SIKUKUU YA UBATIZO WA BWANA
Somo
I: Isa 42:1-4, 6-7
Zab:
29:1-2, 3-4, 3, 9-10
Somo
II: Mdo 10:34-38
Injili:
Mt 3:13-17
Nukuu:
“Tazama
mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa
naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu,” Isa 42:1
“Mwanzi
uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu
kwa kweli,” Isa 42:3
“Mimi,
Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa
uwe agano la watu, na nuru ya mataifa,” Isa 42:6
“Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya
kuwa Mungu hana upendeleo; bali
katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye,” Mdo 10:34-35
“habari
za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu
naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na
Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye,” Mdo 10:38
“Lakini
Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?”
Mt 3:14
“Yesu
akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki
yote. Basi akamkubali,” Mt 3:15
“Naye
Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia,
akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake,” Mt 3:16
“na tazama,
sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa
naye,” Mt 3:17
TAFAKARI:
“Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa
naye.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo kwa furaha kubwa Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana.
Swali ambalo hutujia hata kama hatutaki ni hili: Je, Yesu alihitaji kubatizwa?
Jibu ni ndiyo na hapana! “Ndiyo” ya ubatizo wa Yesu imelenga katika
“kielelezo,” “Mfano wa kufuata,” yaani kupitia mfano huo tunao uthibitisho
pasipo shaka wa maneno haya Yesu, kwamba, “Mimi
ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh
14:6. Mamlaka ya Maneno haya ya Yesu (Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima)
yanawekwa wazi na nafsi ya tatu na ya kwanza ya Mungu mwenyewe pale Mbingu
zilipofunguka, “Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake, na tazama,
sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa
naye,” Mt 3:16-17
Ubatizo
aliokuwa anaufanya Yohana Mbatizaji ulikuwa ubatizo wa maji kama ishara ya toba
ya kweli ikiwa ndiyo, maandalizi ya ubatizo wenyewe wa Roho Mtakatifu na Moto,
Lk 3:16. Ubatizo huu wa toba haukumwondolea mtu dhambi, na kwa maana hiyo, hata
Yohana Mbatizaji alihitaji ubatizo wa Roho Mtakatifu na Moto. Yohana Mbatizaji
anaweka jambo hili wazi kwa kuonyesha hali ya kusita pale Yesu alipomwendea ili
abatizwe naye. Naye anamuuliza Yesu, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja
kwangu?” Mt 3:14.
Je,
ubatizo wa Yohane Mbatizaji ulikuwa ni kupoteza muda? La hasha! Kwa neno
“maandalizi,” linabeba dhana nzima ya uwepo wetu hapa duniani. Mahali hapa siyo
sehemu ya kudumu, bali tunapita kuelekea umilele. Hivyo kuufikia umilele ambao
sasa unawezekana ndani na katika Kristo, maandalizi ni muhimu ikiwa ni pamoja
na kuishi katika hali ya neema. Huku ndiko kufanya toba ya kweli kama ilivyo
ubatizo ule wa maji ambao ulikuwa ni kuwaandaa watu katika kweli na haki ambayo
ukamilifu wake upo kwa Kristo mwenyewe. Lengo la toba ni ondoleo la dhambi.
Hivyo, “Yohana alitokea,
akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi,” Mk
1:4. Na ondoleo hili la dhambi sasa ni Kristo Mwenyewe kwa kupitia Sakramenti
ya upatanisho/kitubio. Kwa maana “hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa
maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi
kuokolewa kwalo,” Mdo 4:12.
Wapendwa wana wa Mungu,
ahadi za Mungu kwetu zinatufikia pale tunapofanya toba ya kweli na majuto ya
dhambi zetu. “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani
kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote
wafikilie toba,” 1Pet 3:9. Mungu leo ametimiza ahadi yake kwa uvumilivu wa watu
wake kwa kazi iliyofanywa na Yohane Mbatizaji. Kristo Yesu ndiye kielezo halisi
cha Ubatizo wa Roho Mtakafu na Moto. Hizi ndizo “habari
za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu
naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na
Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye,” Mdo 10:38. Huyu ni Mwanangu,
mpendwa wangu, ninayependezwa naye!
Tangu
sasa neema na baraka zimefunguliwa kwa watu wote. Mlango huu umefunguliwa hata
kwa wale walioonekana ni wapagani kwa njia ya maono ya Petro alipokuwa akisali
na mbingu zikafunguka, na chombo kikashuka kama nguo kubwa, wakiwemo aina zote
za wanyama wenye miguu minne, watambaao, na ndege wa angani, Mdo 10:11-12.
Kadiri ya maono haya, Petro alisita kupokea maagizo ya Mungu kwa sababu ndani
yake walikuwepo wanyama wale waliokatazwa kuliwa nao ni najisi, Mdo 10:14. “Pamoja
na hayo, wanyama hawa hamtawala katika wale wenye kucheua, na katika wale walio
na kwato; ngamia, kwa sababu yuacheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na wibari, kwa sababu yeye hucheua
lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na
sungura, kwa sababu hucheua, lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo
kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu. Msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga
yao; hao ni najisi kwenu,” Law 11:4-8.
Wapagani hawakuchangamana
na Wayahudi, na mbaya zaidi Wayahudi wale ambao kwa namna ya pekee ndio
walikuwa Kanisa la Mwanzo. Hizi ni changamoto ambazo zitapelekea kuwepo kwa
Mkutano/Mtaguso huko Yerusalemu, Mdo 15:1-41. Kuchangamana kwao ni najisi kama
ilivyokuwa kula nyama za wanyama hawa au kugusa mizoga yake. Badala yake “sauti ikamjia,
kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule. Sauti
ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe
najisi,” Mdo 10: 13, 15. Neno “Ondoka uchinje ule,” linatupa
uthibitisho wa kufunguliwa neema na baraka kwa watu wote wenye hofu ya Mungu.
Tendo hili
linathibitishwa na Petro mwenyewe huko Kaisaria kwa ujumbe uliotumwa kwake na Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu,
aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, Mdo 10:22. Mtume Petro kwa
kuona tendo hili kubwa likitokea hata kwa wapagani kushukiwa na Roho Mtakatifu,
anatoa hitimisho la Imani na kusema, “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana
upendeleo; bali katika kila taifa
mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye,” Mdo 10:34-35.
Hivyo
kumcha Mungu na kutenda haki ndicho kibali chakukubaliwa na Mungu. Kibali hiki
ndicho kielelezo cha utakatifu wetu. Na utakatifu huu ndio cheo chetu mbele ya
Mungu licha ya utofauti rangi zetu, familia zetu, koo zetu, makabila yetu, na
utaifa wetu. Haya yote yaliyo ya kibinadamu bila utakatifu wa Mungu katika
kumcha na kutenda haki hayana fadhila yoyote mbele za Muumba wetu.
Kwa
maana hiyo, ubatizo wa Bwana leo ni kielelezo na mfano wa hayo yote
niliyoyasema. Kwa maneno mengine Yesu kama Yesu hakuhitaji ubatizo huo katika
maana ya ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi, Mk 1:4. Na
hivi ndivyo Yesu alivyothibitisha ukweli huu kwa kumtaka Yohana Mbatizaji
akamilishe hili la kuwa kielelezo, na kumwambia, “Kubali hivi
sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali,” Mt 3:15.
Na huu ndio ule utabiri aliousema Nabii Isaya kwa mtumishi yule
atakayepewa Mamlaka na Mungu juu ya watu wake waliomridhia. “Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu,
ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye
atawatolea mataifa hukumu,” Isa 42:1. Mamlaka yake ni pamoja na kutoa hukumu ya
haki na kweli. “Mimi, Bwana,
nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe
agano la watu, na nuru ya mataifa,” Isa 42:6. Je, ujio wa Mjumbe huyu wa Mungu
ni mabadiliko ya kila kitu ambacho kilikuwa hapa mwanzo? La hasha! “Mwanzi
uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu
kwa kweli,” Isa 42:3.
Je,
Mjumbe huyu wa Mungu atafanya nini basi kwa hali yetu ya kila siku? Kuhusu
ukweli wa jambo hili, Yesu akiwa ndiye Mjumbe halisi wa Mungu na upendo wa
Mungu kwa wanadamu, (Wewe ndiwe Mwanangu,
mpendwa wangu; nimependezwa nawe) mwenyewe
anasema hivi, “Msidhani ya kuwa
nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka
mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka
,hata yote yatimie,” Mt 5:17-18. Ndugu yangu, amri za Mungu ni zile zile na
mafundisho ya Kristo ni yale yale yanayotuongoza kumjua Mungu, kumpenda Mungu,
kumtumikia Mungu, na Mwisho turudi kwake Mbinguni. Mimi na wewe yatupasa kuwa
waaminifu kwa amri hizi na kuziishi ikiwa ni pamoja na mafundisho tunayopewa
kila siku. Hii ndiyo maana ya kutimiliza torati. Wayahudi wakati wa Yesu
hawakuwa waaminifu kuhusu Torati. Badala yake waliitafsi ili ikidhi mahitaji na
malengo yao. Waliishi tafsiri hii-TALMUD, kama ukweli wa Mungu uliopotoshwa.
