasadifu wala kuyashabikia haya yasemayo na mapepo. Kumbe tunakumbushwa kuwa makini hasa na vyanzo vya wasifu tupewao. Yesu “Akawakataza sana (mapepo), wasimdhihirishe,” Mk 3:12.

Ndugu yangu, kila kishindo kina maana yake. Mara uyapatapo hayo katika utume wako chukua nafasi ya pekee kuyatafakari kwa kina. Na hapa kwa namna ya pekee tunakumbushwa tusifanye jambo lo lote lile kwa lengo la kujipatia sifa pasipo kweli na haki. Nisifanye pia kwa kutumiza sheria tu pasipo upendo ndani yake kama asemavyo Mtakatifu Augustino wa Hippo “kwa kupenda kwa dhati waweza kufanya vyote. Naye Kristo “kama angekuwa juu ya nchi, asingekuwa kuhani; maana wako watoao sadaka kama iagizavyo sheria,” Ebr 8:4. Kumbe yale tuyatendayo tukitegemea milipuko ya sifa, shangwe, makofi, na nderemo zisizo na siha utoweka vivyo hivyo kama upepo wa kisulisuli.

Wewe na mimi kama wafuasi wake Kristo, Kristo ndiye kuhani yetu Mkuu na Mtakatifu na asiyekuwa uovu na mwenye kutuongoza kuliko kweli na haki. “Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu,” Ebr 7:26. Ni kwa kupitia kuhani huyu Mkuu na Mteule wa Mungu kwa sadaka yake moja pale msalabani tuliondolewa na kusamehewa dhambi zetu. Leo kwa kupitia watumishi wake, waliowekwa wakfu, yaani, mapadre na maaskofu kazi ile ile ya kuwaondolea watu wake dhambi inafanyika. “Maana kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe vipawa na dhabihu; kwa hiyo lazima huyu naye awe na kitu cha kutoa,” Ebr 8:3

Hivyo, ndiye Kristo huyu “ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake,” Ebr 7:27. Ndugu yangu, kwa kupitia Kristo tunapatanishwa kila siku na Mungu, na kwa kupitia Sakramenti ya Upatanisho tunapatanishwa nafsi zetu, Mungu na jirani zetu. Kristo ndiye daraja Imara katika patanisho hizi.

Wapendwa wana wa Mungu, kwa kupitia Kristo Yesu tunatimiza sheria yake katika kuchukuliana mizigo yetu ya kila siku. “Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo,” Gal 6:2. Kuchukuliana mizigo ni pamoja na kuonyana kindugu. Tuchukuliane wapya kila siku na kuona ninawajibika kumsaidia mwenzangu kuenenda katika njia iliyo bora zaidi bila kubeba historia ya mtu kama kigezo cha kutokuona mabadiliko ya kweli ndani yake. Neema ya Mungu hufanya kazi kuliko akili na uelewa wetu wa kibinadamu. Turuhusu neema hizo zifanye kazi kwa wale wote tunaowajibika nao au wanaohitaji msaada na huruma yetu. “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona.” 1Yoh 4:20. Huruma na neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.

Basi tuchukuliane katika upya kila siku. Ni kweli mambo siyo rahisi katika uhasilia wake, ila turuhusu neema za Mungu zifanye kazi nasi tuwe watumishi tu tunao timiza wajibu wetu kwa unyenyekevu, Lk 17:10. Na tuyafanyavyo hayo kwa ndugu zetu, Kristo upata “huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora,” Ebr 8:6. Na yatupasa kufanya hivyo mara zote kwa sababu, “amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake,” 1Yoh 4:21. Hakutakufaidia chochote unapoishi kwa chuki na uhasama. Ufanyavyo hivyo wazidi jipalia moto mwenyewe siku ile ya kiama ya mwisho.

Wapendwa katika Kristo, kuuishi ukristo wetu bila kuwa tayari kuchukuliana mizigo yetu na mapungufu yetu hasa katika msamaha wa kweli bado hatujajua namna ya kumpenda Mungu kwa kuzishika amri zake. “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito,” 1Yoh 5:3. Je, huoni furaha ya kweli unapopatana na ndugu yako au jirani yako? Ni ugonjwa mbaya sana kufurahia mateso ya mwenye haki kwa kutumia vibaya nafasi uliyonayo.

Tumsifu Yesu Kristo

Kwani hasira humwua mtu mpumbavu, Nao wivu humwua mjinga,” Ayu 5:2

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie hekima katika kuona, kuamua, na kutenda. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario