ALHAMISI WIKI YA 3
YA MAJILIO
Somo: Isa 54:1-10
Zab: 30:2, 4, 5-6, 11-12, 13b
Injili: Lk 7: 24-30
Nukuu:
“Imba,
wewe uliye tasa, wewe usiyezaa; paza sauti yako kwa kuimba, piga kelele, wewe
usiyekuwa na utungu; maana watoto wake aliyeachwa ni wengi kuliko watoto wake
yeye aliyeolewa, asema Bwana,” Isa 54:1
“Usiogope;
maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau
aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena,” Isa 54:4
“Maana milima itaondoka, na vilima
vitaondolewa; bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano langu la amani
halitaondolewa; asema Bwana akurehemuye.” Isa 54:10
“Lakini
mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Jueni, watu wenye
mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika majumba ya kifalme,” Lk 7:25
“Lakini,
mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye zaidi ya nabii,” Lk
7:26
“Nami nawaambia, Katika wale waliozaliwa na
wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana; lakini aliye mdogo katika ufalme wa
Mungu ni mkuu kuliko yeyé,” Lk 7:28
“Lakini, Mafarisayo na wana-sheria walilipinga
shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye,” Lk 7:30
TAFAKARI:
"Milima itaondoka, na vilima vitaondolewa; bali wema wangu hautaondoka kwako,
wala agano langu la amani halitaondolewa; asema Bwana akurehemuye.” Isa 54:10
Mpendwa
mwana wa Mungu, na tuanze safari yetu tukilitafakari Neno la Mungu kwa siku ya
leo. Ili
kumjua vizuri Yesu Kristo na uwepo wake katika maisha yako, leo anatupa
changamoto na kutufikirisha kwa undani. Naye anakuuliza wewe na mimi hivi; “Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa
mavazi mororo? Jueni, watu wenye mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika
majumba ya kifalme,” Lk 7:25. Nini maana yake? Ni upendo wa ajabu sana
kwetu wanadamu kwamba, NENO kafanyika Mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Na NENO
huyu ni nani? Mwinjili Yohana anatuambia, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye
Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa
Mungu,” Yoh 1:1-2. Kristo Yesu, ambaye ndiye Neno aliyefanyika Mwili na kukaa
kwetu, ni Mungu. Mungu huyu aliwapenda wote bila ubaguzi kwa sababu ndani ya
kila mmoja wetu kuna chapa yake, Mwa 1:27. Ni dhambi zako na zangu ndizo
zinazotutenga na upendo huu wa Mungu.
Mungu huyu hakuonekana
katika majumba ya kifalme wala kuvaa mavazi nyororo, bali alionekana kwa wote
waliomwihitaji, wanyofu wa moyo, na wale wote walioridhia kauli mbiu yake,
yaani, ‘Ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini Injili-Habari Njema, Mk
1:15. Marafiki zake wa karibu walikuwa wadhambi, wazinzi, watoto, wanawake,
wakoma, watoza ushuru, na wale wote kwa sababu moja au nyingine walitengwa na
jamii husika kwa kutolandana nayo.
Mungu huyu alikuwa na
ndiye hata leo na umilele wote, ‘sauti ya wasio na sauti.’ Leo Kanisa lapaswa
kubeba na kuishi kweli hii ya Kristo Yesu pasipo shaka wala woga, kama sehemu
na elekezo la sauti ile ya Kinabii. Na Kanisa hapa ninamaanisha Wabatizwa wote,
na wale wote waliopewa dhamana na Mama Kanisa kama viongozi katika ngazi
mbalimbali. Naye Yesu anazidi kuhuisha nafsi zetu kwa kuzihoji, “Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam,
nawaambia, na aliye zaidi ya nabii,” Lk 7:26. Kwa maana nyingine, ni
kipi kinachokusukuma kwa Kristo? Je, wamchukulia Kristo kama shirika ya msalaba
mwekundu? Kristo ni nani, na nini katika maisha yako? Je, ni mmoja ya watu
maarufu katika historia? Je, leo Yesu kwako ni Yesu wa historia?
Pamoja na mashaka
aliyokuwa nayo Yohana Mbatizaji, Yesu apindishi kweli iliyo ndani ya Yohana
Mbatizaji. Naye Yesu anasema, “Huyo ndiye
aliyeandikiwa haya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako,
Atakayeitengeneza njia yako mbele yako,” Lk 7:27. Na ndiyo ilivyokuwa
kadiri ya mpango wa Mungu. Mashaka aliyokuwa nayo Yohana Mbatizaji hayana
tofauti na mashaka yetu, hasa pale tunapokumbana na sintofahamu katika maisha
yetu ya kila siku. Wengine tunakoswa na uvumilivu na subira, na mwisho
tunaishia kuaguliwa kwa waganga wa kienyeji, wadanganyifu, na wasio na upeo
kuhusu Mungu aliye hai.
Hata hivyo, Yohana
anabaki kuwa mfano wa kuigwa hata katika hali ya udhaifu wake. Naye Yesu
analithibitisha hilo na kusema, “Nami
nawaambia, Katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana;
lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeyé,” Lk 7:28. Maneno
haya ya Yesu Kristo yanakuwa faraja kubwa kwa wema na wadhambi kwani na
wao-wadhambi, wanayo nafasi mbele ya Mungu. Kinachotakiwa ni utayari wako tu wa
kuacha njia yako mbaya na kuanza yote upya na Mungu, ikiwa ni ndani na katika
Kristo Yesu. “Na watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya
Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohana,” Lk 7:29. Bila shaka jambo
hili halikuwa habari njema kwa wale wote waliojihesabia haki mbele ya Mungu
pasipo Mungu Mwenyewe.
Hawa
ni wale Mafarisayo, waandishi na wana-sheria. Hakika walisahau kuwa sheria
iliyo kubwa kuliko zote ni UPENDO. Hata hivyo, hivi ndivyo ilivyokuwa, “Lakini,
Mafarisayo na wana-sheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa
hawakubatizwa naye,” Lk 7:30. Hawakuona chochote kilicho cha Mungu kutoka kwa
Yohana Mbatizaji. Hata leo bado tuna mitazamo kama hii, yaani, tunamhukumu mtu
kutokana na familia yake, ukoo wake, kabila lake, na utaifa wake, na kusahau
kweli ya kile akisemacho.
Kwa
vile Mungu ni UPENDO na NGUVU yenyewe
isukumayo yote katika mabadiliko yote kuelekea UKAMILIFU wa VYOTE, hatazami
kamwe kama sisi tutazamavyo. Kama alikuumba kwa sura na mfano wake, na
akakubali kuuchukua ubinadamu wetu na kukakaa kwetu-‘Emmanueli’, hawezi kamwe
kuacha sura ile na mfano wake ule upotee bure, Mwa 1:27. Kama kupotea au
kujipoteza ni wewe na mimi katika ujuaji wetu na kiburi chetu. Hivyo leo Mungu
anakuambia wewe na mimi kama alivyowaambia wana wa Israeli kwamba, “Imba, wewe
uliye tasa, wewe usiyezaa; paza sauti yako kwa kuimba, piga kelele, wewe
usiyekuwa na utungu; maana watoto wake aliyeachwa ni wengi kuliko watoto wake
yeye aliyeolewa, asema Bwana,” Isa 54:1. Ni furaha iliyoje kwa maamuzi haya ya
Mungu yasiyotazama historia yako na yangu iliyombaya, zaidi ya kuanza upya
naye? Mungu aseme nini tena ili umwamini?
Kukuondoa
hofu iliyo ndani yako na yangu pia, Mungu anatuambia, “Usiogope; maana
hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu
ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena,” Isa 54:4. Ndugu
yangu, Mungu hatazami historia yako mbaya, bali utayari wako wa kuanza upya
naye. Yesu analisema hili vizuri sana katika mfano wake ule wa wale
walioajiriwa siku moja kwa mida tofauti na kulipwa ujira sawa, Mt 20:1-16.