Yesu anawarudisha kwenye mizizi la sheria ya Mungu, yaani Torati itimizwe kama
yalivyokuwa makusudi ya Mungu na siyo ya mwanadamu.
Kazi
hii ya Yesu ni kuweka wazi yale yote yaliyo giza, na kuwaweka watu wote huru.
Na haya ndiyo yaliyotabiriwa na Nabii Isaya juu wa Mtumishi huyu wa Mungu
kwamba, “kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale
walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa,” Isa 42:7. Maneno haya ya Nabii
Isaya yanarudiwa na Yesu mwenyewe alipoianza kazi yake rasmi ya kupambana na
giza ili sote kutuweka huru. Naye Yesu anasema, “Roho wa Bwana yu
juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha
huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka
wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Ndugu yangu niliyesafiri nawe katika
tafakari hii, leo tunapofanya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, ni wakati wa
kukumbuka maneno haya ya Yesu unapoutazama ubatizo wako wenyewe. Kwa ubatizo
wako haya aliyoyasema Yesu yametimia ndani ya moyo wako. “Leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk
4:21b. Ndugu yangu wauthamini ubatizo wako?
Marieta
ni mwanafunzi wa dini ambaye mara baada ya mafundisho yake alibahatika kupata
Sakramenti tatu kwa wakati mmoja, yaani, Sakramenti ya ubatizo,
Kimpaimara/kuimarishwa, na Ekaristi Takatifu. Kwa Sakramenti ya ubatizo
alipakwa Mafuta Matakatifu utosini na kifuani. Na kwa Sakramenti ya Kipaimara
alipakwa mafuta Matakatifu ya Krisma kwenye paji la uso. Na baadaye alipokea
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.
Baada
ya tukio hili, Marieta hakuonekana tena Kanisani. Sakramenti hizi za mkupuo
zilikuwa ndiyo tiketi ya ‘bye bye.’ Marieta alijichanganya sana na malimwengu
na kwa waganga wa kienyeji ndiko kulikokuwa hija yake. Waganga hawa walimtengeneza
kweli kweli. Alipewa chale utosini, paja la uso, kifuani na kiunoni kama mkanda
wa Rombo mcheza filamu.
Lakini
pamoja na kinga hii kama alivyoambiwa na magwiji hawa, Marieta hakuacha
kuweweseka na kupandisha maruhani kila mara. Marafiki zake walimshauri awe
anakwenda Kanisani kusali. Hata hivyo maruhani haya humwangusha chini na
kugaagaa wakati ule wa kufukiza ubani na Mageuzo. Je, tatizo lipo wapi?
Ndugu
yangu, wewe uliyebatizwa umeingia mkataba na Mungu na kuwa kiungo cha Kristo.
Unapousaliti ubatizo wako kwa kwenda kwa waganga wa kienyeji, na kupigwa chale
sehemu zile ulizopakwa Mafuta Matakatifu ya Krisma unausaliti ubatizo wako na
kujiweka wakfu kwa shetani. Kwa tendo hili unakosa kinga kwani hata malaika
mlinzi wako anaondoka kwa sababu mwili wako kama hekalu la Roho Mtakatatifu ni
chafu, 1Kor 6:19. Hivyo utembeapo njiani mwili wako unakuwa kama mnara wa simu,
na unasomeka hivi muda wote; “network is full.” Pepo yeyote anayerandaranda
lazima akuingie kwa sababu huna kinga tena. Haya ndiyo mateso ya wengi leo.
Ponya
yako katika tatizo hili lazima ufanye ukiri kwa toba ya kweli, kujuta dhambi, na kuziungama dhambi zako ili upate uponyaji
ndani yako. Kiti cha huruma ya Mungu kipo muda wote na kwa wakati wowote.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi
tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo
alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi
tuenende katika upya wa uzima,” Rum 6:4
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, na unayenipenda upeo, asante kwa neema na baraka zako zisizo na
ukomo. Amina.
No hay comentarios:
Publicar un comentario