domingo, 8 de enero de 2017

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 1 YA MWAKA-I


JUMANNE WIKI YA 1 YA MWAKA-I

Somo: Ebr 2:5-12

Zab: 8:2ab, 5, 6-7, 8-9

Injili: Mk 1:21-28

Nukuu:

“Maana hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali fulani, akisema, Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie?” Ebr 2:5-6

“Umemfanya mdogo punde kuliko malaika, Umemvika taji ya utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako,” Ebr 2:7

 “Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake,” Ebr 2:11

 “Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi,” Mk 1:22

 “Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii!” Mk 1:27

TAFAKARI:Yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake.”

Wapendwa wana wa Mungu,  Mungu wetu sio Mungu wa kushindwa hata kidogo. Kwa maneno mengine, Mungu ninaye mwamini hawezi kuliumba jiwe kubwa kiasi chochote kile unachoweza kufikiria alafu ashindwe kulibeba jiwe hilo. Huyo siye Mungu ninayemwamini! Je, waamini Mungu anaweza? Licha ya udogo wetu na udhaifu wetu, Mungu hachoki kutumwagia neema na baraka zake. Lengo la Mungu ni kukupata wewe na mimi kwa sababu kwa upendo wake na ilivyo mpendeza katuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Ni katika hali na upendo huu, Mungu “hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali fulani, akisema, Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie?” Ebr 2:5-6. Hakika ni upendo tu!

Na wakati ulipotimia na alivyoona inafaa, Mungu aliingia ndani ya historia yetu, Gal 4:4-5, na kuyaratibisha yote kuelekea katika ukamilifu wa kila alichokiumba. Hapa ndipo Neno yule wa Mungu, Yesu Kristo, alifanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Licha ya kuwa na asili mbili, yaani, Mungu na Binadamu, ni katika ubinadamu wake huo nasi tunapata nafasi ya kushiriki umungu wa Mungu kupitia Kristo Yesu, Mtu Mpya. Kwa maana hiyo, Mungu  ‘amemfanya mdogo punde kuliko malaika, amemvika taji ya utukufu na heshima, amemtawaza juu ya kazi za mikono yako,’ Ebr 2:7

Ni katika utii na unyenyekevu wa Kristo Yesu licha ya Umungu wake, Mungu Baba ‘ameweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake,’ Ebr 2:8. Ukweli ni kwamba, “vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3. Hakuna kama Kristo Yesu ndugu yangu. Yeye ndiye Njia, Kweli, na Uzima wetu, Yoh 14:6. “Ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu,” Ebr 2:9. Huu ni upendo mkubwa sana kwetu. Hakika Kristo Yesu anatupenda upeo, Yoh 13:1. Je, huamini?

Pamoja na ukweli huo, maisha yetu hapa duniani ni jaribu, dhamana, na jukumu la muda mfupi. Mwonekano wa maisha katika mambo haya makuu matatu tukiyaelewa na kuyaishi vyema, hakuna jambo lolote litakalo tukwamisha kuifikia taji ile, yaani, utakatifu ulio cheo chetu. Hivyo kama wewe na mimi ni wafuasi wa Kristo, yatupasa kuelewa ukweli huu: “Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso,” Ebr 2:10.

Hivyo mateso na hata kifo ndani na katika Kristo Yesu siyo tena laana. Mateso ndani na katika Kristo Yesu yana uhusiano wa karibu na utukufu. Ni kwa maana hii twasema, “hakuna utukufu pasipo msalaba. “Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake,” Ebr 2:11. Tu rafiki ya Kristo tusipo saliti Njia aliyoipitia (mateso, na kifo), Kweli aliyoitangaza na kuiishi (Neno la uzima), na Uzima anaotujali kila siku (kuishi kwa uaminifu Sakramenti Takatifu za Kanisa).

Wapendwa wana wa Mungu, uwepo wa Kristo katika maisha yetu umetuweka karibu sana na Mungu naye ndiye Mungu. Alitamkalo Yesu limejaa mamlaka yote kwani ni neno aliyemwilishwa, Yoh 1:14. “Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi,” Mk 1:22. Litamkwapo jina la Yesu hakuna nguvu yoyote ile na hasa nguvu za giza zinazoweza kustahimili jina hili Tukufu kupita majina yote. “Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza?” Mk 1:23-24. Nguvu na Utukufu wa Kristo hata pepo wachafu wanajua na kukiri. “Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke,” Mk 1:25.

Pamoja na ukweli huo, Yesu hatutaki tubaki katika hatua hii ya miujizamiujiza kama hitimisho la imani yetu. Hivyo anatupa angalizo na kusema, “msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni,” Lk 10:20. Na majina yetu hayatoandikwa mbinguni kama hatuna ukamilifu, yaani,  utakatifu. Bila huu ukamilifu-utakatifu-hatuwezi muona Mungu. Na mwito wa Yesu kwetu ni huu, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu yameandikwa mbinguni,” Mt 5:48.

Nguvu na Mamlaka aliyo nayo Kristo Yesu, hakuna chochote tutakachomwomba kwa imani na dhamiri njema aache kutupatia. Na yote hayo huyafanya kadiri ya mapenzi yake na mahitaji yetu. “Ndiye Mungu mwenye hekima peke yake. Utukufu una yeye kwa Yesu Kristo, milele na milele. Amina,” Rum 16:27. Ukweli huu unathibitika ndani ya sinagogi alivyokinyamazisha kichwa cha pepo mchafu na kuamuru amtoke mtu yule. “Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii!” Mk 1:27. Hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Kuwa na Imani.

Tumsifu Yesu Kristo!

Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina,” Rum 11:36

Tusali: Ee Yesu Mwema, yatazame upya maisha yetu hasa pale tunapo asi kweli yako ndani yetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario