JUMAMOSI WIKI YA 1
YA MAJILIO
Somo: Isa 30:19-21, 23-26
Zab: 147:1-2, 3-4, 5-6
Injili: Mt 9:35-10:1,
6-8
“Na ingawa Bwana
atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa
tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako,” Isa 30:20
“Na tena nuru ya mwezi
itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya
siku saba, katika siku ile Bwana atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya
pigo la jeraha yao,” Isa 30:26
Ndipo alipowaambia wanafunzi wake,
Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke
watenda kazi katika mavuno yake,” Mt 9:37-38
“Na katika kuenenda
kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia,” Mt 10:7
“Pozeni wagonjwa,
fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure,” Mt
10:8
TAFAKARI: “Ufalme wa mbinguni
umekaribia.”
Wapendwa wana wa
Mungu, kauli mbiu hii “Ufalme wa mbinguni umekaribia,” inatualika kujiandaa
kimwili na kiroho. Maandalizi haya yatuguse na kuona umuhimu wa kufanya hivyo. Wakati
mwingine tunajisahau sana na kuishi bila mwelekeo wowote hasa kiroho. Ufalme wa
Mbinguni kwanza ni mwito binafsi kwa sababu hatujui siku wala saa. Hivyo ni
mwaliko kwa kila mmoja binafsi, na pili wote kwa ujumla. Hiki ndicho Yesu
anachowataka wafuasi wake wakifanye. “Na katika kuenenda kwenu, hubirini,
mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia,” Mt 10:7. Ufalme huu wa mbinguni uliokaribu unajidhihirisha kwa
matendo makuu ya Mungu ya upendo na huruma yake. “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni
pepo; mmepata bure, toeni bure,” Mt 10:8.
Matendo haya ya huruma na upendo yaanze hapo ulipo kadiri ya nafasi yako na
wito wako.
Ufalme
wa Mbinguni ambao tunausubiri ni hali ile ya kuanza upya vyote na Mungu. Kuanza
huku upya na Mungu kunatudai kujiandaa vyema mwili na roho. Huku ndiko
kutakakotupelekea kuponywa majeraha yetu. “Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua,
na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile
Bwana atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao,” Isa
30:26.
Wapendwa wana wa Mungu, tutumie vizuri muda huu kujiweka
vyema mwili na roho ili ufalme huo utakapofika tuwe tayari kuupokea. Chambua
mahusiano yako na Mungu, jirani, na mazingira yako ya kila siku. Je, katika
mahusiano hayo ni wapi palipokosa afya? Nenda kwa tabibu ili upate tiba
stahiki. Sakramenti ya upatanisho inatuwezesha kuyarejesha mahusiano yetu na
Mungu, Jirani, na mazingira yetu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi zaeni matunda
yapasayo toba,” Mt 3:8
Tusali:-Ee Yesu Mwema,
nakutumainia, na kwa nguvu na neema zako, niyaanze yote upya pamoja nawe. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario