lunes, 19 de diciembre de 2016

TAFAKARI: DECEMBA 21, WIKI YA 4 YA MAJILIO


DECEMBA 21, WIKI YA 4 YA MAJILIO

Somo: Wim 2:8-14

Zab: 33:2-3, 11-12, 20-21

Injili: Lk 1: 39-45

Nukuu:

Mpendwa wangu alinena, akaniambia, Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako,” Wim 2:10 

Maana tazama, kaskazi imepita, Masika imekwisha, imekwenda zake,” Wim 2:11

 Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu,” Lk 1:41

“akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa,” Lk 1:42

“Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?” Lk 1:43

“Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana,” Lk 1:45

TAFAKARI: “Na heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.”

Wapendwa wana wa Mungu, somo letu la kwanza kutoka katika kitabu cha “Wimbo ulio bora,” linaelezea mahusiano ya karibu kati ya Mungu na viumbe vyake kwa lugha ya picha. “Mpendwa wangu alinena, akaniambia, Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako,” Wim 2:10. Hata hivyo lugha hii ya picha inagusa agano jipya la Kimasiha kati ya Mungu na watu wake. Wakati wa ukamilisho wa tendo hili haupo mbali tena kama ilivyokuwa huko nyuma. “Maana tazama, kaskazi imepita, Masika imekwisha, imekwenda zake,” Wim 2:11. Hivyo ni halali kabisa kutumia maudhui haya ya uhusiano fumbo kati ya Mungu na viumbe alivyopendezwa navyo.

Fumbo hili linaonyesha ukaribu uliopo kati ya wawili wapendanao na walio wapenzi wa kweli kabisa. Ni upendo usioficha chochote na ulio wazi kwa kila kitu. Ni upendo uliotayari kupokeana na kuchukuliana katika hali zote licha ya mapungufu yaliyopo kwa upande mmoja, yaani, kwetu sisi wanadamu. Upendo huu wafananishwa na wakati wa kupelea katika msimu wa kawaida wa mwaka yaani, “Mtini wapevusha tini zake, Na mizabibu inachanua, Inatoa harufu yake nzuri; Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako,” Wim 1:13. Mwisho, upendo huu unachukua fumbo la Hua na kutoka, kwa lengo la kukutana na yule ampendaye.

Hapa ndipo tunapoona hatua kuelekea kile kilichokuwa ndani “kinadharia” na kufanywa katika uhalisia wake. Hili ndilo Mungu analolitaraji kulifanya katika kipindi hiki cha kuja kwake, yaani, Majilio. “Hua wangu, mafichoni mwa jabali, Katika sitara za magenge, Nitazame uso wako, nisikie sauti yako, Maana sauti yako ni tamu na uso wako mzuri,” Wim 2:13. Fumbo hili la njiwa/hua ndiyo fumbo zima la kumwilishwa kwa NENO na kukaa kwetu. Mama Bikira Maria kwa “ndiyo” yake, yote yanafanyika. Hii ndiyo habari tunayoisika katika Injili yetu ya leo.

Wapendwa wana wa Mungu, Bikira Maria akiwa amejaa Neema na kwa mtazamo wa  hekalu la Mungu, anaifunua neema hii na kuipeleka kwa wengine. Bikira Maria anabeba habari njema ya wokovu wetu. “Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda,” Lk 1:39. Ni furaha hiyo ya Kimasiha aliyojawa nayo inamsukuma kuondoka na kuelekea kwa binamu yake Elizabeti. Hakika furaha ni kama kikohozi hakuna awezaye kuzuiya!

Elizabeti, binamu yake Bikira Maria, anatafsiri tendo hili la maamkio haya yaliyogusa mwitikio wa ndani katika nafsi yake kama tendo la kinabii. “Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu,” Lk 1:41. Elizabeti anafunuliwa na kutambua fumbo lililojificha ndani ya Bikira Maria na Ukuu wa Kichanga kilichokuwa tumboni mwake, na kujinyenyekeza. Naye “akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa,” Lk 1:42. Hakika ndani ya tumbo la Maria ambayo ndiyo Terbenakulo la kwanza, kumefichwa subira yote katika historia yote ya Israeli na wokovu wa mwanadamu.

Kutokana na ukubwa wa jambo hili, Elizabeti anajihoji na kusema, Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?” Lk 1:43. Hakika Mungu hubaki kuwa Mungu, njia na mipango yake ufunuliwa kwa wale tu wajinyenyekezao kumwelekea Yeye. Ni katika hali hii, Bikira Maria naye anaamini pasipo shaka matendo makuu ya Mungu yaliyofichwa ndani mwake. Ni katika mazingira haya tunaona wimbo ule wa Bikira Maria “Magnificant,” wa kumsifu Mungu kwa makuu yake kwake ambaye hana chochote cha kujivunia zaidi kustaajabu Makuu ya Mungu.

“Ndiyo” ya Bikira Maria inafanya kazi ya Mungu, Mpango wa Mungu, ambao unafanyika kwetu pia. Hakika Bikira Maria katosheleza kabisa katika safari hii ya wokovu kwa kuinurisha nuru ile iliyofifishwa na Hawa mzazi wetu wa kwanza. Bikira Maria ni Mama yetu sote na vizazi vyote hadi mwisho wa nyakati. “Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana,” Lk 1:45. AMINA!

Tumsifu Yesu Kristo!

Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli,” Isa 29:19

Tusali:-Mungu uyaonaye yote ndani yetu, tunyenyekeshe pale tunapojiinua kutokana na ubinadamu wetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario