SIKUKUU YA
BIKIRA MARIA MAMA WA MUNGU
JANUARI
1
Somo I: Hes 6:22-27
Zab: 67:2-3, 5, 6, 8
Somo II: Gal 4:4-7
Injili: Lk 2:16-21
Nukuu:
“Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya
wana wa Israeli; nami nitawabarikia,” Hes 6:27
“Hata ulipowadia utimilifu wa wakati,
Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya
sheria,” Gal 4:4
“Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali
u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu,” Gal 4:7
“Wakaenda
kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini,”
Lk 2:16
“Lakini Mariamu
akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake,” Lk 2:19
“Wale wachungaji
wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na
kuyaona, kama walivyoambiwa,” Lk 2:20
“Hata zilipotumia
siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika
kabla hajachukuliwa mimba,” Lk 2:21
TAFAKARI:
“Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote,
akiyafikiri moyoni mwake.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Leo ni mwaka Mpya. Tulio hai tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa yale yote
aliyotujalia na hasa yale tuliyokutana nayo kwa mwaka tuliouaga, tukijua kwamba
kila jambo lilikuwa na sababu yake na mapenzi ya Mungu ndani yake. Leo
tunapouanza mwaka kwa namna ya pekee Mama Kanisa anaadhimisha siku hii kwa
Heshima ya Mama Bikira Maria Mama wa Mungu. Kuuanza mwaka Mpya twahitaji baraka
za Mungu, tukisafiri pamoja na Mama Bikira Maria Mama wa Mungu kama mfano hai wa
kuiga na kufuata.
Kadiri ya somo letu la
kwanza, wana wa Israeli iliwapasa kuliweka jina la Bwana juu ya mambo yote na
ndivyo walivyobarikiwa. “Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa
Israeli; nami nitawabarikia,” Hes 6:27. Wana wa Israeli walilishika na kulibeba
jina la Mungu kama ilivyo uhusiano kati ya mke na mume. Jina hili la Bwana
liliathiri kwa kiasi kikubwa mafanikio yao, wakati mwingine ilikuwa balaa
walipoliasi jina hili. Hivyo hatima ya maisha yao ilitegemea namna
walivyolichukulia jina hili la Mungu aliye hai. Ndivyo hivyo basi wakati wana
wa Israeli walipokuwa uhamishoni na katika unyonge wao, jina la Mungu
lilinajisiwa katika mataifa, Eze 36.
Ni kwa namna hiyo hiyo
tunaona kwamba wana wa Israeli walipowekwa huru kwa maajabu makubwa ya Mungu,
jina la Mungu lilitakatifuzwa, liliinuliwa juu kabisa kutoka unyonge na
kudhalilishwa, na kutakatifuzwa, Eze 36. Ni kutoka katika mtazamo huu kulitaja
jina la Mungu na watu wake ni chanzo cha baraka na dhana ya ukarimu. Hivyo
kuuanza mwaka na kuumaliza yatupasa kuweka vipauwa mbele muhimu na hasa kwa
maisha ya kiroho.
Kipauwa mbele namba
moja ni kukaa ndani ya jina la Mungu na neno lake. Huko ndiko kwenye uzima wa
kweli. Kristo ni Mzabibu nasi ni matawi. “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi,
akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi
hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5. Uzima huu twaupata pia kwa kulishika
neno lake; kulisoma, kulipokea, kulitafakari, kulitafiti, na kulikumbuka kusiko
kikomo. “Amin, amin, nawaambia, Yeye
alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele;
wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani,” Yoh 5:24.
Kipauwa
mbele namba mbili ni kulishwa na kuhuishwa kila mara kwa kupokea Masakramenti
katika hali iliyo safi, hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Ndani ya
Sakramenti hii ya Ekaristi Takatifu, tunakaa ndani na katika Kristo, na kupata
uzima wa milele. Mwili na damu ya Kristo ni chakula na kinywaji cha kweli. Naye Yesu anasema, “Aulaye
mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya
mwisho. Kwa maana mwili wangu ni
chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu
yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh 6:54-56.
Pamoja na makuu
tuyachotayo kutoka Sakramenti hii, neema na baraka zake, Mtume Paulo anatupa
angalizo juu ya Mwili huu na Damu hii ya Kristo. “Basi
kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili,
atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Ndugu yangu,
kabla ya kuijongea meza hii ya Bwana jihoji kwanza nafsini mwako. Je, nastahili
kwa hali niliyo nayo? “Lakini mtu ajihoji
mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe,” 1Kor 11:28. Tusiogope
macho ya watu, na wala tusipende kushiriki Sakramenti hii na Karamu hii ya
Upendo kwa mazoea.
Kipauwa mbele namba tatu tusiache kamwe
kupatanishwa kwanza na Mungu kwa Sakramamenti ya Upatanisho au Kitubio. Jambo la kusikitisha leo Sakramenti hii
ya Upatanishao imekuwa kama ‘kituo cha polisi.’ Walio wengi leo wanataka
kuhalalisha dhambi. Sakramenti hii ya Upatanisho imewekwa rasmi na Kristo
mwenyewe katika Kanisa, na wahudumu wake ni wale walioteuliwa {kuhesabiwa haki
na Mama Kanisa}, kupakwa mafuta, na
kuwekwa wakfu, {Mapandre na Maaskofu} na kwa ajili hiyo huadhimisha Sakramenti
hiyo. Hapa tunakutana na Huruma ya Mungu, Msamaha wa Mungu, na Kupatanishwa na
Mungu. Naye Yesu anasema, “Wo wote mtakaowaondolea
dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh
20:23. Ndugu yangu tuijongee Huruma ya Mungu, Msamaha wa Mungu, na Kupatanishwa
naye {nafsi, jirani, na mazingira}. Mwaka huu tunaouanza unatudai kuishi katika
ukweli huu kama kweli twautaka uzima ndani yetu.
Somo letu la pili na
Injili linafafanua fumbo zima la kumwilishwa, Neno akafanyika mwili akakaa
kwetu, Yoh 1:14. Na hapa ndipo tunapoona nafasi ya Mama Bikira Maria Mama wa
Mungu tunaye msherehekea leo katika tendo hili zima. Tendo hili limetokea
katika utimilifu wa wakati, baada ya muda mrefu wa kusubiri. “Hata ulipowadia
utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke,
amezaliwa chini ya sheria,” Gal 4:4. Tendo hili limebeba sehemu kuu mbili kwa
wakati mmoja; kwanza linawapa watu uwana wa Mungu kwa kuwafungua kutoka sheria
ya Musa. “Wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa
Mungu,” Gal 4:7.
Sehemu ya pili,
kumwilishwa kwa neno kumefanyika katika hali ya kibinadamu na kwa sheria,
yaani, kwa Kristo kuzaliwa na mwanamke chini ya sheria ili kumkomboa huyo
mwanadamu aliye katika sheria. Sheria
inamweka Kristo katika historia ya wokovu, yaani katika historia ya watu wake.
Mwanamke ni kati ya watu, yaani, ndugu zake Kristo aliokuja kuwaweka huru na
kuwakomboa kwa kuwafanya kama yeye, yaani, wana wa Baba. Kwa maana hiyo, “Kwa
kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya
kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na
roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu,” Rum 8:15-16.
Katika hali hii ya
kumwilishwa, tunaona katika Injili yetu ya leo kwamba waamini wa kwanza wa
tukio hili ni wachungaji ambao wapo karibu ya Maria Mama yake Yesu na Mtoto Yesu, walio jiachia wazi kwa Mungu.
Hapa Bikira Maria ni Mama kwa utayari na NDIYO yake kwa Neno la Mungu, kwa
uamini wake na ukimya ambao unamfanya kupokea fumbo hili: “Hapo mwanzo
kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye
Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa
Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:1,14. Mapaswa na
ubora wa wana wa Israeli ulikuwa ‘kusikiliza Neno la Mungu.’ Katika tendo hili,
Bikira Maria ndiyo kielelezo cha ukamilifu na utimilifu wa Neno hili la
kumwilishwa kwa NDIYO yake. “Mariamu akasema,
Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema,” Lk 1:38a.
Fumbo hili ndilo linalomwinua Bikira Maria katika nafasi hii ya juu kabisa
Binadamu kuwekwa. Hivyo katika shina la Daudi limetoka chipukizi ambalo ndilo
tumaini na jibu la Mungu kwa watu wake.
Nafasi ya Maria katika
tendo hili la utayari wake, yaani Neno kumwilishwa ni uchungu, mateso, na
furaha. Yusufu mumewe katika sintofahamu hii anataka kumwacha kwa siri. “Naye
Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu
kumwacha kwa siri,” Mt 1:19. Ndiyo ya Bikira Maria kwa Mungu inakuwa mwanzo wa
aibu, ugumu wa kueleweka na mumewe, na maumivu. Hata pamoja na hali hii Bikira
Maria hakuwa sababu ya kuzuia mapenzi ya Mungu yasitendeke kwa sifa na Utukufu
wa Mungu na watu wake aliowaridhia. Sauti ya Mungu ilimfikia Mama Maria kupitia
mwanaye Yesu Kristo aliyemzaa, Simeoni, na wachungaji. Maria aliyaweka yote
haya na kuyatafakari moyoni mwake. U
Mama wa Bikira Maria na upana wa kifua chake wa kuyabeba mambo makuu na mazito
haukuishia pale horini tu, bali aliendelea kuubeba U Mama huo wa Mungu na hali
hiyo hadi Msalabani. Hapa ndipo aliposhuhudia kifo katili dhidi ya mwanaye
mpenzi ambaye hakuwa na kosa lolote zaidi ya wema aliyotutendea.
Hakika Mama Bikira
Maria aliyastahimili na kuyashiriki kikamilifu mateso ya mwanaye Yesu Kristo. “Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama
mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene,” Yoh 19:25.
Pamoja na huzuni na uchungu aliokuwa nao Mama Bikira Maria na Yesu ambaye kwa
sasa alikuwa tayari kesha wambwa juu msalabani, Yesu analikabidhi Kanisa (kwa
mitume) na jumuiya yote ya waamini kwa Mama yake. “Basi Yesu alipomwona mama
yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake,
Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na
tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake,” Yoh 19:26-27. Huyu
ndiye Mama Bikira Maria Mama wa Mungu tunaye msheherekea leo. Huyu ndiye
tunayetaka kuanza naye mwaka huu mpya tukiwa na imani pasipo shaka kwamba
tutamaliza naye mwaka huu salama kama ilivyokuwa NDIYO yake wakati ulipotimia
pale horini, na kuendelea na NDIYO yake hadi mwisho pale msalabani
ulipotundikwa wakovu wetu na UTUKUFU wa
Kristo na wetu. Hakika yatupasa
kumshangilia Mama Yetu Bikira Maria, Mama wa Mungu.
Nilipokuwa likizo
nyumbani nilikumbuka tukio la miaka mingi iliyopita mara baada ya kumaliza
mwaka wa Malezi huko Mahanje Songea. Nilikuwa na furaha kubwa sana ya
kuchaguliwa na kuendelea na masomo ya sekondari katika Seminari ya watawa wa
Mt. Fransisco wa Assis huko Maua Seminary-Moshi.
Nikiwa nyumbani
Arusha-Njiro najiandaa kwa kuanza masomo hayo ya kidato cha kwanza, niliugua
homa ya miguu na kuhisi kupooza na kutoweza kutembea tena. Niliona kama vile
ndoto yangu ya kuwa siku moja Mtawa na Padre kuanza kutoweka. Mama yangu Mzazi
alinihudumia kwa upendo mkubwa; kuniogesha na kunisaidia hudumu nyingine
nilizohitaji kwa hali ile niliyokuwa nayo. Nakumbuka alinibeba mgongoni mwake umbali
usiopungua zaidi kilomita 15 hivi kwenda na kurudi, kwani wakati ule hapakuwa
na usafiri wa daladala na bodaboda kama ilivyo sasa. Safari hii tulikuwa
tunaelekea hospitali ya KCMC-Moshi kwa vipimo zaidi. Hakika Mama yangu
alitaabika sana nami. Jambo la ajabu sikuona kukerwa na hali ile niliyokuwa
nampatia.
Nilipata vipimo na
kurejea nyumbani Arusha-Njiro. Mungu alivyomwema kwa watu wote na nyakati zote,
baada ya wiki kama mbili hivi nilianza kupata hauweni. Tarehe za kufungua
Seminari zilipowadia nilikuwa tayari kwa masomo na mwenye afya ya kutosha.
Hivyo mwaka huu baada
ya miaka kadhaa kupita, Mama yangu Mzazi naye alipatwa na homa ya miguu kama
ilivyokuwa kwangu ila kwa tatizo tofauti. Nikiwa likizo ilinipasa kumuhudumia,
hasa kumwinua kitandani na kumkominisha kila siku mara baada ya kuadhimisha
Misa kigangoni kwetu St. Josephina Bakhita Korona-Njiro. Ilinipasa pia kumpikia
kwani karibu ndugu zangu wote wameolewa na kuoa hivyo wanamiji yao. Wajukuu
aliokuwa anaishi nao Mama yangu nyumbani asubuhi hadi jioni iliwapasa kuwa
shuleni {shule ya upili}. Hivyo muda mwingi nilikuwa naye. Nilimbeba ingawa
siyo mgongoni hadi KCMC kwa matibabu. Nilitumia muda mwingi kumfurahisha kwa
kumchezea gitaa na kuimba. Kwa kweli nilijaribu kurudisha shukrani zangu japo kwa
uchache aliyonitendea miaka hiyo mingi iliyopita.
Leo ninamshukuru
Mungu Mama yangu anaendelea vizuri licha kwamba hajapona kabisa. Huu upendo ni
sehemu tu ya upendo niliouonja kwa Mama kwa namna alivyotesema na kutaabika
nami bila kuchukizwa na karaha nilizompatia. Hakika kama nikiambiwa leo nilipe
alichonitendea sintoweza kufanya hivyo hata nikipewa miaka 1000 na Mungu ya
kuishi nikiwa nafanya kazi usiku na mchana. Sintoweza kulipa kwa sababu kadiri
nitakavyoishi na kuwa hai, ni kwa kipimo hicho hicho deni hili
litakavyoongezeka hata kama yeye atakuwa kesha kufa.
Wapendwa wana wa
Mungu, kwa sadaka na matojitoleo ya Mama Maria, Mama wa Mungu na hasa kwa NDIYO
yake katika fumbo hili la kumwilishwa, mimi na wewe tuna deni kubwa sana la
lipa licha ya kwamba Mwanaye Yesu Kristo kesha tulipia deni letu, dhambi zetu
kwa sadaka yake pale msalabani. Kwa upande wa kwanza, deni hili ni kuishi
upendo wa kweli na haki kwa kila aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni kwa
sababu ya upendo huu Kristo alikubali kuyatoa maisha yake kwa ajili yako na
yangu. “Amri
yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko
huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:12-13. Ni kwa kumkomboa
huyu aliyeumbwa kwa sura na mfano wake, Mungu anaruhusu mwanaye ateseke kwa
ajili yangu na yako, na Mama Bikira Maria kushiriki mateso haya ya mwanaye. Na
sehemu ya pili ya deni hili ni kuwa watakatifu kama Baba yetu wa Mbinguni
alivyo Mtakatifu. Utakatifu huu tunaupata kwa kuishi vyema na kuzitumia vyema
karama zetu kila mmoja kadiri ya wito wake, kwa kutimiza utume wake vyema.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi ninyi
mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48
Tusali: Ee Yesu Mwema,
niongoze katika kweli na haki. Amina
Herini kwa Mwaka Mpya, 2017
Herini kwa Mwaka Mpya, 2017
No hay comentarios:
Publicar un comentario