Baada ya manung’uniko ya baadhi ya wale walioanza kazi wa kwanza na kufikiri
kwamba wangelipwa zaidi, Mt 20:12, Yesu anawajibu bayana kwa kuonyesha Upendo
huu wa Mungu usio kipimo na kusema: “Rafiki,
sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari? Chukua iliyo yako, uende zako; napenda
kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe. Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama
nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema? Vivyo
hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho,” Mt
20:13-16. Kwa Mungu hakuna kuwahi au kuchelewa, ni utayari wako tu wa kuanza
yote upya Naye.
Mungu
wetu hana ubaguzi kwa yoyote yule, au chochote kile alichokiumba kwa sababu kwa
kufanya hivyo, yaani, ubaguzi ni sawa na
kujibagua Yeye mwenyewe. Mungu yupo tayari kuyakamilisha yote aliyoyaanzisha
ndani yako na vyote alivyo viumba ili vifikie ukamilifu wake. Na kwa kufanya
hivyo, Mungu ujifunua kwa kila kitu alichokiumba, na utukufu wake uonekana kwa
kila alichokiumba. Hii ndiyo nguvu ya Upendo wa Mungu kwa kila alichokiumba
kuelekea katika kusudi na malengo yake Mungu, yaani, UKAMILIFU wake. Ni nguvu
hiyo ndani yake na kwa kila kilichoumbwa na Mungu, “Kwa sababu Muumba wako ni
mume wako; Bwana wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye
Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote,” Isa 54:5. Je, unajambo lolote
ulilo nalo waweza kujisifia au kujivunia kuwa ni lako? Jibu ni hapana! Hata
pale tunapojivunia hayo Mungu anakuambia hivi; “Kwa kitambo kidogo nimekuacha;
lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya,” Isa 54:7. Maneno haya ya Mungu
yanadhihirisha wazi kabisa, MAISHA NI DHAMANA.
Na
kama maisha ni dhamana, wewe na mimi ipo siku itatupasa kutoa hesabu yake. Na
hesabu hiyo haitakosa kuongozwa na maswali haya mawili muhimu; moja, umefanya
nini kuhusu vipaji na karama nilizokupa? Na la mwisho ni hili; umefanya nini na
upendo wa Mwana wangu Yesu Kristo aliyekupeda hadi kuyatoa maisha yake kwa
ajili yako pale Msalabani? Ni kweli hapa na pale Mungu huyafunga macho yake
tunapofanya vibaya kwa ubinadamu wetu, ingawa anayomatumaini makubwa kwa kila
mmoja wetu kumrudia. Naye anasema, “Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso
wangu dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu, asema Bwana,
Mkombozi wako,” Isa 54:8. Rehema ya Mungu uendana na utayari wako na wangu wa
kufanya toba ya kweli na majuto, ingawa ni kweli kwamba Neema na Huruma ya
Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Na neno hili la Mungu linathibitisha hiki
nilichosema, yaani, ‘Neema na huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.’
Naye Mungu anasema, “Kwa maana jambo hili limekuwa kama maji ya Nuhu kwangu;
maana kama nilivyoapa ya kwamba maji ya Nuhu hayatapita juu ya dunia tena,
kadhalika nimeapa ya kwamba sitakuonea hasira, wala kukukemea,” Isa 54:9.
Ndugu
yangu, tuukumbatie Wema, Neema, na Huruma ya Mungu. “Maana milima itaondoka, na
vilima vitaondolewa; bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano langu la
amani halitaondolewa; asema Bwana akurehemuye.” Isa 54:10. Mungu daima anataka
kuyakamilisha yote aliyoyaanzisha ndani mwako. Mimi na wewe tumeumbwa tuishi
milele. Amina!
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kwa kitambo
kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya,” Isa 54:7
Tusali:-Ee Yesu Mwema,
asente sana kwa kunipenda kama nilivyo. Nijalie neema ya kuishi yale
aliyoyakusudia Mungu ndani ya maisha yangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario